JE UKO KATIKA KUELEKEA NDOA TAKATIFU?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze.
Mimi Peter Katika maisha yangu ya ujana nilikusudia tangu zamani  kufunga ndoa nikiwa na miaka 24 lakini haikuwezekana hadi nilipotimiza miaka 28 ndipo nikaoa. Miaka minne hiyo sio kwamba nilikuwa ninamchumba na wala sio kwamba miaka hiyo minne nilikuwa natafuta. Nilidhani kuwa kufunga ni jambo rahisi tu kama nitajiandaa kwa pesa na makazi lakini hiyo pekee haikutosha kufanya mambo kuwa rahisi katika kuelekea ndoa.
Sikuwahi kuona upinzani mkubwa katika maisha yangu kama upinzani wa kuelekea kufunga ndoa ndio maana kijana nakuletea ujumbe kama huu ili ukusaidie katika maamuzi yako ya kuelekea katika ndoa. 
Najua huwa kuna mambo mengi sana katika kipindi cha wachumba kuelekea ndoa.
Huwa kuna mambo mengi sana katika kijana kuelekea kupata mchumba ili waingie katika ndoa takatifu.
Wengi huwa wako katika maswali mengi sana, kama huyu ndiye mke/Mume Mwema? 
Je maisha ya ndoa yakoje?
Kwanini kuna wanadoa wanaishi vizuri sana katika ndoa zao na wengine ni mapigano tu kila siku?
Vijana husumbuka sana katika maswali hayo.
Ukweli ni kwamba ndoa ni paradiso ndogo kama tu wanandoa wote wawili wakijitambua na kumtanguliza BWANA YESU  katika maisha yao. 
Yakobo 4:7 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.''

Kumtii MUNGU kwa wanandoa ni jambo la lazima kama wanahitaji ndoa yao iwe na baraka za MUNGU.
Leo sizungumzii ndoa ila nazungumzia vijana wanaotarajia kuingia katika ndoa, Ndoa nimeshaiandikia masomo mengi sana lakini leo nataka kuongelea wanaotarajia kuingia katika ndoa zao.

 Waefeso 4:27 ''wala msimpe Ibilisi nafasi.''

Ukimpa shetani nafasi katika maisha yako ya ujana hakika atakuharibia kila kitu, ndio maana Neno la MUNGU linakutaka kwamba usimpe shetani nafasi hata moja katika ujana wako.

Ewe kijana au binti unayetarajia kuoa au kuolewa jitahidi sana kuepuka mazingira yeyote yanayoweza kukusababishia uasherati.
Hata mchumba kama unaye anaweza kukuacha kabla ya ndoa kama tu utamkubalia mfanye uasherati maana atagundua kwamba wewe ni rahisi sana na kama umemkubalia yeye basi atajua kabisa kwamba wewe hata wengine aidha umeshawakubalia hivyo hivyo au utawakubalia baadae hivyo anakushusha viwango, kutoka mchumba anayetakiwa amuoe na kukuona tu kama malaya fulani asiye na akili.

Yakobo 4:4 '' Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa MUNGU? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa MUNGU. ''

  Najua unatamani sana kuolewa na mume mwema lakini mume mwema hapatikani katika kundi la wazinzi na waasherati hivyo kataaa uasherati katika maisha yako.
Najua kanisa unatamani kuoa mke mwema lakini mke mwema siku zote hapatikani katika kundi la waasherati.
Kukataa uasherati ni kupalilia ndoa njema baadae ambayo haitakuwa na kutokuaminiana.
Unaweza kwa sasa ukadhani unamkubalia huyo kijana ili mfanye ngono kwa kudhani unatengeneza kumbe unaboamoa maana huyo huyo baada ya ngono atageuka na kuanza kukuona kama kahaba tu unayekubali hovyo hovyo.

 '' Maana Haya Ndiyo Mapenzi Ya MUNGU, Kutakaswa Kwenu, Mwepukane Na Uasherati- 1 Thesalonike 4:3.''

Mabinti wengi hawaolewi kwa sababu ya tabia ya zinaa.
Zinaa ni dhambi mbaya sana.
Zinaa inanajisi mwili na roho pia.
Dhambi zote ni nje ya mwili lakini zinaa ni katika mwili na zinaa huacha maagano ya kishetani.katika mwili.


1 Kor 6:18 ''Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. ''

Mr & Mrs Peter Mabula.
Unaweza ukatamani sana kupata mchumba lakini wachumba hawaji kumbe ni kwa sababu ya uasherati wako ambao uliufanya zamani na kukuachia maagano.
Inawezekana kabisa sura yako ni nzuri sana na mtaani wanakuita miss lakini hujawahi kupata mchumba kwa sababu tu ya maagano ya uasherati ulioufanya zamani.
Inawezekana kabisa una umbo zuri sana na mitaani vijana hukupigia miluzi kila mara lakini hujawahi kupata mchumba halisi kwa sababu ya maagano ya uasherati uliofanya.
Ndugu, jitenge na zinaa katika maisha yako.
Zinaa ni uzinzi na uasherati tena Zinaa ni uzinifu.
Izike dhambi ya zinaa leo kwa kuacha uzinzi na uasherati.
Okoka leo na kama umeokoka tayari basi badilika kuanzia leo kwa kuanza kumcha MUNGU wa mbinguni.

BWANA YESU anakungoja umpokee na uache dhambi zote ikiwemo zinaa ili akuandike jina lako katika kitabu cha uzima.
Bora kupeleka watu 2 mbinguni kuliko kuwa na kundi la waumini zaidi ya 3000 wanaoenda jehanamu.
Ndugu zangu ni wakati wa kuokoka.
Ni wakati wa kumpokea BWANA YESU anayeokoa.
Ni wakati wa kuishi maisha matakatifu.
Kuna makanisa hata hawana habari na YESU wala hawana habari na kuishi maisha matakatifu.
Kuna makanisa vijana ni waasherati sana na hawajawahi kukemewa wala kutengwa wala kufukuzwa.
Ukiwa kiongozi katika kanisa kama hilo utakuwa huwasaidii watu wako kwenda mbinguni bali ziwa la moto.
Uasherati kwa vijana wateule wakati mwingine unaweza kusababishwa na viongozi wasio na makali ya kukemea.
Lakini uasherati huo ukiota mizizi ndio chanzo cha vijana wengi kujikuta hawaoi wala hawaolewi, maana kuishi kwao tu ni kama wameoana.


Yohana 4:24 ''MUNGU ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. ''

Kama kijana uko katika kundi la waasherati nakuomba sana jitenge leo na uasherati na anza kumcha MUNGU katika kweli.
Mwabudu MUNGU wa mbinguni katika Roho na kweli daima.
Uasherati wa leo unaweza kuja kukufanya maisha yako yote usipate mke au wewe mwanamke usipate mume. Utakuja kusema una laana kumbe laana ni wewe mwenyewe.


 Ukijaribu kumchanganya MUNGU utakuwa unajichanganya wewe mwenyewe. Ni heri uwe moto tu au uwe baridi tu.
Kama kanisani uko na kwenye uasherati pia uko usitarajie kupata mchumba mwema kutoka kwa MUNGU.
Kama kwenye kwaya uko na kwenye disko uko usitarajie kupata kitu chema kutoka kwa MUNGU.
Kama unatamani kumpata mke mwema au mume mwema wakati wewe hata hufanani kuwa mwema basi hakika tarajia kumpata wa kufanana na wewe yaani utampata mzinzi mwenzako, maana na wewe pia ni mzinzi. Na huyo mzinzi utakayempata usidhani hata siku moja kwamba umepewa na MUNGU bali utakuwa umepewa na tamaa yako ya macho.
Ni muhimu sana wewe kumcha MUNGU katika ujana wako na hiyo itakusaidia kuwa mcha MUNGU mzuri katika ndoa.
YESU anaokoa hata leo hivyo okoka ndugu na kama umeshaokoka geuka na acha michanganyo yako ya dhambi.
Jitahidi sana kukumbuka pia kwamba hakuna mbingu ya wazinzi na wala waasherati.


 '' Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; -Isaya 1:16-19 '' 

 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments