KWA KUWA MMEKUWA WATEULE WA MUNGU, WATAKATIFU, WAPENDWAO.

Na Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze neno la MUNGU wa mbinguni.

Wakolosai 3: 12-17 ''Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama BWANA alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye.''

Waliompokea YESU kama BWANA na Mwokozi wao hao ni wateule wa MUNGU watakatifu wapendwao sana.
Ni watu wazuri sana hawa maana wanamtii MUNGU.
Lakini leo MUNGU ana Neno juu ya wateule wake kwa lengo la kuwafanya walitii Neno lake.
Katika maandiko hapo juu kuna mambo kumi na mbili ambayo yanamhitaji mtu wa MUNGU kujua na kutendea kazi ili ampendeze MUNGU aliyemuokoa.

Hebu jifunze ufafanuzi huu wa Neno la MUNGU.

1. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa REHEMA.
- Rehema ni Neema anazozipata Mwanadamu kutoka kwa MUNGU.
-Neema kubwa zaidi tunayoipata sisi wanadamu ni kusamehewa dhambi kama tukitubu katika KRISTO.
Moyo wa rehema ni moyo wa toba, ni vizuri kuwa na moyo wa toba.
Thamini rehema za MUNGU kwako.
Neema nyingine kutoka kwa MUNGU ni ulinzi wa MUNGU na n.k
Ni lazima tuwe na moyo wa rehema maana MUNGU wetu ana mpango na sisi kwa ajili ya uzima wa milele.
Mathayo 5:7 ''Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.''

2. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa UTU WEMA.
-Kama mtu wa MUNGU unapaswa kuwa mtu mwema.
Mtu mwema hutenda mema na sio mabaya.
Mtu mwema humtii MUNGU katika matendo yake yote.
Warumi 12:21 ''Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.''
3. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa UNYENYEKEVU.
-Unyenyekevu unatokana na kunyenyekea.
Ni muhimu sana wateule wa MUNGU wakawa wanyenyekevu kwa MUNGU.
Mtu myenyekevu hawezi kuwa na mazoelea ya ibada bali kila siku mbele za BWANA kwake ni siku mpya.
1 Petro 5:6 ''Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa MUNGU ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;''

4. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa UPOLE.
-Upole ni jambo la muhimu sana kwa mteule wa MUNGU.
Ninachotaka ujue ndugu ni kwamba; upole sio ukimya kama watu wengine wanavyodhani.
Upole ni hali ya utulivu na utaratibu.
Mtu mtulivu hatukani wala hafanyi maamuzi ya kukurupuka.
Upole hutufanya tuwe wataratibu katika tuyatendayo kiasi kwamba ni ngumu kunaswa na shetani.

Mathayo 5:5 '' Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. ''

5. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa UVUMILIVU.
Mvumilivu hula mbivu.
Katika maisha ya wokovu wakati mwingine uvumilivu ni jambo la muhimu sana.
Uvumilivu ni silaha kubwa ya kuyashinda majaribu.
Uvumilivu ni hali ya kustahimili machungu.
Unaweza ukatukanwa kwa sababu ya wokovu wako lakini wavumilivu husonga mbele na YESU daima.

Mathayo 24"13 '' Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. ''

6. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa KUCHUKULIANA.
-Kuchukuliana ni kubebeana mizigo.
Kuchukuliana ni kuvumiliana maana hatuna viwango sawa vya kiakili, kiroho na kiufahamu au kiuelewa.
Kuna Kanisa mchungaji hata darasa la saba hakufika lakini waumini kanisani kwake wapo hadi wenye PHD, Lakini kwa sababu watu hao wanamfahamu MUNGU wao wanaendelea vyema kiroho na Mchungaji Yule ndiye baba yao wa kiroho, kila kitu kiko safi.
-Unaweza kukuta katika Kwaya kuna waimbaji wengine hawajui kabisa kuimba vizuri lakini kwa sababu wanakwaya wote wanajua thamani ya kuchukuliana basi wanaendelea mbele bila kudhalilishana.
Wafilipi 2:3 ''Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. ''

7. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa KUSAMEHEANA.
-Kusameheana ni jambo la lazima kwa mteule wa MUNGU, maana asiposamehe na yeye hawezi kusamehewa na MUNGU.
-Mteule wa MUNGU ni mtu anayesamehe wanaomkosea maana hata asipowasamehe hatapata faida yeyote bali hasara.

Mathayo 6:14-15 ''Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. ''


8. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa UPENDO.
-Wateule wa MUNGU ni lazima wawe na upendo kwa watu wote.
-Kuwashuhudia injili wale ambao hawajaokoka ni upendo mkuu.
Kuwapenda wateule wenzako ni jambo zuri la kupendeza kwa MUNGU na kwa wanadamu.
Wakolosai 3:14 '' Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.''

9. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa SHUKRANI.

Kumshukuru MUNGU ni jambo la lazima kwa wateule wa MUNGU.
Uzima aliokupa MUNGU, Afya na ulinzi wake kwako ni mambo ya kumshukuru sana MUNGU.
Mimi naamini kila mtu kila siku anayo mambo saba ya kumshukuru MUNGU haijalishi mtu huyo yuko katika magumu kiasi gani.
Ukiitafakari miaka yako tu lazima utamshukuru MUNGU maana wanaoondoka kila leo ni wengi sana. Una viungo vyote, unaona, unasikia, unatembea na kukimbia, hakika una haki ya kumshukuru MUNGU.
Una kazi, una biashara, umekula na umelala vizuri yote hayo ni sehemu tu ndogo katika yale unayotakiwa kumshukuru MUNGU kwayo.

Zanuri 136:1-3 ''Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuruni MUNGU wa miungu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuruni BWANA wa mabwana; Kwa maana fadhili zake ni za milele.''

10. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa KULIWEKA NENO LA KRISTO MOYONI.

Neno la KRISTO ndilo Neno la MUNGU lote.
Neno la MUNGU huwekwa moyoni na sio pengine.
Kama huwa unatabia ya kuliweka Neno kwenye karatasi tu kisha baadae unaitupa, nakuomba kuanzia leo anza kuliweka Neno la MUNGU Moyoni,
Kuandika kwenye Daftari kile unachojifunza ni jambo jema lakini naomba hiyo ikusaidie kuupitia baadae ujumbe huo uliouandika ili ukae moyoni.

Wakolosai 3:16 '' Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu.''

11. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa KUFUNDISHA NA KUFUNDISHWA.

Wateule wa MUNGU ni mawakili wa siri za MUNGU, hivyo inawapasa sana kujua kufundisha walio nje ya KRISTO ili waje ndani ya Wokovu wa KRISTO.
Wateule wa MUNGU wako katika Darasa la Mwalimu ROHO MTAKATIFU, Hivyo wanapaswa sana kuwa na mioyo ya kufundishwa Neno la MUNGU na kulitii.
1 Petro 2:2 '' Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa(Neno la MUNGU), ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;''

12. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa KUKUBALI KUONYWA.
-Wakati mwingine mteule unaweza kufanya yasiyotakiwa hivyo unaitaji maonyo kukuweka sawa.
Mfano, Unaweza ukampenda mchumba ambaye viongozi wako wameona kabisa kwamba mchumba hiyo hajatulia hivyo wanakuonya. Kama huna moyo wa kukubali kuonywa utaona wanakudhalilisha kumbe wanakusaidia.
Mithali 15:32 '' Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe; Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu.''

BWANA YESU Amekaribia Kurudi. Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.

Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments