JE, MNAMLIPA BWANA HIVI?

Na Askofu Mkuu Zakaria Kakobe
 
L
eo, tena, tunazidi kusonga mbele katika kijifunza KITABU CHA YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tunajifunza YOHANA 10:28-42.  Pamoja na kwamba kichwa cha somo letu ni “JE, MNAMLIPA BWANA HIVI?“, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho tunayojifunza katika mistari hii, katika vipengele tisa:-
(1)  MIMI NA BABA TU UMOJA (MST. 28-30);
(2)  VITA MFULULIZO KWA MKRISTO (MST. 31);
(3)  JE, MNAMLIPA BWANA HIVI? (MST. 32);
(4)  KUZIITA KAZI ZA MUNGU KWAMBA NI ZA SHETANI (MST. 33);
(5)  MIMI NIMESEMA NDINYI MIUNGU (MST. 34-36);
(6)  MAANDIKO HAYAWEZI KUTANGUKA (MST. 35);
(7)  KUAMINIKA KWA KUZITENDA KAZI ZA BABA (MST. 37-38);
(8)  MLANGO WA KUTOKEA KWA KILA JARIBU (MST. 39);
(9)  USHINDI MKUBWA BAADA YA VITA VIKALI (MST. 40-42).
(1)            MIMI NA BABA TU UMOJA (MST. 28-30)
Maneno haya aliyoyasema Yesu, “Mimi na Baba tu Umoja“, hayazungumzii Umoja kwa namna finyu tunayoielewa wengi wetu.  Maneno haya mahali hapa, yanamaanisha kwamba “Mimi nina uwezo uleule (MMOJA) alionao Baba“.  Yesu anawapa watu uzima wa milele, kama Baba naye anavyofanya (MST. 28; YOHANA 5:26).  Hakuna mtu anayeweza kuwapokonya watu katika mkono wa Yesu, maana ni mkuu kuliko wote, kama vilevile asivyoweza mtu yeyote kuwapokonya watu katika mkono wa Baba (MST. 28-29).  Maandiko yananena waziwazi kwamba YESU NI MUNGU kama alivyo Baba (TITO 2:13; 1 YOHANA 5:20).  Yesu na Baba NI UMOJA.  Yesu Kristo ni mkuu kuliko wote.  Mkuu wa ulimwengu, shetani hana kitu chochote anachoweza kukifanya kwa Yesu Kristo (YOHANA 14:30).  Hatuna haja ya kuogopa nguvu zozote za giza za shetatani, tunapokuwa na Yesu Kristo.
(2)            VITA MFULULIZO KWA MKRISTO (MST. 31)
“Wakaokota mawe TENA ili wampige“, ni maneno yanayotufundisha juu ya vita MFULULIZO kwa Mkristo awaye yote, na zaidi sana kwake yule aliyejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote.  Katika Kiyunani neno linalotumika katika mstari huu, ni tofauti na lile la YOHANA 8:59, ingawa katika Kiswahili neno hilohilo “WAKAOKOTA“, limetumika.  Neno la Kiyunani linalotumika hapa ni “EBASTSAN“ lenye maana “WAKABEBA“ mawe makubwa, mazito, ili wampige kwa hayo.  Mwanzano waliokota mawe madogo madogo, na sasa wanabeba makubwa zaidi!  Ni muhimu kujifunza hapa kwamba Shetani hataacha kutupiga vita katika maisha yetu yote ya Ukristo.  Kila siku atazidi kuongeza mbinu zake ili aupige wokovu wetu, ili aupige utumishi wetu na kuziharibu huduma zetu, azipige ndoa zetu, azipige kazi na biashara zetu, aupige ujauzito tulioupata, azipige mali tulizo nazo n.k.  Hata hivyo, hatuna haja ya kubabaika.  Kama Bwana wetu Yesu alivyoshinda, sisi nasi hatuna budi kushinda.  Watakatifu waliotutangulia, walipigwa vita wakati wote, lakini hawakukata tamaa na kukubali kushindwa!  Tuige mfano wao (2 WAKORINTHO 4:8-10, 16-18).
(3)            JE MNAMLIPA BWANA HIVI? (MST. 32)
Yesu Kristo alifanya mengi mema kwa watu hawa.  Aliwaponya vipofu waliokuwa ndugu zao, aliwaponya vilema, mabubu, viziwi, wenye pepo, wakoma na wenye mateso ya kila namna.  Aliwapa mikate na samaki pamoja na divai kwa miujiza mikubwa na mengi mengine yaliyokuwa mema.  Aliwafanyia mema maelfu kwa maelfu.  Je walimlipa nini hapa?  Walibeba mawe makubwa ili wampige kwayo!  Kizazi hadi kizazi, Mungu amefanya mengi mema kwa wanadamu lakini wanadamu wamemlipa mabaya.  Maswali ya Mungu kwa wanadamu anaowatendea emma ni haya, “Je, mnamlipa Bwana hivi?  Je, memeona dhuluma gani kwangu?  Je, nimewatenda nini?  Je, nimewachosha wka habari gani?“ (YEREMIA 2;5; MIKA 6:3; KUMBUKUMBU 32:6).  Wanadamu wengi hata leo, ndivyo tulivyo.  Muntu atatutunza na kutupa uhai, kutusomesha na kutupa kazi nzuri, lakini malipo yetu kwake itakuwa kulewa pombe, kuvuta sigara, kucheza dansi.  Wengine wameumbwa na kupewa sura nzuri, na malipo yao kwa Mungu, imekuwa ni kufanya uasherati na uzinzi!  Wengine wamekuja Siku ya Matendo ya Ajabu, na Mungu akawapa miujiza mingi ya kikazi, kibiashara, kifamilia, kutolewa pepo, kukponywa n.k., lakini malipo yao, yamekuwa kufanya dhambi na kumpuuza Mungu na neno lake.  Je, tunamlipa Bwana hivi?  Kufanya hivi ni sawa na kubeba mawe mazito na kumpiga.  Haitupasi kufanya hivi!  Kuna jambo jingine la kujifunza hapa.  Kama ilivyokuwa kwa Yesu, sisi nasi tutawafanyia watu wengi mema, lakini watatulipa mabaya na kutuchukia bure.  Haya yaliwapata watakatifu waliotutangulia, hivyo yatatupata na sisi, hatupaswi kuona ajabu (ZABURI 35:12-15; YOHANA 15:20, 24-25).
(4)            KUZIITA KAZI ZA MUNGU KWAMBA NI ZA SHETANI (MST. 33)
Yesu hapa anasema iliyo kweli kwamba Yeye ni Mungu, na watu hawa wanamwambia ANAKUFURU!  Yesu Kristo alipotoa pepo, walisema anatoa pepo kwa mkuu wa pepo, Beelzebuli, wakamkufuru na kuziita kazi za Mungu kwamba ni za Shetani!  (MATHAYO 12:22-24, 31; 9:32-34).  Yesu alipofanya kazi yake ya kusamehe dhambi, walisema pia anakufuru! (MATHAYO 9:1-3).  Ndivyo ilivyo, kizazi hadi kizazi, wamekuwepo watu waliojiona wao wako upande wa Mungu na kwa makosa makubwa wakawaona wengi waliokuwa wanamtumika Mungu kwamba wao wanafanya kazi za Shetani (ISAYA 66:5).  Hata wengine wamewaua watu wa Mungu, na kudhani kwamba wanamtolea Mungu ibada (YOHANA 16:2).  Hata leo ni vivyo hivyo, wako watu wengine ambao wamefunga na kuomba kwa Jina la Bwana wakiomba kazi mbalimbali za Mungu zisambaratike, huku wakidhani kwamba ni kazi za Shetani.  Haitupasi kutoka haraka kwa kukimbia katika mambo ya jinsi hii na kujikuta tumemkufuru Yesu Kristo (ISAY 52:12).
(5)            MIMI NIOMESEMA NDINYI MIUNGU (MST. 34-36)
Kwa Neno la Mungu, Mungu aliwaweka watu kadha kuwa viongozi wa Israeli waliokuwa wanatoa maamuzi.  Mungu mwenyewe, aliwaita Watumishi hawa wa Mungu, “MIUNGU“, na wana wa Aliye juu (ZABURI 82:1-6).  Ndivyo ilivyo hata leo, watu walioitwa na Mungu katika Utumishi wake, Baba huwaheshimu (YOHANA 12:26), na kuwaita “miungu“!  Sisi nasi Mungu anatuagiza kuwapa heshima MARADUFU KULIKO watu wengineo (1 TIMOTHEO 5:17).  Sasa hapa Yesu anasema, “Ikiwa hawa waliojiliwa na Neno la Mungu, waliitwa miungu, na wana wa Aliye juu, sembuse Yeye Yesu ambaye ndiye NENO LA MUNGU lenyewe? (UFUNUO 19:13,16).  Huyu yesu aliye Neno la Mungu, kuna ubaya gani akisema yeye ni Mwana wa Mungu au ni Mungu, maana Yeye ni ZAIDI SANA ya watumishi wake hawa!
(6)            MAANDIKO HAYAWEZI KUTANGUKA (MST. 35)
Yesu hapa anatufundisha kwamba maandiko hayawezi kutanguka.  Tusidanganywe na wanadamu wanaojaribu kuchuja maandiko na kuyatangua maandiko.  Hwa wanapotuambia ubatizo wa kunyunyiziwa maji usoni unatosha wakati hauko kabisa katika maandiko, wanatudanganya.  Tutahukumiwa kwa maandiko!  Maandiko yanasema amwahaye mkewe au mumewe na kumwoa au kuolewa na mwingine azini (LUKA 16:18), na wazinzi hawatauridhi Ufalme wa Mungu (1 WAKORINTHO 6:9), maandiko haya hayawezi kutanguka.  Tusikubali kudanganywa na wanadamu kwamba tutaishi na wake au waume wasio wa kwetu na kusalimika!  Maandiko pia yanasema “Msifuatishe namna ya dunia hii“ (WARUMI 12:2), na tena tusitende kwa mfano wa mataifa (KUMBUKUMBU 17:15).  Maandiko haya hayawezi kutanguka.  Kufikiri kwamba kuna wokovu pamoja na kukali nywele, kuweka rasta na rangi za kucha na midomo na kuvaa dhahabu, heleni na bangili, na kuwa kama mataifa, kufanya hivi ni kutafuta hukumu.
(7)            KUAMINIKA KWA KUZITENDA KAZI ZA BABA (MST. 37-38)
Tunaweza tukawa na madai ya haki kwamba baba yu ndani yetu nasi tu ndani ya Baba, ikiwa tunazitenda kazi za baba yetu aliye mbinguni.  Kucheza dansi na kuwa na ushabiki wa mipira ya ligi, na kusikia kipindi cha michezo cha mbili kasorobo, kufanya hivyo siyo kuzitenda kazi za baba yetu wa mbinguni.  Madai yetu kwamba tumeokoka, yatakuwa na msingi tu pale ambapo tunazitenda kazi anazoweza kuzitenda Mungu.  Tukiwa tunavuta sigara, kunywa pombe, kusema uongo, kujaa hasira na chuki, masengenyo n.k.
(8)            MLANGO WA KUTOKEA KWA KILA JARIBU (MST. 39)
Hapa walitafuta tena kumkamata, lakini akatoka mikononi mwao.  Hatupaswi kuogopa majaribu.  Kwa kila jaribu kuna mlango wa kutokea.  Kama Yesu alivyotoka mikononi mwa Shetani atatupa neema ya kufanya hivyo kwa Jina lake tukimwomba (1 WAKORINTHO 10:13).
(9)            USHINDI MKUBWA BAADA YA VITA VIKALI (MST. 40-42)
Baada ya Yesu kukabiliwa na vita hivi vikali na kunusurika kupigwa mawe, alikwenda ng’ambo ya Yordani kuitenda kazi ya Mungu na WENGI WAKAMWAMINI HUKO.  Ushindi mkubwa katika Utumishi wa Mungu hutokea baada ya vita vikali na Shetani.  Hatupaswi kubabaishwa na vita.  Tukiona vita imepamba moto, tujue ushindi mkubwa unakuja!
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Comments