SILAHA NANE(8) ANAZOZITUMIA SHETANI KUKUSHAMBULIA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Warumi 6:12-13 ''Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake; wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa MUNGU kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa MUNGU kuwa silaha za haki.''

Kuna silaha nyingi sana ambazo shetani anaweza kuzitumia ili kumshambulia mwanadamu.
Nimekuandalia silaha Nane(8) tu lakini ukweli zipo silaha zaidi ya 50 ambazo shetani anaweza kuzitumia kukushambulia. Biblia kwenye andiko nililoanza nalo inasema kwamba dhambi isitawale miili yetu. Hatutakiwi kutoa vitu vinavyotuhusu katika miili yetu na nafsi zetu kuwa silaha za shetani kutushambulia.
Shetani hammshambulii mtu bila kupata mlango wa kupitia ili kumshambulia mtu huyo. Shetani anatafuta mlango kwako ili apate nafasi ya kukushambulia, mlango wa shetani unaitwa dhambi na dhambi utatenda kwa sababu ya wewe kuwa mbali na MUNGU.
Kwenye hizi silaha 8 naamini utanielewa na hutaruhusu shetani atumie silaha hizo kukushambulia tena.

Silaha 8 Ambazo shetani huzitumia kukushambulia.

1. Hasira.
Waefeso 4:26-27 '' Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi.''
Hasira sio jambo baya kama hasira hiyo haitumiwi na shetani.
Ukiruhusu sana moyo wako utawaliwe na hasira mbaya ipo siku hasira hiyo itakutumia kuamua vibaya. Kuna watu wamewahi kujipeleka jehanamu kwa kujiua wao wenyewe kwa hasira, na Biblia iko wazi ikisema ''Usiue''  hivyo hata wewe huruhusiwi kujiua na ukijiua unajipeleka ziwa la moto hata kama ulikuwa unaishi maisha matakatifu sana, ukijiua umetenda dhambi na nafasi ya kutubu unakuwa huna.
Mithali 14:17 ''Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga; Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa.''
 Kuna hasira ya kawaida na kuna hasira ya kipepo kabisa.
Kuwa na hasira ya kawaida kwa muda kidogo tu sio dhambi ila hasira hiyo ikitumiwa na shetani inazaa dhambi mbaya.
 Ayubu 5:2 ''Kwani hasira humwua mtu mpumbavu, Nao wivu humwua mjinga.''
Kuwa na hasira kisha hasira hiyo isikutumie kufanya dhambi sio jambo baya. Hakuna mwanadamu ambaye hana hasira, hata sisi tuna hasira na shetani ndio maana tunahubiri injili ya KRISTO ili watu waache kuonewa na shetani baada ya kuokolewa na BWANA YESU. Mwalimu anaweza akawa na hasira kidogo juu ya wanafunzi wake ambao amewafundisha muda mrefu lakini hawaelewi hivyo anaweza akawaadhibu kidogo, hasira hiyo sio dhambi. Askofu anaweza akawa na hasira na viongozi aliowachagua na kuwashusha cheo kama viongozi hao hawatumizi wajibu wao, hasira hiyo sio mbaya.Hasira ikimtumia mtu kipepo ndipo itazaa dhambi na kuleta maumivu kwa wengine. Uwe na hasira ila usitende dhambi kupitia hasira hiyo. Hasira zako zinaweza kuwa silaha ya shetani kukushambulia wewe mwenyewe. Kuna watu leo wako magerezani wanalia kila mara wakijilaumu kwa hasira zao ambazo ziliwapelekea kuua au kujeruhi na jambo hilo kupelekea wao kufungwa miaka mingi gerezani. Hao hasira iliwatumia vibaya na shetani aliutumia huo mlango kuwashambulia na kuwatesa sana na kutesa ndugu zao au wapendwa wao au watoto wao waliokuwa wanawategemea sana.
 Ndugu uwe na hasira ila usitende dhambi.
Ufunge mlango huo ambao shetani anaweza kuutumia kukushambulia.
Mithali 29:11 ''Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote; Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.''
 
2.  Uvivu.
Mithali 19:15 ''Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa.''
Uvivu ni hali ya kutotaka kufanya kazi.
Uvivu ni hali ya kuwa na ulegevu katika kazi na ulegevu ni hali ya kulegea.
Uvivu ni hali ya kutokuwa na bidii katika kufanya kazi.
Kuna madhara mengi katika uvivu wa kufanya vitu vyema.
Kuna madhara ya kufanya kazi ya MUNGU kwa ulegevu/Uvivu.
Yeremia 48:10A ''Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya BWANA kwa ulegevu;''

Shetani anaweza kukuletea uvivu na uvivu huo kuwa silaha ya kukushambulia au kushambulia ndoa yako au kipato chako.
Kama mama kwenye ndoa yake ni mvivu iwe ni kufua, kupika, kuosha vyombo au kumwandalia mumewe, Hilo linaweza kuwa pando la shetani la kuishambulia ndoa hiyo.

Biblia hapo juu imesema kwamba kwa mvivu kutakuwa na njaa maana yake kutakuwa kumepungukiwa. Kama hufanyi kazi naamini utapungukiwa, Kama wewe ni mkulima lakini  hulimi hutapata mazao mazuri, huko ndiko kupungukiwa na huko ndipo kuteswa na shetani kupitia mlango wa uvivu ulioufungulia.
Baba kwenye ndoa yako hutakiwi kuwa mvivu maana utajikuta unamfundisha mke wako na watoto wako uvivu.
 

Mhubiri 10:18 '' Kwa sababu ya uvivu paa hunepa; Na kwa utepetevu wa mikono nyumba huvuja.'' 

Kuna watu ni wavivu kufanya kazi na ndio hao hao uvivu wao huwapelekea kuwasema vibaya wale wanaofanya kazi kwa bidii na kufanikiwa, uvuvi hapo umetumika kama silaha ya shetani kukushambulia.
Ukiwa mvivu kusoma Neno la MUNGU hutajua mambo mengi ya MUNGU na hivyo kupelekea kukosa hofu ya MUNGU na jambo hilo kukufanya uwe dhambini kila wakati.
Kama ni mvivu wa kwenda kanisani kwenye ibada hutajua mpango wa MUNGU juu ya maisha yako na hali hiyo  kukufanya uishi kama kipofu katika maisha ya kiroho.
Usiwe mvivu ndugu katika mambo ya MUNGU na usiwe mvivu katika kazi njema isiyo ya dhambi aliyokupa MUNGU ili ikupe kipato, tenda kwa haki na usimdhulumu mtu yeyote na MUNGU atakubariki sana.

 3. Chuki.
Mithali 10:18 ''Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.'' 

Chuki ni dhambi na chuki hupelekea kuchukia, kuchukiana au  kuchukiza.
Chuki ni hali ya kutokupenda watu.
Maana nyingine ya chuki inaitwa roho mbaya.
Chuki ni pando la shetani la kugombanisha watu wa MUNGU.
Chuki huzaa kinyongo na huzaa fitina na visasi, hayo yote ni machukizo kwa MUNGU.

Mithali 26:26-27 '' Ingawa chuki hufunikizwa kwa hila; Uovu wake utadhihirika mbele ya kusanyiko. Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia.'' 

Shetani anaweza akakupandia chuki ndani yako na hiyo chuki ikawa ni silaha yake ya kukushambulia kila wakati.
BWANA YESU katika Neno lake amesisitiza sana upendo hivyo wewe ukikosa upendo maana yake umebeba chuki. BWANA YESU anakutaka uwapende hata adui zako katika ulimwengu wa mwili na uwaombee.
Luka 6:27 ''Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi,'' 

Kinyume cha upendo ni chuki hivyo kama huna upendo basi wewe utakuwa na chuki na chuki hiyo shetani anaweza kuitumia kuwa silaha yake ya kukushambulia wewe. Kama  mmoja alikuwa anamchukia dada  mmoja kwa chuki isiyokuwa na sababu, alimlaani na kuisemea mabaya familia ya yule dada. Yule dada wala hakumchukia yule kaka bali alikuwa anamuombea. Miaka kama mitano ikapita  na wote wakapata kazi. Baada ya miaka kadhaa baadae yule dada akahamishiwa mjini aliko yule kama na yule dada ndio akawa mkuu wa kazi wa yule kaka. Chuki iliendelea kumtesa yule kaka na chuki hiyo kuwa silaha ya shetani kumshambulia.
Mithali 19:17-19 '' Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA.''

4. Udhaifu wa kuomba.

'' ombeni bila kukoma; 1 Wathesalonike 5:17.''
Umewahi kujiuliza usipoomba itakuwaje?
Maombi ni jambo la muhimu sana kwa watu wa MUNGU.
Usipoomba maana yake hutaki kupokea na hutapokea kwa sababu hujaomba.
shetani naweza kukunyima muda wa maombi ili tu isopokee kutoka kwa MUNGU na kwa hali hiyo shetani aendelee kukuonea kila siku.
 ''Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake(MUNGU), ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. 1 Yohana 5:14-15''

Tunashinda kwa maombi kupitia jina la YESU KRISTO.
Tunawashinda wachawi na wakuu wa giza kwa maombi katika damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO..
Maombi katika jina la YESU ndio silaha yako kuu ambayo shetani anaiogopa sana.
 YESU leo anasema kwako kwamba;
'' Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. Yohana 14:13-14''


Kuna watu wana uvivu wa kuomba na kuna watu wana udhaifu kabisa wa kuomba. Mvivu wa kuomba anaweza akawa anaomba kwa ulegevu au mara chache chache sana lakini mdhaifu wa kuomba anaweza kuomba vibaya na anaweza asiombe kabisa.

5. Kiburi.

Kiburi ni silaha mbaya sana ambayo shetani huitumia kama silaha ili kuwashambulia wanadamu.
Ukipandiwa kiburi ndani yako wewe unakuwa na hatari mbaya sana.

Mithali 16:18-20 ''Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko. Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini, Kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi. Atakayelitafakari neno atapata mema; Na kila amwaminiye BWANA ana heri.'' 

Kiburi hakifai na kinatakiwa kiondoke kwa kila mtu.
Ukiona kiburi ujue maanguko ya ndugu huyo yako karibu ndivyo Biblia inavyosema hapo juu.
 Kiburi ni roho ya shetani inayowaingia watu na kuwatumikisha kipepo.
Wengi leo wakihubiriwa wanadharau ni kwa sababu ya kiburi kilicho ndani yao.
Hakuna ambaye anaweza kuchukia uzima wa milele, lakini kwanini watu wakiambiwa habari za uzima wa milele wanawatukana hata hao wahubiri? ni kwa sababu ya roho ya kiburi.
Hakuna asiyetaka kupona lakini kwanini mtu akiambiwa aende kwenye maombezi anaanza kuwatukana waombaji ambao hata hajawahi kuwaona? Ni roho ya kiburi inasumbua wengi.
Ndugu yangu, usikubali kuwa na roho ya kiburi.
Kama roho ya kiburi inakutesa hakikisha unaomba kwa MUNGU ili iondoke.

Kiburi ni silaha ambayo shetani anaweza akaitumia ili kukumaliza.
Wengi sana wamekosa mbingu kwa sababu ya roho ya kiburi.

''Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa. - Mithali 29:23''
6. Uchungu.
Waebrania 12:15 ''mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya MUNGU; shina la UCHUNGU lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.'' 

Uchungu ni hali anayokuwanayo mtu baada ya kufikwa na jambo baya la kuumiza sana.
Wakolosai 3:19 ''Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao.''
Kumbe upendo unaweza kufuta uchungu na kumpe mume anatakiwa asiwe na uchungu na mkewe na kumbe mke naye hatakiwi kuwa na uchungu na mumewe.
 Waefeso 4:31-32 ''Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi.''
 
Inawezekana kabisa umepata uchungu  baada ya kutendewa jambo fulani au baada ya kutokea tukio fulani lakini napenda kukuambia kwamba uchungu unaweza kuzaa dhambi na madhara mengi sana kama uchungu huo ukitumiwa na shetani kwako.

Kuna watu wamewahi kufiwa na wao wakaamua kujiua.
Aliyekufa kama alikuwa mteule wa KRISTO anaenda mbinguni na alijejiua kwa sababu kujiua ni dhambi kama ilivyo dhambi ya kuua basi anaenda motoni na kwa jinsi hiyo kutengana milele na huyo mpendwa wake aliyekufa kwanza. Kuna watu hudanganyana kwamba kama uliyempenda sana amekufa basi na wewe unaweza kujiua ili uende ukaungane naye aliko, huo ni uongo wa shetani wa kupiga ndege wawili na kwa jiwe moja na kuwafanya mmoja au wote wasiende uzima wa milele.
Uchungu hata kama utakupata naomba uwe wa muda tu na usikubali uchungu huo  ukufanye uingie katika dhambi.
Uchungu unaweza kukufanya ulipize kisasi na kwa njia hiyo unakuwa umetenda dhambi kwa MUNGU na pia kwa njia hiyo unaweza kufungwa au kufukuzwa au kuadhibiwa.
Uchungu wako ukitumiwa na shetani ni hatari sana.
Kuna mtu baada ya kuambukizwa ukimwi na yeye amewaambukiza mamia wengine wasio na hofu ya MUNGU, Huyo kwanza anatenda dhambi na pili anaua na tatu ni kosa kisheria na kwa kosa hilo anaweza akafungwa, hata kiafya hiyo ni hatari. Uchungu wako shetani anaweza akautumia kujihesabia haki wewe na kujiona ulionewa na kujiona una haki ya kulipiza kisasi kumbe ndio unajimaliza kabisa huko unajiona.
Ni Hatari sana.

7. Uzinzi na uasherati.


Waefeso 5:3-5 '' Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa KRISTO na MUNGU. ''

Hii ni silaha mbaya sana na inawatesa wengi sana.
Waasherati Ni Wale Ambao Hawajafunga Ndoa Wakifanya Ngono Wao Kwa Wao Au Hata Wakifanya Ndoa Na Wale Walio Kwenye Ndoa Ni Dhambi Kuu,
Wazinzi Ni Wanandoa Wakitoa Nje Ya Ndoa Zao Ni Machukizo Makuu.
'' Maana Haya Ndiyo Mapenzi Ya MUNGU, Kutakaswa Kwenu, Mwepukane Na Uasherati- 1 Thesalonike 4:3.''
Kuna watu wengine hata kwenye kitabu cha uzima mbinguni hawamo na kila siku wanaenda kanisani tatizo ni uzinzi na uasherati ambao wanauendekeza kwa siri. 

Ni mbaya sana na Biblia inasema hawana akili hata moja wazinzi wote wa kiume na wa kike.

Mithali 6:32-33 ''Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika.''



8. Kutokusamehe.

Kusamehe ni jambo ambalo linawaumiza na kuwatesa watu wengi sana. Kusamehe ni jambo la lazima kwa mtu anayeutaka uzima wa milele.
Shetani anaweza akatumia kutokusamehe kwako kuwa silaha yake ya kukushambulia katika maisha yako.
Unaweza ukakosa baraka za MUNGU kwa sababu tu umeshindwa kuwasamehe na kuwaachilia watu waliokukosea. Usiposamehe na wewe hautasamehewa na MUNGU.

Mathayo 6:14-15 '' Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.''

 Maana tatu za Neno ''Kusamehe'' ni hizi; A.  Kusamehe ni Kuacha kuwa na kinyongo kwa jambo baya ulilotendwa. Mfano umesalitiwa lakini ukimsamehe maana yake hutakuwa na kinyongo wala chuki na mtu huyo aliyekukosea. B.  Kusamehe ni mumwacha mtu huru  baada ya kukutendea jambo baya. Mfano ulimlaani mtu au kumfukuza kazi lakini kama umemsamehe utambariki na kuifuta laana na kumrudisha kazini. C. Kusamehe ni kukubali kwa hiari  kuiachia haki yako. Mfano mtu amekudhulumu pesa nyingi na hana uwezo wa kukulipa kwa sasa hivyo unamsamehe na kumwachia ile pesa ambayo ni haki yako kabisa maana huyo mdeni wako hana kwa sasa au anayo lakini nguvu ya msamaha inaweza kumwacha na pesa hiyo.
 
Yakobo 4:7 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.'' 

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments