KOMBOA LANGO LA MUDA WAKO ILI UPATE ULICHOPOTEZA

Na Mwl Christopher Mwakasege
UTANGULIZI
Muda ni miongoni mwa vipengele vya Mungu ambavyo anakusudia kila mwanadamu avijue ili aweze kuenenda kama Mungu anavyotaka.

Lengo la somo hili ni ili ujue sababu ya Mungu katika Roho Mtakatifu akuongoze kuenenda na kuomba juu ya muda kama Mungu alivyokusudia.

Waefeso 5:15-17
‘’ Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; MKIUKOMBOA WAKATI KWA MAANA ZAMANI HIZI NI ZA UOVU. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana’’.

Mistari hii ina mambo mengi sana ambayo tutakwenda nayo kwa siku 8. Na Msisitizo upo kwenye mstari wa 16 Yaani MKIUKOMBOA WAKATI KWA MAANA ZAMANI HIZI NI ZA UOVU

Huu mstari umebeba mambo mengi sana na mazuri.

NATAKA KUKUWEKEA MSINGI WA MAMBO 7 YALIYO MBELE NA HAYA YATAKUPA KUTAFAKARI KILA KIPENGELE

_’’ Neno la Mungu lisipojibu maswali ya wanadamu ya kila siku linapoteza thamani ya neno kuwa kiongozi, kioo, taa na nuru kwa mtu_ na pia
‘’Neno la Mungu lisilo ambatana na na uwepo wa Mungu ni rahisi sana kuingiliwa na maneno mengine na si rahisi kujua kama tayari limeingiliwa’’

Biblia inasema
Marko 16:20 Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, NA KULITHIBITISHA LILE NENO KWA ISHARA ZILIZOFUATANA NALO

Uwepo wa Mungu ukiwepo kwenye neno la Mungu, Mungu hupata nafasi ya kulithibisha neno lake na kumzuia shetani asipate nafasi ya kuweka maneno yake.

ZINGATIA
Kwa mtu yeyote anayefundisha neno la Bwana na uhusiano wake na Mungu haupo sawa sawa na akiendelea kufundisha na watu wakalifurahia hilo neno uwe na uhakika kuwa baada ya muda atapoteza thamani ya mafundisho yake kwa sababu uwepo wa Mungu wa kuthibitisha maneno yake haupo nae, na ataishia kutafuta na kuleta neno la kuwafurahisha watu.

Ni muhimu sana kuchunga jambo hili, ukiwa unafundisha neno la Mungu hakikisha uhusiano wako na Mungu uko vizuri na usiende kwa mkumbo.

Somo hili ji jipya sana kwa watu wengi, lakini Mungu akusaidie kujua kuwa anasema na wewe wakati huu.

MAMBO SABA YA KUZINGATIA

1. Kuna wakati unaohitajika kwa ajili ya kuishi kwa mafanikio katika wakati huu uitwao *Zamani hizi* ila wakati huo umetekwa. Angalia vizuri *Waefeso 5:15-17 hasa angalia mstari wa 17 ‘’ *Kwa sababu hiyo msiwe wajinga*, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana’’
Ukiwa unafundisha somo kwa jicho la Mwalimu si jambo la kawaida kuona sentensi inaanza neno la *kwa sababu* yaani hata katika kiingereza huwezi kuanza na neno *because* . Ila kwenye biblia inawezekana, kwa hiyo ukifuatilia vizuri ina maana thamani ya mstari wa 17 inatokana na mstari wa 16. Kwa hiyo kuna wakati tunatakiwa kuwa nao ila sasa hatuna.

*2* Ile kwamba wakati huo unahitaji kukombolewa ina maana una thamani kwa aliyeuteka na kwako pia.

*3* Kuukomboa wakati maana yake ni kuwa anayeukomboa wakati akubali kuingia gharama katika kuutoa wakati huko ulikotekwa ili uweze kutumika ipasavyo na aliyeukomboa.

Neno ukombozi linatokana na neno la kiingereza redemption likiwa na maana ya kurudisha kitu cha thamani.
Na ukweli ni kuwa huwezi kukomboa kitu kisichokuwa na thamani kwako na hakikuwa chako . Mfano Kama unakomboa ardhi ina maana ina thamani kwa mtu aliyekuwa ameiteka na wewe ili uikomboe ni lazima uingie gharama ya kuikomboa.

Kwa mfano Mungu alipokuwa analikomboa taifa la Israel kutok taifa la Misri ina maana ilikuwa na thamani kwake kuliko hasara ya kuliacha liendelee kubaki utumwani. Kwa hiyo thamani ya mwanadamu kwa Mungu ni sawa na uhai wa Yesu na ndio maana Yesu alikufa ili aweze kutukomboa.

Neno ukombozi katika biblia halijataja vitu vingi sana ila miongoni mwa vilivyotajwa ni muda, Roho na ardhi/nchi

4. Ikiwa wakati unahitajika ili mtu aweze kuishi wakati huu kwa hekima na katika mapenzi ya Mungu ina maana wakati unaweza *kubeba aina ya maisha na wakati huo huo unapitisha aina ya maisha kwa watu. Waefeso 5:15-17*

‘’Soma tena hiyo mistari, na Biblia inasema kabisa kuwa kwanini muda ukombolewe ni kuwa ili tuweze kwenda kwa zamani hizi ina maana kuna muda ambao una hekima ya kutembea katika zamani hizi na ndio maana tunataka ukombolewe ili tuulete kwenye maisha haya ya kwetu na utupitishe kwenye mapenzi ya Mungu na utumike kupitisha maisha mazuri kwetu.

5. Aliye na mamlaka juu ya muda/wakati anakuwa pia na mamlaka juu ya maisha ya kila kinachohusika na muda huo.

6. Aliyeteka muda wako asingetaka utembee kwa jinsi ya kiroho ya kuwa muda wako umetekwa na kwa hiyo ndiyo hali iliyosababisha uwe na maisha uliyonayo.

Ukitaka kuishi maisha yaliyo ndani ya muda Fulani hakikisha unashughulika na muda na sio maisha maana ukicontorl muda unacontrol maisha.

Matendo ya mitume 17:26 ‘’ Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea
NYAKATI ALIZOZIAMURU TANGU ZAMANI*, na mipaka ya makazi yao;

Mungu hakumuumba mwanadamu kabla hajaweka majira na nyakati kwa hiyo muda kwa Mungu ni muhimu sana. Na katika *Mwanzo 1:1 Hapo mwanzo Mungu aliumba….*
Ina maana Mungu anaishi kwenye hali ya umilele yaani hafungwi na muda. Kwa hiyo biblia inaposema hapo mwanzo ina maana Mungu aliumba mwanzo ili aweke majira na nyakati.

Hivyo basi kuna uhusiano mkubwa sana kati ya muda, mbingu na ardhi. Ukisoma *1 Nyakati 12:32 Wana wa Isakari walijua majira na nini cha kufanya katika hayo majira na wao ndio walikuwa viongozi.*

*Yohana 2:1-4 Yesu alisema mama wakati wangu bado,* Yesu aliujua wakati wake kwa hiyo hakufanya jambo lolote nje ya muda yaani alikuwa anakwenda na muda.

Kwa mfano kama wewe umezaliwa Tanzania mkoa wa Arusha, ina maana kuna muda wa kwako, muda wa Arusha na Muda wa Tanzania.

Muda unatakwa uwe sawa, ila baada ya dhambi kuingia ilivuruga kabisa utaratibu wa Mungu na unakuta muda wa mtu na mkoa wake na nchi ziko tofauti.
*Kuna baadhi ya mikoa ukienda unajiuliza hivi na huku ni Tanzania au sio maana unakuta watu wanaishi maisha ya mwaka 70 wakati sasa ni 2016. Na ukiwauliza leo ni tarehe ngapi watakupa tarehe sawa kabisa na Dar es Salaam ila hali zao za maisha ziko tofauti kabisa.*

Muda ndio umeficha aina ya maisha na vitu ambavyo Mungu anavifanya na ukijua kwenda na muda utafaidika sana hapa duniani. Ndio maana Yesu aliwashangaa sana Mafarisayo na waandishi walipokuwa wanataka kujua ishara kuhusu masihi na walishindwa kusoma majira na nyakati za Mungu.

Hili si kwao tu maana watu wengi sana wana saa ila hawana muda, mara utasikia kuwa ngoja nipoteze muda kidogo hapa, ukiona una hali hiyo ujue muda wako umebanwa.

Na jiulize ukiwa unafanya kazi huwa unafaidika na muda huo, je mwajiri huwa anafaidika na muda huo? Na serikali inafaidika na muda huo? Na ukiona muda wako umeibiwa au umepotea rudi tu kwa Bwana ili akurudishie ile miaka iliyoliwa na nzige. Na huwezi omba Mungu akurudishie miaka iliyoliwa na nzige wakati hujui kama muda wako umeliwa.

Yesu alipoulilia mji yaani Yerusalemu alisema laiti ungejua muda wa kujiriwa kwake lakini sasa umefichika usionekane, na usipojua muda wa kujiriwa kwako ni vigumu sana kuweza kujiandaa na hatua za mbele na kujipanga na gharama zilizopo ambazo zitabadili maisha yako jumla kabisa.

Wana wa Israel hawakujua muda wao kuwa unakwenda kubadilika baada ya mzee Yusufu kufariki na akatokea Farao asiyemjua Yusufu kabisa. *Na dhiki ikawajia na iliwatesa sana.* Ukitaka kufupisha dhiki hauna haja ya kuanza kupamba na dhiki bali shughulika na muda ulioleta hiyo dhiki. Na usipokomboa muda wako ina maana utapoteza vyote vilivyomo ndani ya huo muda.

Yesu ni Alpha na Omega lakini yeye yupo kwenye hali ya umilele.

Amekuwa Alpha na Omega kwa sababu ili aweze kutusaidia kuhusu masuala ya muda.

Mungu akusaidie kujua na akupe macho ya Rohoni kuweza kuona hili jambo.

MUNGUAKUBARIKI SANA
 

Comments