MSAMAHA NI ULINZI KWAKO

Na Mtumishi Dk Frank P. Seth

“Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe.Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe” (Luka 17:3, 4).
“Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu” (Marko 11:25)

Ukitaka kuishi maisha ya JANA na hayo yakawa KAMBA mguuni ya kukushika usile RAHA za maisha ya LEO na KESHO (mema ya nchi), endelea kutoSAMEHE!
Kuna kusamehe kwa namna tatu: Kwanza, KUJISAMEHE mwenyewe kwa sababu umefanya jambo ambalo hukupenda kulifanya; Pili, kumsamehe mtu aliyekukosea kwa sababu AMEOMBA MSAMAHA na Tatu, kumsamehe mtu aliyekukosea kwa sababu UNATAKA KUVUKA hatua nyingine ya KUFANIKIWA.
Ukiangalia Luka 17:3&4, utaona BWANA Yesu ametumia neno, “jilindeni”, yaani pateni ulinzi au kuweni salama kwa kusamehe! Faida ya MSAMAHA ni kwa ANAYESAMEHE kwanza, ndipo huenda kwa MSAMEHEWA.
Faida ya kusamehe tunaiona kwenye Marko 11:25, ili usamehewe makosa yako, IMEKUPASA kusamehe wengine makosa yao. Kwenye sala ya Bwana, tunasema “utusamehe KAMA tunavyowasamehe waliotukosea” (Mathayo 6:12). Kipimo cha kusamehewa ni jinsi unavyosamehe wenzako! Kuna watu wanadhani wasipomsamehe mtu wanamkomoa! Kimsingi, hapo unajikomoa mwenyewe!
Faida nyingine ya KUSAMEHE ni kuwa na AMANI moyoni mwako. “Huwezi kumwona Mungu usipokuwa na amani na watu wote” (Waebrania 12:14); Utawezaje kuwa na amani na watu ambao hujawasamehe? Watu ambao una kinyongo nao? Usisahau, kumwona Mungu sio tu huko baada ya maisha haya (kufa), hata kumwona katika mambo yako ya kila siku Akikupigania! Uchungu na vinyongo ni ADUI yako, Jilinde!
Watu wengi ni WAGONJWA [magonjwa yasiyoambukizwa kama presha, msongo wa mawazo, shinikizo la damu, nk.] kwa sababu wamebeba UCHUNGU (bitterness) na VINYONGO (resentment). Hali hii inauwezo wa kuathiri mfumo wako wa MAWAZO na MAAMUZI. Mfumo wa mawazo na maamuzi ukiathirika, UCHUMI wako na MAENDELEO yako ya kimwili na kiroho yanaathirika pia. Jilinde!
Kuna mtu alisema, “kutokusamehe ni sawa na kunywa sumu ukitarajia mtu mwingine afe.”
Frank P. Seth

Comments