KAZI TATU ZA VIJANA KANISANI

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
BWANA YESU atukuzwe mtu wa MUNGU.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Maisha Ya Ujana Yana Mambo Mengi Sana, Mengine Mabaya Na Mengine Mazuri. Wakati Wa Ujana Ndio Wakati Wa Kuchagua Mfumo Wako Wa Kuishi.
 Kijana; Uchaguzi Wako Wa Leo Ndio Picha Yako Halisi Ya Baadae. Ukichagua Mema Leo Utapata Baraka Baadae. Ukimchagua BWANA YESU Leo Utavuna Uzima Duniani Kisha Uzima Wa Milele. 
 Kumtegemea KRISTO Ni Baraka Na Kutokumtegemea KRISTO Ni Hasara Kuu. Chagua Kumtegemea KRISTO Maana Ni Pekee Anayetoa Uzima Wa Milele.
Vijana katika kanisa ni wa muhimu sana.
Vijana katika kanisa kama wakijitambua hakika kanisa hilo litakuwa baraka sana maana vijana ndio wenye nguvu za kufanya kazi ya MUNGU kwa urahisi zaidi.
Biblia inasema kwamba vijana wamkumbuke muumba wao wakati wa ujana wao, maana yake wamtumikie muumba waowakati wa ujana wao maana wakiwa wazee itakuwa ngumu kutumika kwa viwango vizuri.

Mhubiri 12:1-2 '' Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo. Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua; ''

Kibiblia kumtumikia MUNGU iko katika makundi mawili.
-Kumtumikia MUNGU ni kumwabudu na kulitii Neno lake.
-Kumtumikia MUNGU ni kufanya kazi yake.

Kijana anatakiwa kutumiza utumishi huo wote kwa MUNGU.
Leo nimekuandalia kazi 3 za kijana kanisani.


1.  Kazi ya kwanza ya kijana kanisani ni  Kushuhudia Wengine Wokovu Wa KRISTO Na kumtumikia KRISTO. 
 Kama Ulikuwa Hujui Naomba Leo Ujue Kwamba Kazi Ya Kwanza Ya Mkristo Yeyote akiwemo kijana Ni Kuleta Watu Kwa KRISTO.

Marko 16:15-16 ''Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.'' 

Kazi ya kuwaendea watu wote ili waje kwa YESU ni ya kanisa zima wakiwemo vijana.
Kwa sababu vijana ndio wenye nguvu zaidi maana hawajazeeka basi hao ndio wanatakiwa kuongeza juhudi zaidi katika kuwashuhudia mataifa habari njema za ufalme wa MUNGU zilizo pekee katika KRISTO YESU.
 Biblia inaendelea kusema kwamba;
 ''Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.-Mathayo 10:7-8''
MUNGU amekuokoa wewe kijana uli uwe njia ya wengine kuja kwa MUNGU, Ukinyamaza wewe kijana kuwaita watu kwa YESU jua tu kwamba unasababisha watu wengi sana waende jehanamu.
Biblia inaendea kukuagiza kwamba;

 ''Haleluya. Mshukuruni BWANA,liitieni jina ,Wajulisheni watu matendo yake-Zaburi 105:1'' 

Usipowajulisha wewe ndugu zangu kuhusu wokovu wa MUNGU hakika utakuwa husimani katika nafasi yako kama mteule wa KRISTO.
MUNGU anakutaka wewe ndugu uwashuhudie watu wote habari za wokovu wa KRISTO wa injili inayookoa.
Vijana wa zamani walifanya kazi hiyo ndio maana mimi na wewe tukafikiwa na neema ya MUNGU ya wokovu.
Injili ni kama kijiti ambacho ukikabidhiwa na wewe unatakiwa umkabidhi mtu mwingine ili wote muwe washindi, usikubali kushinda peke yako tu.
MUNGU anakuagiza piga kelele wala usiache ili tu tuwarudisha wanadamu katika mpango wa uzima juu yao.
Isaya 58:1 '' Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao.''

 Usipokuwepo Kwenye Eneo Lako Pengo Lako Litaonekana Hivyo Una Wajibu Wa Kuwepo Siku Zote Kwenye Eneo Lako La Utumishi Kwa MUNGU. Umeitwa Kumtumika KRISTO Hivyo Mtumikia Siku Zote Sio Siku Fulani Tu. Je Umekaria Kipawa Chako Au Unakitumia Kwa Utukufu Wa MUNGU? Kuna Watu Wakiona Wenzao Wanaimba Kazi Yao Inakuwa Tu Kusema "ningekuwa Mimi Ningeimba Vizuri Zaidi.". Anajua Anaweza Kuimba Vizuri Lakini Hajiungi Na Kwaya Au Praise & Worship Team Na Alichobakiza Ni Majungu Tu. Unakuta Mtu Akiwaona Wenzake Wanashuhudia Mitaani Zake Yeye Ni Kujisifu Na Kuwakatisha Tamaa Wanaoshuhudia Huku Yeye Hajawahi Kumshuhudia Mtu Hata Mmoja Ingawa Anaweza Kabisa Kushuhudia Watu Na Wakaokoka.
 Ndugu Mtumikie MUNGU Katika KRISTO Kwa Bidii Sana. Unao Muda Mchache Wa Kutumika Hivyo Tumika Kwa Bidii Sana Na Uaminifu.
Yeremia 48:10a '' Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya BWANA kwa ulegevu; ''

