JINSI YA KUITUNZA NA KUILINDA NDOA YAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ndoa ni makubaliano rasmi matakatifu  kati ya mwanaume  mmoja na mwanamke mmoja kuishi pamoja kama mume na mke na kuthibitishwa na kanisa pamoja na wazazi wa pande zote mbili.
Ndoa ni taasisi nyeti sana kiasi kwamba inatakiwa kulindwa sana na wahusika.Kuna ndugu mmoja aliwahi kuniuliza maswali mawili;
Swali la kwanza aliniuliza; ''Mchungaji Peter Mabula, tangu uingie katika ndoa yako hamjawahi kupigana na mke wako au kutukanana?'' Nikamjibu hatujawahi hata siku moja na hatutegemei kufanya hivyo hata siku moja.
Akauliza swali ya pili kwamba, ''Mchungaji, Katika magumu kwenye ndoa yenu mfano kutokuwa na pesa kwa wakati huo haukutokea mgogoro katika yako na mke wako?'' Nikamjibu kwamba haujawahi kutokea mgogoro wowote na ndoa ni paradiso ndogo hakika. Ndugu yule alihuzunika sana na kuniambia kwamba mimi nina bahati lakini yeye katika ndoa yake hana hiyo bahati kama yangu. Nikamwambia kwamba wala sio bahati ila kuishi maisha ya kumcha MUNGU na Kumtegemea na kumtumikia huleta ushindi.
Sijui kwa upande wako ndugu yangu unayesoma somo hili, una maswali kama hayo au wewe unayo maswali sanba zaidi kwa sababu ya matatizo katika ndoa yako.
Nakuomba ijue ndoa, jua misingi mizuri ya ndoa, mjue na kumfuata aliyeiumba ndoa, iheshimu ndoa yako na ijali ndoa yako maana ni yako peke yako na mwenzi wako tu.

Mwanzo 2:24 ''Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.''
 
Kwa ambaye uko katika ndoa ilinde ndoa yako kwa kuiheshimu na kumuomba MUNGU, ielekeze ndoa yako katika maisha ya kumcha MUNGU kupitia Wokovu wa YESU KRISTO.
Wokovu huambatana na utakatifu wa kweli.
Wokovu huambatana na kuongozwa na Neno la MUNGU, Kwa kulitii Neno la MUNGU na kuliishi.

  Waefeso 6:14-17 ''Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa ROHO ambao ni neno la MUNGU;''


Wanandoa ni muhimu sana wakailinda ndoa yako kwa kuwa wakweli, kama uongo utatawala ndoa yenu lazima mashaka pia na kutokuaminiana vitatawala.
Wanandoa wanatakiwa kuishi maisha ya haki, maisha ya haki yanaongozwa na utakatifu wa kweli.
Peter & Scholar Mabula
Kuna wana ndoa hufunga ndoa kanisani lakini baada ya muda huachana na kanisa, hujitenga na fundisho la Neno la MUNGU ndio maana matatizo katika ndoa huanza kutokea. Kwa haraka haraka kwa wanandoa hao tunaweza kusema walikuwepo kanisa ili kufanikisha kufunga ndoa na sasa wako duniani, hiyo ni mbaya sana.
Mtu haokoki ili akapae tu mke au mume huko kanisani bali mtu anaokoka ili aende uzima wa milele.
Mtu hampokei YESU kwa sababu ya ndoa ila kwa sababu ya ufalme wa MUNGU.
Huwa kuna mishale ya shetani ambayo hutumwa katika ndoa na mishale hiyo wanaoweza kuidhibiti ni wanandoa walio thabiti katika KRISTO na niwaombaji.
Magomvu unaweza kuwa ni mshale wa shetani katika ndoa yenu.
Viburi na kutokuwa na hamu na mwezi wako vinaweza kuwa ni mishale ya shetani katika ndoa yako.
Kushinda kutimiza haki zote za ndoa kwa mwenzi wako inaweza kuwa ni mshale wa shetani uliorushwa katika ndoa yako.
Ili kuitoa mishale hiyo ya shetani na mawakala zake unatakiwa uwe karibu sana na KRISTO na uwe ni muombaji.
Ukiwa mbali na KRISTO hata uwezo wa kuomba vizuri hutakuwa nao ndio maana nasema kwamba ni hatari sana wanandoa kujitenga na kanisa kwa sababu tu ya ndoa yao.
Ndugu, ilinde ndoa yako na itunze sana huku ukimhusisha MUNGU ambaye ndiye aliyeiumba ndoa na ndiye aliyeianzisha ndoa kwa watu wake ili watu hao waiheshimu ndoa na waishi pamoja kwa kusaidiania na kushauriana katika mambo mema ili wasiukose uzima wa milele aliouandaa MUNGU kupitia YESU KRISTO.
 
