MUNGU ANATAKA UFANIKIWE(2)

Na Mwl. Christopher Mwakasege.
Bwana Yesu asifiwe milele!
Mungu anasema hivi: “Nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho” (Yeremia 29:11)
Hii inaonyesha ya kuwa Mungu anayo mawazo kadhaa, ambayo anataka ayaweke ndani ya moyo wa mtu, ili yaweze kumjulisha na kumwongoza katika kutekeleza mpango, utakaofanikisha maisha yake.
Wiki iliyopita nilikupa wazo la 1 nalo lilikuwa linasema hivi: “Ombea kwa Bwana mji unaohusika na maisha yako”.
Wiki hii nataka tuangalie wazo la 2, nalo ni hili : “Wazo la Mungu linaloweka moyoni mwako sababu zinazomfanya Mungu atake kukufanikisha”.
Kumbuka: Mungu hawezi kukufanikisha kwa kutumia mpango wako, bali kwa kutumia mpango wake aliouandaa kwa ajili yako!
Kumbuka tena ya kuwa: Mungu hawezi kukufanikisha kwa ajili ya kutimiza malengo yako, bali kwa ajili ya kutimiza malengo yake aliyonayo!
Tena – Mungu hawezi kukufanikisha kwa sababu tu ya kukufanikisha! Ni lazima anazo sababu muhimu za kukufanikisha!
Ukizijua sababu zinazomfanya Mungu aamue kumfanikisha mtu; na ukajiunganisha nazo kwenye fikra zako na katika nia yako; uwe na uhakika mkono wa Mungu utakuwa pamoja nawe katika kukufanikisha!
Baadhi ya sababu ambazo Mungu anazitumia ili amfanikishe mtu ni hizi zifuatazo:
Sababu ya 1: Ni ili aweze kumsaidia mtu aishi na mafanikio na kuyatumia, bila ya mafanikio hayo kumwangamiza. Mithali 1:32 inasema: “Kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza”. Mungu hapendi mafanikio yawe chanzo cha wewe kuangamia. Mungu anataka akusaidie ufanikiwe, lakini pia akusaidie uishi na mafanikio na uyatumie, bila ya kutoa nafasi kwa mafanikio hayo kukuangamiza. Ndio maana inabidi akusaidie maeneo yote sawa na 3 Yohana 1:2 kwamba: “Ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo”.
Sababu ya 2: Mungu anakufanikisha ili iwe rahisi kupanua “shughuli” alizokupa uzifanye! Mungu anasema: “…Miji yangu kwa kufanikiwa itaenezwa huko na huko tena…” (Zakaria 1:17). Ikiwa kwa kuifanikisha Miji – miji hiyo inapata fursa na nguvu za kuenea; ina maana kwa kumfanikisha mtu, Mungu anatoa fursa na nguvu kwa mtu huyo “kuenea” au kupanua shughuli azifanyazo!
Sababu ya 3: Mungu anakufanikisha ili mafanikio hayo yakupe kukubalika na kusikilizwa na watu wanaokuzunguka! Mtume Paulo anashuhudia akisema wenzake walimpa “mkono wa kuume wa shirika” pale “walipo – kwisha kuijua ile neema” aliyopewa (Galatia 1:9). Ukisoma kwa kutafakari Mithali 17:8 na Mithali 18:16 utaona ya kuwa: Kipawa cha mtu kikifanikiwa, huwa kinamfanya afanikiwe na huyo mtu aliye na hicho kipawa …na kufanikiwa huko kunamfungulia mtu huyo kukubalika na kusikilizwa!
Sababu ya 4: Mungu anakufanikisha ili uwe baraka kwa wengine (2 Korintho 9:10,11) na kwa uzao wako (Mwanzo 22:17 – 18 )!
Sababu ya 5: Mungu anakufanikisha ili uweze kutimiza agizo ambalo Mungu amekupa! Hii ndiyo sababu mojawapo iliyomfanya Mungu amfanikishe mfalme Sulemani katika 1 Mambo ya Nyakati 22:11.
Hizi ni baadhi tu ya sababu zinazomfanya Mungu aamue kumfanikisha mtu. Naamini zitakupa msukumo wa kutaka kupata mafanikio kwa msaada wa Mungu katika Kristo!


 Nataka liingie hili ndani ya moyo wako ya kuwa Mungu anapenda ufanikiwe, na anapenda na Yeye ashiriki katika kufanikiwa kwako huko; lakini kutumia mpango wake, alionao kwa ajili yako!
Mtazamo huu na msimamo huu wa Mungu, tunauona tunaposoma mstari wa Yeremia 29:11 usemao: “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.
Zipo aina nyingi za mawazo ya Mungu, zinazounda mipango aliyonayo kwa ajili yako, ili uweze kufanikiwa. Tuangalie aina ya 1 ya wazo mojawapo la Mungu, alilolikusudia kuliweka moyoni mwako, ili liweze kukujulisha na kukuongoza katika mpango wake, utakaofanikisha maisha yako.
Wazo hilo ni hili: “Ombea kwa Bwana mji unaohusika na maisha yako!”
Wazo hili linatokana na agizo la Mungu kwa wana wa Israeli alipowaambia ya kwamba: “Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa Bwana; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani” (Yeremia 29:7).
Neno hili “amani” lililoandikwa mara tatu katika mstari huu wa Yeremia 29:7 lina maana ile ile ya neno “amani”, lililotumika katika mstari ule wa Yeremia 29:11. Neno hili “amani” lilivyotumika katika mistari hii miwili lina maana ya “mafanikio”
Ndani ya agizo lililomo katika mstari huu wa Yeremia 29:7 nataka ujifunze na kutilia maanani yafuatayo:
1. Kwamba; Kufanikiwa kwako katika kitu unachokifanya, kumeunganishwa na kufanikiwa kwa mji unaokaa au unaoishi. Mji ukifanikiwa kimaendeleo na wewe unatakiwa ufanikiwe vile vile! Mji ukifanikiwa kimaendeleo, wakati wewe mkaazi wake umekwama kimaendeleo, ina maana umeshindwa kupata mbinu za kujiunganisha katika mafanikio ya mji huo! “Kwa maana katika amani (mafanikio) yake mji huo ninyi mtapata amani (mafanikio)”! Haya ndiyo ambayo Mungu aliwaambia wana wa Israeli – na anakuambia na wewe pia leo!
2. Kwamba; Ili mji unaokaa ufanikiwe kimaendeleo, unahitaji pia maombi yako. Biblia inasema: “Kautakieni amani (mafanikio) mji …mkauombee kwa Bwana” (Yeremia 29:7). Kuuombea mji kunamwonyesha Mungu haja uliyonayo moyoni mwako, ya kutaka msaada wake, ili aweze kukupa mbinu zitakazokuunganisha na mafanikio ya mji huo, ili na wewe ufanikiwe!
3. Kwamba; Maombi unayoombea mji, yanatoa nafasi kwa Mungu “kufuatilia” aina ya maendeleo yanayoufanya mji ufanikiwe! Hii ni kwa sababu si kila mafanikio unayoyaona katika mji yanakufaa na wewe pia! Biblia inasema: “Kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza” (Mithali 1:32)! Na Mungu asingetaka ujiunganishe na mbinu zilizopo katika mji zinazowaangamiza wanaozitumia kufanikiwa! Mbinu za mafanikio kama hizo, ndizo zinazofanya “mji” ukifanikiwa – unajikuta hautaki kumsikiliza Mungu…na wakaazi wake wanakuwa hawataki pia kumsikiliza Mungu! Mungu anasema: “Mimi nalisema nawe wakati wa kufanikiwa kwako; lakini ulisema sitaki kusikia …” (Yeremia 22:21). Mafanikio yanayokufanya usimsikilize Mungu hayakufai.
4. Kwamba; Ukilitazama kwa mtazamo huu suala la kuombea mji ili ufanikiwe, utajikuta unaombea mji zaidi ya mmoja! Wana wa Israeli walipopewa agizo la kuombea mji wa Babeli walikuwa mbali na kwao. Na walipokuwa huko uhamishoni walijikuta wanauombea pia mji wa Yerusalemu ambako ndio kwao! Kwa hiyo ukiombea “Babeli” yako, usisahau kuombea na “Yerusalemu” yako, maana maombi ya miji inayotumika kukupa kipato chako, yanaunganisha mafanikio ya miji hiyo na kule kufanikiwa kwako!
5. Kwamba: Hata kama mji huupendi, wewe uombee, ili kuonyesha utii wako kwa Mungu, ili akufanikishe katika kipindi ulichomo katika mji huo! Nina uhakika wana wa Israeli hawakuupenda mji wa Babeli, lakini bado walitakiwa wauombee katika kipindi walichokuwa huko!

 Mungu anataka ufanikiwe katika maisha yako! Tena – anataka ashiriki katika kufanikiwa kwako, kwa yeye kukupa mpango wake, ambao anataka akuongoze katika kuutumia, ili ufanikiwe!
Hii ndiyo sababu inayomfanya Mungu aseme: “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani…” (Yeremia 29:11). Kwa tafsiri pana zaidi tunawezeshwa kujua ya kuwa – Mungu anayo mipango (mawazo) aliyotupangia, ambayo ni mipango ya kutufanikisha (amani)!
Kwa jinsi ya kibinadamu, ungejua ya kuwa kuna mtu aliye na mpango kwa ajili yako, ambao umeandaliwa ili ukiutekeleza ufanikiwe, ungenyamaza usiufuate?Sidhani kama ungenyamaza! Najua ungetaka kujua uhakika wa jambo hilo; na baada ya kujihakikishia, ungekwenda kuufuata huo mpango ulipo na kuutekeleza!
Biblia inatueleza ya kuwa Mungu anao mpango wa namna hiyo kwa ajili yako! Na njia mojawapo anayotumia kukupa mpango huo, ni kuweka moyoni mwako mawazo yanayohusu mpango huo!
Leo nataka nikushirikishe wazo la 3 ambalo Mungu ataliweka moyoni mwako, kama sehemu ya mpango wake, ili likusaidie kufanikiwa.
Wazo hilo ni hili: “Pokea mikakati ya Ki – Mungu ya kukuwezesha ushinde upinzani na ushindani dhidi ya mafanikio yako!”
Mkakati wa 1: Jifunze kuutegemea upendo wa Mungu juu yako! Warumi 8:35,37 tunasoma hivi: “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda”.
Mkakati wa 2: “Keep focused” kwenye ushindi bila kuvuruga mtazamo wako wa ushindi kwa wewe kuhangaika kushindana na wale wanaoshindana na wewe! Hii ni kwa sababu, biblia inauliza hivi: “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate” (1 Wakorintho 9:24). Hiki kipengele cha mwisho cha mstari huu kwa tafsiri ya biblia ya kiingereza inasomeka hivi: “Run in such a way that you win!”
Mkakati wa 3: Jiombee ili Mungu akusaidie mawazo yako ndani yako, yasipingane na mawazo ambayo Mungu anakuletea moyoni mwako, yaliyobeba mpango wake kwa ajili yako! Nia ya maombi ya jinsi hii ni ili upate msaada wa Mungu kuangusha “mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo” (2 Wakorintho 10:5) – ndani ya moyo wako mwenyewe!
Mkakati wa 4: Jizoeze kuwa na tabia ya kukaa katika maombi kwa muda mrefu, ili ushinde upinzani unaotoka kwenye mwili wako, unaokukwamisha usifanye mpango wa Mungu! Hii ndiyo sababu iliyomfanya Yesu awaambie wanafunzi wake hivi: “Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni muombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu” (Mathayo 26:40,41).
Mkakati wa 5: Fahamu cha kufanya unapoona ya kuwa shetani ameinuka kukuzuia usifanye mpango wa Mungu! Unapokutana na upinzani wa shetani, biblia inasema: “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” (Waefeso 6:11,12).
Hii ni baadhi ya mikakati inayotuonyesha ya kuwa katika mipango ya Mungu aliyonayo ya kukufanikisha, hana mpango wa kuona hufanikiwi – hata kama utakutana na upinzani au ushindani!
Kifikra – kaa mkao wa mtizamo wa kushinda na kufanikiwa! Ile kwamba umesoma ujumbe huu, ujue nimekuombea na ninakuombea ushinde vikwazo na ufanikiwe!

Comments