CHEO NA MADARAKA YAKO KANISANI UNAVITUMIAJE?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Cheo na madaraka yako kanisani unavitumiaje?
Neno Cheo maana yake ni daraja la mtu katika kazi yake.
Daraja ni eneo la kuvukia ili uingie katika eneo jingine.
Kwenye kazi ukipandishwa cheo kimoja kwenda kingine maana yake umevuka daraja fulani na kwenda eneo jingine.
Madaraka maana yake ni uwezo wa kupanga na kufanya mambo fulani anayopewa mtu.
Cheo ni wadhifa katika utendaji.
Wadhifa ni cheo anachokuwanacho mtu.
Kuna tofauti kati ya cheo na madaraka, lakini wakati mwingine cheo huambatana na madaraka.
Kuna watu wana cheo lakini hawana madaraka na kuna watu na cheo na madaraka pia.
Kuna viongozi wengi hawajui waibu wao katika uongozi.
Kuna viongozi hawatumiii uongozi wao kwa utukufu wa MUNGU.
BWANA YESU kama kiongozi mkuu alipokua alisema kwamba amekuja kutumia na sio kutumikiwa, lakni leo viongozi wengi makanisani hutaka kutumikiwa na sio kutumika.
Lakini kuna Neno MUNGU analisema leo kuhusu wenye vyeo kanisani au wanaotarajia kupata vyeo kanisani, pia MUNGU ana Neno juu wenye madaraka kanisani na wanaotarajia kupata madaraka kanisani.
 

2 Yohana 1:9 '' Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya KRISTO, yeye hana MUNGU. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana BABA na MWANA pia.'

Biblia haikatazi watu kupanda vyeo ila inatoa angalizo kwa wanaopanda vyeo kwamba kama wataruhusu vyeo vyao kuwaondoa katika kusudi la MUNGU la injili ya KRISTO ni hatari kwao.
Inawezekana kabisa ulikuwa muumini tu wa kawaida lakini sasa umekuwa kiongozi wa kwaya, huko ni kupanda cheo.
Inawezekana kabisa ulikuwa Mzee wa kanisa na sasa umekuiwa mchungaji, huko ni kupanda cheo.
Inawezekana kabisa ulikuwa shemasi na sasa ni mzee wa kanisa, huko ni kupanda cheo.
Inawezekana kabisa ulikuwa Mchungaji na sasa umekuwa askofu, huko ni kupanda cheo.
Inawezekana kabisa ulikuwa askofu lakini sana umekuwa askofu mkuu, huko ni kupanda cheo kiuongozi katika kanisa.
Vyeo viko vingi sana kanisani.
Lakini unakitumiaje cheo chako? 
Je cheo chako unakitumia kwa manufaa ya kuuinua ufalme wa MUNGU au unakitumia cheo chako kuinua maisha yako?
Biblia inasema Apandaye cheo kisha asidumu katika fundisho la KRISTO huyo hana MUNGU na Hana YESU hata kama ni kiongozi kanisani.
Mchungaji Mzinzi Huyo hana YESU hata kama anaitwa mchungaji kanisani.
Askofu Mwizi hana YESU hata kama watu wanamheshimu kiasi gani.
Cheo chako jitahidi sana kisikuondoe katika KRISTO.
Cheo  chako hakikisha hakikuondoi katika utakatifu.
Kupanda cheo huwa kunaambatana na mambo mengi.
Kupanda cheo hupelekea kupanda hadhi pia.
Kupanda cheo hupelekea kupanda heshima pia.
Lakini naomba pia ujue kwamba licha ya hayo lakini ukweli muhimu pia ni kwamba kupanda cheo kanisani haina maana kwamba kiwango chako cha utakatifu kimeongezeka.
Hakikisha unakidhibiti cheo chako ili kisikutumie vibaya ukahama kwenye kusudi la MUNGU.
Kuna tofauti kati ya cheo kukitumia kwa kusudi la MUNGU na cheo kukutumia wewe.
Watumishi wengi hawatumii vyeo vyao kwa ajili ya injili ya KRISTO bali wao huruhusu vyeo viwatumie vibaya.
Ndio maana Kuna maaskofu kuonana nao hadi uandike barua ya maombi. Kama Askofu yuko busy ni sawa lakini sidhani kama hadi kanisa linaiga uongozi wa kidunia kwa kutaka tu watume maombi kwa barua ndipo watuone, huko ni cheo kukutumia vibaya.
Cheo hakitakiwi kikutumie bali wewe ndio ukitumie cheo kwa utukufu wa MUNGU.
Cheo chako kanisani kisikufanye uache kuhubiri injili ya KRISTO ya utakatifu na sasa unahubiri tu upendo, na unahubiri upendo kwa sababu umekosana na aina fulani ya watu.
Cheo chako kitumie kuwafikia watu wengi zaidi kwa injili na sio kupanda cheo kwako ndiko kukuondoa katika kuwafikia watu kwa injili.
 Uongozi wa kanisani ni lazima uwe tofauti na uongozi wa duniani.
Katika uongozi wa duniani kuna vitu hutumika kama vyeo katika jamii.
Utajiri wa mtu ni cheo moja kwa moja katika jamii.
Utajiri unaweza kukufanya uonekane una cheo, hayo ni mambo ya kidunia.
Tajiri anaweza kwenda hata ikulu muda wowote katika baadhi ya mataifa au makampuni makubwa japokuwa hana cheo ila utajiri tu.
Maskini anaweza asifike huko ila tajiri kwa sababu ya utajiri wake anaweza kufika.
Elimu kubwa inaweza kumfanya mtu aonekane ana cheo hata kama hana.
Wasomi wanaweza hata wakaenda popote katika maofisi ya viongozi wakubwa katika jamii kwa sababu tu ya elimu zao.
Maskini au mtu asiyesoma ni ngumu sana ghafla tu kuruhusiwa kwenda ofisi kubwa.Ndiposa Biblia inasema ; 
'' Lakini ndugu asiye na cheo na afurahi kwa kuwa ametukuzwa; bali tajiri kwa kuwa ameshushwa; kwa maana kama ua la majani atatoweka. Maana jua huchomoza kwa hari, huyakausha majani; ua lake huanguka, uzuri wa umbo lake hupotea; vivyo hivyo naye tajiri atanyauka katika njia zake.-Yakobo 1:9-11''

 Jambo kubwa na muhimu ni kwamba, Je cheo chako unakitumia au kinakutumia?
Je unakitumia cheo chako kwa utukufu wa MUNGU au unatumika kipepo katika cheo chako?
Kuna watumishi hata madaraka yao hawayajui ndio maana migongano makanisani ni mingi. Mfano mzee wa kanisa anatakiwa ajue mipaka ya madaraka yake ili asikosane na mchungaji wake, mzee wa kanisa hawezi kutangaza kuwatenga baadhi ya waumini maana hiyo sio kazi yake na iko nje ya madaraka yake, huo ni mfano tu mmoja katika ile mifano mingi ya watu wenye vyeo na madaraka katika kanisa kutokujua madaraka yao na mipaka ya madaraka yao.
Kama ni jambo la Askofu mkuu tunatakiwa tumwachie yeye na sio sisi ndio tunaliamua jambo hilo.
Shemasi hawezi kuitisha kikao cha viongozi wote wa kanisa bila kuruhusiwa na Mchungaji.
makundi makundi katika makanisa chanzo chake ni viongozi wa kanisa kuhama katika kusudi la MUNGU na kutokujua mipaka yao ya madaraka na vyeo.
Nabii Samweli yeye aliamua kuwasomea waisraeli madaraka ya mfalme ili wajue.

1 Samweli  10:25 '' Kisha Samweli aliwaambia watu madaraka ya ufalme, akayaandika katika kitabu, akakiweka mbele za Bwana. Samweli akawaruhusu watu wote, waende kila mtu nyumbani kwake.''

Inatakiwa pia waumini wajue ukomo wa madaraka ya viongozi wao, ili kiongozi akiamua  kwenda nje ya Neno basi asaidiwe  ili kuondoa mang'ung'uko katika nyumba ya MUNGU.
Cheo chako kitumie kwa utukufu wa MUNGU.
Kupewa uenyekiti wa kwaya sio ndio iwe nafasi yako ya kuzini na wanakwaya, kuna ziwa la moto kwa wazinzi ndugu.
Kuwa kwako mhubiri wa sunday school sio ndio iwe nafasi yako ya kumsema vibaya mchungaji wako mbele ya waumini, wewe hubiri injili na sio majungu.
Kuwa kwako mama mchungaji ni cheo lakini jitahidi sana usitumie nafasi yako hiyo kuwanyanyasa wamama, usitumie nafasi yako hiyo kuwapangia mabinti vijana wa kuwaoa.
Kuwa kwako askofu kusiwe chanzo cha kuharibika kwa kanisa.
Tumia cheo chako vizuri ndugu.
Uongozi wako uelekeze kwenye Neno la MUNGU na sio vinginevyo.
Kuna viongozi wengi kanisani lakini wote MUNGU anawapenda kama wanatenda vizuri katika vyeo na madaraka yao.
 
2 Timotheo 2:19-22 '' Lakini msingi wa MUNGU ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, BWANA awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la BWANA na auache uovu. Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina.
 Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho BWANA, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema. Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao BWANA kwa moyo safi. ''


 Ndugu uliyesoma ujumbe huu ubarikiwe sana.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments