AINA TANO(5) YA MASWALI AMBAYO WATU HUKUULIZA WEWE.

Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe mpendwa wa MUNGU.
Karibu nikujuze ujumbe wa Neno la MUNGU katika siku hii njema sana.
Leo nazungumzia maswali.
Somo hili ni ufunuo ambao ulikuwa unaongea ndani yangu miezi michache iliyopita wakati nikiwaZanzibar.
Kwa kuelezea maana ya Neno Swali ni kama ifuatavyo;
Swali ni jambo linalotakiwa kujulikana jawabu lake.
Swali ni kitu kinachoulizwa.
Maswali ni maneno yanayoambatana na alama ya kuuliza.
Alama ya kuuliza ni taarifa tu kwamba yanahitajika majibu katika jambo hilo.
Usijibu kila swali haraka haraka tu bali ijue kwanza nia ya muuliza swali kabla hujamjibu.
Biblia inasema mambo mengi kuhusu maswali, hebu acha tuanze kama ifuatavyo;

2 Timotheo 2:23'' Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi. ''

Kama mteule wa MUNGU ni lazima tu utakutana na maswali mengi, iwe ni kuhusu wokovu wako, imani yako, maisha yako au hata huduma yako.
Ijue nia ya anayekuuliza swali ndipo umjibu swali lake.
Nilianza huduma ya kuhubiri mtandaoni mwaka 2012.
baada ya mwaka kupita nikajigundua kwamba nilitumia muda mrefu sana mtanadaoni lakini ujumbe nilioandika ulikuwa mchache sana, yaani chini ya lengo. Kwa haraka sana niligundua kwamba muda mwingi sana mtandaoni nilikuwa najibizana tu na watu ambao hata hawakuwa na nia ya kujua, ila wengi wao walikuwa wanatumikA kipepo ili kuhakisha sifanye chochote katika huduma yangu ya kupeleka injili ya KRISTO kwa watu wote kupitia mtandao.
Ni mara nyingi MUNGU alinionya lakini sikuwa naielewa lugha yake alipokuwa nasema nami. Baada ya kuielewa sauti ya MUNGU juu ya maswali nilijikuta najibu maswali mengi lakini yanayowasaidia waulizaji. Kuna siku ndugu mmoja aliniuliza swali Inbox, nilipotaka kumjibu nikakatazwa  rohoni. sikumjibu chochote yule ndugu na baada siku kadhaa akaniambia kwamba alikuwa ananijaribu tu ili ajue nitasema nini. Baada ya hapo muda wangu nimeutumia vizuri sana katika kuandaa masomo ambayo yalikuwa yana majibu ya maswali mengi ya watu, maana ndivyo nilivyomuomba MUNGU. Kwa kulijua hilo nilijikuta kila mwaka naandaa masomo zaidi ya mia na themanini na masomo hayo kuwasaidia wengi. Ndugu ninapofundisha haya sina nia kwamba usiwe unajibu maswali bali ijue nia ya swali kabla ya kumjibu mtu.
Biblia hapo juu iko wazi kabisa ikisema tujiepushe na maswali ya kipumbavu.
Kumbe pia wakati mwingine huwa kuna maswali ya kipumbavu, na Biblia inasema maswali ya aina hiyo tujiepushe nayo.
Kuna  maswali ambayo kama tuking'ang'ana  nayo yanaweza kutunajisi au kutupunguzia nguvu ya MUNGU ndani yetu.
Usikubali swali likakunajisi, usijibu uongo bali jibu iliyo kweli.
Kama hujui jibu ni heri ukawa muwazi tu na fanya juhudi kwa kuuliza kwa wanaojua ili wakusaidie.
Binafsi mimi napenda sana kuulizwa maswali lakini nimejifunza kwamba ni lazima kwanza niijue nia ya muuliza swali ndipo nimjibu.
Mimi naamini kwa sekunde kama tano tu zinatosha kujua nia ya muuliza swali ndipo umjibu.
Biblia hapo juu inasema tujiepushe na maswali ambayo hayawapi watu wa MUNGU elimu na ufahamu wa kiMUNGU.

AINA TANO(5) ZA MASWALI AMBAYO WATU HUKUULIZA WEWE.

1.  MASWALI YA MTEGO ILI UNASWE.

Mwanzo 3:1 '' Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana MUNGU. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema MUNGU, Msile matunda ya miti yote ya bustani?''

Eva ni mfano mmoja katika mingi ya watu ambao waliulizwa maswali ya mtego ili wanase. Eva alinasa kwenye mtego wa swali la shetani.
Swali na mtego linaweza likakusababishia ukanasa na ukatenda dhambi.
Ukiijua nia ya anayekuuliza swali kwamba swali  kuna mtego ndani yake, jitahidi ujibu kwa hekima na maarifa ili usinase katika mtego.
Katika watu ambao hukuuliza maswali mbalimbali naomba ujue kwamba ndani yao wapo pia ambao hukuuliza maswali ya mitego hivyo uwe makini.

Luka 6:45 ''Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.''

Mtu anaweza akakutega katika swali lake ili ufunguke. Kwa sababu mtu hunena yale yanayoujazayo moyo wake kama andiko linavyosema hapo juu, basi kupitia swali na mtego unaweza kujikuta unatoa hata siri kwa adui yako wa kiroho maana utajikuta unafunguka tu kumbe ulitegwa.
Jifunze kwa BWANA YESU ambaye yeye kuna wakati mafarisayo walipokuwa wanamuuliza maswali ya mitego yeye alikuwa anawauliza swali kwanza na wao, wakijibu anawasaidia zaidi kupitia maswali yote mawili yaani swali walilomuuliza na swali alilowauliza.
Mama unaweza ukaulizwa maswali ya mtego na marafiki zako au au majirani zako kumbe katika mtego huo inayotafutwa ni ndoa yako ili ivunjike. ndugu ijue nia ya muuliza swali kabla ya kumjibu. na sio lazima ujibu maswali yote bali tumia akili na pambanua kwa lugha ya rohoni kuhusu swali hilo.
Mtu hunena yale yaujazayo moyo wake. Hivyo unaweza kutegwa kupitia swali na watu wakaona kile kijazacho moyo wako maana ndicho kitakachotoka kwako.
Unaweza hata ukamsema vibaya mchungaji wako kupitia swali la mtego uliloulizwa. Ndugu Uwe makini sana na maswali ya mtego.

2. MASWALI YA KUTUMWA NA MTU MWINGINE ILI AJUE JAMBO FULANI KWAKO, KWA NIA YAKE.

 Mathayo 2:8 '' Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.''

Katika andiko hili tunaona Mfalme Herode alitaka kujua kuhusu mtoto YESU ili amuue. Kwa kutaka kujua kuhusu YESU aliamua kuwatumia Mamajusi lakini MUNGU aliwaonya wale mamajusi ili wasipite njia ile alikuwako Herode.
Alitaka wakaulize ulize hukusu YESU kisha wampelekee taarifa. Huyu Mfalme alikua na nia yake  mbaya dhidi ya YESU.
Hata wewe ndugu kuna watu wanaweza kukuuliza maswali kumbe wametumwa tu ili majibu yako wayapeleke kwa aliyewatuma.
Ndugu ijue nia ya muuliza swali kabla ya kumjibu.
Ukishagundua kwamba anayekuuliza swali sio yeye anayetaka kujua majibu bali ni aliyemtuma basi uwe makini sana katika majibu yako.
Unaweza ukamjibu mtu vizuri tu na ukamuelekeza vizuri ukidhani unamsaidia kumbe unatoa siri kwa adui zako kiroho ili wakushambulie vizuri. Ndugu ijue nia ya mtu anayekuuliza swali ndipo umjibu.
Akina Herode ni wengi leo na hutuma watu ili kuuliza uliza kuhusu wewe kumbe wana mpango mbaya dhidi yako.

Binti au kijana unaweza kuulizwa ''Je mnaoana lini na mchumba wako?''
Ukigundua kuna ajenda ya siri kupitia swali hilo hakikisha hutoi siri zako.
Unaweza ukauliza ''Je, Una mchumba?'' Kumbe anayekuuliza ana mpango wa kukuharibia. Ndugu, heri uulizwe maswali na watumishi wa MUNGU wenye lengo la kukusaidia kiroho hapo utakuwa umefanya vyema. Nakuomba ndugu uwe makini sana katika kujibu maswali, ijue nia ya muuliza swali kabla ya kumjibu. ukigundua nia yake ni njema basi mjibu lakini ukijua kuna tatizo sehemu heri mwambie utamjbibu siku nyinge au kataa swali lake.

3. MASWALI YA KUJARIBU AU  KUKUPIMA.

Marko 10:2 '' Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu.''

Mfarisayo wakamwendea YESU na kumuuliza maswali ya kumjaribu. Ndugu hata leo mafarisayo bado wapo na wanaweza kukuuliza maswali ya kukujaribu.
 Usikurupuke ukiulizwa swali la kukujaribu maana unaweza ukakosea kupitia swali hilo.
Unaweza ukaleta aibu kwa sababu ya swali hilo.
Ijue nia ya muuliza swali kabla hujamjibu. kama anakupima basi mpime na wewe. Ona BWANA YESU alivyoaanza kuwajibu hao waliomuuliza swali la kumjaribu, aliwarudishia jibu kwa njia ya swali na
jaribu lao likavunjika. Marko 10:3 YESU baada ya kuulizwa swali la kujaribu akajibu kwa kusema  ''Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? ''

Ndugu, uwe makini na maswali ya kukujaribu.
Malkia mmoja alimuuliza maswali ya kumjaribu Mfalme mwenye hekima, lakini alijibiwa na kujishangaa mwenye, na akajikuta anatoa zawadi nyingi kwa Mfamle Sulemani.

1 Wafalme 10:1 ''Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la BWANA, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo. ''

Kujaribu kunaweza kuambatana na fumbo ndani yake hivyo uwe makini sana na maswali unayoulizwa.
Ndugu, ijue nia ya muuliza swali kabla hujamjibu.


4.  MASWALI YA DHIHAKA.

Luka 23:9-11 '' Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lo lote. Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana. Basi Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato. ''

Kuna watu wanaweza kukuuliza maswali ya dhihaka hivyo uwe makini sana.
Nimewahi kukutana na maswali ya dhihaka lakini mimi sikujibu kitu.
Hata BWANA YESU alipoulizwa maswali ya dhihaka na Herode yeye hakujibu kitu. Wasaidizi wa Herode na makuhani walijaribu kumlazimisha ili ajibu maswali yale lakini BWANA YESU Hakujibu, walimlazimisha maana waliona kama anamdhalilisha mfalme herode lakini yeye bado hakujibu kitu, askari ambao ni walinzi wa Herode walijaribu kumlazimisha YESU ajibu lakini yeye Biblia inasema hakujibu Neno.
Ndugu, ukikutana na maswali ya dhihaka uwe makini maana unaweza kurusha ngumi na kujikuta unatenda dhambi kisa swali tu la dhihaka.

Mfano wa swali la dhihaka ni mtu akukute kanisani unamwabudu MUNGU katika roho na kweli tena umeokoka, kisha aseme ''Hivi na wewe una MUNGU?''
Hiyo ni dhihaka maana kwanza amekukuta uko kanisai na unamwabudu MUNGU katika Roho na kweli tena umeokoka.
Maswali ya dhihaka ni mengi sana hasa kutoka kwa wapinga KRISTO hivyo ndugu jihadhari sana na maswali ya dhihaka maana unaweza ukanajisika kwa sababu tu ya swali.
Ijue nia ya muuliza swali kabla hujamjibu swali lake.

5.  MASWALI YA KUTAKA KUJIFUNZA.

Mthayo 18:21-22 ''Kisha Petro akamwendea akamwambia, BWANA, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? YESU akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.'' 
 
Haya ndio maswali bora kabisa.
Ni heri kila anyekuuliza swali awe ana lengo la kutaka kujua na kujifunza lakini sio wote huuliza maswali haya.
Ndugu, Nakuomba usiache kumjibu mtu anayekuuliza swali kwa lengo la kujifunza.
Binafsi mimi Napenda sana kuulizwa maswali lakini yawe maswali ya namna hii, yaani kwa lengo la kujifunza.
Kwenye andiko hapo juu tunajifunza kwamba Mtume Petro alikua kwenye ufahamu wake anajua kwamba mtu akimkosea basi kumsamehe mara saba ndio mwisho kabisa wa kusamehe. Alimuuliza BWANA YESU swali hilo akafafanuliwa vizuri kabisa na kupitia jibu la BWANA YESU kwa Petro aliyekuwa anataka kujifunza tunagundua kwamba. Kusamehe ni jambo la lazima kwa wateule wa MUNGU. 
Kusamehe na kusahau ni tabia ya MUNGU hivyo tunapotubu yeye anatusamehe.
Kuna madhara kwa kutokusamehe.
Maswali kama haya ni maswali mazuri sana na yana faida kwa watu wengi. Yamkini Mtume Petro asingeuliza swali hilo kwa BWANA YESU hakika hata mimi na wewe tusingejua kwa usahihi kiasi cha mwisho cha kuwasamehe watu.
 
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
 Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments