JIFUNZE JINSI MAOMBI YALIVYOWEZA KUWAANGAMIZA WAAMALEKI

Na Mtumishi Generali Geoffrey Mwanza Wambua,
The Global Evangelism Ministries (Kenya)


Bwana Yesu asifiwe?
Baada ya jamii ya Israeli kusafiri kwa muda mrefu jangwani la Sini walifika mahali palipoitwa Refidimu ambayo inamaanisha eneo la mapumziko.
Watu hawa walikuwa wachovu na wenye kiu lakini hawakuwa na maji ya kunywa kwani ni jangwani.
Walianza kumlalamikia Musa; naye huku akiogopa kupigwa mawe akamlilia MUNGU naye akamwamuru kupanda juu ya mlima Herobu na ile fimbo take kisha agonge mwamba.
Baada ya Musa kugonga mwamba maji yalitoka na watu wakanywa.
Mwamba huu unaashiria YESU Kristo katika agano jipya ndiye anatajwa kama jiwe la Israeli.
1Korintho 10:4 " Wakanywa pia kinywaji kile cha kiroho; maana walikunywa kutoka ule mwamba wa kiroho uliowafuata, mwamba huo ulikuwa ni Kristo mwenyewe".
Watu hawa walipomlalamikia Musa; naye alimwomba MUNGU wa mbinguni na MUNGU akampa suluhu.
Kumba matatizo yetu tukimwomba MUNGU atatupa suluhisho! Kumbe maombi yana nguvu kiasi hicho!
Baada ya watu kunywa maji wakajisikia shida imewaisha wakaona kuwa hakuna tena maana ya kuendelea kuomba; nao wakalala na kujipumzisha; wakasahau kuwa adui anaweza kuwavamia.
Wakati wamejisahau Waamaleki wakawashambulia kwa nyuma.
Linganisha kitabu cha Kutoka 17:8 na
Kumbukumbu 25:17-18 " Kumbukeni kitendo cha waamaleki mlipokuwa safarini kutoka Misri walivyowashambulieni huko njiani mkiwa wanyonge na kuwapiga wale wote waliokuwa nyuma yenu wamechoka.Waamaleki hawakumwogopa MUNGU"
Hapa ndipo Musa alimteua Yoshua mwana wa Nuni kwenda vitani kupambana na waamaleki; wakati Musa aliwaita Haruni na Huri juu ya mlima kufanya maombi.
Kutoka 17:9 "Musa akamwambia Yoshua "chagua wanaume uende ukapigane na waamaleki.Kesho nitasimama juu ya kilima nikiishika ile fimbo ya MUNGU".
Waisraeli hawakuwa na uzoefu wa kupigana vita wala silaha za vita ila walikuwa na imani na MUNGU wao.
Wewe unayelia leo maana unapitia hali ngumu; sioni haja ya ulie; mwite Yehova kwa imani ndani ya YESU.
Musa hakuangalia uzoefu wa vita walokuwa nao Waamaleki; alijua kuwa ijapokuwa waamaleki walipigana kimwili; alitambua kuviendea vita kiroho.
Waefeso 6:12 "Maana vita vyetu si vya nyama na damu bali ni dhidi ya jeshi ovu la giza tunapigana na watawala; wakuu na wenye nguvu wanaomiliki ulimwengu huu wa giza"


Baada ya Musa kulielewa jambo la vita, akawaita Haruni na Huri na kupanda nao mlimani (kuomba).
Mpendwa tatizo/changamoto linapokujia unachukua hatua gani? Unaanza kulalamika? Unaanza kumlaumu MUNGU?
Wakiwa juu mlimani; Musa alifanya ishara ya kuinua mikono juu huku Yoshua kule chini bondeni anapigana vita dhidi ya waamaleki.
Kutoka 17:11 "Ikawa wakati wote Musa alipoinua mikono yake juu, waisraeli walishinda na alipoiteremsha waamaleki walishinda".
Kwanini Musa anaomba akiinua mikono yake juu; si angeomba tu mikono ikiwa chini?
Zaburi 141:2 "Sala yangu uipokee kama ubani; niinuapo mikono yangu kwako, unikubali kama sala ya jioni"
Waamaleki walionekana kushindwa wakati mikono ya Musa nabii wa MUNGU ipo juu lakini iliposhushwa waisraeli walikuwa wakishindwa; sasa tegemeo la ushindi ni la nani lilikuwa mikononi mwa Musa.
Lakini ikafika mahali Musa mtumishi wa MUNGU akachoka kwa maana ilikuwa vigumu kwake kuiweka mikono juu wakati wote.
Kwa sababu ya hali ngumu pengine ya njaa; jua kali;uchovu wa kawaida Musa akachoka; ikabidi apewe msaada wa kuhakikisha mikono yake imewekwa juu wakati wote.
Je; wakati wewe unaomba unainua mikono yako kunyenyekea mbele za YEHOVA MUNGU? Au unajiona wa maana sana na kusema huwezi kujichosha kwa kuinua mikono yako juu?
Haruni na Huri wakatambua siri iliyokuwepo kuwa ushindi ulipatikana tu mikono ya Musa ilipokuwa juu ndipo wakachukua jiwe na kumkaliza huku wakiishikilia mikono ya Musa juu.
Mstari wa 12 "Haruni na Huri wakachukua jiwe wakaliweka karibu na Musa naye akaliketia huku mmoja akiuinua mkono wa kulia na mwingine wa kushoto.Yoshua akawakatakata waamaleki"
Ndugu hawa waliamini kweli kuwa maombi ya Musa yalikuwa na nguvu sana na alibidi kusaidiwa ili ushindi kwa Israeli kwa jumla upatikane.
Ni mara ngapi unapata nyumba yenu ina matatizo na badala uwasaidie wenzako unajitenga mbali nao?
Ni ngapi unaona tatizo kwa ndoa yenu na badala ya kumsaidia mkeo/mmeo unakaa kando aumie pekee?
Mambo yenu yatafanikiwa tu mkiunganisha mikono pamoja na mshirikiane.
Maombi ya kusaidiana itawafaa zaidi na mtaenda mbali kwani mtashinda hiyo hali inayoonekana ngumu katika maisha yenu.
Wewe ni Musa; MUNGU atakutumia mtu akushike MIKONO na kuku-support; wewe ni Haruni na Huri MUNGU anataka uiinue mikono ya mtu ili mpate kushinda.
Wewe ni Yoshua; kuna mtu mahali anaomba kwaajili yako; tia bidii kupigana utashinda.


Hebu fikiria kuwa kama kamanda wa jeshi la Waamaleki angetambua siri iliyokuwa juu ya kushindwa kwao ilikuwa ni maombi ya Musa aliyekuwa mlimani akiomba; basi ina maana angeachana na Yoshua na kumwendea Musa ili kukatiza network ya ushindi wa Israeli.
Ina maana basi unapopigana katika ulimwengu wa kiroho; usijaribu kufichua siri ya ushindi wako maana adui atataka kutumia siri hiyo ili akushinde.
Ni vizuri kuficha siri ya asili ya nguvu za MUNGU wa mbinguni kwani hata baadhi ya marafiki zako ni maajenti tu wa shetani wametumwa kwako ili kukupeleleza wakuue.
Waamuzi 16:4-5 "Baada ya hayo Samsoni alimpenda mwanamke mmoja aitwaye Delila ambaye aliishi katika bonde la Soreki.Wakuu wa Wafilisti wakamjia Delila wakamwambia "Mbembeleze Samsoni ili ujue asili ya nguvu zake ili tuweze kumkamata na kumfunga.Ukifanya hivyo kila mmoja wetu atakupa vipande thelathini vya fedha"
Umeona kuwa si kila ajiitaye rafiki kwako ambaye ni rafiki? Ninajua kuwa habari hii imewagusa wengi sana mioyoni kwani walisalitiwa kwa njia tofauti wa waliojipendekeza marafiki wa kweli kwao! Pole sana!
Basi baada ya Yoshua kuwakatakata waamaleki MUNGU akamwambia Musa:
Kutoka 17:14-15 "Liandike jambo hilo katika kitabu liwe ukumbusho na kulikariri masikioni mwa Yoshua kuwa nitawafuta kabisa waamaleki duniani.Musa akamjengea MUNGU na kuiita "Yehova Nissi" (MUNGU ni Bendera yangu....."
Baada ya MUNGU kuwashindia Waisraeli vita; wakamjengea madhabahu;Walivunja madhabahu ya miungu ya Waamaleki na kujenga madhabahu ya Yehova MUNGU.
MUNGU anakutaka uvunje madhabahu ile ilijengwa kwenu ya ulevi; uasherati; fitina; chuki; familia kutosikilizana nk na umjengee madhabahu yake (ulete wokovu kwenu).
Isaya 11:12 "Naye ataweka bendera kuwaashiria mataifa kuwakusanya waisraeli waliodharauliwa; kuwaleta pamoja watu wa Yuda waliotawanywa na kuwarudisha toka pembe nne za dunia"
Baada ya kumjengea Mungu madhabahu; yeye atakuregeshea kila chako kilichoibwa; kilichotawanywa; maisha yako mazuri yaliyofungwa; nyota yako iliyokaliwa; kazi; mafanikio kwani ndivyo ilivyokuwa kwa Waisraeli hawa waliomjengea MUNGU madhabahu.


Tumejifundisha pia jinsi mtu wa rohoni anavyoweza kutambua jinsi ya kushughulikia vita vinapomjia na tukaona Musa alikuwa rohoni na kutambua kilichohitajika baada ya Waamaleki kuwavaamia Waisraeli.
Kuna Watu leo ambao wakati wamevamiwa na adui(tatizo) badala ya kulikabili kirohoni wanaliendea kimwili.
Mfano:
Umeoleka na umetambua kuwa mumeo anakula uroda na mwanamke wa kando; badala uliendee tatizo hili rohoni ki maombi kwa kung'oa roho ya uzinzi kwa mumeo; wamtafuta mwanamke mwenzio kimwili umpige.
Hapa utanoa manake shetani ambaye ndiye mcochezi wa uzinzi huu atamficha mwanadada huyu wa kando kisha hautamuona; baadaye utamrukia mumeo na kuanza vita vya makonde na papo hapo mtaachana huku kusudi la shetani la kuvunja ndoa yako likifanikiwa!
Wakati vita vya kiroho vimezuka kwa Kanisa lenu si uchukue hatua ya kulikimbia Kanisa kisa na maana umekwazwa; komaa kiroho na uokoke kwa kujua shetani ameinuka; kwani nabii Musa alielewa tatizo lao na akajipanga ki-maombi; erevuka na uokoke !
Tatizo la watu wengi leo hawaelewi Biblia na kupenda kuifuata; wanasoma ila hawaifuatilii huku wakipotea kwani wamekosa ukweli ambao utawaweka huru.
Watu wengine hawataki kujiombea wakati wa tatizo wao wamezoea kuwaendea wanaowaita manabii na waombezi ili kuambiwa shida zao na kuombewa.
Musa na Yoshua,Haruni na Huri hawakuwaendea manabii na waombezi; wao walijiamini na kuvikabili vita wenyewe; wakiwa na imani ndani yao wakaomba kwa Jina la Bwana Yesu.
Uvivu wa maombi utakumaliza ndugu yangu; jifundishe kujiombea kwa imani yako huku ukitenda mema ndani ya Bwana Yesu Kristo.
Unapoomba naomba uyatilie haya moyoni:
-MUNGU hayasikilizi maombi ya mwenye dhambi hata kama anatoa sadaka na zaka na dhabihu.
-MUNGU hayajibu maombi ya mtu anayeomba halafu anaenda kutenda dhambi.
-MUNGU hana haja/hasikilizi maombi ya mtu wa njia mbili; yaani leo uko maombi na kesho umeenda kwa mganga/au unasengenya.
-Ili maombi yako yasikiwe ni lazima uombe kwa Jina la Yesu Kristo pekee na wala sio kwa mwingine yeyote yule (Matendo 4:12;Yohana 14:13-14)
-Imani yako mwenyewe ndio itakuponya katika maombi; ukingoja imani ya mchungaji au mwombezi wako; utatembea kiati kiishe soli.
-Jifundishe kuambatanisha maombi yako na sadaka kila mara.

Kwa mawasiliano ya maombi ya siri ya kutubu dhambi hii; nipigie:
Generali Geoffrey Mwanza Wambua,
The Global Evangelism Ministries (Kenya)
+254 724 656 653
geoffreymwanza@yahoo.com

Comments