TUMIA MADARAKA YAKO YA SIRI KUWASHINDA MAADUI ZAKO KATIKA ULIMWENGU WA ROHO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mteule wa MUNGU yeyote anayo madaraka ya siri katika ulimwengu wa roho.
Wewe mteule wa KRISTO uliyeokolewa na KRISTO YESU unayo madaraka ya siri katika ulimwengu wa roho.
Yanaitwa madaraka ya siri kwa sababu wanadamu wanaweza wasijue hadi pale utakapoonyesha madaraka yako ya siri kwa njia ya maombi.
Madaraka yako ya siri yanatokana na kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na kuanza kuishi maisha matakatifu katika yeye huku ukiomba kwa imani katika MUNGU.

Waefeso 3:8-12 ''Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake KRISTO usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za MADARAKA YA SIRI HIYO, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika MUNGU aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya MUNGU iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika KRISTO YESU Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.''

Sio wateule wote huyatumia vizuri madaraka yao ya siri.
Yawezekana hujanielewa vizuri ila ngoja nianze hivi;
Eliya hakuwa na cheo serikalini lakini alipoonyesha madaraka yake ya siri walisalimu amri hata wenye madaraka ya kiserikali wote. 
Kwa maombi Eliya alifunga mvua na wakataharuki nchi nzima(1 Wafalme sura ya 17, 18 na sura ya 19)
Wachungaji na maaskofu wana madaraka ya siri ndio maana wanaweza kuwakemea hata viongozi wakuu wa nchi kama ni waumini wao kanisani.
Binti mmoja majirani zake walikuwa wachawi na walikuwa na uadui naye. Siku moja alimua kufunga na kuomba ili kuwaharibu wachawi wale. madaraka ya siri yalipotumika vizuri wale wachawi wote saba(7) waliukimbia mji ule na kuhamia mji mwingine sawasawa na maombi ya yule dada wa kawaida sana ila ana YESU KRISTO ndani yake.
Biblia inasema kwamba wateule wa MUNGU wmefanikiwa kuzijua siri za ufalme wa MUNGU
BWANA YESU siku moja akawaambia watumishi wake kwamba wao wamejaaliwa kuzijua siri za Ufalme wa MUNGU.
Marko 4:11 ''Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa MUNGU, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano,''
 
Kuhama kwa wachawi hawa kunaweza kushangaza kidogo kama ni kibinadamu tu, maana hawakuja jeshi la polisi kuwaambia wachawi wale wahame wala mahakama hakuamuru watu wale wachawi wahame ila madaraka ya siri ya mteule wa MUNGU yalifanya kazi.
Mama mmoja yeye alikuwa muombaji sana ila alikuwa na sauti ndogo sana kiasi akawa wakati mwingine akidhani hatimizi lengo la maombi kwa maana sauti yake ilikuwa ni ndogo kuliko waombaji wengine. Mama yule akapata ufunuo wa ajabu siku moja ambapo akachuma kiboko kizuri na kuanza kukitumia katika maombi. Huku anaomba huku anachapa angani kama kwamba anamchapa mtu. Kesho yake waliokuja wabaya wake wote, wachawi walikuja kwake asubuhi wanalia wakimuonyesha migongo yao ikiwa na alama za damu na alama za viboko vikali sana walivyochapwa, walimlalamikia yule maana lakini walikoma kuiroga familia yake yule mama. Hayo ndio madaraka ya siri ya mkristo aliyeokoka na ambaye ana KRISTO ndani yake. Yule maana alichokuwa anafanya ni kutamka tu kwa njia ya maombi kwamba ''Nawachapa wachawi wote wanaonifuatilia na kuroga familia yangu, nawachapa kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai'' anatamka kisha anachapa na hakika hao wachawi walichapwa kule kule walipokuwa ambako ni mbali lakini katika ulimwengu wa roho hakuna umbali.
Sijui kama huwa unayatumia vizuri madaraka yako ya siri ili kuharibu kazi zote za shetani katika eneo lako.
MUNGU anasema;
'' angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.-Yeremia 1:10''
Ukiyatumia vyema madaraka yako ya siri hakika utaweza kung'oa kazi zote za mawakala wa shetani.
Utaweza kubomoa kazi zote za wachawi, waganga na wakuu wa giza.
Utaweza kuharibu kila roho za shetani zinazowatesa watu.
Utaweza kuangamiza kila uchawi na mchawi, uganga na mganga, mkuu wa giza na giza lake na mshirikina na ushirikina wake.
Ukisha kufanya hayo itakuwa kwako ni rahisi sana kujenga ufalme wa MUNGU katika eneo lako, familia yako, ukoo wako na jamii yako.
Ukiweza kuyatumia vizuri madaraka yako ya siri hakika itakuwa ni rahisi sana kupanda baraka na uzima katika maisha yako.
Ndugu yangu uliyeokoka unao maadui na maadui hao kuwashinda ni lazima ujue kuyatumia madaraka yako ya siri na uyatumie kwa njia ya maombi na imani hakika utashinda.
'' Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.-Waefeso 6:12-13''

