KUMKUFURU ROHO MTAKATIFU NA MADHARA YAKE

Na Dk Frank P. Seth
“22 Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. 23Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? 24Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. 25Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. 26Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? 27Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu. 28Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. 29Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake. 30Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya. 31Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa.32Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao” (Mathayo 12:22-32).
Dhambi haijawahi kuwa tishio wala kitu kigumu kwa BWANA Yesu kusamehe isipokuwa moja tu, kumkufuru Roho Mtakatifu; kwa njia mbili: kwa kutenda dhambi au kunena (Mt. 12:31). Kutenda dhambi kunaweza kuwa kwa kuwaza, kunena na kutenda. Hawa Mafarisayo walitenda kwa “kuwaza”, yaani, “Yesu akiyajua mawazo yao…” (MT. 12:25). Mtu atafanya nini ili iwe ni KUMKUFURU Roho Mtakarifu?
Nimesikia watu wakisema kwamba “haiwezekani kwa Mkristo kumkufuru Roho Mtakatifu”, mimi nasema “sio rahisi lakini inawezekana kwa sababu ya kukosa maarifa”. Sijui ushahidi wa kimaandiko juu ya kauli hiyo ya “haiwezekani”, ila nawaambia leo, sio vigumu kama unavyodhani; Mwombe Mungu akusaidie usifanye hiyo dhambi kwa maana haitasamehewa kwenye ulimwengu wa sasa na ule ujao (MT. 12:32).
Angalia, Ibilisi asikudanganye kwamba tayari umeshamkufuru Roho Mtakatifu. Nimekutana na watu wenye HOFU kwamba tayari wameshamkufuru Roho na wamejiaminisha kwamba HAWATASAMEHEWA tena kwahiyo KUTUBU haisaidii tena. Uwe makini, Ibilisi naye anajua maandiko, akikubana hapo unaweza ukaangamia kwa kukosa maarifa.
Maswali muhimu: Kwanini kumkufuru Roho Mtakatifu ni jambo kubwa sana kwa Bwana Yesu? Je! Kufanya kitu gani ni kumkufuru Roho Mtakatifu? Nitajuaje kama nimeshamkufuru?
i. Umuhimu wa Roho Mtakatifu kwa Bwana Yesu
Kwa Bwana Yesu, umuhimu wa Roho Mtakatifu ni sawa na umuhimu wa BABA yake, na pasipo Huyo Roho, Yesu hajakamilika; Hao watatu ni UMOJA. Thamani ya Roho Mtakatifu ni KUBWA kuliko akili za mwanadamu zinavyoweza kueleza; kama ilivyo ukuu wa Mungu Baba. Siri ZOTE za Baba zimefichwa na hufunuliwa kadri ROHO apendavyo. Ndani yake ndimo kuliko na siri ya UUMBAJI, UZIMA na UFUFUO. Kama sio Roho Mtakatifu, hadi leo Bwana Yesu angekuwa kaburini. Hii SIRI na UWEZO wa kufufuka hana mwingine ila Roho Mtakatifu peke yake.
Kabla ya Uumbaji, Roho Mtakatifu alikuwepo ili yote yafanyike kama Baba alivyotaka kufanya (Mwanzo 1:1, 2). Na kwa Neno, yaani Yesu, VYOTE vilifanyika, pasipo YEYE hakuna chochote kilichofanyika (Yoh. 1:1-5). Linganisha mistari hii:
“1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. 3Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.4Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.5Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza (Yohana 1:1-5).
- [neno ‘Naye’ maana yake ni kiwakilishi cha NAFSI; Tofauti ya ‘neno’ na ‘Neno’ ni, hii yenye herufi kubwa ni Jina]
- [‘Huyo mwanzo’; huyo aliyeitwa ‘Mwanzo’ ambaye Alikuwa kwa Mungu, naye ni NAFSI pia]

NA
“1 Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. 2Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. 3 Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru” (Mwanzo 1:1-3).
- [Mungu alitamka Neno; Yesu aliumba.]
Ukiangalia mistari hii kwenye kitabu cha Mwanzo na Yohana, utagundua kwamba BABA, MWANA na ROHO walikuwepo pamoja, wakifanya yote kwa pamoja kwenye uumbaji.
Kazi alizozitenda Bwana Yesu akiwa duniani zilifanyika kwa Roho Mtakatifu sawa na mapenzi ya Baba (YN. 4:34). Kwa mfano, BWANA alitoa pepo kwa Roho Mtakatifu (MT. 12:28); Alihubiri kwa Roho Mtakatifu (Luka 4:18); Aliongozwa na Roho Mtakatifu (LK. 4:1); nk. Kwa mistari hii, Pasipo Roho Mtakatifu, BWANA asingefanya lolote.


“22 Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. 23Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? 24Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. 25Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. 26Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? 27Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu. 28Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. 29Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake. 30Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya. 31Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa.32Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao” (Mathayo 12:22-32).
Swali letu ni, Je! Ukifanya nini ndio umemkufuru Roho Mtakatifu? Ukiangalia tena hii mistari, “Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. 25Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia....” (MT. 12:24b, 25a); Katika mistari hii, utaona kwamba Mafarisayo walisema “mawazoni” mwao kwamba “huo muujiza Bwana aliofanya ametumia nguvu za giza”! BWANA akayajua MAWAZO yao.
Kwahiyo, ONYO la kumkufuru Roho Mtakatifu lilikuja kutokana na MTAZAMO wa hawa Mafarisayo, ambao walidhani kwamba Roho iliyokuwa ikitenda kazi ni roho za mapepo na wala sio Roho wa Mungu.
Muujiza maana yake: ni jambo lisilo tarajiwa; ni jambo lisilo la kwaida; ni jambo linalotokea kwa namna isiyo ya kawaida; ni jambo ambalo liko nje ya uwezo wa mwanadamu na mifumo yake; nk.
Muujiza wa Kimungu unapotokea, mambo mawili yanaweza kutokea: Kwanza, wapo watakao mtukuza Mungu [wataona utukufu wa Mungu]; Pili, wapo wengine wataona jambo jingine kutokana na upeo wao wa kupambanua mambo ya rohoni. Kwenye MT. 12: 22-32, waliona utendaji wa pepo mchafu!
Kwa mfano, niliishi nyumba moja na bwana mmoja Mfaransa, kwa takriban miezi mitano. Katika mazungumzo yetu, ambapo wakati mwingine nilipomshuhudia habari za Mungu wetu, yeye alisema kwa ujasiri, “hakuna Mungu”. Siku moja akasema, “kwangu [yaani kwa huyo Mfaransa] ni rahisi kuamini kwamba Vampires wapo ila siamini kwamba Mungu yupo”.
Sasa angalia, huyu ndugu hajawahi kukutana na matendo makuu ya Mungu, hajasoma biblia wala haendi kanisani, haangalii kabisa mambo ya Mungu hata kwenye TV tu; hajui lolote juu ya Mungu isipokua jina tu analosikia kwa watu. Kwa lugha nyingine, hana IMANI kabisa [kumbuka, imani huja kwa kusikia neno la Kristo...(ROM.10:17)].
Katika maisha ya huyu ndugu, ameona katuni na senema nyingi za Vampires (majitu ya kufikirika na yakutisha). Akilini mwake anajua kwamba Vampires hawapo mahali popote duniani; hivyo ni vitu vya kufikirika tu kama ilivyo Tom and Jerry. Hakuna mahali duniani utakutana na Tom na Jerry; ndivyo ilivyo Vampires, hakuna mahali wanapatikana. Ila kwa huyu ndugu, kwa maana ndicho KILICHOPO NDANI yake, ni rahisi KUAMINI kwa maana hana kingine.
Mtego huu ndio uliwakuta Mafarisayo. Hawana mifano mingine wa miujiza isipokuwa ile ya Beelizebuli. Sasa angalia, kinachofanya hawa Mafarisayo au watu wa namna yao KUANGAMIA ni kukosa maarifa ya Kimungu. Upeo wao wa kuona mambo ya kiriho ulikuwa chini sana kuliko upeo wa BWANA, ndio maana hawakuweza kuwasiliana au kuelewana katika kiwango kimoja cha kiroho. Wakamwita Roho Mtakatifu Beelizebuli!
Mara nyingi, BWANA aliwaita Mafarisayo na wafuasi wao VIPOFU kwa maana walikuwa wanaangalia lakini hawaoni! “Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili (MT. 15:14); “Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia” (MT. 23:24). “13Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa” (MT. 13:13). Kwa maana hii, wakati Roho Mtakatifu yuko kazini, wao wanaona Beelizebuli na “kusema” maneno ya kufuru dhidi ya Roho wa Mungu.
Kwa somo hili, nakushauri, usikimbilie kuita kazi ya mtumishi yoyote ANAYEJIITA mtumishi wa Mungu kwamba ni kazi ya kipepo; yaani anatumia nguvu za giza. Kama huna ufunuo mahususi (karama ya kupambanua roho), ni aheri ukae kimya kwanza. Hata hivyo, wewe ni nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine?
“Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha” (RUM. 14:4). Angalia, “kwa bwana wake mwenyewe yeye atasimama au kuanguka..” Neno “bwana” limeanza kwa herufi ndogo, inamaana hata kama sio mtumishi wa Mungu (Bwana) bado huna uhalali wa kumhukumu! Ndani ya shamba la Ngano kuna MAGUGU, kila mtu anajua; Sio kazi yako kung’oa magugu (MT. 13:25).
Kumbuka, kuna namna nyingi sana Roho Mtakatifu anafanya kazi na watu duniani hata leo, kwa mtindo ambao hujajua wewe, kumbe! Huo mtindo upo kwenye maandiko ni wewe tu ndio hujui. Angalia, Roho Mtakatifu hatapingana na maandiko.
TAHADHARI, sio kila kinachofanana na Mungu ni cha Mungu. Ndio maana wachawi wa Misri walijaribu kufanya mambo kama Musa alivyofanya. Je! Haikuwa nguvu za giza? Ndio, kwa hao wachawi ilikuwa ni nguvu za giza, ila kwa Musa ilikuwa ni Roho Mtakatifu mwenyewe. Pamoja na kujua maandiko, bado kazi ya roho Mtakatifu ya kupambanua roho ni muhimu sana ili kujua utendani wa roho mbalimbali.
-------Itaendelea------
Frank P. Seth

Comments