MAMBO YA KIPAUMBELE CHA JUU

Na Mtumishi Dr. Frank P. Seth

“1Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala. 2Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato. [.....]. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. 8Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato” (Mathayo 12: 1, 2 & 7).
Katika kutafuta-tafuta sana kwenye maandiko, na kujifunza MAISHA na TABIA za BWANA Yesu, nimeshangazwa sana na jinsi ambavyo ALITOFAUTIANA sana na watu wengi ambao kwa wakati huo walikuwa ndio waalimu, wanasheria na viongozi wa dini.
Katika kutafakari zaidi, nikaona dhahiri kwamba, kwa viwango vya dini zile za Kiyahudi, yaani Mafarisayo na Masadukayo, BWANA hakuwa ametimilika. Alionekana kupungua sana.
Kwa mfano, katika mistari hapo juu, naona REHEMA ikiwa juu kwa vipaumbele kuliko SADAKA. Je! Umeona dini zetu na madhehebu yetu ya sasa yameweka wapi rehema ukilinganisha na sadaka?
Maana ya Rehema: Rehema ni HURUMA ambayo humpelekea mtu KUFANYA jambo JEMA ili kumsaidia mtu bila kujali KUSTAHILI kwake huyo mtu kufanyiwa jambo hilo.
Angalia hapa, “Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi” (Maombolezo 3:22) maana yake ni kwamba, kwa hali zetu hatustahili kupokea jambo jingine kutoka kwa Mungu kwa sababu tumepungua kila mahali ila ameamua kutokutuangamiza kama ambavyo tungestahili. Hiyo ni Rehema imesababisha sisi hatuangamii.
Sasa angalia, unadhani mambo ya HUDUMA, KANISANI kwako, WATUMISHI wa Mungu ni muhimu kuliko watu wa NYUMBANI kwako? Je! Ni muhimu kuliko MASKINI mlangoni kwako? Je! Utahesabiwa haki sana ukimwacha mjane na yatima mtaani mwako na kuhangaika na kujenga MASINAGOGI? Je! Unadhani SADAKA zako na REHEMA ni kipi kitahesabiwa kua na kipaumbele cha juu zaidi?
Angalia, fanya la kwanza na usiache la pili. Weka vipaumbele vyako sawasawa.
Frank P. Seth.

Comments