TAFUTA WOKOVU NA SIO DINI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo nazungumzia Wokovu.
Wokovu ni mpango wa MUNGU  Kumuokoa Mwanadamu.
Wokovu U Katika BWANA YESU Peke Yake.

Matendo 4:10-12 '' jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la YESU KRISTO wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na MUNGU akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.''

Wokovu unapatikana katika KRISTO YESU pekee.
Kuna tofauti kubwa katika ya kuwa muumini na Kuokoka.
Kuna tofauti kati ya kuitwa Mkristo na Kuokoka.
YESU hakuja duniani kuwafanya watu kuwa wakristo bali alikuja kuwaokoa wanadamu.
YESU hakuleta dini duniani bali alituletea mfumo wa maisha ambao unaanza na sisi kumpokea yeye kama Mkombozi wetu kisha tunaanza kuishi maisha matakatifu yanayoagizwa na Neno lake.
Dini haimpeleki mtu mbinguni ila anayepeleka watu mbinguni ni BWANA YESU tu.
Dhehebu halimpeleki mtu mbinguni ila anayepeleka watu mbinguni ni BWANA YESU tu.

Wkovu unaanza na kumpokea BWANA YESU.
Warumi 10:9-10 '' Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.''
 
Ndio maana waliomfuata YESU mwanzo waliitwa tu wanafunzi wa YESU.
Kama wewe umeokoka hakika wewe ni mwanafunzi wa YESU.
Kama wewe hujaokoka hakika bado hujawa mwanafunzi wa YESU  hata kama unamtaja YESU kila siku mara 7.

1 Timotheo 2:5-6 ''Kwa sababu MUNGU ni mmoja, na mpatanishi kati ya MUNGU na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu KRISTO YESU; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.''
 
 Wale waliouhitaji uzima wa milele walimpokea YESU na kuanza kuishi maisha matakatifu katika yeye.
Wale waliolisikia Neno la MUNGU na wakajigundua kwamba bila YESU hawawezi waliamua kumpokea BWANA YESU.
Wale ambao walikuwa mbali na MUNGU muumba wao walipolisikia Neno la injili ya wokovu wa KRISTO walimua kuokoka.
Mmoja wa waliamua kuokoka baada ya kuona ushindi wa KRISTO kwa watumishi wake ni huyu hapa Askari ambaye hakujizuia kujua kuhusu Wokovu;

  '' kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini BWANA YESU, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.- Matendo 16:30-31''

Kumbe ni rahisi kabisa kuokoka.
Ndugu huyu aliuliza afanyeje ili aokoke?, akimbilie wapi ili aokoke?
Auze nini ili apate kuokoka? atoe shilingi ngapi ili apate kuokoka?
Jibu la Mitume lilikuwa ni rahisi sana yaani ''Mwamini BWANA YESU, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako''
Hata leo kuna watu wengi wanatamani kuokoka na jibu ni hilo hilo kwamba ''Mwamini BWANA YESU, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako '' 
Mwamini YESU KRISTO na utaokoka.
Sio umwamini Musa tu au Eliya, Sio Umwamini mtume au nabii, sio umwamini Maria au Yusufu bali umwamini YESU KRISTO hakika utaokoka.

Kumwamini YESU ni kufanya mambo mawili;
1.Kumwamini YESU ni kumkubali awe mwokozi wako na kumtii yeye na Neno lake.
2. Kumwamini YESU ni kumtegemea kupitia maombi na utakatifu.

Biblia iko wazi sana ikisema kwamba pasipo YESU KRISTO hakuna mwanadamu hata mmoja ataingia uzima wa milele.
 
 Yohana 14:6-7 '' Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na BABA; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona.''

Kumjua YESU ndio kumjua MUNGU aliye hai.
Kumfuata YESU ndio kumfuata MUNGU aliyeumba mbingu na dunia.
Wokovu Ni Mpango Wa MUNGU Wa Kumtafuta Mwanadamu Ili Huyo Mwanadamu Apate Haki Ya Uzima Wa Milele. 
Wokovu Ni Katika BWANA YESU KRISTO Pekee.
 Hakuna Wokovu Katika Amri Za Musa.
Warumi 3:20-22 ''kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria. Lakini sasa, haki ya MUNGU imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya MUNGU iliyo kwa njia ya imani katika YESU KRISTO kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; ''

 Ukimpenda MUNGU chukia dhambi ila kama bado unapenda dhambi tambua ya kwamba bado hujampenda MUNGU.

Hakuna Wokovu Katika Kuheshimu Au Kuabudu Sanamu.
 Isaya 44:9-11 '' Wachongao sanamu, wote ni ubatili; wala mambo yao yawapendezayo hayatafaa kitu; wala mashahidi wao wenyewe hawaoni, wala hawajui; ili watahayarike. Ni nani aliyejichongea mungu mmoja, au aliyesubu sanamu isiyofaa kitu? Tazama, wenziwe wote watatahayari; na mafundi, hao ni wanadamu; na wakusanyike pamoja, wakasimame; wataogopa na kutahayari pamoja.''
 
 Hakuna Wokovu Kwa Mariamu. 
Mariamu Hawezi Kumuokoa Mtu Hata Mmoja, Mariamu Hawezi Kumsaidia Mtu Hata Mmoja Jambo Lolote Lile, Hata Mariamu Alimhitaji Mwokozi.
Matendo 1:14 '' Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.''

Baada ya BWANA YESU kufufuka tunaona wanafunzi wake akiwemo Mariamu wakidumu katika kusali na kuomba. Tena akina Petro na Yohana ndio walikuwa viongozi wa wanafunzi hao na sio Mariam. 

 Wokovu Wa roho Ya Mtu Ni Mabadiliko Ya Kiroho  kupitia Kumpokea YESU KRISTO na  Neno Lake Na Kuwa Na Imani Katika yeye KRISTO YESU Na Kutubu Dhambi Zote.

 1 Petro 1:18-23 ''Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini MUNGU, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa MUNGU. Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo. Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la MUNGU lenye uzima, lidumulo hata milele. '' 

 Mpango Wa MUNGU Wa Wokovu Unatuhusu Mimi Na Wewe. Ndugu, Hakikisha Unaishi Maisha Ya Wokovu.
 Kuikiri Imani Ni Jambo Jema Sana. Kumkiri BWANA YESU Ni Kuikiri Imani Ya Uzima Wa Milele.
 Ndugu Mkiri BWANA YESU Kokote Uliko. Ujulishe Ulimwengu Kuhusu Njia Pekee Ya Uzima Wa Milele Ambayo Ni Kumpokea BWANA YESU
Matendo 4:12 '' Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.  '''

 Kuokoka kuna faida sana kwako ndugu.
Ukiokoka unapokea mamlaka ya kuteketeza kazi za shetani, tumia mamlaka hiyo kuharibu kazi zote za majini katika maisha yako.
 Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA; ''
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments