BARAKA YAKO INAWEZA KUZUILIWA AU KUFUTWA KWA SABABU YA UASI WAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


BWANA YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kila mtu najua kabisa anahitaji baraka kutoka kwa MUNGU lakini naomba ujue kwamba baraka zako zinaweza zikazuiliwa Kwa Sababu Ya roho Ya Uasi Uliyonayo. 
 1 Samweli 15:22-23 ''Naye Samweli akasema, je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme. '

Mfalme Sauli alikuwa ni mfalme wa Israeli. MUNGU alimpa Sauli baraka ya kuwa Mfalme wa Israeli, Baraka ni baraka haijalishi iwe baraka kubwa au ndogo. Huyo alipata Baraka kubwa sana sana lakini baadae alianza uasi kwa MUNGU. Mfalme akaanza kutenda dhambi na akaanza kutaka msaada kwa waganga wa kienyeji. Uasi huo ukawa mbaya sana kwa MUNGU ambaye ndiye aliyempa baraka ya kuwa mfalme. Tangazo la MUNGU linaletwa na Nabii Samweli kwa Mfalme kwamba kuasi kule kumesababisha baraka yake ya ufalme iondolewe kwake. Mfalme Sauli alikuwa bado anaipenda baraka aliyopewa na MUNGU na alitamani kuendelea kubaki katika nafasi hiyo lakini uasi wake kwa MUNGU ulifuta ufalme wake na akapewa kijana mdogo Daudi.  Leo inawezekana kabisa wewe ndugu, MUNGU amekupa baraka fulani lakini kama utamuasi MUNGU hata hiyo baraka yako inaweza kuondolewa kwako.
Kuna watu MUNGU aliwapa baraka za ndoa lakini walipomsahau MUNGU aliyewapa ndoa hiyo MUNGU naye aliwaacha na sasa ndoa zao ziko katika migogoro mikubwa sana na hawaelewi chanzo cha migogoro yao ni nini, kumbe ni uasi wao.
Kuna mtu mmoja alikuwa anamuomba sana MUNGU ili ampe kazi nzuri, MUNGU akampa kazi lakini baada ya miezi mitatu tu tangu ndugu yule apate kazi nzuri na ya heshima aliasi kwa MUNGU. MUNGU aliwatumia watumishi wake kumuonya ndugu yule ambaye baada ya kubarikiwa aliacha na kwenda kanisani, yule ndugu wakati huu alianza kiburi na akaanza kuwadharau hadi watumishi wa MUNGU waliokuwa wanamuombea usiku na mchana. Nini kilifuata? Baada ya miezi miwili baadae alifukuzwa kazi na baada ya hapo alijaribu kutafuta kazi kwa zaidi ya miaka miwili bila kupata kazi. Ndugu zangu uasi kwa MUNGU unaweza kuifuta baraka yako. Kama umeamua kuwa na YESU basi hakikisha unakuwa na YESU hata wakati ukiwa na pesa na hata wakati ukiwa kiongozi mkubwa katika jamii au serikali au kanisa.
 Neno La MUNGU Haliwezi Kupinduliwa, Liko Imara Daima. Ndugu Simama Katika Neno La MUNGU Na Ulitii Hilo Maana Ndio Uzima Wako na uzima wa baraka yako.

Kumbukumbu 30:19-20 ''Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kumpenda BWANA, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi BWANA aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.'

Hata wakati wa kubarikiwa Mche MUNGU.
Hata wakati wa kuingia katika baraka ya ndoa endelea kumtii MUNGU.
Hata wakati MUNGU atakupa kazi nzuri na mshahara mzuri basi mche MUNGU zaidi na mtolee sadaka na zaka maana huo ndio uzima wako na uzima wa baraka yako.
Hata wakati umemiliki gari au nyumba bado endelee kumtii BWANA YESU na Neno lake.

Kuna watu ni kama hawaonekani kwa sasa kwa sababu ya uasi wao kwa MUNGU.
MUNGU aliwabariki ila wakamsahau na kuasi mbele zake na yeye akawaacha hivyo shetani kuchukua nafsi na kuwaonea na kuwatesa. Lakini ndugu uliye wa aina hiyo nakuambia leo kwamba bado liko tumaini kwa BWANA YESU. Ni kweli siku hizi huonekani tena maana umefilisika baada ya kumwasi MUNGU. Ndugu kuonekana baada ya baraka mpya  inawezekana kabisa ila ukweli mmoja ni kwamba  Utaonekana tena Kama Tu Ukiamua Kuonekana. Kwa toba na  Maombi Na Utakatifu Hakika Utaonekana. Kwa Utulivu kwa YESU Na Kutokuathiriwa Na Mambo Ya Kidunia, Hakika Utaonekana. 
Inawezekana mama ulimwasi MUNGU na kuanza kujichanganya na mambo ya kidunia yaliyo uasi kwa MUNGU.
Inawezekana kabisa kanisani una miaka hujaenda.  Lakini mimi nakuambia kwamba kuonekana tena inawezekana. Kwa kuamua kutubu na kuokoka kwa upya hakika utaenda kuonekana.
Kwa Kuacha Kujichubua kisha uanze utakatifu Hakika Utaonekana. 
Kwa Kuacha Kuvaa Kikahaba Kisha uanze kumcha MUNGU Hakika Utaonekana, utaonekana Na Waoaji na utapata baraka za MUNGU. 
Ukiendelea kuvaa Kikahaba Utaonekana Na Wanaotaka Kukuchezea Tu Na Sio Waoaji. 
Ukiendelea kujichubua Utaonekana Na Wanaotaka Kukuweka Nyumba Ndogo Tu Lakini Ukijitunza na utakatifu Hakika Utaonekana Na Waoaji. 
Kama hutakuwa  Mtakatifu Huwezi Kupata Mtakatifu Lakini Ukiwa Mtakatifu Ni Rahisi Kumpata Mtakatifu.
Uasi wako ndio uliokufanya usipate baraka yako mapema na kwa wakati ufaao.
Badilika leo na usimwache BWANA tena. 
 ''Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;
 bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya.-
Isaya 1:19-20 ''


 Mwimbaji Usigeuke Kinanda Au Gitaa Kwa Kuwaburudisha Watu Wengine Huku Wewe Ukikosa Mbingu Kwa Sababu Ya Dhambi Zako Za Siri. Fanya Uimbaji Wako Kwa Moyo Ukiambatana Na Utakatifu. Kama unafanya uasi kwa MUNGU ni hatari sana.
 Waimbaji wengine ni shida!!! Akitoka kuimba katika madhabahu akitoka nje ya Kanisa hutoamini kuwa ndo yule alie kuwa anaimba na kujidai yupo katika uwepo wa Roho.
Mhubiri wa injili hakikisha hufanyi uasi kwa MUNGU.
Mche MUNGU na dumu katika utakatifu, jua kwamba kile unachohubiria watu basi na wewe unajihubiri maana ni neno la MUNGU. Jua kwamba na wewe ni mwanadamu na kama unamuasi MUNGU basi unastahili adhabu ya MUNGU kama walivyo wanadamu wengine wanaomuasi MUNGU.
Kuna watumishi wengine hudhani kwamba adhabu ya MUNGU haiwahusu hata kama wamemuasi MUNGU. Ndugu yangu naomba ujue kwamba MUNGU anaweza akakuacha upako wote na ukapeleka watu mbinguni lakini wewe huendi kwa sababu ya dhambi zako na uasi wako kwa MUNGU.
 ''Ungama uovu wako tu; ya kwamba umemwasi BWANA, MUNGU wako, na njia zako zimekuwa nyingi kuwaendea wageni chini ya kila mti wenye majani mabichi, wala hamkuitii sauti yangu, asema BWANA.-Yeremia 3:13 ''


Kuna watu uasi wao unaweza kufuta baraka zao.
Kuna watu uasi wao unaweza kufuta safari yao ya uzima wa milele. MUNGU anaweza akakuacha na mali yako na vitu vyako lakini ukakosa kuingia uzima wa milele kwa sababu ya uasi wako ambao hutaki kuutubia, hata kama unatoa pesa nyingi sana kwa kazi ya MUNGU na kwa yatima na wajane, hata kama unatoa misaada mingi sana ya kijamii lakini kama umemwasi MUNGU na unaendelea na uovu wako bila toba basi unaweza kukosa uzima wa milele.
Baraka yako ya uzima wa milele inaweza kufutwa na dhambi zako za uasi kwa MUNGU. Matendo mema tu hayawezi kumuokoa Mtu bali Wokovu wa KRISTO ndio kuokoka kwenyewe, kama unadharau Neno la MUNGU hata matendo yako mema yatakuwa sii kitu. 
Huwezi Kupiga Hatua Katika Ufahamu Wa Neno La MUNGU Kama Huna Muda Wa Kulisoma Neno La MUNGU Na Kulitafakari.
Usifurahi kwa sababu mapepo yanakutii bali mche MUNGU katika njia zako zote.

Luka 10:20 '' Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.''

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments