JE HUWA UNAOMBA KATIKA ROHO MTAKATIFU?

Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze jambo muhimu.

Yohana 14:26 '' Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. ''

BWANA YESU alipokuwa katika huduma yake kabla ya kupaa kwenda mbinguni aliwatangazia wanafunzi wake jambo muhimu sana, yaani ujio wa ROHO MTAKATIFU.
ROHO MTAKATIFU ni ROHO wa MUNGU.
ROHO MTAKATIFU ni MUNGU ndani yetu.
ROHO MTAKATIFU atakaa na sisi milele kama tutadumu katika wokovu na utakatifu.
ROHO MTAKATIFU ni muhuri wa MUNGU ndani yetu.
ROHO MTAKATIFU ndiye msimamaizi wa kanisa la KRISTO duniani.
ROHO MTAKATIFU ndiye mwandishi wa Biblia, akiwatumia wanadamu aliowapenda na kuwaelekeza ni nini cha kuandika, ndio maana unaweza ukaona Musa akiandika habari za uumbaji wakati yeye Musa hakuwepo wakati huo, ila ROHO MTAKATIFU alikuwepo na ndiye aliyemwambia Musa kuandika mambo ya Mwanzo kabisa ya uumbaji wa mbingu na Dunia.
Unaweza ukashangaa unapoona Danieli akiona mambo ya Mwisho wa dunia. Unaweza ukashangaa kuona Mtume Yohana akiona mambo ya Mwisho wa dunia, ni kwa sababu tu ya ROHO MTAKATIFU ambaye yeye ni ROHO wa MUNGU, Anajua yote, ana uwezo wote na anawapenda wanadamu wote wanaomtii KRISTO na Neno lake.
ROHO MTAKATIFU ana  kazi nyingi sana ndani ya mwamini.
Mojawapo ya kazi hizo Biblia imesema hapo juu ni kutukumbusha na kutufundisha.
Ukihudhuria darasa la Mwalimu huyu na ukatii mafundisho yake hakika utashinda duniani.
Kazi ninayoizungumzia leo ni ROHO MTAKATIFU na maombi.
Kazi yake ni kutufundisha hivyo na katika maombi yeye ni Mwalimu mkuu hivyo tukimtii yeye tutakuwa tunapiga kwenye shabaha halisi kupitia maombi yetu.

Warumi 8:26 '' Kadhalika ROHO naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.''

Kazi mojawapo ya ROHO ni kutusaidia ili tuombe inavyotakiwa.
ROHO pia anaweza kutuombea sisi kupitia vinywa vyetu na sio vinginevyo.
inaposemwa kwamba ROHO MTAKATIFU hutuombea ni kwa kupitia maombi yetu. Yaani tutajikuta tunaomba kwa maelekezo yake, hapo anakuwa anatuombea.

Kuomba Katika ROHO MTAKATIFU Ina Maana Mbili(2)


 Maana Ya Kwanza ya kuomba katika ROHO MTAKATIFU Ni Kunena Kwa Lugha.

Matendo 2:4 ''Wote wakajazwa ROHO MTAKATIFU, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama ROHO alivyowajalia kutamka.''

Hapa tunaona wanafunzi wa YESU  wengi wakinena kwa lugha mpya, maana yake wakinena kwa lugha wasizojua maana ya maneno wanayoyatamka. Hapo walikuwa wakiomba katika ROHO MTAKATIFU.
Kuna maombi huzuiliwa na shetani lakini sio maombi ya kunena kwa Lugha.
Maombi ya kunena kwa Lugha ni maombi muhimu sana katika kanisa la MUNGU.
Kunena kwa lugha kuna kunena kwa lugha mbili.
Kuna kunena kwa lugha za wanadamu lakini lazima iwe lugha usiyoijua wewe mnenaji.
pia kuna Kunena kwa lugha za Malaika au kwa lugha ya mbinguni.
Lugha ya mbinguni nayo imegawanyika katika makundi mawili. Kuna Lugha ya Malaika na kuna Lugha ambayo hata Malaika hawaelewi maana yake.
Kunena kwa lugha ya mbinguni wakati mwingine unaweza kunena kwa lugha ambayo anayeijua maana yake ni MUNGU BABA, MUNGU MWANA na MUNGU ROHO MTAKATIFU tu, hata Malaika wasijue, ndio maana nasema kunena kwa lugha ni jambo muhimu sana kwa kanisa la MUNGU.

Siku moja katika ibada ya Mkesha nikiwa Zanzibar kuna dada mmoja alinena kwa lugha ya Kiingeleza huku yeye mwenyewe akiwa hajui hata Neno moja la Kiingeleza iwe kulitamka au hata kulijua maana yake, lakini katika ROHO MTAKATIFU yule ndugu aliomba kwa lugha ya kiingeleza hadi nikashindwa kuomba mimi na kuanza kumsikiliza tu maana maneno mengi katika aliyokuwa anaongea nilikuwa nayajua. Siku hiyo nilimnyooshea mikono ROHO MTAKATIFU, maana wasijua  kiingeleza siku hiyo waliongea kiingeleza kuliko hata baadhi ya waingeleza wenyewe.
Ndugu yangu ni muhimu sana kumhitaji ROHO MTAKATIFU na nguvu zake na lugha yake.
Dada yule baada ya mkesha nilimwita na kumuuliza akaniambia hajui lolote na wala hakumbuki hata kama ameongea kiingeleza. Huyo alinena kwa lugha ambayo yeye haifahamu. Inawezekana kabisa Muha au Msukuma au mkurya au mhaya akanena kisambaa au kichaga au kizaramo au kimakonde kama ROHO atampa kunena kwa lugha hiyo, ila awe tu hajui lugha husika anayonena, hapo ni kwa habari ya kunena lugha za wanadamu.

 Ukiona unanena kwa lugha unayoijua wewe unayenena jua kwamba hapo huneni kwa lugha.

 Marko 16:17 ''Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;''

Kunena kwa lugha ni jambo zuri sana na ni agizo la BWANA YESU.
Wateule wa MUNGU wanatakiwa waambatane na kunena kwa lugha. Ndugu kama hujawahi kunena kwa lugha nakuomba tamani kunena kwa lugha huku ukiwa na juhudi katika utakatifu na maombi. Wengi hutamani kunena kwa lugha lakini wanasahau kwamba kunena kwa lugha huja  wakati wa maombi tu katika ROHO. Wao wanapenda kunena kwa lugha ila hawapendi kuomba, hiyo haiwezi kuwezekana hata siku moja.


Maana Ya Pili ya kuomba katika ROHO MTAKATIFU ni Kuomba Kwa Kufuata Maelekezo Ya ROHO MTAKATIFU. 

Waefeso 6:18 '' kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;''

 Siku moja nilipanga kufunga, katika maombi hayo niliandika vitu vya kuombea. Wakati maombi yalipoanza nilijikuta namaliza siku tatu bila kuombea yale niliyokuwa nimeandika kwenye notebook yangu, maana kila nikianza kuomba tu nasikia maelekezo ya kuombea, mara muombee fulani, omba juu ya kitu fulani, tubu juu ya ndugu zako, ombea huduma ya fulani. Niliomba katika maongozo ya ROHO hadi siku tatu zikaisha. Baada ya pale nilikuja kugundua kwamba yale ambayo niliyaandika kwenye daftari yangu yalijibiwa yote na yale niliyoelekezwa na yenyewe yalijibiwa. Huko ni kuomba katika ROHO MTAKATIFU yaani kutii sauti ya ROHO MTAKATIFU katika maombi.
ROHO MTAKATIFU Ndiye Anayejua Hasa Ni Nini Muhimu Kwako Kuombea Wakati Huu.
Ukisikia msukumo wa kuombea jambo fulani jua tu kwamba hilo ndilo muhimu kwako kwa wakati huo na ROHO anakutaka uombee hilo, huko ndiko kuomba katika ROHO MTAKATIFU.

Kuna siku nilikuwa katika wakati mgumu sana, kuna dada mmoja kanisani alijikuta ananiombea mimi tu hadi baadae akanipigia simu na kuniuliza ''uko wapi? na katika hali gani?''
Nikamjibu na akaniambia jinsi alivyoomba sana kuhusu mimi, huko ni kuomba katika ROHO maana umemtii ROHO MTAKATIFU katika maombi.

Kuna siku tulipokua tunakaribia kufunga ibada ya mkesha kanisani mimi niliona ajali ghafla, ikabidi niwaambie kanisa kwamba tuvunje roho za ajali, watu walinishangaa sana maana tulikuwa tunafunga ibada. tulipoomba tukaondoka na kesho yake kaka yangu akanipigia simu kwamba amepata ajali ya gari lakini ni mzima hana hata alama ya ajali. alisema kwamba gari ile iliviringika mara 3 na gari iliharibika sana lakini yeye aliyekuwa ndani ya gari hana hata alama, yaani gari iliumia lakini aliyekuwa ndani ya gari ni mzima, hiyo ni ajabu lakini ukweli ni kwamba tukimtii ROHO MTAKATIFU maana yeye anajua yote tutakuwa tunatenda vyema sana. Ukiomba kwa kufuata maelekezo ya ROHO MTAKATIFU huko ndiko kuomba katika ROHO.

 Yuda 1:20-23 '' Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU, jilindeni katika upendo wa MUNGU, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu  YESU KRISTO, hata mpate uzima wa milele. Wahurumieni wengine walio na shaka, na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.''

 Ni muhimu sana kuomba katika ROHO MTAKATIFU na sio vinginevyo.
Labda acha nitoe tahadhari hizi;
Katika maombi kuna watu hulia sana bila kuomba, hiyo haiwasaidii hata kama watatumia masaa 2 wakilia tu bila kuomba.
Ni heri kuomba huku unalia kuliko kulia bila kuomba.


tahadhali ningine ni hii;
MUNGU hutoa nafasi lakini watu wengi hawakai katika nafasi zao za kihuduma na maombi walizopewa na MUNGU.
Ni muhimu sana kukaa katika nafasi ulipewa na MUNGU na kuitimiza. Maombi yako ya leo yanaweza kuwa msaada mkubwa katika jaribu lako la kesho.



Wakati mwingine kwa mfano unaweza ukafanya hivi;
 "JEHOVAH MUNGU Wangu Najua Bado Hujashindwa, Umenisaidia Katika Mengi Sana Tangu Utotoni Mwangu Hata Leo, Hata Kwa Hili Najua BWANA Utanishindia, Amen.". 

Wakati Mwingine Unatakiwa Kumweleza MUNGU Maneno Kama Hayo Hapo Juu Na Sio Kulia Tu. 
Mtukuze MUNGU Wakati Wa Magumu Yako Sio Kulia Tu. 
Kulia Hailipunguzi Tatizo. 
Kumtukuza MUNGU Huleta Kibali Cha Kulishinda Tatizo.
 Kuomba Ni Kupokea Ushindi na kuomba katika ROHO MTAKATIFU ni kushinda kabisa.
 Ukiwa Kwenye Magumu Sikukatazi Kulia Ila Ni Heri Ukalia Huku Unaomba Na Sio Kulia Tu Kisha Unalala Usingizi.
Omba maombi na omba sana maombi katika ROHO MTAKATIFU.

Asante kama unanielewa ndugu yangu.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments