NI MUHIMU SANA WEWE KUMTEGEMEA MUNGU TU.

Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Yeremia 17:7-8 ''Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda. ''

Amebarikiwa mtu yule amtegemeaye BWANA.
Amebarikiwa mtu yule ambaye BWANA YESU ni tumaini lake.
Amebarikiwa mtu yule anayeishi maisha ya wokovu katika BWANA.
Amebarikiwa mtu yule anayeishi maisha matakatifu katika KRISTO.
Amebarikiwa mtu yule asiyeenda kwa waganga wa kienyeji.
Amebarikiwa mtu yule asiyekwenda kwa wasoma nyota wala  wanajimu.
 ''Nafsi yangu, umngoje MUNGU peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake. Zaburi 62:5''

Ndugu yangu, ni heri kumtegemea BWANA tu.
Ni heri kumtegemea kwa maombi na utakatifu.
Ni heri kumngoja BWANA kwa maombi na utakatifu.
Mtegemee BWANA kama walivyomtegemea akina Shadraka, na Meshaki, na Abednego hata moto wa mfalme Nebukadreza ukashindwa kuwaunguza(Danieli 3:1-30).
 Hawa walimtegemea na kumtamaini BWANA na kifo kilichopangwa kwao hakikufanikiwa kuwapata.
Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake

 Zaburi 118:8-9 ''Ni heri kumkimbilia BWANA Kuliko kuwatumainia wanadamu. Ni heri kumkimbilia BWANA. Kuliko kuwatumainia wakuu.''

Mtegemee BWANA kama Danieli ambaye alitupwa katika shimo lenye simba wakali, lakini simba wale hawakumdhuru kwa lolote(Danieli 6:4-28).
Mtegemee BWANA kama Yusufu alimvyomtegemea, hatimaye BWANA akampa kuwa waziri mkuu wa taifa kubwa la ugenini(Mwanzo 39 Hadi Mwanzo 41).
Mtegemee BWANA kama Paulo na Sila ambao walikuwa Gerezani lakini BWANA akamtuma Malaika wake awaokoe na wakaokoka na adhabu za serikali mbaya(Matendo 16:16-34).
 Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake.

 Mithali 3:5-10 '' Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche BWANA, ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako. Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.''

Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake.
Mtegemee BWANA Kama mama wa Sarepta ambaye alimwamini MUNGU kupitia mtumishi wake Eliya  hata akapata mali nyingi katika kipindi cha njaa kwa taifa lake(1 Wafalme 17:9-24).
Mtegemee BWANA kama mama mshunemu ambaye alimwamini MUNGU kupitia Mtumishi wake Elisha hata akapata mtoto katika ujane wa muda mrefu sana(2 Wafalme 4:8-37).
Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake.

 Zaburi 71:5-6 '' Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU, Tumaini langu tokea ujana wangu. Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa, Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, Ninakusifu Wewe daima. ''

Ndugu mtegemee MUNGU maana ana uzima wako.
Mtegemee BWANA YESU maana ana uzima wako wa milele.
Songa mbele katika wokovu wala usikubali kurudi nyuma.
Kurudi nyuma ni dalili ya mtu kutokumtegemea MUNGU.
Kurudi nyuma ni aibu kubwa kwa waenda mbinguni.
Mtegemee BWANA siku zote na mtumaini BWANA nyakati zote.
Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake

Kutoka 15:11 ''Ee BWANA, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu? ''
 
Mtegemee BWANA Asubuhi na jioni, Mtegemee BWANA mchana na usiku.
Usimwache BWANA hata dakika moja, bali mtegemee BWANA YESU siku zote za maisha yako.
Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake

Kataa dhambi maana kutenda dhambi ni kumkataa MUNGU na Neno lake.
Songa mbele maadamu umemtegemea BWANA.
BWANA haaibishi bali kwa kumtegemea kwako Utapata ushindi, baraka na uzima pia.
Una heri wewe unayemtegemea BWANA siku zote.
Hata katika magumu nakuomba ndugu yangu mtegemee BWANA.
Hata katika Magumu yako  nakuomba mtegemee BWANA maana ana ushindi wako na uzima wako.
Ni nani kama BWANA?
Hakuna aliye kama yeye na hatakuwepo milele aliye kama JEHOVAH MUNGU wetu.

Zaburi 83:18 '' Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote. ''

Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake
Ndugu yangu, usikubali hata siku moja kupunguza upendo kwa MUNGU bali ongeza upendo huo siku zote.

''Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na MUNGU huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu. 1Yohana 5:4''

Asante kama unanielewa ndugu yangu.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments