WARAKA MAALUM KWA WATUMISHI WOTE WA MUNGU

Na King Chavala

#..... Na HAWA NI WABAYA KULIKO SHETANI MWENYEWE#
Shalom!
Naamini unaendelea vizuri kibinafsi na kiutumishi!
Naamini uyafurahia maisha yako binafsi;
Naamini unaifurahia heshima Mungu aliyokupa ama uliyojitwalia baada ya kutambulishwa na Utumishi!
Naamini bado ndani kabisa kuleeee, yaani kule moyoni, unatamani kuwa Mkweli na kumsikia Mungu kama pale ulipookoka ama kujazwa na Roho Mtakatifu!
Yamkini kuna wakati unachepuka ama unateleza na unajitia moyo kuwa "ni makosa madogo tu" lakini kumbe yanajenga mazoea na kuwa tabia!!

Jiulize Mwenzangu, Je sasa na zamani, upi ni wakati mzuri wa Utumishi wako? Je unasoma neno sasa kuliko zamani? Ama sasa umeyazoea maandiko maana yamejaa kichwani? Je unafunga na kuomba sasa kuliko zamani? Au kupindi hiki umekuwa karibu zaidi na Mungu, kwahiyo huhitaji kufunga?
Je Vipi Utoaji wako, umeimarika au sasa umeweka nafsi yako kupokea tu maana wewe ni Mtumishi?
Marafiki Je? Ni wale au umetafuta wa Viwango vyako? Vipi Heshima yako kwa Mchungaji wako? Au hata lile kanisa umehama, maana sio la hadhi yako?

Kwa miaka hii 12 ya Utumishi, Nimejifunza mengi sana na naendelea kujifunza na ujue kabla ya miaka hiyo nilikuwa Mkristo wa kufanya mambo kanisani kama wajibu ama Mazoea tu na baadae nikajijua kuwa Ninayo nafasi kubwa ya kuwaleta wengine kwa Yesu na kuuheshimisha Ufalme wa Mungu; Lakini katika hiyo miaka Nimefanya Ujinga ama Uzembe mwingi na nikiona ni sawa tu, kwasababu ya kutumika huku ukiangalia ulimwengu unavyokwenda na Kumbe Shetani hufanya kila juhudi ya kukupoteza "slightly"; yaani unakuwa bize na yale unayoita Utumishi kumbe ni Tamaa zako na Kiburi tu!
Tumezoea kusema na wengi tunaona kuwa Adui mkubwa kwetu ni Shetani na wote wanaoripoti kwake kama Mapepo,Vibwengo na Majini, Wakuu wa Anga na majeshi yote ya giza kwa majina yake na hata huwa tunafundisha na kuhubiri, zaidi huomba na kukemea, lakini kumbe wako maadui wabaya zaidi ambao huwa nasi na hata tusione haraka#
Na hawa ndio "MAADUI WATATU" wakubwa, wa kupambana nao kabla hata ya hao niliowataja hapo juu, maana uwanja wao wa kujidai ni Udhaifu wako, ukichochewa na upungufu wa Neno moyoni; na kina cha Ushindi wao ni pale unapoyaacha matakwa ya Mungu na kuanza kulinda heshima binafsi, kwa lugha ya heshima tunaita "kiburi cha Utumishi"
Na ifahamike kuwa Maadui hawa watatu wanafahamiana na wanashambulia kwa kusaidiana kama Timu, kwahiyo unaweza ukasema, Mimi ni huyu tu ndio amenipiga ila hao wengine Hapana! Na ukashangaa uko chini na wote wako juu yako, kwasababu tu ulipuuzia hapo kwanza ulipoonywa! Yaani kama hivi ambavyo unasoma hapa na unaona haikuhusu!

A.PESA
Pesa ni kitu kizuri sana na usipokuwa nazo hata hauonekani, wengine wameona pesa ni shetani na wengine utajiri wameamini ni dhambi.
Pesa ina nguvu kiasi cha kushawishi moyo ufanye makao mahali ilipo....Mahali hazina yako ilipo ndio na moyo wako upo na Kuna msemo mmoja wa kizungu unasema "People made Money, but now money make people Mad!"
# Pesa ni nzuri sana lakini ikiwa juu yako ama ikikutawala, haifai hata kidogo...inaweza kukutawala ikiwa haipo, maana yake ikija kidogo tu,inakuhamisha mstarini na inakufanyia maamuzi na pia inaweza kukukalia ikiwa nyingi, maana yake hauwazi kingine zaidi ya yenyewe!

Ni dhahiri kuwa Maisha huanzia chini kwenda juu na pesa huwa hazipo,yakiwepo mawazo, lakini baadae huja na usipokuwa makini zinaweza hata kuua yale mawazo yaliyosababisha zije, Mungu hataki tuwe masikini ila pia hataki tuwaze hela na mafanikio zaidi yake!!
Kuna Nadharia huko mitaani ambazo zinaumiza, lakini ndio hivyo inatupasa kusimama mahali palipobomoka..."Wanasema Kufanya Biashara na Wapendwa Utakuwa masikini", Wengine wanasema Kuwaajiri wapendwa ni kujirudisha nyuma!!
hapo mwanzo nilikuwa nachukia sana hayo maneno, lakini ndio naona uhalisia....Yaani Mtu ambaye unaamini huyu ni Mtumishi ama ameokoka na unamwamini kabisa hata mkafanya Biashara ama ukamkopesha pesa, huyo ndio ANAKURUSHA/ANAKUSUMBUA au ANAKUCHELEWESHA...Na kila akija anakuja na Maandiko na upole wa kujitetea na kwasababu ulimwamini na labda hata hukusumbuka kuandikishiana na wala hukuweka riba...basi ana ujasiri wa kuendelea mbele tu na hata akikuona wala haoni aibu kabisa!!

Nikiacha hilo,Ukiandaa Tamasha na kuna kiingilio,mtu anakuja na akikuona anasema "Aaah Chavala, hata mimi nilipe kiingilio kweli!?" halafu itafikiri hela yenyewe kubwa yaani, sasa hapo amekutia moyo ama anakurudisha nyuma??
Kwenye Makundi ama hao wenye timu za huduma...Wanakwenda huko ama wanafanka huduma na huko wanapewa sadaka fulani, unashangaa yule kinara ama kiongozi ama aliyesindikizwa hawazi kabisa juu ya hawa, zaidi ya kusema Ahsante na hapo anangoja aitwe kwingine ili awatumie!!
Kanisa linapata shida kwenye pesa, kwasababu kwanza hakuna "Financial Transparency", na makanisa mengi yanataka kukiendesha kwa sadaka za kila jumapili, hivi kweli hatuwezi kuona kama zile zilizokuja ni mbegu na sio mkate???
Makanisa mengi wachungaji wametengana, makundi mengi ya huduma yanakufa na Watumishi wengi wanapoteza mwelekeo kwasababu ya Pesa; lazima tujue kuwa mahali inapohitajika pesa,acha itumike pesa na sio blaa blaa na ikiwa ni biashara, basi misingi ya biashara na izingatiwe na sio upendwa!!
Binafsi nimepata hasara mara nyingi sana kwa kuwakopesha bidhaa, kuwakopesha pesa, kuwadhamini mahali, kufanya biashara za ushirikiano na kuwatuma wao kuninulia bidhaa na kufanya kazi bila kulipwa nikiamini nitalipwa sawasawa na maneno ya vinywa vyao!!
Juu ya yote nimejifunza kitu kikubwa sana kwenye Kutoa na Kujitolea...wewe unayependa vitu vya bure, unayependa kupewa/kusaidiwa na kuhurumiwa kila wakati endelea tu...ila mimi Bwana akinipa "assignment" naamini provision inaanza na pesa yangu. Na ni fahari sana kuwekeza kwenye Ufalme wa Mungu!!
UKITAKA PESA ISIWE ADUI KWAKO, zingatia haya;
1.Usitamani pesa wala mali ya mtu bila kujua Utukufu nyuma ya mchakato wake wa kupata
2.Usitake pesa ama utajiri wa haraka haraka, ingawa sijasema ujicheleweshe kufanya kazi!
3.Uwe mwaminifu kwa kila pesa inayopita mkononi mwako, ikiwa ni ya watu...ipeleke, kama ni chenji irudishe na hata kama ni yako usifanyie matumizi ambayo hukuipangia awali!
4.Lazima Kuweka Akiba katika Ufalme wa Mungu, yaani Sadaka na Mbegu na uwekezaji mwingine kwenye Ufalme wa Mungu ndio uwe kipaombele! (Usijikopeshe Limbuko wala Zaka na usiache kutoa Sadaka kila uendapo Ibadani)
5.Usiwe msiri kupita kiasi kuhusu pesa, kwa Mwenza wako,kanisani kwako ama kwenye Huduma yako!
6.Pesa ina kanuni zake ili ikufae, kama Uwekezaji na Uzungushaji.....huduma ama msaada wowote wa thamani kumbuka kuulipia!
7.Usotoe toe pesa hovyo; Usitapanye; Usitumie zaidi ya ulizo nazo na Usije kumuonea mtu ama kumdharau yeyote kwa jeuri ya pesa...Kumbuka pesa si zaidi ya Utu na Utu si zaidi ya Ufalme wa Mungu!

B.KIBURI
Mtu akipanda hatua na mambo yake yakaanza kufahamika,labda Utumishi ama pesa yake, basi kuna tabia kadhaa huwa zinaanza kujitokeza, kwa mfano kuanza kuwadharau marafiki wa zamani na hata kuwatenga; Tumeona kwa macho,kuna watu walikuja mjini mikono nyuma, tukawashika mkono na kuwabeba maana ndio utumishi,lakini walivyofika tu mahali pa kuwa Maarufu, yaani hata salamu tu mtu anaipokea kwa "machejo"!
KIBURI ni pale unapoanza kuona wewe uko juu zaidi ya yeyote yule, wewe una hadhi ambayo huwezi kwenda popote pale tu, Unajiona wewe ndio wewe,kuvaa na kula wewe na kujitenga wewe!!

Unakuta...Mtumishi alikuwa anatembea huku na kule kuomba kuhubiri,lakini leo akialikwa anauliza "mko wangapi ama mnategemea kuwa wangapi vile?"; Zamani alikuwa huku na kule kuomba Interview kwa Radio, leo akiombwa redioni anasema, "Mimi siwezi kufanya Interview na karedio kanakooshia ۤ*!!
Muimbaji leo akiitwa mahali,anauliza Nitaimba saa ngapi!? Nyimbo ngapi?....na kama ni mkesha anasema, Usiku sana siwezi maana kesho nina huduma!
Studio ile ya pale mwanzo aliomba kurekodi kwa kuhurumiwa...leo anasema, Mimi siwezi fanya kazi na studio mchwara kama ile!!

Zingatia sana haya ili Usianguke na huyu Adui, ambaye huambatana sana na Umaarufu;
1.Usiache wa kuchoka kulijaza Neno la Mungu moyoni mwako!
2.Usikubali kulegeza vipimo vya Utumishi wako kwasababu ya chochote kile; Hadhi na heshima ya Kweli ipo katika Utumishi wa kweli(Don't Compromise)
3.Makelele yanapozidi, wewe "chutama", yaani ukisifiwa usidhani ndio sasa unaweza kutembea angani,huo ndio muda wa kudumu kwa Maombi
4.Usije ukathubutu ama ukafika mahali ukaanza kujiona Wewe badala ya lile kusudi ulilolibeba, kumbuka Yule Mwanapunda alitandikiwa nguo kwasababu alimbeba Yesu!
5.Kuubali Kuchungika, kubali kukaa chini ya Usimamizi; Hata ufike Viwango vingi, bado unatakiwa kujifunza na kuonywa kila mara...Lazima Uwe na Baba wa Kiroho,lazima uwe mahali panapotambulika na Uwe na Washauri(Mentors) na uwe tayari kuwasikiliza na kuwatii watu hao ambao wapo kukusaidia wewe!
6. Kumbuka ili uzidi kuwa juu na Imara, unahitaji kuzidi kushuka na Kunyenyekea!!
7. UKING'ANG'ANA Kupanda Viwango kila siku, nina uhakika hautachoka kujua Mbingu zinasema nini kuhusu hatma yako,na kama ukibaki hapo...huwezi kuwa na Kiburi hata mazingira yakulazimishe!!

C.NGONO
Nilisema hawa maadui watatu wana tabia ya Kusaidiana ama kutegemeana, yaani unajikuta mara Umekuwa Maarufu na wala hukujiandaa...ghafla Pesa inaanza kuja kwa wingi, ghafla yale mambo yaliyokuwa magumu zamani,sasa hivi yanakwenda tu, mahali ulikuwa huwezi kwenda sasa unakwenda...na unavyozidi kupanda na kufanya hayo, kwa mbaali kiburi kinaanza kuja na unajikuta umezungukwa na makelele mengi, kila mahali unasikia sauti za sifa na wengine wanakutafuta kwa simu yako na mitandao ya kijamii!
Huwa wanaanza kama wapendwa ama watia moyo ama mashabiki ama watu ambao wanabarikiwa sana na huduma ama Utumishi wako na kwahiyo unafungua milango kwa kupokea hongera na mara unajikuta uko kwenye "Chat", utani utani...mara key za Chat zinahama....sasa mnachat hata Usiku wa manane na kwasababu Dhambi ni Mchakato, unapoendelea kusema, ngoja niishie hapo tu....na hivi una hela ama na gari,unajiambia aaah kwani nini! Nitatubu tu....mara huyu hapa....umeshavua chupi/boxa na unabaki kukodoa mimacho!!
Kibaya zaidi ukikutana na wengine ambao dhamira zao zilishakufa,basi unajikuta unapata moyo wa kufanya tena na kwahiyo unajikuta unafanya na kufanya na kufanya tena na hapo Uongo unakuja na kuwa wakili na unaanza sasa kuigiza utumishi na huku unaendelea kudungunyua! Na kama usipopata Neema kama hii, basi unaendelea kujitia moyo na kuona hayo ndio Maisha!!
Wengine wakikosa ama wakishindwa kuwapata, basi wanaishia kujichua/Punyeto(Masterbation)
Wengine hujifariji kwa kufanya "Kisses and Romance" na kusema......wala hatukufanya chochote!
Wengine hawafanyi hayo yote,lakini mara wakimwono mtu, humtafakari mpaka wakalowa, ikitokea wamekumbatiana ndio hatari zaidi, watajichafua saa hiyo na Usiku wataota tu!

Katika hili nina haya ya kukushauri
1. Mara zote unajikuta kwenye mtego ama mazingira ambayo unaona kabisa unaweza kuanguka...Usianze kuomba...kimbia...tena Kimbia sana!
2.Usikubali kuingia ama kuwa kwenye mahusiano yoyote yale ambayo yanakuharibia ama yanakuvuta mbali na Mungu wako
3.Weka mipaka ya mawasiliano na mazoea na watu wa jinsia tofauti na wewe...mfano Mida ya kuwasiliana na aina ya jumbe za kushirikishana!
5.Kama umempata mtu...fuata mchakato kwa usafi na ukishampata na kuwa kwenye Agano la Ndoa, acha kabisa mawasiliano na wale marafiki ama wale uliowatazamia zamani(ex-friends)
Na kama bado...usiseme ngoja nimalizie kabisa kabla ya Ndoa!
6.Na Mtumishi kumbuka Mungu kwanza>>>Familia>>>Kisha huduma na baadae Biashara ama kazi! Usije ukampata mwenza na bado ukaifanya huduma muhimu kuliko huyo...lazima Utimize Wajibu wako kikamilifu!
7.Chunga sana vitu ambavyo nafsi yako inakula kwa kuona na kusikia...usijiamini kupita kiasi wala usijiendekeze katika uharibifu!

Ahsante kama Umenielewa
Maadui hawa hawana Nani wala nani, aliyeoa ama aliye bado, anayechipukia na aliye maarufu....Ukifungua tu mlango, umeshaanguka!!
Watu wenye Vipaji/Ushawishi/Maarufu ama wanaonekana sana na wengi, ndio wana hatari kubwa sana maana shetani anajua akimnasa mtu kama huyo atakuwa ameabisha Ufalme kwa kiasi cha juu na kuwavunja moyo wengi!!

Ikiwa umekwama katika moja wapo katika hili, tafadhali Sema usaidiwe, Nenda kwa Mchungaji wako ama mtumishi yeyote unayemwamini ama mimi na Usaidiwe maana Ukishupaza shingo hapo,utavunjika ghafla!!
Na kama Mungu amekusaidia kuwa Salama ama akikusaidia kutoka hapo, basi Jichunge na Usimwamini mtu zaidi ya Mungu maana yeye pekee ndio atupaye nguvu za kupata Utajiri na atujaliaye kukaa Salama!!
Nimesema kwa sehemu, kwa kadri nilivyojaliwa Neema na Kumbuka hakuna awezaye kuwashinda hawa kwa nguvu zake binafsi; Kukiri Udhaifu na kuomba Mungu ndio kutakuweka salama! Nilishapiga sarakasi hapo enzi za Ujinga, na kuna wakati Nilienenda kwenye wokovu na Utumishi wa mazoea na Kweli kabisa, wakati huo sikuwahi kuwa na AMANI, FURAHA NA UTULIVU WA KWELI kama vile mwanzo nilipookoka tu, na baada ya kujua kuwa Nahitaji KUWA MKWELI, KUISHI MAISHA YA KWELI NA KUSEMA KWELI DAIMA, hata kama ni ngumu!
Achana na sarakasi, achana na mafundisho pori, achana na mbinu mbalimbali za kujipatia pesa madhabahuni...Maandiko yanasema "Wa madhabahuni hula vya madhabahuni" sasa Usitafute wala kutega nyavu madhabahuni, huo ni Uhuni!!
Fanya kazi kwa bidii, ili uachane na hayo MAISHA ya kusibiri mialiko na sadaka maana hivyo vimekufanya uwe mzembe na hata huwezi kufikiri sawasawa!!

Ninakuombea sana, Mungu akusaidie Upone na Uchomoke hapo; Hakuna ajuaye siku wala saa ya Mwana wa Adamu, ni heri ukawa tayari wakati wote, Neema ya Mungu inatosha!
Bwana akubariki, katika Jina la Yesu, Amen!

Mwalimu/Mshauri
(Dady/Uncle)
King Chavala
+255 713 883 797
lacs.project@gmail.com
👣Walk The Talk
🏹Unaruhusiwa kuwashirikisha na wengine!

Comments