Je! unaamini ya kuwa Mungu anataka ufanikiwe katika maisha yako?

Na Mwl. Christopher Mwakasege.
Bwana Yesu asifiwe sana!
Je! unaamini ya kuwa Mungu anataka ufanikiwe katika maisha yako? Je! unajua ya kuwa Mungu ana hamu sana ya kushiriki katika kukufanikisha?
Ikiwa umeusoma na kuutafakari mstari huu wa Yeremia 29:11 utakuwa na majibu moyoni mwako juu ya maswali hayo mawili.Mstari huo unasema hivi: “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.
Ni dhahiri ya kuwa katika mawazo hayo ya Mungu, tunapata mipango na mikakati anayotaka tujue na tuitekeleze – kwa kushirikiana naye – ili tuweze kufanikiwa, kama anavyotuwazia!
Leo nataka nikushirikishe wazo la 4; ambalo ni kati ya mawazo anayokuwazia, ili uweze kulitumia kufanikiwa.
Wazo hilo ni hili: “Uwe mwangalifu juu ya vyanzo vya fedha na matumizi yake katika kugharimia mafanikio yako!”
Kumbuka jambo hili: Hakuna mafanikio yasiyo na gharama! Na katika mazingira ya uchumi tulionao ulimwenguni kwa sasa, fedha ni sehemu muhimu ya kusaidia mafanikio ya watu – lakini ikiwa itapatikana na kutumika kwa uangalifu!
Kumbuka tena ya kwamba: Fedha ni fedha tu! Uwe mkristo au usiwe mkristo – fedha ni fedha tu! Uwe umeokoka au hujaokoka – fedha inabaki kuwa fedha tu! Uwe mzee, au uwe kijana, au uwe mtoto – fedha inabaki kuwa fedha tu!
Thamani ya fedha inaweza kuyumba, lakini misimamo yake na sababu za kuwepo kwake katika mazingira ya uchumi wa sasa – haviyumbi!
Biblia tukiisoma inatupa sababu kadha wa kadha zinazomfanya Mungu aweke katika moyo wa mtu anayetaka kumfanikisha, wazo la kumtaka awe mwangalifu juu ya vyanzo vya fedha na matumizi yake katika kugharimia mafanikio yake!
Hebu tutafakari kwa pamoja, sababu mojawapo inayohusu “uaminifu wako juu ya fedha!”
Kutokuwa mwaminifu juu ya fedha ni kikwazo kikubwa cha mafanikio ya mtu, au familia, au kanisa, au kampuni, au nchi! Mipango mingi inakwama kufanikiwa kwa sababu ya wahusika kukosa uaminifu juu ya fedha zinazohusu mipango hiyo.
Kufuatana na Kutoka 18:21, usipokuwa mwaminifu juu ya fedha, unaweza kuikosa au kuipoteza nafasi ya uongozi! Hii ni kwa sababu biblia inaweka wazi ya kuwa uaminifu juu ya fedha, unatakiwa uwe kigezo muhimu cha mtu kupewa au kutopewa nafasi ya uongozi!
Na kufuatana na Luka 16:10, usipokuwa mwaminifu katika “fedha” chache, itakuwa vigumu kwako kuwa mwaminifu kwenye “fedha” nyingi! Tena, kufuatana na Luka 16:12, usipokuwa mwaminifu kwenye “fedha” ya mwingine, utakuwa umejikwamisha kupata “fedha” yako mwenyewe!
Ukisoma Mathayo 25:21,23, utaona ya kuwa, ukiwa mwaminifu juu ya fedha kidogo, utapewa uangalizi wa matumizi ya fedha nyingi!
Uaminifu juu ya fedha ni zaidi ya kuwa mtunzaji mzuri wa fedha! Pamoja na kuwa mtunzaji mzuri wa fedha – ikiwa na maana ya kuwa huzipotezi hizo fedha , bado biblia inaweza kukunyima sifa ya kuwa mwaminifu juu ya fedha hiyo!
Ukisoma mfano wa mtu aliyepewa talanta moja ya fedha (Mathayo 25:24 – 30), alionekana hakuwa mwaminifu juu ya fedha hiyo, kwa kutoitumia ipasavyo kama ilivyokusudiwa na mwenye fedha ingawa aliitunza bila kuipoteza!
Tunaona mfano mwingine katika Luka 19:20 – 24, mtu aliyepewa fungu moja la fedha, kuonekana hakuwa mwaminifu juu ya fedha hiyo, kwa sababu hakuitumia fedha kama ilivyokusudiwa na mwenye fedha…ingawa aliitunza na hakuipoteza!
Kwa hiyo, kibiblia haitoshi kuwa mtunzaji mzuri wa kutoipoteza fedha, ili uitwe mwaminifu! Bali unahitaji uitunze fedha ili itumike kama ilivyokusudiwa!
Mafanikio ya maisha yako yanategemea pia utunzaji wako wa fedha zilizopo mkononi mwako, au zinazopita mkononi mwako, ili uzitumie kama ilivyokusudiwa! La sivyo unaweza ukawa na fedha na usiwe na mafanikio!
Naamini utajipanga vizuri juu ya jambo hili!

Comments