Roho Mtakatifu anavyoongoza wana wa Mungu, kutembea na Mungu katika maeneo mbalimbali ya maisha yao-2

Na Mwl Christopher Mwakasege.
Shaloom!
Bwana Yesu asifiwe sana!
Tunaendelea na mfululizo wa 2, wa somo hili la “Roho Mtakatifu anavyoongoza wana wa Mungu, kutembea na Mungu katika maeneo mbalimbali ya maisha yao”.
Ukisoma kitabu cha Matendo ya Mitume 16:6-10, utaona ya kuwa, Paulo na Timotheo walikabiliwa na changamoto nzito ya kutaka kujua mapenzi ya Mungu kwao ni yapi – kati ya kwenda kuhubiri Frigia, au Galatia, au Misia, au Bithnia, au Troa, au Makedonia!
Inawezekana walipelekewa mialiko ya kwenda kuhubiri injili, toka sehemu zote hizo 6, kwa wakati mmoja. Na walikuwa na kazi kubwa ya kufanya maamuzi waende wapi!
Biblia inatuambia ya kuwa wakati wanapita “katika nchi ya Frigia na Galatia”, walijikuta “wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia”. Na inavyoonekana baada ya kukataliwa huko, walimwomba Mungu awaruhusu kulihubiri neno lake maeneo ya Misia na Bithinia.Biblia inasema – “lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa”! Na ndipo usiku ule ule Roho Mtakatifu akawapa kujua kwa njia ya maono ya kwamba walitakiwa kwenda Makedonia!
Swali la msingi la kujiuliza hapa ni kutaka kujua Roho Mtakatifu alitumia njia ipi “kuwakataza” na “kuwanyima ruhusa” kuhubiri neno la Mungu, maeneo ambayo hayakuwa katika mapenzi ya Mungu kwao – kwa wakati huo – kuhubiri neno lake huko?
Kwa kusoma habari za huduma ya Paulo, tunajua ya kuwa Mungu wakati mwingine aliwahi kumpa ruhusa na kibali cha kuhubiri injili nchi ya Galatia! Kwa hiyo – si kila wakati walizuiwa kwenda Galatia na Asia. Tukisoma kitabu cha 1 Wathesalonike 2:18, Paulo anasema: “tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na shetani akatuzuia”! Hii ilitokea wakati akina Paulo walipotaka kwenda nchi ya Thesalonike kuhubiri neno la Mungu.
Hii inatupa kujua ya kuwa Paulo na wenzake, walifikia kiwango kizuri sana cha usikivu mioyoni mwao, kiasi cha kuweza kutofautisha kati ya kuzuiwa na Roho Mtakatifu; na kule kuzuiwa na shetani!
Je, wewe unaweza kutofautisha kati ya kuzuiwa na Roho Mtakatifu kufanya jambo; na kule kuzuiwa na shetani kufanya jambo? Akina Paulo waliwezaje kutofautisha kati ya kuzuiwa na Roho Mtakatifu, na kule kuzuiwa na shetani?Jibu la swali la hilo ni hili: “Walipata ufahamu huo kwa njia ya Roho Mtakatifu kushuhudia pamoja na roho zao!”
Ukiijua njia hii inavyofanya kazi – itakuwezesha na wewe, kwa sehemu kubwa sana, kufanya maamuzi katika maisha yako! Kwa mfano – uamuzi kama Mungu anataka uolewe na nani? – na usiolewe na nani! Au uoe nani na usioe nani?Au Mungu anataka usome kozi ipi na usisome kozi ipi! Au ufanye kazi ipi au usifanye kazi ipi! Au ufanye huduma ipi na usifanye huduma ipi!
Ni muhimu ujue ya kuwa Roho Mtakatifu hushuhudia pamoja na roho zetu (Warumi 8:16); kwa kuweka huo ushuhuda wake katika dhamiri zetu (Warumi 9:1).
Fahamu ya kuwa “dhamiri” ni sauti ya roho na nafsi yako, inayokupa mitizamo na misimamo ya mienendo yako ya kila siku – ili utembee katika mapenzi ya Mungu kwa kufuata uongozi wake; na maelekezo yake!
Roho Mtakatifu anavyo vitu kadhaa anavyovitumia ili kushuhudia pamoja na roho yako – kwa kutumia dhamiri yako, ili upate kujua yaliyo maelekezo ya Mungu kwako ni yapi!
Kufuatana na kitabu cha 2 Wakorintho 7: 8 – 11, kitu kimojawapo anachotumia Roho Mtakatifu kuongoza (au kushuhudia) maisha yako kwa kutumia dhamiri yako ni hiki: “huzuni ya Mungu”.
Roho Mtakatifu anapoweka moyoni mwako hali ya kusikia “huzuni”, fahamu anataka ujue yafuatayo:
(i) Kwamba: ulchoamua kufanya au unachokifanya kutakuletea hasara katika maisha yako;
(ii) Kwamba: Unahitaji kuacha kufanya hicho unachofikiria kukifanya, maana ukiamua ukikifanya kitakuletea hasara kwenye maisha yako;
(iii) Kwamba: unachokifanya unatakiwa uache kukifanya, kwa maana ukiendelea kukifanya kitakuletea – hasara kwenye maisha yako;
(iv) Kwamba: msimamo ulionao si mzuri – na unatakiwa uubadilishe – la sivyo ukiendelea na msimamo huo unaweza kupata hasara.
(v) Kwamba: Ili iwe rahisi kwako kutii ushuhuda au ujumbe huo wa Roho Mtakatifu unahitaji, kuingia kwenye maombi ya toba, ili Mungu akusaidie ubadilike na kubadili msimamo huo uliomhuzunisha Mungu!
  

kwa nini wakati mwingine unapata huzuni moyoni mwako, bila ya sababu inayoeleweka kwa haraka ya kutokea kwa huzuni hiyo moyoni mwako!

  kwa kuangalia “huzuni ya Mungu” ilivyomsaidia Yesu, na kwa ajili hiyo, kumpa nafasi Roho Mtakatifu kumwongoza Yesu katika kuyafanya mapenzi ya Mungu kwenye maisha yake.
Nakushauri upatapo nafasi soma kwa upya habari zinazoeleza maombi ya Yesu, kwenye bustani ya Gethsemani, kama ilivyoandikwa kwenye kitabu cha Mathayo 26:36 – 46. Tujifunze kwa kutafuta majibu ya maswali yafuatayo:
Swali la 1: “Kwa nini Yesu alisikia huzuni moyoni mwake?”. Biblia inasema Yesu “akaanza kuhuzunika na kusononeka” (Mathayo 26:37). Na akawaambia “Petro na wana wawili wa Zebedayo” aliokwenda nao kwenye bustani ya Gethsemani ya kwamba: “Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa…” (Mathayo 26:38).
Mungu aliweka “huzuni yake” ndani ya moyo wa Yesu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, ili kumjulisha Yesu mambo yafuatayo:
(i) Kwamba: Uamuzi aliokuwa nao moyoni mwake utaleta “hasara”, ikiwa ataamua kuutekeleza! Soma pia 2 Wakorintho 7:9 – 11.
(ii) Kwamba: Uamuzi aliokuwa – nao moyoni mwake, ulikuwa ni kinyume na mapenzi ya Baba yake (Mungu), aliyokuwa amempangia ayafanye akiwa duniani.
(iii) Kwamba: anatakiwa afanye maombi ya “toba” kwa ajili ya kujiweka wakfu kwa upya, ili Mungu ampe nguvu za kumsaidia kuubadili msimamo wake, na badala yake ayafanye mapenzi ya Baba yake aliyokuwa anasita kuyafanya, kwa sababu ya udhaifu wa mwili wake!
Fahamu hili ya kuwa mambo haya aliyojulishwa Yesu kwa njia ya huzuni kushuhudia moyoni mwake, ndiyo mambo ambayo na wewe unajulishwa kwa njia ya huzuni ya Mungu inapowekwa moyoni mwako kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Swali la 2: “Je, huzuni ya Mungu ndani ya Yesu ililenga maamuzi yapi ya Yesu yaliyokuwa kinyume na mapenzi ya Mungu?
Yesu alipokuwa anaomba alisema: “Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe” (Mathayo 26:39)
Yesu alitaka “kikombe” kimuepuke akiwa na maana ya kuwa “ikiwezekana” aepushiwe kifo alichopangiwa kufa kwa njia ya msalaba, kilichokuwa mbele yake! Yesu alikuwa anajua ya kuwa kati ya mapenzi ya Baba yake aliyotakiwa ayafanye akiwa hapa duniani, ni kufa msalabani, kwa ajili ya kumsaidia mwanadamu.
Kule kusita kulikoingia moyoni mwa Yesu juu ya jambo hilo, ndiko kulikomfanya Baba yake aweke moyoni mwa Yesu huzuni, ili kumjulisha Yesu ya kuwa hakubaliani naye juu ya kusita kule!
Yesu alijitetea kwa kusema; “roho” yake ilikuwa “radhi”, au roho yake ilikuwa na utayari wa kuyafanya mapenzi ya Baba yake, ya kufa msalabani; lakini alisikia kusita kufanya hivyo kwa sababu ya “mwili” wake uliokuwa “dhaifu”! Kwa tafsiri nyingine alikuwa anasema mwili wake ulikuwa unamgomea kuyafanya mapenzi ya Mungu, kwa sababu ya udhaifu wa mwili wa kukosa utayari wa kufa msalabani!
Swali la 3: Kwa nini huzuni huwa inakuja na vitu vingine zaidi ndani ya moyo wa mtu?
Ndani ya mtume Paulo, kuna wakati kuliingia “huzuni nyingi” iliyoambatana na “maumivu yasiyokoma moyoni” mwake (Warumi 9:2).
Na ndani ya Yesu kuliingia “huzuni nyingi kiasi cha kufa”, pamoja “na kusononeka” (Mathayo 26:38, 39).
Hali hiyo ilimfanya Yesu asimamishe huduma yake, na ajitenge na watu! Na hata miongoni mwa wanafunzi wake aliamua kubaki na watatu tu, aliowapa nafasi ya kuona na kushiriki “dhiki” (Luka 22:44) aliyokuwa nayo siku ile!
Fahamu hili: “huzuni” inapokuja “nyingi” moyoni mwako ikiwa imeambatana na vitu vya ziada, ina maana ya (i) Kukuonyesha uzito wa ujumbe uliobebwa kwa ajili yako; na (ii) Ujue msisitizo wake kwako juu ya uharaka wa kubadili ulichoamua, au unachofanya – kwa kuwa muda wa wewe kupata “hasara” umekaribia sana, ikiwa utaendelea hivyo.
Swali la 4: “Kwa nini huzuni ilimsukuma Yesu kuomba kwa mzigo sana?”
Biblia inasema Yesu “akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini” (Luka 22:44).
Fahamu hili ya kwamba: huzuni inapozidi ndani yako ikiwa na msukumo wa kuomba, ni ili ujue ya kuwa (i) hilo jambo ulilolibeba kinyume na mapenzi ya Mungu, ni gumu mno kwako kuweza kuliacha; (ii) na kuwa unahitaji msaada wa Mungu ili akusaidie kuliacha!
Na huo msukumo wa kuomba utakaa na wewe bila kukuachia hadi moyo wako ukubali kubadilika na kumpa Mungu nafasi ya kukusaidia!
Hata kama utachoka kuomba kabla hujavuka moyoni juu ya jambo hilo – itamlazimu Mungu kukuinulia watu wa kukuombea kwenye hali hiyo uliyonayo (Mathayo 26:40,41), au itamlazimu kukutia “nguvu” ili wewe mwenyewe uzidi kuomba hadi uvuke (Luka 22:43,44).
Msaada huu wa Mungu kwa ajili yako utakuja kwako hasa unapoonyesha moyoni mwako kuwa unahitaji msaada wa Mungu katika hilo.
Swali la 5: “Utajuaje kuwa umevuka kwa ushindi ikiwa huzuni imeingia moyoni mwako kwa jinsi hii?”
Ikiwa umevuka moyoni mwako yatatokea yafuatayo: (i) huzuni itaondoka moyoni mwako, na badala yake itaingia furaha ya Bwana (Isaya 61:3); (ii) furaha hiyo ya Bwana uliyoipata moyoni mwako itakupa nguvu ya kufanya mapenzi ya Mungu uliyokuwa unasita kuyafanya (Nehemia 8:10); na (iii) Utapata “pumziko” moyoni mwako (Mathayo 26:45,46), na (iv) Utapata imani itakayokupa uhakika wa kuwa Mungu yupo upande wako (Yohana 8:29).
Angalizo: Huzuni inapoingia moyoni mwako, usikubali kulala “usingizi” hata kama macho yako yanakuwa “mazito” kama wanafunzi wa Yesu walivyofanya! Badala ya kuomba – Yesu “akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni” (Luka 22:45). Ukilala badala ya kuomba unapokuwa unasemeshwa na Roho Mtakatifu kwa njia ya huzuni, utajikuta umefanya jambo litakalokuletea hasara maishani mwako!
Nakuombea Mungu akusaidie katika hili…ili usipate hasara katika maisha yako!

Comments