HIVYO HIVYO WANAWAKE NA WAJIPAMBE KWA MAVAZI YA KUJISITIRI, PAMOJA NA ADABU NZURI.

Scholar Mabula.
 Na mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe mpendwa.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

1 Timotheo 2:9-10 ''Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani; bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa MUNGU.''

Wanawake wanatakiwa wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri.
Wanawake wanatakiwa wavae mbele za watu mavazi ya kujisitiri.
Nilikuwa najiuliza, kwanini Biblia inaagiza wanawake wavae mavazi ya kujisiri?
Mbona haikusema wavae mavazi yenye rangi nzuri?
Mbona haikusema wavae mavazi ya bei kubwa tu?
Nikagundua kwamba vazi linaweza kuwa la bei kubwa lakini likawa linadhalilisha.
Vazi linaweza likawa na rangi nzuri lakini ni vazi la kikahaba.
Biblia inaagiza kuvaa mbele za watu vazi la kujisitiri.
Kamusi ya kiswahili sanifu inasema kwamba Kujisitiri maana yake kuficha kitu cha aibu ili kisionekane.
Ni kuficha jambo la aibu ili lisionekane.
Ni  kuficha aibu.
Mtu kuwa uchi mbele za watu ni aibu.
Walakini kuna baadhi ya wanawake  hawaioni hiyo aibu ndio maana hawavai mavazi ya kujisitiri.

MUNGU kupitia Neno lake ndiye aliyeagiza kwamba wanawake wavae mavazi ya kujisitiri, je mwanadamu anayeshindwa kumtii Muumba wake, huyo atakuwa anamtii nani?

Mwanamke aliyeokolewa na BWANA YESU anatakiwa awe tofauti na wanawake wa kidunia.
Watu wa kidunia humtii shetani ndio maana kwao kuvaa kikahaba mbele za jamii ni jambo la kawaida tu.
Tunajua kabisa ulimwengu wote uko katika yule mwovu lakini wewe mwenda mbinguni hakikisha hunaswi na unajisi wa dunia.

1 Yohana 5:19-20 ''Twajua ya kuwa sisi tu wa MUNGU; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu. Nasi twajua kwamba Mwana wa MUNGU amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake YESU KRISTO. Huyu ndiye MUNGU wa kweli, na uzima wa milele.''

Dunia hukaa katika yule mwovu.
Watu wanaoitii dunia hukaa katika uovu.
Kulipinga agizo la MUNGU la kukutaka kuvaa mavazi ya kujisitiri mbele za watu ni taarifa tu kwamba unaitii dunia badala ya MUNGU.
Wanawake wa kidunia wanaweza wakajipamba mitaani kwa vimini na ujezebeli, lakini mwanamke wa KRISTO natakiwa ajipambe kwa mavazi ya kujisitiri na adabu safi.
Ninaposema mavazi ya kujisiri sina maana ya yale mavi ya kidini yaliyo na maagano ya kipepo.
Sina maana ya mavazi ya kijadi yaliyo na maagano na mizimu.
huko sio kujisitiri bali kumtukuza shetani.
 
Njia mojawapo ya kumjua mwanamke mwenye adabu nzuri ni kuangalia uvaaji wake mbele za jamii.
Kabla sijaoa kuliwahi kutokea mabinti ambao walihitaji tuingie katika uchumba lakini uvaaji wao tu ilikuwa ni taarifa kwangu kwamba natakiwa nikae mbali sana na wao.
Nilikuwa nimepanga chumba katika nyumba ambayo ilikuwa na wadada ambao walikuwa wanavaa sana kikahaba. Walikuwa wanavaa kimitego wakidhani wanaweza kunishawishi. Namshukuru MUNGU nimwabuduye maana tangu niokoke November 2008 ufahamu wangu ulibadilishwa. Nikiwa nimeokoka nikiumuona mdada  akiwa amevaa kikahaba, kwangu mimi humuona tu kama mtu mmoja wapo wa wenye mapepo hivyo anahitaji kusaidiwa kiroho.

Mwanaume mwenye adabu akimuona binti asiye na adabu katika uvaaji wake humchukulia kama kahaba tu  anayetafuta wanaume hivyo hujiepusha naye.
Kuvaa mavazi ya aibu ni dhambi.
Kuvaa kikahaba mbele za watu ni kosa kabisa mbele za MUNGU.
MUNGU anasema;
 '' Twaa mawe ya kusagia, usage unga; Vua utaji wako, ondoa mavazi yako, Funua mguu wako, pita katika mito ya maji.  Uchi wako utafunuliwa, Naam, aibu yako itaonekana. Nitalipa kisasi; simkubali mtu ye yote.-Isaya 47:2-3''

Leo mwanamke Una uhuru wa kuamua.
Una uhuru wa kuvaa kikahaba au kufaa mavazi ya kujisitiri lakini MUNGU anaona na waovu siku ya mwisho watalipwa sawasawa na matendo yao.

Kuna wengine huvaa mavazi marefu lakini mepesi kiasi kwamba huonekana kwa ndani mwili wake, huko ni kutembea uchi na huko sio kujisitiri.
Kuna wanawake wengi huvaa nguo ndefu kidogo lakini ni nyepesi na wakati huo huo ndani hawajavaa nguo za ndani, huo ni ukahaba unaochipukia.
Kuna wanawake kwa sababu ya kuupenda ulimwengu, akishauliwa juu ya kujisitiri mwili wake huona kama anaonewa kumbe ukweli ni kwamba anasaidiwa.
Hata makanisani leo kumejaa aibu katika mavazi ya baadhi ya wanawake.
Nilienda kusali kanisa fulani siku moja.
Binti mmoja mwenye sauti nzuri sana alikuwa akiimbisha wimbo wa kuabudu kabla ya Neno la MUNGU. Katika uimbaji huo nilitamani kuondoka ibadani, unajua ni kwanini?
Binti alikuwa anaimba vizuri sana na kwa viwango vya kimataifa kabisa kwa habari ya sauti.
 Alikuwa anaimba kwa vitendo ndipo hapo nilipojikuta natamani kuondoka.
Katika wimbo huo kulikuwa na kipengele cha kusema hivi; ''Tunainama mbele zako MUNGU wetu'', wakati akiimba hivyo alikuwa anainama ili kuwafanya na kanisa zima wainame. Sasa wakati anainama matiti yake yote yalikuwa yanaonekana kama mtu tu ambaye yuko uchi kabisa. kwa sababu alikuwa amevaa nguo ya juu ambayo iliziba chuchu tu lakini sehemu nyingine ya titi  ilikuwa wazi, pia inaonekana alikuwa amevaa sidiria isiyofaa hata kidogo maana alipokuwa akiinama huku anaimba matiti yake kama yalivyo yalikuwa yanaonekana. Nilijuta hata kwanini nilimwangalia yule mwimbaji maana alinitoa katika uwepo wa nguvu za MUNGU kabisa maana nilijikuta namshangaa tu anavyodhalilisha wanawake.
Pia katika kipengele hicho cha kusema '' Tunainama mbele zako MUNGU wetu'' Yule binti alipokuwa tu anainama mgongo wote ulikuwa unabaki wazi kabisaaaa. Ni aibu ya mwaka, ni kukosa adabu hata mbele za MUNGU. Ni hatari sana kwa kanisa kama hatutakemea ushetani huo kuingia kanisani.

BWANA YESU analishauri kanisa leo akisema;  
'' mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli.-Waefeso 4:22-24'' 

kuvaa Kikahaba mbele za watu ni uti wa ya kale na ni  kuzifuata tamaa zidanganyazo.
Biblia pia hapo juu inasema Wanawake na wajipambe kwa nguo za kujisitiri pamoja na adabu njema.
 Mwanamke wa adabu huheshimiwa.

Mithali 11:16a ''Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; ''

Kama huna adabu huwezi kuheshimiwa na watu wenye adabu.
Mwanamke anatakiwa ajipambe kwa nguo za kujisitiri mbele za watu.
Maumbile ya mwanamke yanamhitaji sana avae nguo za kujisitiri na adabu mbele za watu.
Kuna ambao hata waliwahi kutendewa mabaya na baadhi ya wanaume, kwa sababu wanaume wale waliwaona hawa kuwa ni wanawake makahaba wasio jali utu wao na thamani ya kuumbwa kwao.

Ndugu, kama unapenda kuvaa uchi uchi hakikisha unavaa hivyo chumbani kwako tu na sio mbele za watu.
Mbele za watu hakikisha unavaa nguo za kujisitiri.
Haitakiwi kumuheshimu baba mkwe wako tu huku wengine ukiwa huwaheshimu. Kuna wanawake huvaa kwa kujisitiri na adabu mbele za wakwe zao tu. Ndugu, nakuomba waone watu wote kuwa sawa na wakwe zako hivyo vaa kiadabu mbele za watu wote.
Hapa Dar mitaani nikiwa natembea si mara moja wala mara mbili bali mara nyingi nimewahi kukuta wanawake hasa mabinti wakiwa wamevaa nguo za kikahaba wakiwa wamekaa, na kwa bahati mbaya huchoka kubana miguu na kujikuta wakitanua miguu na kuonekana  ndani kabisa ya miili yao, ni aibu na fedheha kubwa.
Ni ujinga mfululizo huo.

Nguo zisizo za kujisitiri zitakufanya uitwe kahaba japokuwa wewe sio kahaba.
Wnawake wanapaswa wajipambe  kwa utakatifu na moyo wa adabu.
Haina maana kwamba wanaume hawakosei katika uvaaji, hao kuna siku yao nitawachambua vizuri tu ila leo wanawake naomba mmtii MUNGU hata katika mavazi yenu mbele za watu.
Kumbuka ukisasa unawapeleka wengi pabaya.
Ukisasa unawapeleka wengi kuzimu hata kama kanisani walikuwa wahudhuriaji, ni hatri sana.
Kuvaa nguo za kuacha matiti nje hilo ni tangazo la shetani ili afanye kazi yake ya kuuteka ulimwengu ili uingie dhambini na kukosa mbingu.
Mwanamke, Tumbo lako kweli ni zuri sana lakini kuvaa nguo za kuliacha tumbo lako wazi mbele za watu huko ni kuvaa kikahaba na ni kujidhalilisha wewe mwenyewe.
 Kuvaa wigi ni taarifa tu kwamba unahitaji kusaidiwa kiroho.
Kujichubua ili uwe ni mweupe wewe ni mwabudu shetani maana humweshimu MUNGU aliyekuumba vizuri.
Wanawake wa zamani hawakuwa wanavaa mawigi lakini hatuoni popote kwenye Biblia wakidharauliwa au kusemwa kwamba hawajapendeza.

Mwanamke, muonekano wako wa nje ni moja ya taarifa sahihi ya muonekano wako wa ndani.
Kigauni cha kuvaa mtoto wa miaka 12, lakini wewe mama mwenye umri zaidi ya miaka 30 unavaa ni aibu yako, maana kwa wewe kuvaa kivazi hicho magoti na mapaja yako yanakuwa nje, hiyo ni taarifa tu ya kwamba unahitaji msaada wa kiroho haraka sana.
1 Yohana 2:15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. ''

Asante kama unanielewa ndugu yangu.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments