Je! UMEOKOKA? - II

Na Frank P. Seth

Je! Umeokoka? Ni swali ambalo watu wengi wamekutana nalo na wengi wamejikwaa kujibu kwa sababu wanadhani siku walipoongozwa ‘sala ya toba’ ilikuwa ni mwisho wa mambo, kumbe! Ndio walipewa tiketi ya KUSHINDANA kwa HALALI ili wapewe TAJI siku ya mwisho (Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali, 2TIM. 2:5).
Angalia neno hili, “9Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. 10Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu” (Warumi 10:9, 10).
Neno “utaokoka”, linamaanisha wakati UJAO. Sasa angalia, 'wakati ujao' unahesabiwa kuanzia pale ulipoMKIRI Yesu na KUMWAMINI, japo haishii hapo; UKIENDELEA kumkiri na kusimama katika imani HADI mwisho (wa uhai au dunia), ndipo UTAOKOKA. Kwa maana hii, aliyeamini na kukiri JANA, LEO akarudi nyuma, je! Bado Ameokoka kwa sababu alikiri jana?
Kwanini UKIKIRI na KUAMINI ndipo UTAOKOKA?
Wokovu ni UWEZO na KIPAWA. Angalia hapa, “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake” (Yohana 1:12). Ukiamini UTAOKOKA na kinachokuwezesha kudumu katika wokovu ni ule UWEZESHAJI (kipawa) uliopewa.
“25Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno, wakisema, Ni nani basi awezaye kuokoka? 26Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana” (Mathayo 19:25, 26). Mistari hii inanionesha kwamba kuna UWEZO apewao mtu ili aweze KUOKOKA kila siku, na weze kuvumilia mpaka mwisho. Huo uwezo ndio UNAOMFANYA mtu aitwe mwana wa Mungu.
Kwanini unahitaji UWEZO ili uendelee KUOKOKA?
Jibu jepesi ni kwamba huwezo kuokoka kwa NGUVU zako mwenyewe (MT. 19:25, 26). Sasa angalia jambo hili, kwa sababu siku ULIPOMPOKEA Bwana ilikuwa ndio mwanzo wa MASHINDANO, imekupasa kushindana na mbele yako kuna TAJI; kwa hiyo unahitaji UWEZO wa KUSHINDA.
Angalia baadhi ya mambo ambayo imekupasa KUSHINDA kwa huo UWEZO uliopewa. “9 Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. 10Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. 11Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. 12Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. 13Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. 14Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja” (MT. 24:9-13).
Utagundua kwamba dhiki, uadui wa watu (watu kuwachukiao, hivyo kukufanyia mambo mabaya, saa nyingine bila sababu ya msingi), usaliti na mateso mbalimbali, hayo ndio MAMBO yatakayoKUPIMA kwamba wewe UMOKOKA au LA! Yaani ‘atakayevumilia’ mpaka mwisho (sentensi iko kwenye wakati ujao, yaani baada ya mapito hayo), kwa ajili ya JINA LA BWANA (MT. 24:9), huyo ndiye ATAKAYEokoka.
Sasa angalia, hawa watakaosalitiwa na kupita kwenye mateso, sababu ya MSINGI ya kupita humo ni kwa ajili ya Jina la Bwana! Yaani kwa sababu ya imani yao; wanapita kwenye moto wakati wengine wako vizuri. Kama tu ilivyokuwa kwa Shedrak, Meshak na Abednego, kwa sababu ya IMANI yao kwa Mungu wanapata shida ambayo wenzao hawapati! Je! Uko tayari kuvumilia hadi mwisho?
Kumbuka, mateso mengi na magumu zaidi kupona, ni yale ambayo watu hupata hutoka kwa watu wa KARIBU, kuliko hata yale yasababishwayo na watu wa mbali. Laiti ungalijua kwamba uongo wa kwanza kati mume na mke ni ule uliofanyika Eden, Hawa alipokubali uongo wa Shetani na kuupeleka kwa mumewe (fikiri mkeo/mumeo anakukosesha na unaadhibiwa kwa ajili yake); mauaji ya kwanza yalitokea kati ya ndugu na ndugu (Habili na Kaini); Biashara ya kwanza ya binadamu ilifanyika katika familia ya Yakobo pale Yusufu alipozwa na ndugu zake; Kabla sijasoma habari za ubakaji magazetini, nilianza kusoma kwenye familia ya Daudi, mtoto mmoja alipombaka mwingine (Amnoni na Tamari); hadithi ya mtoto kulala na mke wa baba yake kwa nguvu, mtoto wa Daudi (Absalom), nk.
Huu ni USALITI mkubwa ambao kwakweli UPENDO wako kwa hao watu unaweza KUPOA kabisa. Kumbuka, upendo wako ukipoa kwa watu wa NYUMBANI mwako, unaanza kuwa mbaya kuliko asiyeamini; kwa sababbu huwezi tena kuwahudumia na kuwatunza ipasavyo. Umeona changamoto hiyo? Lakini, atakayevumilia mpaka mwisho ndiye ATAKAYEOKOKA.
“Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini” (1 Timotheo 5:8).
Kwa somo hili, kuhesabiwa KUOKOKA ni sasa (saa ya wakovu ni sasa, 2Kor. 6:2); ila UTAUPIGANIA huo wokovu wako hadi siku ya mwisho. Atakayevumilia mpaka mwisho ndiye ATAKAYEOKOKA.
Frank P. Seth

Comments