Waebrania 13:4-5 ''Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.''

Kwa ambaye hujaingia katika ndoa ni muhimu sana ukafundishwa mafundisho ya  ndoa kanisani maana kuna vitu vingi sana unahitaji kuvijua ili kuifanya ndoa yako iwe kielelezo chema kwa kanisa na jamii.
Watu Wengi Huingia Katika Ndoa Bila Maandalizi Muhimu. Maandalizi Sio Suti Na Shela Tu, Maandalizi Sio Vyombo Na Mabegi Tu. Maandalizi Mazuri Ni Ya Kiroho Ndipo Maandalizi Ya Kimwili Yanafuata. Usidhani Kwamba Ukishindwa Kumcha MUNGU Kabla Hujaoa Au Kuolewa Eti Utaweza Kumcha MUNGU Wakati Wa Ndoa, ni ngumu sana hiyo.
 Ni Muhimu Sana Kujifunza Kumcha MUNGU Kama Sehemu Yako Muhimu Ya Maandalizi Yako Ya Kuingia Kwenye Ndoa Ndipo Itakuwa Rahisi Kwako Kumcha MUNGU Ukiwa Kwenye Ndoa. Kuna Watu Walisema Siku Wakioa Ndipo Wataacha Pombe Lakini Matokeo Yake Kwenye Ndoa Ndipo Na Pombe Waliongeza Badala Ya Kuacha. Kuna Waliodhani Kwamba Wataacha Uasherati Wakiingia Katika Ndoa Lakini Walisahau Kwamba Uasherati Ni roho Ya Shetani Ambayo Haiondoki Kwa Sababu Umeingia Kwenye Ndoa, Bali Inaondoka Kwa Sababu Umeamua Kumcha MUNGU Na Kuliishi Neno La MUNGU.

Yoshua 24:14 '' Basi sasa mcheni BWANA, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye BWANA.'

Wandoa ni muhimusana kumcha MUNGU katika mpango wake wa wokovu.
Kabla hamjampokea BWANA YESU mlikuwa kwa shetani au misri kwa jina jingine lakini baada ya kumpokea BWANA YESU mumekuwa wateule wa MUNGU mnaotakiwa kumcha MUNGU na Kumtumikia. Kumtumikia MUNGU sio lazima uwe Mchungaji au mhubiri, Kibiblia kumtumikia MUNGU ni pamoja na kuishi kwa kulitii Neno la MUNGU.
Kumtumikia MUNGU ni kuishi maisha matakatifu ayatayo MUNGU.
Kama utamtumikia MUNGU kwa wewe kuishi maisha matakatifu hakika adui hatapata nafasi katika ndoa yenu. Maana shetani akipanga awakute mko bar hatawaona maana nyie muda huo mtakuwa mko kwenye maombi au kwenye semina za Neno la MUNGU.
Ni Muhimu sana kumcha MUNGU na kumtumikia.

Zaburi 34:9 '' Mcheni BWANA, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.''

Kuna makosa mengi ambayo baadhi ya wanandoa hukosea katika ndoa zao na kuibua tatizo.
Kuna wengine japokuwa hawatendi dhambi ila ni kama hawajitambui kama wako katika ndoa.
Wewe Mwanandoa, Je Unajua Kwamba Uko Katika Ndoa?. Unamtajataja Mchumba Wako Wa Zamani Kwa Mkeo/mmeo Wakati Sasa Uko Katika Ndoa Ndio Maana Migogoro Katika Ndoa Yako Badala Ya Kupungua Ndio Inaongezeka. 
Hiyo Inaharibu Ndoa Yako Na Kuleta Migogoro. 
Ni Kweli Uliwahi Kuwa Na Mchumba Zamani Lakini Mkaachana Na Sasa Umeolewa/kuoa Kwingine Hivyo Mtu Wa Muhimu Kwako Sasa Ni Mkeo/mmeo Na Sio Yule Uliyewahi Kuchumbiana Nae. Ni Mbaya Sana Kila Muda Unamtajataja Mchumba Wa Zamani Ambaye Kwa Sasa Hakuhusu Tena, Sio Kila Mara Unamsifia Tu Uliyeachana Nae Zamani Ambaye Kwa Sasa Hakuhusu Tena Kwa Lolote Lile. Kama Angekuwa Muhimu Kwako Ungemuoa Huyo Au Ungeolewa Na Huyo Lakini Kwa Sababu Hana Sifa Za Kuwa Mwenzi Wako Wa Ndoa Ndio Maana Hukumuoa/hakukuoa. Ndugu Heshimu Sana Ndoa Yako. Mweshimu Mumeo Na Wewe Mume Mweshimu Mkeo.
Itunze ndoa yako na dumisha utakatifu huku ukitumia hekima na maarifa ya kiMUNGU.
 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments