USHUHUDA WA MWALIMU MWAKASEGE

Na Mwl Christopher Mwakasege, Kwenye picha Mwl Mwakasege akiwa na mkewe Diana Mwakasege.

“Roho Mtakatifu anavyoongoza wana wa Mungu kutembea na Mungu katika maeneo mbalimbali ya maisha yao”.
Leo nataka nikushirikishe kile kilichonisukuma kujifunza jinsi Roho Mtakatifu anavyoongoza watoto wa Mungu, na kwa kujifunza hili nipate kujua Mungu anavyoongea na watu!Sifundishi somo hili kwa sababu tu ya kutafuta somo la kufundisha, la hasha! Bali ni kwa sababu Mungu aliyenifundisha mimi, anataka nikushirikishe na wewe yale niliyojifunza kwake!


Niliokoka mwaka 1983 nikiwa nyumbani kwa wazazi wangu, walipokuwa wanafanya kazi eneo la Rongai lililoko “West Kilimanjaro” – mkoani Kilimanjaro.Jambo mojawapo lililojitokeza ndani yangu baada ya kuokoka, lilikuwa ni kiu kubwa ya kutaka kumjua Mungu zaidi na kumtumikia! Na kadri siku zilivyokuwa zinaendelea – kiu hiyo pia ilikuwa inaongezeka!


Miaka miwili baadaye – yaani mwaka 1985, liliingia moyoni mwangu wazo la kutaka kuacha kazi niliyokuwa nafanya serikalini mjini Arusha, ili niende chuo cha biblia kusomea uchungaji.Nilitafuta chuo cha biblia cha kusomea uchungaji – nikapata! Nilizungumza na viongozi wa chuo hicho, juu ya namna ya kujiunga na chuo chao ili kusomea uchungaji – wakanielekeza! Nikatafuta wafadhili wa kulipia gharama zangu za kusomea uchungaji – nikawapata! Nikatafuta nyumba ya kukaa na familia yangu nikiwa chuoni – nikapata!


Mambo hayo yalinichukua karibu muda wa mwaka mzima kuyakamilisha! Nikaanza kufuatilia kutaka kujua utaratibu wa kuacha kazi niliyokuwa nafanya serikalini, ili nikajiandae kwenda chuo cha biblia kusomea uchungaji.Siku moja nikiwa nimekaa kwenye uwanja mbele ya nyumba niliyokuwa naishi wakati ule, jioni baada ya kutoka kazini, nilishangaa na kushituka kuona Mungu akinisemesha wazi wazi moyoni mwangu!
Mungu akaniambia: “Mimi sikukuita uwe mchungaji! Chuo unachotaka kwenda kusoma kinaandaa wachungaji, wakati wito wako wewe si uchungaji. Kaa ulipo, usiache kazi kwa sasa, nitakwambia nilichokuitia, na nitakufundisha mwenyewe namna ya kuenenda kwenye wito huo!”


Maneno ya ujumbe huo yalinishitua na kunishangaza sana! Nilishangaa kwa sababu ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kumsikia Mungu waziwazi akisema moyoni mwangu, na kunielekeza cha kufanya!Nilishituka kwa kuwa niliwaza juu ya watu wengi “niliowasumbua” katika kutafuta chuo cha biblia ili nijiunge nacho – huku wakiwa na utayari wa kunisaidia! Moyoni iliingia “hofu” na kujiuliza namna ya kuwaambia kuwa uchungaji si wito wangu, na kwamba nilifanya makosa kuwaomba wanisaidie kabla sijamsikia Mungu juu ya kile alichoniitia!Lakini Mungu alinisaidia katika hilo – maana niliwatafuta, na nikawaomba msamaha kwa usumbufu wangu kwao!


Wakati huo huo niliingia katika maombi mbele za Mungu ili anifundishe kusikia sauti yake! Maana baada ya kosa hilo nililolifanya – nikatambua ya kuwa kuishi bila ya kujua Mungu anaongeaje na watu, ili awape maelekezo yake, kuna gharama kubwa sana kwa mwanadamu!Na baada ya maombi hayo, Mungu alianza kunifundisha jinsi ya kuisikia sauti yake, na namna ya kuongozwa na Roho Mtakatifu wake. Na hata sasa bado anaendelea kunifundisha!


Baadhi ya njia anazotumia kusema na kuongoza watu wake alizonifundisha ni hizi:
(i) Kutambua “neno la biblia” lililotumwa kwangu binafsi ili linisaidie na kuniongoza (Isaya 55:11).
(ii) Kwa kufuata “ushuhuda wa Roho Mtakatifu” ndani ya roho yangu (Warumi 8:14, 16);
(iii) Kwa kuyatambua na kuyaelewa “Mawazo yake” anapoyaweka moyoni mwangu (Yeremia 29:11);
(iv) Kwa kutumia “amani yake” moyoni mwangu (Wakolosai 3:15);
(v) Kwa kutumia “huzuni yake” moyoni mwangu (2 Wakorintho 7:8 – 11);
(vi) Kwa kutumia “Uhuru wa Roho Mtakatifu” ndani ya moyo wangu (2 Wakorintho 3:17);
(vii) Kwa kutumia “dhamiri yangu” katika Roho Mtakatifu (Warumi 9:1);
(viii) Kwa kutumia “maono” ya Ki – Mungu (Matendo ya Mitume 26:19,20);
(ix) Kwa kutumia “Karama za Roho Mtakatifu” (1 Wakorintho 12: 4 – 11);
(x) Kwa kutumia ndoto (Ayubu 33:14,15)
Usikose kusoma somo la wiki ijayo nitaendelea kukupa maelezo zaidi juu ya njia hizi zinavyofanya kazi!

Comments