CHAKULA CHA WATOTO

Na Askofu mkuu Zakaria Kakobe.
            Tunaendelea kujifunza Biblia katika sura ya 15 ya kitabu cha MATHAYO. Ingawa kichwa cha somo letu ni “CHAKULA CHA WATOTO“, hata hivyo tuna mengi zaidi ya kujifunza. Tutaliangalia somo letu la leo katika vipengele vitatu:-
(1) ALAMA ZA MAFARISAYO;
(2) MPANGO WA MUNGU WA WOKOVU;
(3) CHAKULA CHA WATOTO.

(1) ALAMA ZA MAFARISAYO Katika sura ya 15 pekee ya kitabu hiki cha Mathayo, “Mafarisayo” wanatajwa katika MST. 1 & 12. Katika sura zilizotangulia pia tumeona Yesu akitaja sana habari za “Mafarisayo”. Katika MATHAYO 16:11-12, Yesu anatuonya kujilinda na mafundisho ya Mafarisayo. Sasa basi, tutawezaje kuwafahamu Mafarisayo na mafundisho yao? Tutawafahamu kwa alama zifuatazo:- 1. HULITANGUA NENO LA MUNGU NA KUYASHIKA MAFUNDISHO YALIYO MAAGIZO YA WANADAMU (MATHAYO 15:6-9; MARKO 7:13; YOHANA 17:17); 2. HUMHESHIMU MUNGU KWA MIDOMO TU ILA MIOYO YAO IKO MBALI NAYE (MATHAYO 15:8-9; TITO 1:16; YOHANA 4:23-25); 3. KAZI YAO NI KUTAFUTA MAKOSA (MATHAYO 15:2; 12:1-2; LUKA 14:1-3; MITHALI 28:9); 4. HUJIFANYA WANAFUATA MAAGIZO YA MUSA HUKU WAKIMKANA (MARKO 7:10-12; TITO 3:4-8; 1 WAKORINTHO 10:14) – Musa aliandika habari za Yesu (YOHANA 1:45; 5:46). Musa alisema kwamba watu wamsikie Yesu atakapokuja kwao na kwamba mtu yeyote ambaye hatasikia neno la Yesu, Mungu atalitaka kwake (KUMBUKUMBU LA TORATI 18:15, 18-19; linganisha na YOHANA 12:48; MATHAYO 17:1-5); 5. HUTAWADHA KWA NJE TU NA KUACHA MIOYO YAO MICHAFU (MARKO 7:4; MATHAYO 23:25-28).

(2) MPANGO WA MUNGU WA WOKOVU (MATHAYO 15:21-24) “Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli”, haimaanishi kwamba Yesu hakuja kwa ajili ya wengine wasio Waisraeli. Katika mpango wowote unaopangwa, yeye anayeupanga ana haki kuamua kwamba ataanzia wapi katika kuutekeleza na anaweza kuweka awamu mbalimbali za utekelezaji wa mpango huo. Katika Mpango wa Mungu wa wokovu, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo ilikuwa kuleta wokovu (unaojumuisha uponyaji) kwanza kwa Waisraeli (YOHANA 1:11; MATHAYO 10:6). Awamu ya pili ilikuwa kuwapa ulimwengu wote uliosalia wokovu (MATHAYO 21:423; YOHANA 10:16; 11:49-52; WARUMI 1:16; 9:24-30; MATENDO 15:13-18; WAEFESO 3:1-11).

(3) CHAKULA CHA WATOTO (MATHAYO 15:21-28) Watu wasio Waisraeli yaani Mataifa, walipewa jina “MBWA” na Waisraeli. Yesu Kristo alilitumia jina hili kwa sababu ulikuwa usemi wa kawaida ulioeleweka na kutumiwa na kila mtu Nyakati za Biblia (1 SAMWELI 17:43; 2 SAMWELI 3:8, 9:8). Jina “MBWA” halikuwa tusi ila lilieleza hali halisi iliyokuwapo. Mbwa hawakuwa wakitunzwa kwa kutengenezewa chakula kizuri na wale waliowafuga ila walitupiwa makombo tu. Hawakuruhusiwa kama ilivyo leo kukaa ndani ya nyumba kuwa karibu sana na wanadamu. Mataifa waliitwa “mbwa” kwa jinsi ambavyo hawakuwa na “haki ya ndani” walizokuwa nazo Waisraeli. Mungu alihesabiwa kukaa katika nyumba ya Waisraeli peke yao. Hao tu ndio waliokuwa watoto wake (1 WAFALME 8:13). Baba anawajibika kuwapa kwanza watoto wake chakula. Ingawa anaweza kumpa chakula mtoto wa wengine hata hivyo kizuri kitakuwa cha watoto wake kwanza. Watu tuliookoka ni watoto wa Mungu (YOHANA 1:12). Kutokana na kuwa watoto, chakula cha uponyaji, kufunguliwa kutokana na nguvu za giza n.k.; vyote hivi ni HAKI YA WATOTO KATIKA FAMILIA YA MUNGU. Kama hapa mbwa alipewa makombo basi sisi watoto tutapewa uzima tena uzima tele. (MATHAYO 7:7-11; MARKO 9:23; ZABURI 103:13; ISAYA 49:14-16). ………………………………………………………………………………………….
          Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la! Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
           Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..


Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe Fungua
Tovuti       : http://www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : http://www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube  : http://www.youtube.com/user/bishopkakobe

Comments