SIWEZI KUIACHA DINI YANGU


                   
Na Askofu Mkuu Zakaria Kakobe.

Mungu amenipa neema ya kuwaombea watu wenye magonjwa sugu, na wote wenye matatizo mbalimbali; na kwa neema ya Mungu nimeshuhudia Mungu akiwaponya na kuwabariki maelfu ya watu, kwa miujiza mikubwa, baada ya kufanyiwa maombezi. Kutokana na huduma hii, nimekuwa na neema ya kukutana na maelfu ya watu wenye matatizo mbalimbali, wanaotoka nchini mwetu, na mataifa mbalimbali duniani; na kwa jinsi hiyo nimejifunza mambo mengi sana, kutokana na maongezi yangu na watu hawa.
Nakumbuka siku moja, miaka kadha iliyopita, alinijia ofisini kwangu, baba mmoja wa makamo, akihitaji maombezi.  Baba huyu alikuwa anaumwa ugonjwa mbaya wa UKIMWI, na alikuwa ana hali mbaya sana.  Baba huyu alikuwa anaharisha mfululizo na homa zisizokwisha, na tena alikuwa ana majipu, mwili wote; yaliyokuwa yakitoa usaha kila mahali mwilini.  Kwa sababu hiyo, aliandamwa na mainzi wengi.  Alikuwa amedhoofu sana, na hata kutembea ilikuwa shida.  Mwili wake ulikuwa umebaki mifupa tu.  Baba huyu alikuja na gari akiendesha mwenyewe, kwa kutokutaka mtu mwingine ajue mambo yake.  Kukaa kwenye kiti na kuendesha usukani wa gari ilikuwa shida sana, maana makalio yote yalijaa vidonda.  Hata hivyo alijikokota na kufika.
Kwa kusaidiwa na wahudumu, hatimaye akawa amekalia kiti ofisini kwa shida sana, akiwa amekaa kiupande –upande kama anayelala.  Akaanza kuzungumza kwa shida sana kama mtu anayeweza kukata roho wakati wowote, “Kilichonileta hapa ni kuombewa juu ya hali yangu hii mbaya unayoiona.  Ndugu na marafiki zangu wengi walikuja ukawaombea na magonjwa yao mbalimbali sugu waliyokuwa nayo, yakaisha.  Na mimi wamenishawishi nije kwako uniombee.  Ingawa ugonjwa wangu hauna tiba wala kinga, nimeona na mimi nije kwako nijaribu”.
Nikamwambia “karibu sana,” kisha nikamweleza, “Ndugu yangu ni kweli kabisa kwamba yasiyowezekana kwa wanadamu yanawezekana kwa Mungu” (MATHAYO 19:26).
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

                    Akaanza kuzungumza kwa shida sana kama mtu anayeweza
                                                kukata roho wakati wowote
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kwamba, hata kama tukipona sasa hivi kwa muujiza mkubwa, siku moja bado tutalazimika kuiaga dunia hii.  Lazaro alikuwa amekufa na kuzikwa kaburini siku nne.  Kwa muujiza mkubwa Yesu akamfufua (YOHANA 11:32-45).   Lakini je, yuko hai hata leo?  Jibu ni kwamba alikufa tena.  Wote waliopata miujiza mikubwa katika huduma ya Yesu Kristo, hatimaye walikufa tena.  Kwa hiyo jambo la msingi, ni kuandaa kwanza maisha yetu ya baadaye tutakapokuwa tumeiaga dunia hii, maana Neno la Mungu linasema utafuteni kwanza ufalme wa Mungu, na haki yake, na hayo yote mengine mtazidishiwa (MATHAYO 6:33).
Kwa hiyo tunachotakiwa kukifanya ni kukiri kwamba sisi ni wenye dhambi, na kuhakikisha tumetubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha, na kumwomba Mungu atuwezeshe kuishi maisha ya utakatifu ambapo hapana mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao (WAEBRANIA 12:14).   Mtu awaye yote akitubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha kutoka moyoni, Yesu Kristo humsamehe mara moja (YOHANA 6:37) msamaha huo huambatana na wokovu, maana Neno la Mungu linasema katika LUKA 1:77, “Uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao”.
Kwa hiyo tukikiri sisi ni wenye dhambi na kisha tukatubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha, tunaokoka, yaani tunakwepa adhabu ya moto wa milele; na jambo hilo la kuokoka ni hapa duniani, kabla ya kufa; maana Mungu anapendezwa na watakatifu walioko duniani (ZABURI 16:3).  Ni nani kati yetu anayeweza kusema hajakasirika, au kusema uongo, au kufanya dhambi nyingine tangu kuzaliwa?  Jibu ni kwamba, sisi sote tumefanya dhambi, na mtu akisema hana dhambi, anajidanganya mwenyewe wala kweli haimo ndani yake (1 YOHANA 1:8-10).  Kwa hiyo, kama uko tayari, kabla ya kukuombea juu ya ugonjwa wako, nitapenda kwanza nikuongoze sala ya kutubu dhambi  zako au sala ya toba.  Je uko tayari?”
Nilipomaliza maneno hayo, akasema, “Mimi, hata kwa vipi, siwezi kuiacha dini yangu.  Mimi kwa sasa, nina umri wa miaka 52, na tangu kuzaliwa kwangu mimi niko katika dini yangu hii, ambayo pia ilikuwa ya wazazi wangu.   Muda wote wa maisha yangu, sijasikia Kiongozi wangu wa dini akinieleza habari ya kuokoka hapa duniani.  Kwa hiyo siko tayari kupokea elimu mpya katika umri huu.  Kama ni kufa bila kuokoka, siyo hoja, niache hivyohivyo.  Mimi kilichonileta hapa ni kuombewa, siyo kuhubiriwa mambo ya wokovu, yaliyo tofauti na yale niliyoelezwa na viongozi wa dini yangu.  Kama unataka kuniombea, niombee.  Kama hutaki basi, lakini ujue kwamba mimi siwezi kuiacha dini yangu”.
Baada ya maneno yake hayo, niliishiwa nguvu, hata hivyo nilimwombea, kwa kumuwekea mikono, ingawa sikuona nguvu ya Mungu ikipita katika mikono yangu.  Nikiona hivyo mara nyingi najua mgonjwa yule hawezi kupokea chochote.  Na ndivyo ilivyokuwa.  Mgonjwa yule aliondoka ofisini baada ya maombezi, na siku chache zilizofuata nikapata habari kwamba amefariki dunia.  Alikwenda wapi baada ya kufa?  Jibu ni kwamba, kama aliendelea kukataa wokovu mpaka siku ya kufa kwake, Biblia inasema, tusidanganyike, wenye dhambi hawataurithi ufalme wa Mungu, kwa namna yoyote ile (1 WAKORINTHO 6:9-10;  WAGALATIA 5:18-21;  UFUNUO WA YOHANA 21:8). 
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .  .   
                                   Baada ya maneno yake hayo,  niliishiwa nguvu              
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

          Biblia inasema katika 2 WAKORINTHO 2:11, “Shetani asije akapata kutushinda kwa kuwa hatukosi kuzijua fikra (Mbinu) zake.  Mbinu kubwa sana ya shetani anayotumia kuwapeleka mamilioni ya watu katika moto wa milele, ni kuwafanya watu waishike sana dini yao, badala ya kulishika Neno la Mungu. Biblia inaposema tushike sana tulicho nacho, inatuambia tulishike sana Neno la Mungu, siyo dini yetu, kama walimu wengine wanavyofundisha.  Tunasoma waziwazi katika UFUNUO WA YOHANA 3:10-11, “kwa kuwa umelishika neno………shika sana ulicho nacho….”  Ni muhimu kufahamu kwamba watu waliolipinga sana Neno la Mungu na kisha kumsulibisha Yesu na kumwua, walikuwa ni watu walioshika sana dini, viongozi wa ngazi ya juu.  Biblia inasema katika MATHAYO 27:20, “Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu”.
Wakuu wa makuhani, yaani viongozi wa juu wa dini, hawa pia ndiyo waliomdhihaki Yesu msalabani wakati akiteseka.  Biblia inasema katika MATHAYO 27:41-43, “Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe.  Yeye ni mfalme wa Israel; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anataka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu”.
Unaona Wakuu wa makuhani hawakumwamini Yesu, na walipinga kabisa wokovu aliokuwa anahubiri.  Jina “Yesu” maana yake “atakayewaokoa watu wake na dhambi zao” (MATHAYO 1:21). Hivyo mtu yeyote asiyeamini juu ya kuokoka, hamwamini Yesu!  Wakuu wa makuhani hawakumwamini Yesu, kinyume chake walimwita “mjanja, mwenye mafundisho ya udanganyifu!” (MTHAYO 27: 62-64). Hapa tunajifunza kwambatukiyashika tu yale tunayoambiwa katika dini zetu bila kuyalinganisha na Neno la Mungu, tunaweza tukawa upande wa wakuu wa makuhani waliomsulibisha Yesu bila kujifahamu.
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

               Wakuu wa makuhani walimwita Yesu, “mjanja”, mwenye mafundisho
                                           ya udanganyifu   (MATHAYO 27:62-64)               
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

           Mpendwa msomaji, ikiwa tunataka kuingia mbinguni hatuna budi kulishika Neno la Mungu, siyo dini.  Biblia inasema katika ZABURI 119:9, “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake (ya kwenda mbinguni)? Kwa kutii, akilifuata neno lako”.  Biblia hapa haisemi kwa kutii, akiishika dini yake, bali kwa kutii akilifuata Neno la Mungu.  Mpendwa msomaji, kumbuka kwamba mtu anapokufa hataulizwa kwamba alikuwa dini gani, kitakachoangaliwa ni utakatifu, ambao pasipo huo haiwezekani kumwona Mungu (WAEBRANIA 12:14).  Kulishika Neno la Mungu ndiyo kumshika Yesu, maana Yesu anaitwa Neno la Mungu (UFUNUO WA YOHANA 19:13).  Ni muhimu kufahamu pia kwamba, dini haiwezi kumpa mtu uwezo wa kushinda dhambi.  Ndiyo maana wengi walioko magerezani, na watu wengi ambao ni makahaba, walevi, wavuta bangi, watukanaji, majambazi, wezi, washirikina, n.k.,  wana dini zao, lakini dini hizo hazikuwawezesha kushinda dhambi.
Mpendwa msomaji, najua una dini, tena dini nzuri tu, lakini je, jihoji mwenyewe na uwe mkweli. Je, una uwezo wa kushinda dhambi?  Jibu ni la!  Je, leo, unataka uwezo huu wa kushinda dhambi  na kuokoka?  Najua unataka.  La kufanya sasa, fuatisha sala hii kwa dhati kutoka moyoni,  “Mungu Baba, natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Naomba msamaha kwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.  Nipe uwezo wa kushinda dhambi kuanzia leo.  Asante kwa kunisamehe, na kuniokoa, katika Jina la Yesu.  Ameni”.
Sasa umeokoka tayari.  Kwa imani tu, kirahisi namna hii, umesamehewa na kupokea wokovu.  La kufanya sasa, ili uzidi kulishika Neno la Mungu, usikubali kufungwa na dini.  Usiseme kana yule baba, “ Siwezi kuiacha dini yangu”.  Ukiwa na msimamo huu, siyo rahisi kumpendeza Mungu.  Lazima uwe tayari kutangatanga na kutafuta kanisa ambalo linahubiri wokovu, ambalo utalishwa Neno la Mungu na kushiba kiroho.  Watu wanaowafundisha watu na kuwaambia wasitange-tange, hawajui maandiko yanasema nini.  Maandiko yanafundisha kutanga- tanga, mpaka tufike mahali tunaposhiba kiroho.  Biblia inasema katika ZABURI 59:15, “Watatanga-tanga hao wakitafuta chakula; wasiposhiba watakesha usiku kucha (wakitanga-tanga)”.  Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa (MATHAYO 5:6).  Watashibishwa kwa jinsi gani?  Ni mpaka watange-tange na kutafuta kiliko chakula cha kiroho, siyo dini!  Hapo ndipo Bwana Mungu atakapowaongoza mahali penye chakula cha kiroho cha kuwashibisha.  Neno la Mungu linasema katika ZABURI 107:4-5, 7, 9, ”Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; hawakuona mji wa kukaa.  Waliona njaa, waliona na kiu, nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao.  (Bwana) akawaongoza kwa njia ya kunyoka, wapate kwenda mpaka mji wa kukaa.  Maana hushibisha nafsi yenye shauku, na nafsi yenye njaa huijaza mema.
Kumbuka ukianza kutanga-tanga, wazazi, ndugu, na marafiki watakuambia. “Kwa nini unaacha dini ya wazazi wako?”  Hoja hiyo haina mantiki.  Dini zote katika nchi yetu zina umri usiozidi miaka 200. Kabla ya hapo, watu wote katika nchi yetu walikuwa na dini za asili.  Zilipokuja dini hizi, babu zetu ndiyo walianza kutanga-tanga na kuziacha dini zao za asili.  Sasa wewe ukitanga-tanga, kwa nini ulaumiwe? Kama lawama hizi zina msingi, basi walaumiwe babu zetu waliocha dini za asili.  Kwa nini wao walitumia uhuru wao na kutanga-tanga, halafu sisi tukatazwe kutanga-tanga, na kuambiwa tusiache dini za wazazi wetu?  Anayekuzuia kutanga-tanga, anataka ushike dini badala ya kulishika Neno!  Uwe na busara. Mitume wale kumi na wawili wa Yesu, waliacha dini zao za mwanzo, Mtume Paulo, yeye naye aliacha dini yake ya mwazo (WAGALATIA 1:14-16).  Kama hawa walitanga-tanga, kwa nini sisi tukitanga-tanga, iwe nongwa?
. .. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .    ………..

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.
                                                         UBARIKIWE NA BWANA YESU!!!


Kwa Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe    Fungua    

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Comments