Hawa ni maadui wakali kabisa lakini ukiwa na KRISTO YESU na ukajua jinsi ya kuyatumia madaraka yako ya siri hakika utashinda kirahisi sana.
Maadui zako ni wafalme wa kipepo katika ulimwengu wa roho.
Maadui zako ni mamlaka zote za kishetani katika ulimwengu wa roho.
Maadui zako ni wakuu wa giza wote.
Maadui zako ni majeshi yote ya pepo wabaya(majini).
Kuwashinda maadui hao unatakiwa uwe upande wenye nguvu sana yaani upande wa YESU KRISTO na ujue kuyatumia madaraka yako ya siri kwa maombi.
Utakuwa upande wa YESU KRISTO kwa kumpokea yeye kama BWANA na Mwokozi wako na kuanza kuishi maisha matakatifu ukilifuata Neno la MUNGU.
Wanaotumia madaraka yao ya siri hushinda.

Zaburi 34:7 ''Malaika wa BWANA hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.''
Ukiyatumia vizuri madaraka yako ya siri hakika malaika wa MUNGU watafanya kituo kwako unayemcha MUNGU na kukuokoa.
 Nabii Elisha aliyatumia vizuri madaraka yake ya siri ndio maana alizungukwa na maelfu ya malaika(2 Wafalme 6:16-23).
Kwa nini Elisha alizungukwa na Malaika wa MUNGU?
Ni kwa sababu ''Je! Hao(Malaika) wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu? ''
Elisha alikuwa na haki ya kuhudumiwa na malaika kwa habari ya ulinzi maana Malaika ni roho watumikao wakitumwa na MUNGU BABA ili kuwahudumia wateule wa MUNGU watakaouridhi Wokovu.

 Ngoja nikupe ushuhuda wangu mfupi wa siku moja mwaka 2012.
Mimi Peter Mabula Nilihamia Dar es salaam kutokea Zanzibar mwanzoni mwa mwaka 2012. Nilitafuta chumba cha kupanga na kupata Kawe jirani na Malingo. Katika Nyumba ambayo nilipanga kulikuwa na vyumba 5 na vyote walikuwa wanakaa wapangaji tu, wanawake 3 na mwanaume mmoja kila mtu na chumba chake, na mimi nikaongezeka tukawa wanaume 2. Nilipofika tu siku ya kwanza mmoja wa wale wadada aliniuliza kama nitaiweza hiyo nyumba maana vituko vya uchawi ni vingi sana. Nikamwambia nitaweza, akasema kwamba katika uwanja wa nyumba hiyo kila siku huwa kunapigwa ngoma usiku za wachawi na huwa wanafanyia kikao hapo wachawi. Akaendelea kusema kwamba kuna wakati wakichungulia huona kabisa kundi la wachawi wengine vifua wazi na wengine wamevaa ngozi za wanyama wakicheza kwa kuzunguka eneo hilo. Akasema wiki nzima kabla ya siku hiyo ya mimi kuhamia pale walikuwa hawajalala kabisa kwa sababu ya makelele ya wachawi katikati ya usiku. Nilimjibu kwa haraka tu kwamba tangu siku hiyo niliyofika mimi wataanza kulala vizuri maana BWANA YESU niliyenaye atatushindia. Yule dada alicheka tu na kutikisa kichwa akiwa kama ananishangaa jinsi ninavyojiamini kwa suala ya wachawi wale. Ni kweli kabisa usiku hawakufanya kikao hao wachawi na kesho yake yule dada akanijulisha jambo hilo na kushangaa sana. palikuwa kimya kwa muda mrefu sana hadi mimi nahama pale. Nikiwa pale pale kuna bibi mmoja wa miaka kama 80 walikuwa wanamsema kwamba ni mchawi sana na ndio kiongozi wa wachawi. Jirani na chumba changu ndipo kulikuwa na njia ya kwenda bombani ambayo walikuwa wanaitumia watu wengi akiwemo na yule bibi na familia yake. Siku moja muda kama saa tano asubuhi nilijisikia kuomba na katika kuomba kule nikajisikia kwenya nyuma ya chumba changu ambako ndiko kulikuwa njia ya kupitia watu kwenda kwenye maji. Kwa Imani nilitamka maneno haya ''Naziba hapa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO, Yeyote mchawi atakayepita hapa apondwe kwa jina la YESU KRISTO.'' Kisha nikachora kwa fimbo eneo lote la njia ile na kusema ''Huo ndio mpaka ambao hawawezi kuuvuka wachawi wote wanaosumbua watu wema katika mtaa huu''. 
Baada ya kumaliza maombi hayo niliingia ndani kwangu na kuwasha computer lakini hata kabla computer haijafunguka nikamuona yule Bibi ambaye watu walikuwa wanadai ni mchawi sana akiwa amebeba dumu akienda kuchota maji. Nikasogea dirishani katika eneo ambalo nililiombea. Yule bibi alisogea taratibu katika eneo hilo na alipokanyaga tu usawa wa pale nilipopachora kwa mti aliganda na kuanza kutetemeka huku akitamka maneno ambayo sikuelewa maana yake. Yule bibi aliganda kama dakika moja akijaribu kuondoka na kushindwa. Baadae kidogo akaweza kupata nguvu za kutoka katika lile eneo na kuokota dumu lake na kuanza safari ya kurudi nyumbani kwake huku akifyonza sana na kuongea maneno ambayo sikuyasikia. Safari ya bombani ikaishia hapo. Baada ya tukio hilo yule bibi sikumuona tena nje kwa wiki nzima. Siku moja nilikuja kutembelewa na wageni na wakati wanasindikiza nilipita jirani na nyumba ya yule bibi maana ndio njia ya kupita watu wote mtaani wakitaka kwenda barabarani. Nilifika katika usawa wa nyumba yake akaniita yule bibi na kuniambia kwamba mbona sijaenda kumtembelea maana ameugua wiki nzima na ilikuwa karibia kufa. Nikamwambia sikujua kama ameugua, kisha akasema mbona hata pole simpi? nikasema baada ya kuwasindikiza wageni nitamletea samaki maana wale wageni waliniletea samaki mimi. Ni kweli baada ya kurudi nilienda na kuchukua samaki kisha nikawaombea wale samaki ili kama kuna hila ya shetani isifanikiwe kisha nikampa yule mama na akafurahi sana. Wakati huu alikuwa amedhoofika sana na macho yamekuwa mekundu sana. Kumbe madaraka ya siri ya mkristo muombaji hayakuishia tu kumgandisha yule mchawi bali alipigwa na pigo la ugonjwa mbaya usiojulikana. Baada ya hapo yule maama aliniheshimu sana na akawa rafiki yangu sana huku akiwa ni mtu wa kujitetea sana pasipo sababu.
Ndugu, Madaraka ya siri ni muhimu sana kuyatumia.
Somo hili kwa ufafanuzi mkubwa zaidi litakuwa katika kitabu ambacho nakiandaa. Ukipenda kunichangia mchango wako wa hiari nichangie maana nahitaji kuchapisha vitabu 2000 vya masomo ya MAOMBI na kingine masomo ya UJANA, UCHUMBA na Ndoa. Na vitabu hivyo  vitakavyokuwa chanzo cha kuchapisha vitabu vingi vya masomo tofauti tofauti kila mwaka. Nakuomba unisapoti katika hili na nawashukuru sana wale ambao wameanza kunichangia.
 namba yangu ni 0714252292, jina PETER MABULA, tuma tu kutoka katika mtandao wowote na pesa hiyo itafika. pia unaweza kunipigia ili kujiridhisha kabisa kabla ya kutuma au unaweza kunifuata inbox au kwa email ili kupata maelezo zaidi. na kuangalia masomo yangu yote ambayo sasa yamefika 5010 Fungua blog ya Maisha ya ushindi kisha juu kulia utaona Label Imeandikwa Peter Michael utayaona yote.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments