HAKIMU ALIYE TOFAUTI NA MAHAKIMU WOTE

Na Askofu Mkuu Zachary Kakobe 
    
Siku ya kufa kwa mwanadamu fulani, ni siku ya mwisho wa dunia kwa mtu huyo.  Iko siku ya mwisho wa dunia kwa watu wote ulimwenguni, hata hivyo, iko siku ya mwisho wa dunia kwa mtu mmoja mmoja binafsi, nayo ni siku ya kufa kwake.  Nani kati yetu anayeijua siku ya kufa kwake?  Hakuna hata mmoja aijuaye.  Siku tusiyoidhani, ndipo tunapokutana na kifo.  Kifo siyo lazima kije kwa mtu baada ya kuugua kwa muda mrefu.  Hakuna kanuni.  Tunaweza tukapatwa na ajali, tunaweza tukalala usiku, halafu ndiyo ikawa mwisho wetu n.k.  Kifo hakina uzee au ujana au utoto.   Watoto wengine wamefariki na kuwaacha babu zao wakiwa hai! Ndiyo maana Biblia inasema katika MHUBIRI 9:12, “Maana mwanadamu naye hajui wakati wake; kama samaki wanaokamatwa katika nyavu mbaya, na mfano wa ndege wanaonaswa mtegoni, kadhalika wanadamu hunaswa katika wakati mbaya, unapowaangukia kwa ghafla”.
Sasa basi, baada ya kufa, kipi kinafuata? Bibia inatoa jibu katika WAEBRANIA 9:27, “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu”.  Baada ya mtu kufa, hupewa hukumu yake sekunde ileile.  Hakimu mwenye kuhukumu, hutoa hukumu kwa kila mtu na kuamua kama atupwe katika mateso ya Jehanam ya moto, au aingie mbinguni.
Hakimu huyu ni nani? Hakimu huyu, ni Yesu Kristo.  Maandiko yanaeleza jambo hili waziwazi.  Biblia inasema katika YOHANA 5:22, “Tena Baba hamhukumu mtu yeyote, bali amempa Mwana hukumu yote”.  Neno la Mungu pia linasema katika 2 TIMOTHEO 4:1, “Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake”.  Kwa msisitizo mkubwa, Neno la Mungu linaeleza waziwazi kwamba Hakimu huyu, ni Yesu Kristo (MATENDO YA MITUME 10:36, 42;  WARUMI 2:16).
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

     Watoto wengine wamefariki na kuwaacha babu zao wakiwa ha
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

 Sasa basi, ili kila mmoja wetu ajiweke katika nafasi nzuri ya mafanikio, siku ya hukumu; hatuna budi kufahamu mfumo wa kuhukumu wa Hakimu huyu Yesu Kristo.  Maelfu ya watu, wanahukumiwa kila siku kwenda kwenye mateso ya Jehanam ya moto, kwa sababu ya kukosa kuufahamu mfumo wa kuhukumu anaoutumia Hakimu Yesu Kristo.  Mfumo wa kuhukumu anaoutumia Yesu Kristo, ni tofauti kabisa na mfumo wa kuhukumu unaotumiwa na Mahakimu wa mahakama za duniani.
Katika mahakama za duniani kote, mshitakiwa husimamishwa kizimbani, na kusomewa shitaka au kosa lake.  Baada ya kusomewa shitaka, hakimu humtaka mshitakiwa akiri kosa au akane shitaka.  Mara mshitakiwa anapokiri kosa, kinachofuata ni kuadhibiwa vikali ili iwe fundisho kwa wengine.  Hata kama mshitakiwa akiomba msamaha kwa Hakimu huku akilia machozi, hiyo haitamsaidia kitu.  Katika mahakama hizi za duniani za mahakimu wanadamu, hakuna uwezekano wowote wa mtu anayekiri kosa, kusamehewa na hakimu.  Tendo la kukiri kosa, mbele ya mahakimu wa duniani, wakati wote huambatana na kuadhibiwa vikali bila huruma yoyote.  Ikiwa mshitakiwa atakana shitaka na kusema hakutenda kosa, ndipo kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.  Mfumo huu wa mahakama za duniani, unawafanya wakosaji kukana makosa yao hata kama wanajua fika kwamba walitenda makosa hayo; ili kesi zao zisikilizwe na hata uwepo uwezekano wa kuachiwa huru.  Mfumo huu wa kuhukumu wanaotumia mahakimu wanadamu, ni kinyume kabisa na mfumo wa kuhukumu anaoutumia Hakimu Yesu Kristo.
Mbele za Hakimu Yesu Kristo, mkosaji anapokana kosa na kuanza kujitetea, utetezi wake huo husikilizwi, na mara moja huhesabiwa miongoni mwa watu watakaotupwa katika adhabu ya moto wa milele.  Tendo la kukana kosa mbele za Hakimu Yesu Kristo, huambatana na kuadhibiwa vikali bila huruma yoyote.  Biblia inasema katika YEREMIA 2:35, “Lakini ulisema, sina hatia mimi; bila shaka hasira yake imegeuka na kuniacha.  Tazama, nitaingia hukumuni pamoja nawe, kwa sababu unasema, sikutenda dhambi mimi”.  Mbele za Hakimu Yesu Kristo, mtu anapokiri kosa na kuomba msamaha, husamehewa dhambi zake, na kukwepa adhabu.
Watu wengi wanakwenda kwenye mateso ya moto wa milele, kwa sababu hawako tayari kukiri kwamba ni wenye dhambi na kisha kutubu dhambi zao na kuomba msamaha kwa Yesu Kristo.  Tukitaka kumpendeza Mungu na kukaa naye milele mbinguni, hatuna budi kuiga mfano wa mwana mpotevu.  Yesu Kristo akielezea jinsi mwana mpotevu alivyokiri kosa lake na kwenda kuomba msamaha, anasema katika LUKA 15:17-23, “Alipozingatia moyoni mwake, alisema………… Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.  Akaondoka akaenda kwa babaye.  Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.  Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena.  Lakini baba aliwaambia watumwa wake, lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteni ndama Yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi”.  Unaona!  Sisi nasi tukiwa wepesi wa kukiri makosa yetu na kuomba msamaha kwa Mungu, Baba Mungu atatupenda sana, na kutufanyia karamu kubwa mbinguni milele na milele.
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .Nimekosa juu ya mbingu na mbele zako.  Sistahili kuitwa mwana wako 
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Yesu Kristo anasema katika LUKA 15:7, “Nawaambia, vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda (99) ambao hawana haja ya kutubu”.  Mungu anatafuta watu walio wepesi wa kukiri makosa yao na kuomba msamaha.  Akiwapata watu wa namna hiyo, siyo tu kwamba kutakuwa na furaha mbinguni, bali Mungu atawatumia sana watu hao katika kuonyesha uwezo wake kwa wanadamu.  Daudi alikuwa mtu aliyetumiwa sana na Mungu.  Jitu la miraba minne lililoitwa Goliathi, halikufua dafu mbele ya kijana mdogo Daudi (1 SAMWELI 17:23-24, 37-54).  Daudi alipendwa na Mungu kiasi ya kwamba hata Yesu Kristo alizaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi, na hata anaitwa pia Mwana wa Daudi!  Mungu alipendezwa na daudi kiasi ya kwamba tunasoma katika MATENDO 13:22, “Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua awe mfalme ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote”.
Daudi alifanya mapenzi gani ya Mungu?  Kwa nini Mungu alimtumia sana Daudi?  Alikuwa mtu mwenye roho iliyopondeka.  Alikuwa mwepesi sana kukiri makosa yake na kuomba msamaha kwa Mungu.  Hii ndiyo ilikuwa siri ya yeye kupendwa na Mungu na kutumiwa sana na Mungu.  Katika 1 MAMBO YA NYAKATI 21:8,  tunasoma, “Naye Daudi akamwambia Mungu, Nimekosa sana, kwa kuwa nimelifanya jambo hili; lakini sasa uuondolee mbali, nakusihi, uovu wa mtumwa wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa”.  Mpendwa msomaji, unataka kutumiwa sana na Mungu?  Uwe mwepesi kutubu kama Daudi.
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

  Unataka kutumiwa sana na Mungu? Uwe mwepesi kutubu kama Daudi
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Tofauti nyingine kati ya mahakimu wa dunia hii na hakimu Yesu Kristo ni hii.  Mahakimu wa duniani, kazi yao ni kuwaadhibu tu wakosaji, na kamwe hawawapi msaada wa kuwawezesha kuacha maovu yao.  Hakimu Yesu Kristo, amejaa upendo mwingi sana na rehema.  Hapendi kutuona tunaadhibiwa.  Kwa sababu hiyo, kila mtu anayemwendea katika hali ya kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha, mtu huyo hupata rehema zake.  Rehema zake, ni pamoja na mtu huyo kupewa msaada au uwezo wa kushinda dhambi, na pia wokovu, yaani kuwekwa huru mbali na adhabu ya moto wa milele (MITHALI 28:13;  AYUBU 26:2;  LUKA 1:77).
Mpendwa msomaji, je wewe unaweza ukadai kwamba huna kosa mbele za Mungu?  Je, wewe unaweza kusema hujatenda dhambi?  Biblia inasema katika MHUBIRI 7:20, “Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asiyefanye dhambi”.  Tena Neno la Mungu linasema katika 1 YOHANA 1:8-10, Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.  Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi na kutusafisha na udhalimu wote.  Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu”.
Mpendwa msomaji, unaweza labda ukasema hunywi pombe au hufanyi uasherati na uzinzi, huibi, hutukani au huvuti sigara; lakini je, hujakasirika au kusema uongo tangu uzaliwe?  Kama umefanya lolote kati ya haya, wewe ni mwenye dhambi.  Dhambi moja tu inatosha kutufanya tuhukumiwe na kutupwa katika moto wa milele, tusipokiri makosa yetu mbele za Hakimu Yesu Kristo.  Mpendwa msomaji, uwe kama Daudi, uwe kama mwana mpotevu; usitafute visingizio vya kujihesabia haki na kusema, “Nasali kila Jumapili”, au “Mimi nilipatizwa tangu utotoni”, au “Nina dini yangu nzuri sana”.  Hapa hatuzungumzii dini, tunazungumzia jinsi tutakavyosimama mbele za Hakimu Yesu Kristo.  Ni watakatifu tu watakaomwona Mungu (WAEBRANIA 12:14).
Mpendwa msomaji, wewe nawe, unaweza ukawa mtakatifu, mtu unayempendeza Mungu, ukifuatisha sala ifuatayo ya kukiri makosa na kuomba msamaha kwa dhati kutoka moyoni.  Yesu Kristo atakupenda sana na kukusamehe kwa hakika, na kukupa wokovu, bila kujali kwamba umefanya dhambi nyingi kiasi gani; kwa maana Yeye ni hakimu wa tofauti.  Sema hivi, “Mungu Baba, hakika mimi ni mkosaji, ni mwenye dhambi.  Siwezi kupuuza ukweli huu.  Natubu dhambi  zangu zote kwa kumaanisha kuziacha leo.  Yesu Kristo, nakusihi unisamehe dhambi zangu, na kunipa uwezo wa kushinda dhambi.  Futa jina langu katika kitabu cha hukumu, liandike katika kitabu cha uzima mbinguni.  Asante kwa kunisamehe na kuniokoa katika Jina la Yesu.  Amen”.  Mpendwa msomaji tayari umesamehewa dhambi zako, na kuokolewa.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho ya Neno la Mungu; katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook, Twitter n.k,  kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.
                                                         UBARIKIWE NA BWANA YESU!!!

Comments