KWANINI MUNGU NI BABA?

Na Mtumishi Dr Frank P. Seth

Baba hawi baba bila UHUSIANO. Mungu anachotaka kwetu ni UHUSIANO tena wa KUDUMU sio kuja kwake kama kwa mganga wa kienyeji pale unapokwenda ukiwa na shida tu. Mganga wa kienyeji sio baba yako, ni muuguzi au FUNDI wa shida zako na unamwendea ukiwa na shida tu. Je! Umeona maana ya Mungu kuwa Baba?
Sasa fikiri hivi, Umewahi kukutana na watu ambao wanakutafuta siku wakiwa na shida tu? Yani pale wanapotaka msaada wako ndio wanakutafuta. 

Sifa za watu wanaokutafuta wakiwa na shida tu wako hivi:

1. Ni wanyenyekevu sana wakiwa na uhitaji, utasikia shikamoo nyingi sana kabla hawajaweka shida zao mbele zako.
2. Wanajifanya wanakupenda zaidi pale UNAPOFANIKIWA, yaani ni kama fisi anavyokuchekea kumbe anatamani mnofu wako.
3. Usipowapa wanachokitaka WANAKASIRIKA na kukususa.
4. Wanaanza kukusema VIBAYA kwa watu au wanaacha tu kusema habari zako NZURI (kukusifia) kama ilivyokuwa mwanzo.
5. Watajifanya wako busy kutafuta njia MBADALA ili kukukomoa. Wanadhani wakifanikiwa kwa njia nyingine wamekukomoa.
6. Wanakata tamaa kabisa ya kufanya yale mambo waliyokuwa wakifanya; na wakifanya wanafanya kwa unyonge sana.
7. UHUSIANO wenu unaishia pale wanapokuja kwako mara kwa mara na HAWAPATI wanachokitaka kwako.


Sasa angalia UHUSIANO wa mtu na baba yake:

1. KILA siku yeye ni baba, haijalishi amekupa HAJA zako au la; Yeye ni baba na HESHIMA yake haipungui.
2. KUMFUATA au KUMTAFUTA sio pale ukiwa na mahitaji tu; Unajisikia vizuri na furaha ukiwa na baba hasa mnapokuwa kwenye mazungumzo ya kawaida na burudani (kusifu, kuabudu na kumsikiliza).
3. Humvunjii heshima yake kwa watu wengine eti kwa sababu hajakujibu mambo yako. Yaani, hufanyi USHIRIKINA.
-> USHIRIKINA maana yake ni kumshirikisha Mungu na miungu mingine (ibada ya sanamu). Unatafuta msaada mbadala kinyume na Mungu ili upate MAHITAJI yako.
[Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu (Wakolosai 3:5)].
4. Ukiona mtu ANALIA tu kwa sababu ana shida, wala sio kilio cha FURAHA na SHUKURANI kwa Baba; Iko shida. Sawa, machozi yako yako karibu, kulia ni kawaida yako, hatukatai, mbona hulii kwa furaha au shukrani? Unalia tu kwa sababu ya shida zako binafsi? Hasa zile ambazo unadai bila kujali watoto wengine wa Baba yako kama wamekula au hawajala? Wewe unadai tu baba akupe hata kama wewe ni mchoyo kwa wenzako (mahitaji ya kibinafsi - hulii ukiombea shida za wengine)!
-> Angalia, KIPIMO upimiacho wengine hicho ndicho kitatumika kukupimia mambo yako. "Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa" (Mathayo 7:2).]
5. Baba yako sio panadol, kwamba utamtafuta kichwa kikiuma tu! Sawa, Mungu ukimfanya panadol atakutibu Akitaka, ila utakachokosa ni yale mambo ya UHUSIANO wa mtu na baba yake. Fikiri wewe ni mgonjwa yeyote huko, na fikiri wewe ni mtoto wa daktari. Je! nyie ni sawa japo mtapata dawa ile ile kwa ugonjwa wenu kutoka kwa daktari? UHUSIANO ni muhimu kuliko huduma.

Anayeenda kwa Mungu kama kutafuta dawa tu, akikosa ataenda kwa daktari mwingine, ila yule ambaye daktari ni baba yake, bado atakuwa baba yake hata asipomtibu atakavyo.
6. KIGEZO chako cha sifa kwa baba yako hakipo katika KUTIMIZIWA mahitaji yako ila katika UHUSIANO wenu.

Siku utakapotamani Mungu awe Baba yako; na ukafikia hatua ya kumwona kama Baba yako; yaani unafika mahali huwezi kufanya jambo bila KUMSHIRIKISHA na unahisi UWEPO wake sio ukiwa kanisani tu, utagundua kwamba umeenda hatua nyingine. Amani yako itakuwa kama maji tulivu, hata katika matufani na majanga ya maisha.
Frank P. Seth

Comments