LICHUNGENI KANISA LA MUNGU, SI KWA KUTAKA FEDHA ZA AIBU BALI KWA MOYO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Kanisa ni kundi la watu wanaomwamini YESU KRISTO kama Mkombozi wao.
Kanisa ni la muhimu sana duniani leo.
Amani ya dunia inategemea sana uwepo wa kanisa duniani.
Kanisa la KRISTO ndio lina ramani ya maisha ya uzima wa milele kwa waumini waliookoka na waaminifu.
Katika Kanisa, MUNGU ameweka  viongozi ili kuwakamilisha  wateule wa MUNGU.
Viongozi wana kazi ya Kulichunga  kanisa, kulifundisha kanisa, Kulisimamia kanisa na kuliongoza Kanisa katika Wokovu, Utakatifu na Haki.
MUNGU kupitia ROHO wake amenipa Neno kwa ajili ya viongozi wa kanisa na kwa ajili ya wanaotarajiwa kuwa viongozi baadae katika kanisa. Mwanzo niliogopa kufundisha somo hili maana nawapenda sana maaskofu, wachungaji na viongozi wengine wote wa kanisani maana wanamtumikia KRISTO, Lakini inanibidi tu kusema leo hicho nilichopewa na ROHO MTAKATIFU kusema.

1 Petro 5:2-4 '' lichungeni kundi la MUNGU lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.  Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.'' 


Ndugu zangu lichungeni kanisa la MUNGU mlilopewa.
Lichungeni kwa mafundisho ya KRISTO ya injili ya Wokovu.
Lisimamieni kundi la MUNGU kwa haki na upendo na kwa kweli ya MUNGU ambayo ni Neno la MUNGU la uzima.
Mtumishi wa MUNGU hutakiwi kufanya kazi ya MUNGU kama unalazimishwa bali kwa upendo na uhiari ndivyo MUNGU apendavyo.
Tumikeni si kwa kutaka fedha za aibu bali kwa Moyo.
Tumikeni sio kwa kuwaibia watu pesa zao kwa kuwawekea kiwango cha pesa ndipo muwaombee. BWANA YESU wala hakuagiza hivyo, tena wala hajawahi kuagiza hivyo katika kanisa lake.
Leo Kuna watumishi hawawezi tena kuhubiri utakatifu katika makanisa yao maana kwa kufanya hivyo watawakimbiza baadhi ya waumini muhimu, ambao wamegeuza kanisa kama kichaka chao cha kuficha maovu yao.
Leo kuna baadhi ya watumishi hata hawawezi kukemea dhambi kanisani kwa sababu tu wanajua wakikemea dhambi watawafukuza baadhi ya waumini muhimu wanaotoa pesa nzuri ila ni waovu.



1 Timotheo 4:16 ''Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia. '' 

Leo kuna baadhi ya watumishi huwaiga wengine ili tu na wao wapate fedha kupitia kuiga huko. Mimi Peter Naamini katika ufunuo, lakini siamini katika kuiga ufunuo na siamini katika ufunuo wa kujitungia tu mtumishi kisha anaaminisha watu uongo.
Kupitia kuiga leo kuna watumishi huenda Nigeria na wengine Israeli kufuata mafuta ya upako au chumvi ya upako au maji ya upako.
Wakija wanaanza kuuza mafuta hayo na watu wengi leo hata hawamtegemei YESU tena ina wanategemea mafuta tu.
Rafik yangu mmoja aliwahi kuniambia kwamba yeye kila siku hunyunyuzia tu chumba chake maji ya baraka aliyopewa kanisani. Nikamuuliza huwa unaomba, akasema hajawahi kuomba hata siku moja hata hajui kuomba na wala haitaji kuomba maana maji ya baraka yanamtosha. Nikamuuliza hata maombi ya toba huwa haombi akasema aombe ili iweje wakati maji ya baraka yanatosha kumlinda? Yeye analindwa na maji na sio MUNGU, Yamemuokoa maji na sio YESU KRISTO, ni hatari bora ya mwaka. Ufunuo umedandiwa na hetani na sasa anaumiliki ili kuwapoteza watu wa MUNGU.
Kwenye ufunuo kama huo unajifunza kwamba shetani ameutendea kazi zaidi kuliko hata aliyefunuliwa.
Hata kama kuna mtumishi aliwahi kufunuliwa kuhusu maji ya upako lakini kwa sasa tunaiga tu na kujipotosha wenyewe.
Hata kama huo ni ufunuo ambao  aliwahi kufunuliwa mtumshi fulani zamani, Je na sisi tuige kwa sababu tu ya kupata pesa?

1 Timotheo 6:10 ''Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.''

Kama mafuta hayo  ni mafuta tu ya kawaida yaliyoombewa na mtumishi  na kuwa mafuta ya upako, je kwanini tusinunue hapa hapa kwetu kisha tukayaombea na sio kufuata Nigeria?

 Kumbukeni pia kwanza shetani yuko kazini sasa kwa viwango vingine.
Kujiita mtume au nabii kwa lengo la kutafuta pesa ni ubatili.
Haina maana kwamba mitume na manabii wa kweli hawapo bali wapo tena wengi sana lakini pia hata wanaojiita mitume kwa lengo la kupanda hadhi na kupata pesa nyingi wapo pia.
Kwanza Majina yote ya utumishi yanaheshima sawa mbele za MUNGU.
Kuitwa Mtume au Nabii au Mwinjilisti au Mchungaji au Mwalimu yote yana hadhi sawa mbele za MUNGU.
Kwa sababu jamii ya leo inasaka tu ishara na miujiza basi ndio maana majina ya uchungaji na ualimu na uinjilisti yameonekana ya kawaida sana, lakini majina ya kuitwa mtume  yako chati za juu na majina ya kuitwa nabii yako chati za juu zaidi.
Ndugu zangu, kuitwa kwako mtume hakuna maana yeyote kama haufanyi huo utume.
Kuitwa nabii haina maana yeyote kama unabii wako unajitungia tu na sio kupewa na MUNGU.
Pesa ndio inayowapeleka wengi kujiita mitume au manabii, japokuwa wapo pia watumishi ambao MUNGU mwenyewe aliwaambia kwamba amewaita katika kazi hiyo ya utume au unabii.
Binafsi mimi sijawahi kujiita jina lolote maana sijawahi kusikia sauti ya MUNGU ikisema kwamba wewe ni Mtume, Mwalimu, Nabii, Mchungaji au Mwinjilisti japokuwa nafanya uinjilisti kivitendo lakini sijiiti Mwinjilisti hadi siku ROHO MTAKATIFU atakaponiambia jina.
Kwa sasa nahubiri tu maana kazi ya kuhubiri ni ya wateule wa MUNGU wote.
Nitajiitaje Mchungaji kama sina hata kondoo mmoja ninayemchunga?
Nitajiitaje nabii wakati huwa napewa tu unabii lakini sio nabii maana kuna tofauti kati ya kuwa nabii na mtu kupewa unabii.
Pesa inawafanya baadhi ya watu kujiita mitume au manabii, ni hatari.

Mhubiri 5:10 ''Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba maongeo. Hayo pia ni ubatili.''


Leo kuna baadhi ya watumishi huwaiga wengine ili tu na wao wapate fedha kupitia kuiga huko.
Leo kuna watumishi hata hubuni vitu feki ili tu kujikusanyia waumini wengi kwa lengo la kujiongezea kipato na heshima.
MUNGU hataki hivyo maana ana uwezo wa kuwaleta watu kwa injili tu na si vinginevyo.
Kanisa la MUNGU limejitosheleza, halihitaji uongo ndipo liongezeke.
Neno la MUNGU ndio kiongozi wa kanisa na Neno hilo la MUNGU limejitosheleza wala hatuhitaji kuwashawishi watu kwa ujanja ujanja wetu.
MUNGU anasema leo kwako kwamba;
 ''Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo ROHO MTAKATIFU amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake MUNGU, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.-Matendo 20:28''

Ni muhimu sana kujua kwamba kanisa sio mali yako  bali kanisa ni la KRISTO.
Tamani sana aonekane KRISTO katika kanisa lako na sio kuonekana wewe.
Mtangaze KRISTO YESU na sio kutangaza tu dhehebu lako na kanisa lako na sio kujitangaza wewe.
Wewe huwezi kuokoa watu ndio maana hupaswi kujitangaza sana bali mtangaze anayeokoa watu wote ambaye ni YESU KRISTO.
Wewe ni msimamizi tu katika kanisa na sio mwenye kanisa.
Usiige ufunuo wa wengine kwa lengo la kujiongezea pesa.
Ufunuo wa MUNGU upo kibiblia kabisa lakini kwenye fundisho la Biblia hakuna ufunuo wa kuiga.
Maana tu ya Neno lenyewe Ufunuo ni jambo ambalo lilikuwa limefichwa na sasa kupitia ROHO MTAKATIFU limewekwa wazi. Ndio maana YESU kuna wakati alimponya Kipofu kwa kutema mate chini kisha akachukua matope yale akampaka kipofu na kipofu akapona muda ule ule. Na pia sehemu nyingine tunaona BWANA YESU akiponya vipofu kwa njia nyingine, kwa kutamka tu na sio kupaka matope maana kupaka tope ulikuwa ni ufunuo  na sijaona Mitume popote  wakiiga ufunuo huo bali katika funuo zingine waliombea vipofu na vipofu hao wakapona.
Ndugu Zangu, Lichungeni kanisa la MUNGU si kwa kutaka fedha za aibu, bali kwa moyo.

1 Yohana 2:15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.''

 Asante kama unanielewa ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.

0786719090
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments