MTAKUWA NURU KWELI KWELI


Na Askofu mkuu Zakaria Kakobe.
l
eo, tunajifunza YOHANA 8:25-47, katika Biblia zetu.  Kuna mengi ya kujifunza tunapotafakari mistari hii ingawa kichwa cha somo letu ni ”MTAKUWA HURU KWELI KWELI”.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele kumi na tatu:-

(1)      U NANI WEWE? (MST. 25);
(2)      KUWA NA KIASI KATIKA KUSEMA (MST. 26);
(3)      UWEZEKANO WA KUTOKULIELEWA NENO LA MUNGU (MST. 27);
(4)      KUINULIWA KWA MWANA WA ADAMU (MST. 28);
(5)      SIFANYI NENO KWA NAFSI YANGU (MST. 28);
(6)      SIRI YA KUWA PAMOJA NA MUNGU SIKU ZOTE (MST. 29);
(7)      MATOKEO YA INJILI KATIKA UPINZANI MKALI (MST. 30);
(8)      ALAMA KUU YA MWANAFUNZI WA YESU (MST. 31);
(9)      KWELI ITAWAWEKA HURU (MST. 32);
(10)       MTAKUWA HURU KWELI KWELI (MST. 33-38);
(11)       MATUNDA YA KUWA WATOTO WA IBRAHIMU (MST. 39-44);
(12)       NI NANI ANISHUHUDIAYE YA KUWA NINA DHAMBI? (MST. 45-46);
(13)       ALAMA KUU YA YEYE ALIYE WA MUNGU (MST. 47).

(1)     U NANI WEWE? (MST. 25)
Yesu aliwaambia watu hawa, “Msiposadiki ya kuwa MIMI NDIYE (Masihi au Kristo), mtakufa katika dhambi zenu“ (MST. 24).  Wanamwuliza, “U nani wewe?“, Yesu anawaambia, Hasa neno lilo hilo ninalowaambia (kwamba mimi ndiye Masihi au Kristo mliyekuwa mnamtarajia).  Wako watu wengi leo ambao wanamwona Yesu kama mtu wa kawaida, kama wanadamu wengine waliokuwa manabii.  Mioyoni mwao wanasema,“Yesu ni nani, ana nini cha zaidi?“.  Jibu ni hili, “YEYE NDIYE“, na anayemsadiki hata akiwa mtu wa dini namna gani, atakufa katika dhambi zake na kwenda motoni (YOHANA 3:17-18, 36).

(2)   KUWA NA KIASI KATIKA KUSEMA (MST. 26)
Yesu alikuwa na mengi ya kusema na kuwahukumu watu hawa kwamba ni wakosaji, lakini hakuyasema yote.  Sisi nasi hatuna budi kuwa hivi.  Tunaweza kujua waziwazi kwamba mume wetu ndiye mkosaji na anatusingizia kila siku na kutuona sisi ndiyo wakosaji.  Hata hivyo hatuna budi kuwa na kiasi katika kusema makosa ya wenzetu na kumwachia Mungu awashughulikie na kuwahukumu yeye mwenyewe.  Yesu hapa alimwacha Mungu alitoka kweke yeye asiyemsikiliza  (KUMBUKUMBU 18:18-19).

(3)  UWEZEKANO WA KUTOKULIELEWA NENO LA MUNGU (MST. 27)
“Wala hawakutambua ya kuwa anawatajia Baba“, ni fundisho kwetu.  Watu hawa walilisikia Neno la Kristo huku wanajiona wanajua, wakiwa wamejaa ukaidi na ubishi.  Tukilisikia neno la Mungu katika hali hii, kamwe hatuwezi kulielewa (ISAYA 66:2; 1 WAKORINTHO 8:2).

(4)      KUINULIWA KWA MWANA WA ADAMU (MST. 28)
Yesu Kristo anaitwa Adamu wa mwisho au mtu wa pili (1 WAKORINTHO 15:45-49).  Kwa msingi huu, Yesu anaitwa Mwana wa Adamu.  Yesu aliinuliwa, pale alipotundikwa msalabani kama yule nyoka jangwani, ili amwaminiye awe na uzima (YOHANA 3:14-15).  Dhabihu au sadaka ya wanyama iliyotolewa jioni ilipaswa kuinuliwa juu wakati ilipokuwa inatolewa.  Yesu alikuwa dhabihu hii kwa ajili yetu (ZABURI 141:2; WAEBRANIA 10:12; YOHANA 1:29).  Hakika alipoinuliwa Yesu msalabani watu hawa walifahamu ya kuwa Yesu ndiye (MATHAYO 27:54).  Hatupaswi kungojea mwisho wa dunia ili kumkiri Yesu na kuokolewa.  Tutakuwa tumechelewa.  Tunapopita katika aibu na kudharauliwa kama Yesu msalabani na kuonekana tumeshushwa, ni kinyume, hakika ndipo Mungu anapotuinua!
(5)     SIFANYI NENO KWA NAFSI YANGU (MST. 28)
Kufanya neno kwa nafsi ya mtu, ni kufanya lolote ambalo ni kinyume na mapenzi ya Mungu au Neno lake. Yesu kamwe hakufanya hivi.  Sisi nasi, inatupasa kuenenda kama yeye alivyoenenda (1 YOHANA 2:6).  Kamwe, tusifanye lolote kwa nafsi zetu wenyewe.

(6)    SIRI YA KUWA PAMOJA NA MUNGU SIKU ZOTE (MST. 29)
Siri ya kuwa pamoja na Mungu siku zote, ni kufanya siku zote yale yampendezayo Mungu.  Siku zote Yesu alifanya yale yampendezayo Mungu.  Aliitimiza haki yote!  Hiyo ndiyo iliyokuwa siri ya mafanikio makubwa katika huduma yake.  Mafundisho yake, mahyubiri yake, maombezi yake kwa wenye shida mbalimbali8 n.k., vyote viliambatana na uawepo wa Mungu (LUKA 5:17).  Tukitaka kuona Mungu anakuwa pamoja nasi, inatupasa kuhubiri na kufundisha yale yanayompendea Mungu.  Tukichagua kufanya asiyoyafurahia Mungu, Mungu hutuacha, na badala ya baraka, mapigo hutuandama (ISAYA 66:4).

(7)    MATOKEO YA INJILI KATIKA UPINZANI MKALI (MST. 30)
Mahubiri ya Yesu hapa yaliambatana na upinzani mklai (MST. 13,19, 21-22).  Hata hivyo, matokeo yake yalikuwa ya ajabu wengi walimwamini.  Hatupaswi kuogopa au kukata tamaa kuhubiri Injili katika mazingira ya upinzani mkali.  Mlango mkubwa wa Injili wa kufaa sana, mara nyingi huwa kati ya upinzani mkali (1 WAKORINTHO 16:9).

(8) ALAMA KUU YA MWANAFUNZI WA YESU (MST. 31)
Kukaa katika neno la Kristo, ndiyo alama kuu ya mwanafunzi wa Yesu.  Mwanafunzi wa Yesu, atalipenda Neno la Mungu na kukaa au kudumu katika neno hilo kwa gharama yoyote.  Hawezi kuruhusu chochote kile kimtenge na upendo wa Kristo ulio katika Neno la Mungu (WARUMI 8:35).  Ikiwa hatulipendi Neno la Mungu kama mwanzo, basi tujue tumeacha zamani uanafunzi wa Yesu.  Mtu asiyekaa katika neno la Mungu katika ibada Jumapili, Jumatatu, Jumatano na Jumamosi na kulisoma nyumbani kwake kila siku na kulisikia katika kaseti tena na tena, huyu siyo mwanafunzi wa Yesu.

(9     KWELI ITAWAWEKA HURU (MST. 32)
Kweli ni Neno la Mungu (YOHANA 17:17).  Tukilifahamu Neno la Mungu kuhusiana na kupondwa kichwa kwa shetani pale msalabalni, jinsi Yesu alivyochukua dhambi zetu na magonjwa yetu yote pale msalabani, ushindi tunaoupata katika Kristo, n.k., maarifa haya hutuweka huru mbali na kukandamizwa na shetani.  Shetani HUMUONEA mtu yeyote asiyeifahamu Kweli au neno la Mungu na watu wa Mungu huangamizwa kwa kukosa maarifa ya Neno la Mungu (MATENDO 10:38; HOSEA 4:6).  Kweli pia ni Yesu Kristo mwenyewe (YOHANA 14:6; MATENDO 4:10-12).  Hakuna yeyote mwingine anayeweza kutupa uhuru au ushindi juu ya dhambi, isipokuwa Kweli, Yesu Kristo.  Kuifahamu Dini na kuwa nayo, hakuwezi kutupa uhuru au ushindi juu ya dhambi.

(10)  MTAKUWA HURU KWELI KWELI (MST. 33-36)
Wakamjibu, “Sisi tu uzao wake Ibrahimu wala hatujawa watumwa wa mtu WAKATI WOWOTE, nawe wasemaje, Mtawekwa huru?“  Watu hawa walijihesabia haki kutokana na Ibrahimu baba yao!  Wako watu wengi wa jinsi hii leo.  Wakiambiwa watubu dhambi waokolewe, wanasema, “Mimi ni mtoto au mke wa Mwinjilisti au Mchungaji maarufu“.  Mtu hawezi kuokolewa kutokana na haki ya ndugu yake! (EZEKIELI 14:12-20).  Hapa pia wanasema uongo wa dhahiri kwamba hawajawa watumwa wa mtu wakati wowote.  Wana wa Israeli, walikuwa uzao wa Ibrahimu.  Hawa ndiyo waliokuwa utumwani Misri kwa miaka 430 na tena wakawa utumwani Babeli kwa miaka 70.  Pamoja na Yesu kujua hapa wanasema uongo, lakini hakubishana nao na kutaka kuwahakikishia kwamba wao ni waongo, bali alizidi kuzungumzia msingi wake wa Injili, “Kila atendaye dhambi, ni mtumwa wa dhambi“.  Wakati wa kiuhubiri Injili tusikubali kutolewa kwenye msingi wetu wa Injili na kuanza kubishana!  Kila atendaye dhambi, ni mtumwa .  Ulevi, uvutaji sigara, uasherati, uzinzi, wizi, muziki wa dansi au ushabiki wa mpira wa ligi, yote haya ni utumwa maana hatuwezi kujikwamua na kuyaacha kwa nguvu zetu bila Yesu!  Ingawa Waisraeli walihesabiwa kuwa Taifa la Mungu, watu wa nyumbani mwake hata hivyo walikuwa watumwa.  Mtumwa hakai sikuzote kwa mtu.  Siku moja ataondoka na kuhamia kwingine, lakini mtoto yeye ni mrithi, hukaa siku zote nyumbani.  Waisraeli kwa kuwa ni watumwa, hawatakaa na Yesu milele mbinguni, mpaka wawekwe huru mbali na dhambi.  Watu tuliookoka, tuko huru mbali na dhambi, uhuru wetu siyio wa kufanya dhambi.  Wenye “uhuru“ wa jinsi hiyo ni mataifa (WARUMI 6:17-22).  Mtu akiokolewa, anakuwa huru kweli kweli mbali na uasherati, uzinzi, kunywa pombe, kuvuta sigara, wizi, masengenyo, ushirikina n.k.  Ukimsikia mtu anasema ameokoka na ameacha yote ila bado sigara kidogo na uzinzi kidogo ndiyo vinampa shida, huyu ni mwongo!  Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru  KWELI KWELI mbali na dhambi na kila uasi wa Neno la Mungu.

(11)      MATUNDA YA KUWA WATOTO WA IBRAHIMU (MST. 39-44)
“Mtawatambua kwa matunda yao“ (MATHAYO 7:16), ni kipimo halisi cha kutumia katika kumtambua mtu.  Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu, lakini sasa mnatafuta kuniua, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli.  Ibrahimu hakufanya hivyo, ni maneno ya Yesu kwetu.  Wako watu wengi leo wanaosema wao ni Wakristo yaani watoto wa Kristo lakini wanafanya uasherati, wanakunywa pombe, wanavuta sigara, wanasema uongo, wamejaa hasira, wivu, chuki na masengenyo, wanaiba n.k.  Kristo hakufanya hivyo.  Hivyo hawa ni watoto wake Ibilisi maana ndiye anayetenda hivyo.  Badala ya kujiita Wakristo, wajiite Waibilisi!  Tunaona pia hapa kuhubiri kweli kunavyosababisha maadui.  Watu watataka kutuua au kuzifuta huduma zetu kwa kuzipaka matope, tukihubiri kweli, hata hivyo KWELI LAZIMA ITASHINDA.  Tusonge mbele kama yesu na Mtume Paulo (WAGALATIA 4:16; 1:10).
(12)      NI NANI ANISHUHUDIAYE YA KUWA NINA DHAMBI? (MST. 45-46)
Hiki ni kipimo cha kila mtakatifu.  Hana budi kushuhudiwa na watu wanaomzunguka.  Je, kila mmoja wetu ana ujasiri wa kusema maneno haya kwa watu wanaomzunguka nyumbani, kazini, katika biashara yake n.k.  kama Yesu?  Kama sivyo, madai yetu ya kuwa watakatifu, yana kasoro!

(13)      ALAMA KUU YA YEYE ALIYE WA MUNGU (MST. 47)
Aliye wa Mungu ni yule aliye Msikiaji na Mtendaji wa Neno (MATHAYO 7:24-27; YAKOBO 1:22-24).
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Kwa Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe fungua       
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Comments