UNAWEZEJAE KUJUA KAMA UMEMSAMEHE MTU ALIYEKUKOSEA SANA.?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
BWNA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno la MUNGU.
Najua Kabisa umewahi kukosewa sana na watu na wakati mwingine ulijiapiza kwamba hutawasamehe hata iweje.
Wengine uliwasamehe baada ya muda mrefu sana kupitia.
Wengine uliwasamehe ila hukuwasahau.
Mara nyingine kuna watu husema kwamba wamesamehe lakini ukweli hawajasamehe kabisa. 

Waefeso 4:32 ''tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi.''

Utajuaje kama umemsamehe mtu aliyekukosea sana?
Ili kujibu swali hilo acha kwanza tujue maana ya kusamehe au msamaha.
Maana tatu za Neno ''Kusamehe'' ni hizi;
1.  Kusamehe ni Kuacha kuwa na kinyongo kwa jambo baya ulilotendwa.
Mfano umesalitiwa lakini ukimsamehe maana yake hutakuwa na kinyongo wala chuki na mtu huyo aliyekukosea.
2.  Kusamehe ni mumwacha mtu huru  baada ya kukutendea jambo baya.
Mfano ulimlaani mtu au kumfukuza kazi lakini kama umemsamehe utambariki na kuifuta laana na kumrudisha kazini.
3. Kusamehe ni kukubali kwa hiari  kuiachia haki yako.
Mfano mtu amekudhulumu pesa nyingi na hana uwezo wa kukulipa kwa sasa hivyo unamsamehe na kumwachia ile pesa ambayo ni haki yako kabisa maana huyo mdeni wako hana kwa sasa au anayo lakini nguvu ya msamaha inaweza kumwacha na pesa hiyo..


Mithali 3:3-4 '' Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za MUNGU na mbele ya mwanadamu.''

Kusamehe huwa ni jambo la lazima kwa mteule wa KRISTO maana bila kusamehe hawezi na yeye kusamehewa na asiposamehe hawezi kuingia uzima wa milele.

Mathayo 6:14-15 '' Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.''

Kumbe kusamehe ni jambo la lazima kama na wewe unataka kusamehewa na MUNGU.
Usiposamehe ujue kabisa kwamba hata ukitubu kwa MUNGU ili usamehewe  wewe hakika hutasamehewa maana kanuni ya MUNGU ni kwamba inakupasa kuwasamehe waliokukosea ndipo na wewe uombe msamaha  kwa MUNGU na usitende dhambi tena.
Kumuonya mtu aliyekukosea ni jambo tofauti na kumsamehe mtu huyo
Kulia sana mbele ya aliyekukosea ni jambo tofauti na kumsamehe mtu huyo.
Kumkumbatia aliyekukosea sio kumsamehe mtu huyo.
Msamaha ni msamaha na hayo meingine ni mengine.
Utajuaje kama umemsamehe mtu aliyekukosea sana?
Mama mmoja mke wa mtu alikuwa anaishi na wadogo zake wa kike. Mume wa mama huyo alikuwa ni mzinzi kupindukia. Baada ya miaka miwili yule baba alianza kumalzimisha mdogo wa mke wake ili azini naye. Yule binti alikataa na yule baba mzinifu aliendelea kumlazimisha yule binti ili azini naye lakini binti kwa kumheshimu sana dada yake alikataa siku zote na kumuonya yule shemeji yake, mume wa dada yake. Siku moja yule mama alisafiri na kuwaacha wadogo zake pamoja na mumewe. Yule mwanaume alileta soda usiku na kuwatuma wengine vitu kwa majieani akimuacha yule binti aliyekuwa anataka azini naye, baada tu ya wale kuondoka alimpa soda shemeji yake ili anywe na yule dada bila kujua alikunywa ile soda na kulewa ghafla maana yule baba alikuwa ameweka madawa ya kulewesha. Yule baba akamchukua yule binti chumbani kwake na kuwasubirilia aliowatuma ili warudi na kuwapa majukumu mengine kisha yeye akaingia chumbani na kuzini na shemeji yake ndugu wa kuzaliwa wa mke wake. Alipomaliza kuzini naye yule binti alitoka kwenye mazingira ya pombe na kuanza kulia akipiga kelele. Yule mwanaume alimdanganya kwa vizawadi vingi lakini binti aliendelea kulia tu, Baade alinyamaza lakini alikuwa na maumivu hata kutembea anashindwa maana ni binti mdogo. Yule Binti alichokuwa anasubiri ni dada yake arudi ili amwambie akidhani kwamba kwa njia hiyo atakuwa anmkomesha yule shemeji yake mzinzi. Yule mama aliporudi alimuona mdogo wake akiwa analia kila muda na kumuliza muda huo huo. Yule dada alimwita sehemu nyingine dada yake na kumweleza yote ambayo mume wake amemfanyia. Yule mama badala ya kuchukua ujinga wa mumewe yeye ndio alimbadilikia mdogo wake na kumpiga sana, kisha mumewe aliporudi aliendelea kumpiga mdogo wake Kisha akamfukuza. Yule dada aliteseka sana kuishi sasa kulikuwa kwa neema tu ya MUNGU maana ndugu wote katika ukoo walijulishwa na kumtenga na kumchukia, alikosa pa kwenda lakini MUNGU alimpa watu wema wa kuishi naye hadi alipokuja kupata kazi nzuri na kuolewa. Miaka zaidi ya 5 ilipita tangu afukuzwe uchi na dada yake wa tumbo moja lakini alipoolewa tu yule dada yake akamwambia kwamba kwa sababu yeye alitembea na mumewe hatamsaehe hadi pale ambapo na yeye atatembea na ume wa mdogo wake.
 Msamaha ni kitu cha muhimu sana kwa mtu anayeutaka uzima wa milele. Dada huyu hakufanikiwa kumnasa mume wa mdogo wake  na hadi neema ya MUNGU ilipokuja kugusa baade ndipo alimsamehe mdogo wake ambaye hata hana kosa ila kosa ni la mumewe, kwa sababu binti kipindi anabakwa alikuwa  hata miaka 15 hajafikisha. Msamaha unawasumbua wengi sana.

 Mathayo 5:7 ''Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.''

Neno rehema linahusiana  na neno huruma.
Heri wewe unayeweza kuwahurumia wenzako kwa kuwasamehe makosa yao waliyokukosea maana kwa kufanya hivyo na wewe utahurumiwa na kusamehewa.
Rehema ni msamaha hivyo heri wenye kusamehe maana na wao watasamehewa.
Wakolosai 3:13 ''mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama BWANA alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.''

Utajuaje kama umemsamehe mtu aliyekukosea sana?
 Unaweza kujua kama umemsamehe mtu  kama hutakuwa unaumia Tena juu ya jambo hilo alilokukosea.
Ili uweze kumsamehe mtu  unatakiwa umuombee sana.
Kanuni ya kibiblia ya kusamehe sio lazima uombwe msamaha ndipo usamehe, Bali unasamehe pasipo kuombwa msamaha.

Kuna madhara makubwa katika kutokusamehe ndio maana ni lazima tu tusamehe hata pasipo kuombwa msamaha kwanza.
Kutokusamehe kunaweza kumfanya mtu asiingie Uzima Wa milele.
kutokusamehe kunaweza kuzuia maombi.
kutokusamehe kunaweza kuleta vifungo maishani mwako.

Mathayo 18:21-25 ''Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? YESU akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na BABA yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake. '

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments