JE UNA MCHUMBA AU UNA WACHUMBA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.




BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Uchumba ni hatua ya kuelekea katika ndoa lakini lakini sio kila wachumba wote wanamipango ya kuingia katika ndoa.
Mmoja anaweza kupanga kuingia katika ndoa lakini mchumba wake akawa hana mpango wa kuingia katika ndoa.
Kuna watu wana wachumba wa matazamio tu na sio kuoa/kuolewa.
Uchumba mwingine umeharibika kwa sababu ya uasherati na machukizo mengine.
 Marko 7:21-23 ''Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.''

Uchumba mwingi umeishia kwenye uasherati  na uongo na kufutika uchumba huo, huku uchumba huo ukiacha maumivu kwa upande mmoja.
Uchumba mwingi umeishia kwenye mimba na kuharibiana mipango mizuri ya maisha.
Uasherati ni machukuzo kwa MUNGU.
Uasherati ndio chanzo kikuu cha chumba nyingi kuvunjika.
Wachumba wakiushinda uasherati hakika itakuwa rahisi kwao kuwa na ndoa njema. 

Waefeso 5:3 ''Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;''

Kama mchumba wako anakutajia uasherati na wewe unafurahi hakika nyie wote hamjitambui na hamjui hatari iliyo mbele yenu.
 Ewe Binti Jiulize, umekubali Kuchezewa Ukitarajia Kuolewa? 
Nakupa Pole Sana Maana Unaweza Ukakosa Ndoa Na Ukakosa Na Mbingu Pia. Mwenye Sikio La Kusikia Asikie Leo.

Watongozaji Ni Wengi Sana Ila Waoaji Ni Wachache Sana. Uwe Makini Binti Maana Watongozaji Wanauhitaji Mwili Wako Tu Huku Wewe Hawakutaki, Ndio Maana Hawawezi Kukuoa Maana Huwafai, Wanataka Tu Huo  Mwili wako Wautumie Kisha Miaka au miezi  Michache Ijayo Wakiona Umekongoroka Wanakuacha Na Kutongoza Wengine. Kama Hutamcha BWANA Wakati Huu inaweza kuja  Kukughalimu Sana Baadae.

 Kuna wengine wana matatizo ya kuwatukana ambao wanakuja kuwachumbia
Binti Ambaye Hujaolewa Unayemtukana Kila Mchumba Anayetaka Kukuchumbia, Je Unamjua Atakayekuoa? Unauhakika? 
Kama Kijana Humtaki Kwanini Usimwambie Tu Kwa Upole Na Adabu Kwamba "mimi Sipo Tayari Kuolewa Na Wewe" Na Sio Kumwambia "wewe Mjinga Nini! Nani Akukubali Wewe, Wewe Na Wewe Kwani Ni Mwanaume?".
 Si Lazima Umkubali Kama Humpendi Lakini Ni Ujinga Kumtukana Kisa Anataka Kukuchumbia Ilihali Hana Kazi. Kama Kijana Ni Mcha MUNGU Na Amefuata Taratibu Zote Za Kikanisa Na Utakatifu Nakuomba Usimtukane Maana Hujui Hasa Ni Nani Atakuoa Na Huyo Unayemtegemea Atakuoa Ni Mwanadamu Tu Na Muda Wowote Anaweza Kubadirika. 
Wengine wakipishana na kusudi la MUNGU huja kujuta baadae.

Binti mmoja alipata mchumba na wakaendelea na uchumba kwa miezi 2 kisha wakadanganyana na kufanya dhambi ya uasherati. Baada ya muda mfupi yule binti akawa mimba na kijana akamuacha yule binti akidai alikosea kuchagua. Yule binti akataka kujipeleka jehanamu kwa kutaka kujiua, baadae kidogo siku hiyo hiyo mama yake akamuona na kumhoji na kugundua kwamba yule binti yuko mimba. Mama yule kwa hasira nyingi alimchukua yule binti yake na kumpeleka kwa kijana kisha akamwambia kama ana nguvu basi amwache binti yake. Yule kijana kwa kuogopa maneno ya mama akaanza maisha na yule binti hadi alipojifunga. Baada ya kuzaa yule kijana alitafuta pesa akitaka ampe yule binti ili binti akaanze maisha yake huku yule kijana akidai kwamba alikosea kuchagua. Yule binti akakataa na wameendelea kuishi katika ndoa na wamezaa watoto lakini kipigo ni kikubwa kila mara. Yule binti yuko katika ndoa lakini anasalitiwa na kuonewa akiambiwa alijipendekeza kuolewa. Uchumba huo kwa sababu ya uasherati uliharibika na hata kama mama alilazimisha ndoa lakini bado haijawa ndoa ya furaha na amani. 
Wangapi leo wamezalishwa tu na kuachwa?
Ni wengi hakika ndio maana ROHO wa  MUNGU anatupa ujumbe kama huu ili kuwaponya na kuwasaidia wale ambao wanatarajia kuingia katika ndoa kwamba uasherati ni sumu namba moja ya uchumba.
1 Thesalonike 4:3-5 ''Maana haya ndiyo mapenzi ya MUNGU, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua MUNGU.'' 

Wewe uliye katika uchumba usikubali kutii ushauri mbaya kutoka kwa mchumba wako au marafiki zako maana Kuna Watu Wameachana Na Wachumba Zao Kwa Sababu Ya Kutii Ushauri Mbaya Kutoka Kwa Watu Wabaya ulioleta dhambi na uharibifu.
Binti mmoja alikuwa na wachumba wanne na wote walimwacha kwa sababu ya uongo wake uliokuja kugundulika.
Hebu jiulize tu ndugu, Una Wachumba 4 Na Kila Mchumba Anajua Wewe Ni Mchumba Peke Yake Kwako. Kila Mmoja Anajua Wewe Utakuwa Mke Wake Au Mume Wake. Unaona Raha Tu Kuwadanganya Ili Kuja Kuwaumiza Baadae Baada Ya Kufunga Ndoa Na Mmoja Wao. Ndugu Unayefanya Hivyo Unakosea Sana Na Hakika Hiyo Haifai Kuwako Katika Watu Wa MUNGU. Kama Mtu Humpendi Mweleze Ili Ubaki Na Huyo Mmoja Umpendae, Sio Kuwapotezea Muda Watu Kwa Akili Zako Za Kitoto. Unajua Kabisa Huwezi Kuoa/kuolewa Na Wote Wanne Kwanini Huwaelezi Ili Na Wao Waende Kuchumbia/kuchumbiwa Kwingine Kule Watakapopendwa Kama Asali? . Kuwa Mkweli Na Kusema Kweli Siku Zote Linatakiwa Kuwa Ni Vazi Analotakiwa Kulivaa Kila Mwanadamu Mcha MUNGU.
Ndugu  Mche MUNGU Katika Hali Zako Zote.

Zaburi 106:39-40 ''Ndivyo walivyotiwa uchafu kwa kazi zao, Wakafanya uasherati kwa matendo yao. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya watu wake, Akauchukia urithi wake. '' 

 Uasherati Ni Pepo Baya Sana, Kuendekeza Uasherati Ni Kuyatii Mapepo. Ole Wake Mtu Yule Anayeyatii Mapepo/mashetani maana asipotubu anaweza kuishia pabaya.
Ukianza Vibaya Ni rahisi kumaliza Vibaya. Ukianza Vizuri Ni Rahisi Sana Kumaliza Vizuri Kama Ukiamua Kumaliza Vizuri. Ndugu, Anza Vizuri Leo Kwa Kumpokea YESU Na Kuishi Maisha Matakatifu.
Kijana Akijitambua Wakati Wa Ujana Wake Hata Akamcha MUNGU Siku Zote Hakika Katika Utu Uzima Wake Kuna Vikwazo Vya Kipepo Hata Havitamgusa.

Wagalatia 6:7-8 ''Msidanganyike, MUNGU hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa ROHO, katika ROHO atavuna uzima wa milele. ''

 Kuna wengine wamewaacha wachumba zao kwa sababu tu ya umasikini wa wakati huu. Ndugu inawezekana Kabisa Maskini Wa Juzi Ndio Kawa Tajiri Wa Jana. Inawezekana Kabisa Tajiri Wa Jana Ndio Kawa Maskini Wa Leo. Pia Inawezekana Kabisa Tajiri Wa Leo Ndio Atakuwa Maskini Wa Kesho. Pia Ni Muhimu Sana Kujua Kwamba Maskini Wa Leo Anaweza Kuwa Ndio Tajiri Wa Kesho. Usimdharau Mtu Kwa Sababu Ya Hali Yake Ya Wakati Huu. Binti Usimdharau Kijana Mchumbiaji Na Kuanza Kumdhalilisha Na Kumtangaza Kisa Tu Ni Maskini Leo. Baba Usimdharau Mkeo Kwa Sababu Tu Ya Umaskini Wa Ndugu Zake Wengi Na Wanakutegemea. YESU Ni Wa Wote Na Anaweza Kumbariki Yeyote Na Wakati Wowote.
Muhimu kwako katika kuchagua mchumba hakikisha huyo mchumba ana YESU ndani yake, Ameokoka na anaishi maisha matakatifu katika wokovu.
 Pia elewa kwamba  kuna wacha MUNGU  na wacha shetani  na hao wanachowaza ni uasherati tu na kukuachia maumivu makali baada ya kukuacha au kukubebesha mimba na kukuacha ukihangaika.
Kuna kizazi cha watenda dhambi hivyo jitenge na anayetaka akuingize kwenye dhambi.
Mithali 30:12 ''Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe; Ambao hawakuoshwa uchafu wao. ''
 Usiwe mmoja wa wanaotaka kuingia katika uchumba ili wapate wa kuzini nao.

Unakuta Binti mzuri Kweli Lakini mzinzi, Ajabu analia Kila Siku Kwenye Maombi Ili apewe Mume Mwema. Kuna Wakati analalamika Kwamba ana Mkosi Maana Wengine Wanaolewa Lakini yeye Hapana. Amesahau Kwamba hana Mikosi Ila ana Mkosi Mmoja Tu Uitwayo Uasherati. Kuna Wakati anavaa Kikahaba Ndio Maana Baraka Ya Ndoa Badala Ya Kusogea Karibu Ndio Inasogea Mbali. Siku  binti kama huyu akijitambua Tu ataolewa Lakini akigoma Kujitambua atajikuta anaota Mvi Bila Kuolewa. akijitambua akatubu Na Kuacha Dhambi Hakika ataolewa.
Ni wakati wa kuwa makini sana katika uchumba.
Binafsi pia huwa sishauri uchumba wa muda mrefu maana huo unaweza kuzaa mazoelea mabaya na kuja kuvunjika kabla ya ndoa.
Uchumba wa muda mrefu ni rahisi sana kuzaa uasherati.
Jambo jingine Wachumba Wa Mwendokasi Siku Hizi nao Ni Wengi Kweli. Wanabebeshana Mimba Katika Uchumba Wao Kisha Wanaanza Kuwapelekesha Wachungaji Na Wazazi Wao Kwamba Wawafungishe Ndoa Haraka Kumbe Lengo Lao Sio Ndoa Ila Ni Kuficha Mimba. Ndugu Nakuonya, Mtii MUNGU Na Sio Kuitii Dhambi.
Tambua kwamba ''Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima;-Mithali 11:16A''

  Ndugu usikubali uasherati  na uzinzi kwa sababu kuna Maagano Ya Kipepo Katika Uzinzi Na Uasherati. 
Je, Wewe Una Maagano Mangapi Katika Hili? 
Je, Umewahi Kuyafuta Kwa Damu Ya YESU? 
Je, Unadhani Yalifutika Kama Uliendelea Na Uzinzi au uasherati? 
 Je Unajua Kazi Za Maagano Ya Kipepo Katika Maisha Yako?. Nakuomba Mwendee Mchungaji Wako, Kawe Wazi Mbele Zake Na Mbele Za MUNGU Juu Ya Dhambi Hiyo atakusaidia kwa maombi na ushauri.
Yakobo  4:7-10 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza. ''
  Jambo la mwisho kwa leo ni hili; Kadri Unavyozidi Kumkosea MUNGU Ndivyo Baraka Zako Zinavyozidi kusogea Mbali Na Wewe. Kama Ulikuwa Hujui Naomba Leo Ujue.
Jitahidi kumsogelea MUNGU na sio kusogea mbali na MUNGU.
Msogelee MUNGU kwa kuokoka na kuacha dhambi.
Msogelee MUNGU kwa kuishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU. 
Kama ni wachumba na mlianguka dhambini tubuni na kuacha uovu huo tena.
Mwambieni mchungaji wenu awaombee toba na msikubali kurudi katika dhambi hiyo.
Mkimtii KRISTO na kutokurudia uovu huo hakika haki yenu ya ushindi na uzima mnarudishiwa.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments