MUNGU ANATAKA UFANIKIWE.(3)

Bwana Yesu asifiwe milele!
Leo nataka nikupe wazo la 5, ambalo Mungu ataweka ndani ya moyo wako, ili likusaidie wewe kufanikiwa kimaisha, kwa kutumia mpango wa Mungu alionao kwa ajili yako, kufuatana na aliyoyasema katika Yeremia 29:11.
Wazo hilo ni hili: “Tumia neno la Mungu kutambua fursa zinazoweza kukufanikisha, ukijua kuzitumia ipasavyo”.
Ukisoma Waebrania 4:12,13 utafahamu ya kuwa hakuna kilichofichika mbele ya neno la Mungu! Kwa hiyo hata fursa zinazoweza kukufanikisha kimaisha, haziwezi kufichika mbele ya Neno la Mungu!
Ndiyo maana kufuatana na yaliyoandikwa katika Isaya 55:11, Mungu huwa analituma neno lake kwako, ili pamoja na mambo mengine, liweze kukusaidia uweze kufanikiwa!
Njia mojawapo ambayo neno la Mungu linatumia kukufanikisha linapotumwa kwako, ni kukuwezesha kuzitambua FURSA ambazo ukizitumia ipasavyo utafanikiwa! Hebu tuangalie mifano ifuatayo:
Mfano wa 1: Ukikutana na “Goliathi” – fungua macho uone fursa! Ukisoma 1Samweli 17:25 utaona ya kuwa mfalme Sauli alitangaza ya kuwa: “Mtu yule atakayemuua (Goliathi),…atamtajirisha kwa utajiri mwingi, naye atamwoa binti yake, na kuifanya mbari ya baba yake kuwa huru katika Israeli”.
“Goliathi” alikuwa “tatizo”, na alikuwa “fursa”, kwa wakati huo huo mmoja! Wale waliomwona “Goliathi” kuwa ni “tatizo” kwao, walijikuta wamekwama! Daudi alimwona “Goliathi” kuwa ni “fursa” – na akaitumia kutatua tatizo la wana wa Israeli – na kwa sababu hiyo akatajirishwa!
Kwa hiyo – unapoona jamii inakabiliwa na tatizo, fungua macho uone fursa ndani ya hilo tatizo ili ulitatue! Uwe na uhakika ukifanya hivyo, huo utakuwa mlango wako wa kufanikiwa!
Mfano wa 2: Ukikutana na “wana wa Anaki”, fungua macho ya moyo wako ili uone fursa!
“Wana wa Anaki” au “majitu” au watu wenye maumbo makubwa walionekana “kikwazo” kwa wale wapelelezi 10, na wakakwamisha mafanikio yao kimaisha – na ya wale waliowategemea!
Lakini wapelelezi wawili – Yoshua na Kalebu, walikuwa na mtazamo tofauti juu ya tatizo lile lile la wana wa Anaki!
Yoshua na Kalebu waliwaambia wenzao juu ya mtazamo wao kuhusu wana wa Anaki – wakasema: “msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu” (Hesabu 14:9).
Ina maana waliona “fursa” ya kupata “chakula” chao, au kupata “kipato” chao! Kumbuka: “Goliathi” alikuwa tatizo la sasa; na “Wana wa Anaki” walikuwa tatizo la baadaye!
Kwa hiyo – ukitatua “leo” tatizo la “kesho” au la “baadaye” – ujue unajihakikishia “fursa” ya kupata “chakula” chako cha “leo” na cha “baadaye”!
Kwa hiyo – tatizo la jamii la baadaye, lakini likaonekana “leo”, linakupa fursa “leo” ya kulitatua ili kujitengenezea mazingira ya wewe kufanikiwa! Kumbuka: lile linaloonekana tatizo kwa wengine katika jamii, ligeuze liwe fursa kwako kwa kulitafutia ufumbuzi wake, ili kwako lisiwe tatizo – bali liwe chanzo cha “chakula” chako!
Mfano wa 3: Uhitaji wa kipawa ulichonacho, ni fursa yako ya kukufanikisha!
Ukienda kwa nabii Elisha kutafuta msaada wa ushauri, au wa maombi juu ya hali yako mbaya ya uchumi – ujiandae na jibu la swali hili akikuuliza: “Niambie, una kitu gani nyumbani?” (2 Wafalme 4:2)
Yule mama mjane aliyeulizwa swali hilo alijibu akasema; “sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta”. Kwa kusema hivyo, alikuwa anasema pia ya kuwa chupa ya mafuta aliyokuwa nayo nyumbani kwake, ilikuwa haina thamani kwake!Lakini hakujua ya kuwa thamani ya alichokuwa nacho ilitegemea uwingi wa uhitajiwa wake!
Ndiyo maana nabii Elisha alimwambia akatafute “vyombo vitupu” (2 Wafalme 4:3). Hii ilikuwa inampa changamoto mama mjane ya kutafuta na kuona fursa ya uhitajiwa wa alichokuwa nacho!
Kwa kiingereza cha kiuchumi – alitakiwa atafute “demand” (uhitajiwa) au “market” (Soko) ya alichokuwa nacho – yaani chupa ya mafuta!
Je wewe una ujuzi gani? Una kipawa cha aina gani? Una talanta zipi? Vyote hivi ni fursa kwako ukiweza kupata “demand” (uhitajiwa wake) na “market” (Soko lake)!
Nabii Elisha alimwambia mama mjane “akatafute” “vyombo vitupu” – akitaka ajue ya kuwa afanye juhudi ya kufanya “utafiti” wa uhitajiwa wa alichokuwa nacho!
Na akaambiwa asitafute “vichache”, akitaka ajue ya kuwa kwa kadri ya uhitajiwa wa alichokuwa nacho kuwa mwingi, ndivyo na pato lake linavyokuwa kubwa!
Maombi yangu kwa Mungu kwa ajili yako unayesoma “post” hii – ni Mungu akupe macho ya kuona fursa na moyo wa kujua cha kufanya katika fursa hizo, ili uweze kufanikiwa kuliko ulivyo sasa!

Comments