ROHO MTAKATIFU ANAVYOONGOZA WANA WA MUNGU KUTEMBEA NA MUNGU KATIKA MAENEO MBALIMBALI YA MAISHA YAO.

Na Mwl. Christopher Mwakasege.
Jina la Yesu Kristo litukuzwe milele!
Leo nataka kuanza mfululizo mwingine wa somo, ambao naamini utakuwa wa msaada sana kwako, katika kuimarisha uhusiano wako na Mungu.

Mfano na 1: Tunaposoma kitabu cha Matendo ya Mitume 27:10, tunaona jinsi mtume Paulo alivyoarifiwa na Roho Mtakatifu, juu ya hatari iliyokuwa mbele yake, katika safari aliyokuwa nayo na wenzake.
Mtume Paulo akawaambia wenzake hivi: “naona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi si ya shehena na marikebu tu, ila na ya maisha yetu pia”. Na jambo hili likatokea kweli kama alivyosema!
Swali la msingi la kujiuliza hapa ni kutaka kujua mtume Paulo alijuaje juu ya hatari ile! Roho Mtakatifu alitumia njia gani kumjulisha kwa uwazi namna ile? Je, na sisi leo Roho Mtakatifu anaweza kutujulisha juu ya hatari zilizo mbele yetu na tukauelewa ujumbe wake?
Mfano na 2: Je! Unafahamu mtume Paulo na wenzake walikuwa wanaamuaje juu ya eneo la kwenda kupeleka neno la Mungu? Ukisoma habari zao kwenye biblia, utajua ya kuwa ni kwa msaada wa uongozi wa Roho Mtakatifu.
Kuna wakati walikuwa wakipita nchi za Frigia na Galatia zilizokuwa Asia, wakitaka kulihubiri neno la Mungu huko. Biblia inasema walikatazwa “na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia” (Matendo ya Mitume 16:6).
Biblia inaendelea kutueleza juu ya safari yao hiyo ya kwamba: “Walipofika kukabili Misia wakajaribu kwenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa” (Matendo ya Mitume 16:7). Na baada ya hapo, Roho akawapa kufahamu kuwa, walitakiwa kwenda Makedonia kuhubiri neno huko. Na ndivyo walivyofanya!
Swali la msingi la kujiuliza hapa, ni kutaka kujua walijuaje kuwa katika wazo walilokuwa nalo, Roho Mtakatifu alikuwa anawakataza wasilifanye, au anawanyima ruhusa wasilifanye? Na ikiwa Roho Mtakatifu ana wazo analotaka walitekeleze walilijuaje?
Je! Kwetu sisi – tulio wana wa Mungu kipindi hiki, tunaweza kupata msaada wa Roho Mtakatifu kuhusu mahali pa kwenda, au mahali pa kutokwenda, kama akina mtume Paulo walivyosaidiwa?
Na ikiwa ni hivyo – ina maana si suala la mtoto wa Mungu kuamua kwenda mahali popote atakavyo, bali hili ni muhimu ajue wazo la Roho Mtakatifu aliye naye ndani yake kuhusu safari yake hiyo!
Mfano na. 3: Roho Mtakatifu ndiye aliyemsaidia Yesu kuchagua wanafunzi wake kumi na wawili. Biblia inasema habari hizi za Yesu ya kuwa: “Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume” (Luka 6:12,13).
Habari hii haituambii moja kwa moja ni kwa namna gani, na kwa njia gani Yesu aliweza kufanya maamuzi ya nani amchague, na nani asimchague “miongoni” mwa wanafunzi wengi aliokuwa nao wakati ule!
Kwa msomaji yeyote wa biblia, anajua ni Roho Mtakatifu aliyemsaidia kufanya uchaguzi wa watu wa kukaa naye karibu! Lakini swali la kujiuliza ni kutaka kujua Roho Mtakatifu alimsaidia kwa njia zipi?
Nina uhakika tukijua jinsi Yesu alivyosaidiwa katika hili, itakuwa ni rahisi kwetu kusaidiwa na Roho Mtakatifu kujua watu wa kuwa nao karibu, na watu wa kukaa nao mbali! Pia naamini tunaweza kujua ni nani wa kushirikiana naye, na ni nani wa kutoshirikiana naye!
Biblia inasema katika Warumi 8:24 tunasoma ya kwamba: “wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu”.
Na Yesu akizungumza juu ya Roho Mtakatifu atakapokuja kwenye maisha ya wanafunzi wake alisema: “Lakini yeye atakapokuja huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote;…na mambo yajayo atawapasha habari yake” (Yohana 16:13).
Nataka ujue ya kuwa, ikiwa wewe ni mtoto au mwana wa Mungu, ni haki yako itokayo kwa Baba yako, yaani Mungu, kuongozwa na kutegemea kuongozwa na Roho Mtakatifu!
Uwe mtumishi wa Mungu au usiwe mtumishi wa Mungu – ili mradi tu wewe ni mtoto wa Mungu; Roho Mtakatifu uliye naye amepewa jukumu la kukusaidia, ikiwa ni pamoja na jukumu la kukuongoza katika maisha yako ya kila siku!
Ndani ya mfululizo wa somo hili, tutajifunza njia kadhaa anazotumia Roho Mtakatifu kumwongoza mwana wa Mungu. Kwa hiyo nakuombea kwa Mungu, akuwezeshe kukaa mkao wa kujifunza somo hili!


 Leo nataka nikushirikishe kile kilichonisukuma kujifunza jinsi Roho Mtakatifu anavyoongoza watoto wa Mungu, na kwa kujifunza hili nipate kujua Mungu anavyoongea na watu!Sifundishi somo hili kwa sababu tu ya kutafuta somo la kufundisha, la hasha! Bali ni kwa sababu Mungu aliyenifundisha mimi, anataka nikushirikishe na wewe yale niliyojifunza kwake!
Niliokoka mwaka 1983 nikiwa nyumbani kwa wazazi wangu, walipokuwa wanafanya kazi eneo la Rongai lililoko “West Kilimanjaro” – mkoani Kilimanjaro.Jambo mojawapo lililojitokeza ndani yangu baada ya kuokoka, lilikuwa ni kiu kubwa ya kutaka kumjua Mungu zaidi na kumtumikia! Na kadri siku zilivyokuwa zinaendelea – kiu hiyo pia ilikuwa inaongezeka!
Miaka miwili baadaye – yaani mwaka 1985, liliingia moyoni mwangu wazo la kutaka kuacha kazi niliyokuwa nafanya serikalini mjini Arusha, ili niende chuo cha biblia kusomea uchungaji.Nilitafuta chuo cha biblia cha kusomea uchungaji – nikapata! Nilizungumza na viongozi wa chuo hicho, juu ya namna ya kujiunga na chuo chao ili kusomea uchungaji – wakanielekeza! Nikatafuta wafadhili wa kulipia gharama zangu za kusomea uchungaji – nikawapata! Nikatafuta nyumba ya kukaa na familia yangu nikiwa chuoni – nikapata!
Mambo hayo yalinichukua karibu muda wa mwaka mzima kuyakamilisha! Nikaanza kufuatilia kutaka kujua utaratibu wa kuacha kazi niliyokuwa nafanya serikalini, ili nikajiandae kwenda chuo cha biblia kusomea uchungaji.Siku moja nikiwa nimekaa kwenye uwanja mbele ya nyumba niliyokuwa naishi wakati ule, jioni baada ya kutoka kazini, nilishangaa na kushituka kuona Mungu akinisemesha wazi wazi moyoni mwangu!
Mungu akaniambia: “Mimi sikukuita uwe mchungaji! Chuo unachotaka kwenda kusoma kinaandaa wachungaji, wakati wito wako wewe si uchungaji. Kaa ulipo, usiache kazi kwa sasa, nitakwambia nilichokuitia, na nitakufundisha mwenyewe namna ya kuenenda kwenye wito huo!”
Maneno ya ujumbe huo yalinishitua na kunishangaza sana! Nilishangaa kwa sababu ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kumsikia Mungu waziwazi akisema moyoni mwangu, na kunielekeza cha kufanya!Nilishituka kwa kuwa niliwaza juu ya watu wengi “niliowasumbua” katika kutafuta chuo cha biblia ili nijiunge nacho – huku wakiwa na utayari wa kunisaidia! Moyoni iliingia “hofu” na kujiuliza namna ya kuwaambia kuwa uchungaji si wito wangu, na kwamba nilifanya makosa kuwaomba wanisaidie kabla sijamsikia Mungu juu ya kile alichoniitia!Lakini Mungu alinisaidia katika hilo – maana niliwatafuta, na nikawaomba msamaha kwa usumbufu wangu kwao!
Wakati huo huo niliingia katika maombi mbele za Mungu ili anifundishe kusikia sauti yake! Maana baada ya kosa hilo nililolifanya – nikatambua ya kuwa kuishi bila ya kujua Mungu anaongeaje na watu, ili awape maelekezo yake, kuna gharama kubwa sana kwa mwanadamu!Na baada ya maombi hayo, Mungu alianza kunifundisha jinsi ya kuisikia sauti yake, na namna ya kuongozwa na Roho Mtakatifu wake. Na hata sasa bado anaendelea kunifundisha!
Baadhi ya njia anazotumia kusema na kuongoza watu wake alizonifundisha ni hizi:
(i) Kutambua “neno la biblia” lililotumwa kwangu binafsi ili linisaidie na kuniongoza (Isaya 55:11).
(ii) Kwa kufuata “ushuhuda wa Roho Mtakatifu” ndani ya roho yangu (Warumi 8:14, 16);
(iii) Kwa kuyatambua na kuyaelewa “Mawazo yake” anapoyaweka moyoni mwangu (Yeremia 29:11);
(iv) Kwa kutumia “amani yake” moyoni mwangu (Wakolosai 3:15);
(v) Kwa kutumia “huzuni yake” moyoni mwangu (2 Wakorintho 7:8 – 11);
(vi) Kwa kutumia “Uhuru wa Roho Mtakatifu” ndani ya moyo wangu (2 Wakorintho 3:17);
(vii) Kwa kutumia “dhamiri yangu” katika Roho Mtakatifu (Warumi 9:1);
(viii) Kwa kutumia “maono” ya Ki – Mungu (Matendo ya Mitume 26:19,20);
(ix) Kwa kutumia “Karama za Roho Mtakatifu” (1 Wakorintho 12: 4 – 11);
(x) Kwa kutumia ndoto (Ayubu 33:14,15)
Usikose kusoma somo la wiki ijayo nitaendelea kukupa maelezo zaidi juu ya njia hizi zinavyofanya kazi!

Comments