Michoro ya Kichawi

Na Mchungaji Adriano Makazi,
Ufufuo na Uzima Tanzania (Dar es Salaam)


Kwenye maisha ipo michoro ya giza ambayo husababisha uharibifu wa maisha ya watu. Katika kila tatizo ambayo yanawapata wanadamu huanzia kwenye michoro kwenye ulimwengu wa roho. Matatizo ya ndoa, uchumi, kazi, biashara, kabla hayajanza huanzia kwenye ulimwengu wa rohoni ndipo kutokea kwenye ulimwengu wa mwilini.
Kuna ulimwengu wa rohoni na ulimwengu wa mwilini, mambo mengi yameanzia kwenye ulimwengu wa rohoni. Matatizo mengi ya vifo, mikosi na magonjwa huanzia katika ulimwengu wa roho. Unaweza kumwona mtu anaishi lakini rohoni amechorewa michoro ya giza ambayo imeharibu maisha yake kwenye biashara yake, kazi yake, ndoa yake n.k
Waefeso 1: 3 “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo”
Unapomuona mtu ameshafanikiwa sio bahati mbaya au nzuri bali ni vitu ameanzia katika ulimwengu wa roho. Unaweza kumwona mtu anamtumikia Mungu hana tatizo lolote lakini anaonekana wa kawaida sana hajafanikiwa lakini ni muda wake tu haujafika zile Baraka zake za kwenye ulimwengu wa rohoni kuonekana. Mtu huyu amebariwa tayari katika ulimwengu wa roho ndani ya kristo Yesu.
Lakini unaweza ukawa unafunga na kuomba uko ndani ya wokovu lakini bado hujapokea kile ambacho ulitakiwa ukipokee hapo fahamu kuna tatizo la kushughulikia rohoni.
Waefeso 1: 20 “aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho”
Bwana Yesu ameketishwa katika ulimwengu wa roho hivyo basi biashara inaweza ikaketishwa katika ulimwengu wa roho, ndoa inaweza kuketishwa katika ulimwengu wa roho, kazi inaweza kuketishwa katika ulimwengu wa roho, maisha ya mtu yanaweza yakawekwa mahali katika ulimwengu wa roho.

Waefeso 2: 6 “Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu”
Mtu kabla hajampokea Yesu anaitwa amekufa na akimpokea Bwana Yesu ndani ya moyo wake anaitwa amefufuka.
Yohana 5:24 “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.”
Luka 15:32 “Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”
Yohana 6:63 “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.”
Roho ndiyo inayofanya mwili uendelee kuwepo na kuishi. Ulimwengu wa rohoni ndio unaowezesha ulimwengu wa mwilini ufanye kazi.
Dhambi inaweza kumtenga mtu na Mungu. Tunapokuwa tumempokea Yesu tunakuwa tunazipokea Baraka zote za Mungu kikamilifu, ili kuzipokea Baraka hizo ni muhimu na lazima kutubu na kuzacha dhambi kwa damu ya Yesu.
Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.“
Biblia inaongelea kwa ujumla ulimwengu wa roho na vita tunayoipigana kila siku ni vita ya ulimwengu wa rohoni.
Mtu wa rohoni anapoomba anakua anashindana kwenye ulimwengu wa roho. Mwanadamu ni roho yenye nafsi kwa asili inayokaa ndani ya nyumba inayoitwa mwili. Unapoanza kuomba kwenye ulimwengu wa mwilini unaonekana unaongea maneno lakini kwenye ulimwengu wa roho unavamia kambi ya adui zako wanaochora michoro ya kupindisha maisha yako kwa mamlaka ya jina la Yesu. Ni vizuri unapoanza kufanya kazi au ndoa au biashara lazima ushinde na uone mafanikio hata kabla hayajaonekana sababu ni kanuni ya Mungu mambo yaanzie kwenye ulimwengu wa roho baadae yadhihirike mwilini. Ukishinda rohoni unashinda na mwilini, ukishindwa rohoni na mwilini lazima ushidndwe.

Danieli 10:12 “Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.”
Kumbe unapoanza kuomba unaweza ukajibiwa lakini majibu yako yakazuiwa kwenye ulimwengu wa rohoni usikipate kile ulichokihitaji. Wanaozuia ni falme na mamlaka, wakuu wa giza hili, majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”
Isaya 49:16 Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.
Mungu anasema ametuchora kwenye kiganja chake maana yake anajua njia zetu na mwisho wetu utafika wapi. Mungu anasema anatujua jinsi tulivyo hata kabla hatujajua jinsi tulivyo. Ndiomaana Daudi akaseama kila mahala Mungu yupo hakuna mahala pa kujifichia.
Shetani kazi yake ni kuiga na alikua mbinguni anaijua biblia sana. Kama Mungu anatujua sisi na ametuchora kwenye kiganja chake vivyo hivyo na shetani naye anaweza kuchora michoro ya maisha ya mtu akayapindisha.
Mithali 8: 22 “Bwana alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale.”
Sulemani anaseama Bwana alikua naye tangu mwanzoni mwa njia yake.
Isaya 49: 8 “Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza.”
Yeremia 1: 4 “Neno la Bwana lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.”
Mtu anapokuja duniani anaonekana kwenye ulimwengu wa rohoni atakuja kuwa nani baadaye hivyo wachawi wanaweza kuona na kuamua kuchora michoro ya giza ili asije akafanikisha kusudi lake. Kabla hujachorewa michoro waliokuchorea michoro walishaona na kesho yako.
Mathayo 2: 1 “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.”
Huyu ni mtoto aliyezaliwa lakini inashangaza kwamba ni mfalme amezaliwa. Hao mamajusi kwenye kiebrania ni wachawi na ndio waliomfuatilia nyota yake na kufahamu kuwa ni Mfalme amezaliwa, wao hawakushangaa kwanini amezaliwa kwenye holi la ng’ombe bali walichokiona ni nyota yake na ndio walioifuatilia. Kumbe mafanikio huwa yanaanza kuonekana kwenye ulimwengu wa roho, kama ni uongozi unaanza kuonekana kwenye ulimwengu wa rohoni, kama ni kufanya biashara inaazia kwenye ulimwengu wa rohoni.
Tunajifunza kwenye maisha yetu lazima kila jambo tuliangalie kuanzia kwenye ulimwengu wa rohoni kwanza. Bwana Yesu alipokua anaingia kwenye mji wa Israeli aliuona mji akaanza kuulilia na kusema laiti ungalijua yajayo mabaya yaliyopangwa jii yake ungaligeuka na kuyazuia.
Tumeona mambo yote huanzia kwenye ulimwengu wa roho, kama ni matatizo basi huanzia kwenye ulimwengu wa roho.
Mungu huongea na sisi kutuonya na kutufundisha kwa njia mbalimbali moja wapo ni ulimwengu wa roho kupitia ndoto. Mungu huongea nasi rohoni na ni vizuri kujua kwamba Mungu hawezi kuruhusu mabaya yatupate bila kututaarifu.
2 Wafalme 6: 8 “Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani. Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili. Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je! Hamtanionyesha, ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli? Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala.”
Mfalme wa Shamu alikua amekaa kwenye kikao cha siri chumbani kwake na kulikua hakuna mtu awezaye kujua kikao hiko. Mfalme huyu wa Shamu alikua amejipanga kumvizia mfalme wa Israeli ili amuangamize. Adui hujiandaa ili akuvizie wakati unapoona kuna amani hakuna shida yeyote ile.
Mtumishi wa Mungu ndiye aliyeona mchoro huu akaenda kumtaarifu Mfalme wa Israeli ajihadhari sababu anaviziwa ili auawe wakati huo Mfalme wa Shamu alikua anajiamini siri yake haijulikani.
Jambo hili lilipangwa sirini na Mtumi wa Mungu aliliona akawaokoa ndugu zake. Kumbe hata wewe Mungu anaweza kukuonyesha ukaikomboa familia yako, huduma yako na nchi yako ikawa huru kwa jina la Yesu.

Kuna watu wanaishi maisha ambayo siyo yao, wanaishi maisha ya taabu sababu wamechorewa michoro ya giza/kichawi ambayo lazima iondolewe ili wawe huru, ili lile kusudi ulilotoka nalo mbinguni lazima litimie kwa jina la Yesu.
Leo hii tunafahamu adui yetu anakaa wapi na ni wapi pa kupimga tofauti na zamani tulipokua tunapiga hovyo bila kujua tunampiga nani na wapi. Simama kwa jina la Yesu upigane na kurudisha sehemu unayoona hapo ndipo Mungu amekubariki, futa michoro ya giza waliyokuchorea kwa jina la Yesu. Unatakiwa uwatende adui zako kama walivyokutenda wewe kwa jina la Yesu, Samsoni alisema nitawatenda kama walivyonitenda.
Mithali 26:27 “Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia.”
Shetani hana jipya ni mwizi na mharibifu, anao uwezo aliotoka nao mbinguni na ndio huo anautumia maarifa yake anatumia kujenga utawala wake lakini sisi tunayo maarifa na nguvu zaidi yake na wakala wake kumkabili na kumpiga na kumnyanganya vyote alivyoiba kwa jina la Yesu.
Mungu akiwa pamoja na wewe hakuachi ukaangamia, Mungu akiwa upande wetu ni nani aliye juu yetu, usiogope simama uwe na ujasiri kama Simba sababu umechorwa kwenye viganja vya Mungu.
“Kwa jina la Yesu michoro niliyochorewa naifuta nawarudishia wote walionichorea kwa damu ya Yesu kristo” Amen
Kwenye jamii yapo mambo yanayoendelea kwenye ulimwengu wa mwilini ambayo yameasisiwa rohini. Unatakiwa uyawahi mambo mabaya ya rohoni kabla hayajadhihirika mwilini. Kuna watu wanapatwa na mambo ambayo yalipangwa miaka mingi nyumba, yamekuja kutokea sasa hivi.
Mwanzo 41: 1 "Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto. Na tazama, ng'ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini. Na tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng'ombe wengine ukingoni mwa mto. Kisha hao ng'ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng'ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka. Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema. Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu. Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo. 14 Ndipo Farao akapeleka watu, akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao. Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri. Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani. Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani. Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nalikuwa nikisimama ukingoni mwa mto; na tazama, ng'ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha manyasini. Kisha, tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu. Na hao ng'ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza, wale wanono. Na walipokwisha kuwala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka. Kisha nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa. Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionyesha maana yake. Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja. Na wale ng'ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa. Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu.”
Huu ni mchoro alioonyweshwa mfalme ambao ulipangwa kutokea baada ya miaka 14, Mungu alikua anamjulisha yeye mwenyewe. Bahati nzuri mfalme huyu alikua anajua umuhimu wa ndoto hakupuuza. Ndoto ni bayana hasa inapojirudia sababu ni matokeo ya mambo yajayo, ukiota ndoto mbaya iharibu na kuivunja mara moja kabla haijadhihirika.
Mungu amemwonyesha mfalme wa misri mchoro wa njaa katika nchi yake kwenye ulimwengu wa roho ndotoni na mchoro huo Mtu wa Mungu Yusufu aliushinda akaliponya taifa zima.
Ndoto inaweza kukutoa gerezani kama Yusufu. Mungu bado anatenda kazi na kutujulisha kupitia ndoto hata hivi leo klwenye maisha yetu. Kuna mambo mabaya yanawapata watu wengi kwasababu ya kudharau ndoto au kutokusadiki. Bwana Yesu kabla hajaja duniani kilikaa kikao Mungu akamtuma Bwana Yesu akaja kutukomboa.
Ukiona mambo yamekua magumu fahamu kuna kitu mbele adui amekiona toka kwako hivyo wanajaribu kukizuia unachotakiwa ni kusimama na kupigana ili kufuta michoro yote. Mambo yote duniani huwa yanaanza na michoro yake maana hakuna kinachoweza kuonekana bila mchoro.
Maarifa haya hayana maana yeyote kama hujaomba, unatakiwa usimame kwa mamlaka ya Jina la Yesu uharibu michoro yote ilichorwa kwenye maisha yako. kila mchoro una wachoraji wake, una wasimamizi wake, una watekelezaji wake wote hao ni wakuu wa giza, Falme za giza majeshi ya pepo wabaya, wachawi, waganga, wasoma nyota, wasihiri n.k wanatenda kazi katika ulimwengu wa roho.
Kwa jina la Yesu ninaharibu michoro ya umaskini kwa jina la Yesu, michoro ya magonjwa, michoro ya mikosi naiharibu kwa Damu ya Yesu” simama kwa mamlaka ya Yesu kristo kuharibu michoro yote ya kichawi iliyopindisha maisha yako na utakua huru kwa jina la Yesu.

Comments