 MUNGU Ndiye Hutukamilisha Lakini Juhudi Yako Na Ukamilifu Katika Utumishi Nyumbani Mwa MUNGU Humfanya MUNGU Atukamilishe Mapema. Kumtumikia KRISTO Kuna Faida Nyingi Sana. 
 Wafilipi 4:8  ''Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.''

2. Kazi ya pili ya kijana wa kanisani ni  Kuisha Maisha Matakatifu Siku Zote.
1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''
 
Kuishi maisha matakatifu ni wajibu wa kila mkristo akiwemo na kijana.
Kwa kila kijana anayeutaka uzima wa milele basi hakika ni lazima aishi maisha matakatifu ya wokovu wa KRISTO.
Kuishi maisha matakatifu ni kazi ya kila mtu wa kanisani akiwemo na kijana.
Kijana anatakiwa aufanye utakatifu kuwa ni jambo la lazima na sio hiari maana pasipo na utakatifu hakuna uzima wa milele.

 Mathayo 5:14-16 '' Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze BABA yenu aliye mbinguni.''

Watu wanatakiwa waone matendo mema kwako kijana.
Kama unaishi maisha ya dhambi ni muhimu sana kuacha.
Kila alitajaye jina la BWANA na auache uovu, usikubali kumchanganya YESU na uovu bali timiza utakatfu autakao yeye YESU KRISTO Mwkozi wako.
Acha kupiga punyeto na kujichua.
Acha uasherati na uongo.
Kataa dhambi zote, zipinge dhambi zote, ziepuke dhambi zote, jitenge na dhambi zote, zikimbie dhambi zote na usitende dhambi tena.

 2 Timotheo 2:19 '' Lakini msingi wa MUNGU ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, BWANA awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la BWANA na auache uovu.''

Ujana ni zawadi kutoka kwa MUNGU.
MUNGU anajua umuhimu wa Kijana na shetani anajua umuhimu wake pia.
Ili kuleta mafanikio na matokeo ya haraka Kijana ana uwezo mkubwa sana.
Kijana ni silaha nyepesi mno na hatari sana.
Ndugu, utumie ujana wako kumtumikia MUNGU na kumtukuza yeye bila kusahau kumcha yeye peke yake katika jina la YESU KRISTO.

 


 3.  Kazi ya tatu ya kijana kanisani ni Kumtegemeza Mchungaji wake.
Mchungaji wako ni wa muhimu sana kwako, ni baba yako wa kiroho, anakufundisha kuishi maisha ya kumpendeza MUNGU, Hakika huyo anakutakia mema sana maana anakuelekeza kwenye uzima wa milele.

Mathayo 10:8-10 ''Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana MTENDA KAZI ASTAHILI POSHO LAKE.'' 

Wachungaji MUNGU amewaamuru waache kazi zao nzuri ambazo zingewaingizia pesa lakini amewataka wawe wachungaji, ulishajiuliza ni kwanini mchungaji wako aliacha kazi ili tu amtumikie MUNGU katika uchungaji? je atakula nini wakati hafanyi kazi ya mshahara? Je familia yake itaishije wakati yeye hana kazi ya kumpatia mshahara?
Je watoto wake watasomaje wakati baba yao ambaye ni mchungaji hana kipato chochote?
Ndugu, Nakuomba ujue kwamba MUNGU amekuandaa wewe ili umtegemeze mtumishi wake na yeye MUNGU atakubariki wewe.

Luka 10:7-9 '' Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, MKILA NA KUNYWA VYA KWAO; MAANA , MTENDA KAZI AMESTAHILI KUPEWA UJIRA WAKE. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; waponyeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia.'' 

Kuna wachungaji MUNGU aliwaita ili wamtumikie wakakataa maana kazi zao serikalini walikuwa wanapata mishahara mikubwa sana. Lakini kwa sababu ni MUNGU amesema walitii na kuacha kazi na sasa ni wachungaji huku wakiwa hawana mshahara bali wanategemea sadaka tu na zaka  ambazo na zenyewe ni chache sana sana na zina kazi nyingi kanisani, na ajabu wazee wa kanisa na baadhi ya waumini kila siku wanakaa vikao ili kumsema mchungaji kwamba anakula hela zao bure.
Ndugu, kuna watu wengi wamewahi kuchuma laana kwa sababu ya kuwalalamikia wachungaji , kuna watu hata wamewahi kufa kifo cha mapema kwa sababu tu ya manung'uniko yao kwa wachungaji wao. Ni kweli kuna makanisa makubwa ambayo sadaka zake tu na zaka ni mamilioni. Kwenye kanisa kama hilo mnaweza  kumshauri mchungaji ili muwe mnampatia kiasi fulani cha pesa kutoka katika sadaka na zaka ili kiasi kinachobaki mkitumie kufungulia makanisa mengine au kujenga kanisa, ili isiwe jambo dogo tu kama kununua betri za mic basi hadi kanisa zima litangaziwe kuchanga. Lakini kuna makanisa  ambayo zaka ya mwezi mzima kwa waumini wote hata laki 2 haifiki, sadaka kila wiki haivuki elfu 20 hivyo kwa mwezi sadaka zote ni kama elfu 80. Kanisa kama hilo huwa hamtegemezi mchungaji wao na mchungaji anaishi katika mazingira magumu. Je yeye ataishije? maana akiacha kanisa ili afanye kazi za serikalini MUNGU anampiga. Mchungaji kama huyo akitumia sadaka hiyo ndogo kwa ajili ya chakula cha familia yake, je anakosea? hakika hakosei na unaweza kumlaumu na kumsema vibaya kumbe unabeba laana tu maana wewe MUNGU amekuweka umtegemeze Mchungaji wako lakini wewe umeshindwa.
Mchungaji wangu mmoja yeye alipoona kanisa limemsahau na zaka ni kidogo sana aliliacha kanisa ili akafanye kazi ya kuajiriwa. MUNGU alimpiga na akarudi kwa machozi katika kanisa. Ndugu zangu, kanisa linatakiwa limtegemeze mchungaji wao. Vijana kanisani wanatakiwa wawe mstari wa mbele kumtegemeza mchungaji wao.

YESU Akitaka Umtumikie Utamtumikia Tu. Huwezi Kumfanyia BWANA YESU Kiburi Ukafanikiwa, Ndio maana wachungaji wanamtumikia.
Kuna kanisa fulani wao wamemuacha Mchungaji wao na hali ya mchungaji kiuchumi sio nzuri kabisa, lakini jambo la ajabu watu wa kutoka nje ya kanisa huwa wanamwendea mchungaji huyo na akiweka mikono juu yao na kuwaombea hao hubarikiwa sana lakini watu wa kanisani hamna kitu. Hapo MUNGU analifundisha kanisa juu ya kumtegemeza Mchungaji wao.
MUNGU alipanga mama mmoja amtegemeze mtumishi wake Eliya, Yule mama alivyozingatia alibarikiwa. Na Hata leo MUNGU ameagiza kanisa limtegemeze Mchungaji wao.
MUNGU akamwambia Mtumishi wake kwamba;
 ''Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe. Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama BWANA, MUNGU wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa BWANA, MUNGU wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa kinywa cha Eliya.-1 Wafalme 17:9-16 ''

Wapo wateule wengi wa MUNGU waliojua wajibu wao kwa wachungaji wao na wakabarikiwa, Hebu kama una Nafasi soma 2 Wafalme 4:5-17 Uone jinsi Mama Mshunemu alivyotimiza wajibu wake kwa mtumishi wa MUNGU Elisha na akabarikiwa.
Ni muhimu sana kanisa kuwategemeza wachungaji wao.
Mkimtegemeza Mchungaji wenu vizuri mtamfanya awe busy kuwaombea nini lakini kama hammtegemezi vizuri basi hakika mchungaji wenu atakuwa busy kuombea jinsi atakavyopata chakula kwa ajili ya familia yake na watoto wake.
 Tumeitwa Ili Tumtumikie MUNGU Bila Kujali Umri Wetu. Ndugu, Tumika Kwa BWANA YESU Utafanya Vyema Sana.
  MUNGU Amekuita Katika Utumishi Hivyo Hivyo Ulivyo, Jitambue Na Timiza Wito Wako Haijalishi Wanaokupinga Ni Watu Makumi Elfu.

 Mfano Wa Mtu Aliyeokolewa Na Kutimiza Wito Wake Ni Mtume Petro. Mtume Petro Baada Ya Kuokolewa Na BWANA YESU Hakubaki Na Lile Tumaini Tu Bali Alitembea Katika Utumishi Hadi Watu Wengi Wakwamwamini BWANA YESU Kutokana Na Utumishi Wa Petro Angalia Mfano Matendo 9:32-35

Ndugu yangu nakuomba fanya kazi hizo 3 za kijana katika kanisa la MUNGU, utakuwa unafanya vyema sana na njia yako itaitwa heri na utabarikiwa. 
 Wakolosai 3:1-4 ''Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na KRISTO, yatafuteni yaliyo juu KRISTO aliko, ameketi mkono wa kuume wa MUNGU.  Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na KRISTO katika MUNGU. KRISTO atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.''

 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments