USIKUBALI KUFUNGWA UFAHAMU WAKO NA SHETANI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna watu wamefungwa ufahamu wao na ufahamu huo  hauamui vyema katika baadhi ya maamuzi yao.
Kuna watu wamefungwa ufahamu wako na wachawi.
Kuna watu wamefungwa fahamu zao na watumishi wa shetani.
Kuna wanaume waliooa lakini  wamefungwa fahamu zao na nyumba ndogo ambazo hizi siku zote ni watumishi wa shetani.
Kuna wamama walioolewa lakini fahamu zao zimefungwa kishetani na vijana wadogo walio watumishi wa shetani.
Sijui ndugu yangu kama na wewe uko katika kundi la wasio na ufahamu wa ki MUNGU.
Ni hatari mwanadamu akiendelea kukosa ufahamu wa kiMUNGU.
Kukosa ufahamu wa ki MUNGU ni kukosa hofu ya MUNGU hata unatenda dhambi bila kuwa na wasiwasi wa aina yeyote.
Ni hatari sana kwa mtu ambaye anaendelea kukosa ufahamu.
Biblia inasema kwamba 
 '' Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.-Mithali 10:21B''

Unaweza ukafa kiroho kwa sababu tu huna ufahamu wa ki MUNGU.
Kutoa mimba ni kukosa hofu ya MUNGU, ni kukosa Neno la MUNGU ambalo huleta ufahamu wa ki MUNGU ndani yako.
 Usikubali ufahamu wako uendelee kukamatwa na  mapepo kiasi kwamba  sasa unadhani pombe si dhambi, kupiga punyeto au kujichua unaona sio dhambi.
Leo kuna watu kwa sababu ya kukosa ufahamu wanadhani kwamba kutembea uchi mitaani sio dhambi.
Kuna watu wanadhani kutoa rushwa kidogo sio dhambi.
Kuna watu leo wanadhani kwenda kwa waganga sio dhambi.
Kuna watu leo wanadhani kuuza pombe sio dhambi bali dhambi ni mpaka uivywe pombe hiyo.
Kuna watu hudhani kwamba kuuza sigara sio dhambi bali dhambi ni kuivuta tu.
Kuna watu  Hudhani kwamba kufanya uzinzi wakati wa uchumba ni ka dhambi kadogo, ndugu kuna wengine walikosa uzima wa milele kwa sababu ya kadhambi hako tu.
Kuna wamama katika ndoa zao kwa sababu ya kukosa ufahamu wa Ki MUNGU sasa wamewaruhusu waume zao wawaingilie kinyume na maumbile

MUNGU anasema kwa awaliokosa ufahamu kwamba;  
 ''Kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu; ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda mema hawana maarifa.-Yeremia 4:22''

Ndugu, kuendelea kufanya dhambi huku na kanisani unaenda ni kukosa ufahamu wa ki MUNGU, ni kukubali kuwa mtumishi wa shetani na sio mtumishi wa KRISTO.
Unaweza ukakosa mbingu kwa sababu ya kukubali kwako ufahamu wako utumiwe na shetani ndio maana kwa sasa wewe ni mzinzi unayejisifia kila siku kuhusu uzinzi wako.
Inawezekana wewe ni mtu wa kanisani lakini umejitoa ufahamu wako kwa kuamua kuwa tapeli na mwizi.
Inawezekana wewe ni mtu wa kanisani lakini kwa sababu ya tamaa yako ya kutaka kuolewa sasa uko tayari kuolewa hata na mawakala wa shetani.
Ndugu usijitoe ufahamu wako, Mngoje BWANA na endelea na maombi maana baraka yako ni yako tu na itakuja kwa jina la YESU KRISTO.
Inawezekana wachungaji wamekushauri sana hadi unawachukia kisa tu unataka kuoa au kuolewa  na mtu atakayekusaidia kwenda jehanamu na sio mbinguni. Ndugu naomba tambua kwamba 
Kukubali Kuoa au kuolewa na mtumishi wa shetani ni dalili mojawapo kwamba wewe baadae unaweza ukawa mtumishi wa shetani. Sasa kama unajitoa ufahamu sasa inaweza kuja kukugharimu sana baadae.
Ukioa au Ukiolewa na mtu anayemkataa YESU KRISTO na wokovu wake ipo siku na wewe utamkataa YESU KRISTO na uzima wake.
Na ukifikia hatua ya kumkataa YESU KRISTO na wokovu wake hakika utakuwa tayari unaukataa uzima wa milele, utakuwa unajitenga na MUNGU wa mbinguni na utakuwa unaikimbia mbingu.

Yohana 3:17-19 '' Maana MUNGU hakumtuma Mwana(YESU) ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye(YESU) hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU . Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. ''

Kipi bora kati ya kuolewa na mpinga KRISTO kisha akakusaidia wewe kwenda jehanamu au usiolewe/ usimuoe ili tu kutunza wokovu wako katika KRISTO YESU ulio wa thamani sana?
Kama wengine wamejitoa ufahamu wao hata sasa hawaendi kanisani, wewe usiwaige hao.
Kuna watu fahamu zao zimefungwa kiasi kwamba ukiwaambia habari za kuokoka wanadhani unajipendekeza tu.
Kuna watu ukiwahubiria injili wanakuona kama umekosa kazi tu, fahamu zao ziko kwa shetani ndio maana yaliyo ya uzima wao hawayataki kabisa.
Kama kuna mtu anahubiri kinyume na Wokovu wa KRISTO huyo hana ufahamu.
Ndugu dhambi isikutawale hata ukamsahau YESU KRISTO aliyekuokoa.
Kuna watu hata makanisani Mchungaji akisema ''Sasa kila mtu aombe maombi ya kutubu kwa MUNGU'' Wao watamshangaa huyo mchungaji japokuwa wametawaliwa sana na dhambi.
 
Warumi 1:31-32 '' wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; ambao wakijua sana hukumu ya haki ya MUNGU, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao. ''

Ndugu, kama unaona kabisa kwamba ufahamu wako unadukuliwa na mawakala wa shetani hakikisha unakimbilia katika kiwanda cha kutengeneza fahamu zako ambacho kiwanda hicho kipo mbinguni na unaweza kukiendea kwa maombi yako kupitia jina la YESU KRISTO.
Mtii MUNGU na Neno lake utakaa salama.
Kung'ang'ania dhambi ni kuikimbia mbingu.
Anza kuombea ufahamu wako kuanzia leo ili katika maamuzi yako yoyote basi uamue vyema na sio yale maamuzi ya kuamua kisha baade unajuta.

BWANA YESU yuko anakungoja tu uombe na atakujibu mapema sana.
Yohana 14:13-14 '' Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu(YESU KRISTO), hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. ''

Kuna watu kwa sababu ya mazoelea hudhani kwamba bado wako kwa YESU kumbe matendo yao maovu yalishawaondoa kwa YESU miaka mingi.
Kuna wengi hudhani bado wana ROHO wa MUNGU kumbe uovu wao ulishamuondoa ROHO MTAKATIFU ndani yao siku nyingi.
Kuna watu wanadhani wana ROHO MTAKATIFU ndani yao kumbe wana roho ya shetani kwa sasa na si ROHO MTAKATIFU kama wao wanavyodhani.
Utajuaje Kama Una ROHO Wa MUNGU Ndani Yako?. 
Utajuaje Kama Una roho Ya shetani Ndani Yako?.
 Ukijifunza Kuijua Sauti Ya MUNGU Na Ukafaulu Katika Kuijua Sauti Ya MUNGU, Itakuwa Rahisi Sana Kwako Kuzijua Sauti Za shetani Au Sauti Za Kibinadamu. Maana Utazijua Kwamba Ziko Tofauti Na Sauti Ya MUNGU. 
Ni Muhimu Sana Kuijua Sauti Ya MUNGU Maana Siku Hizi Matapeli Wa Kimwili Ni Wengi Na Matapeli Wa Kiroho Ni Wengi Pia. Mfano Ni Huu; MUNGU Hasemi Na Wewe Binti Kupitia Chipsi Soda Ulizonunuliwa Bali MUNGU Atasema Na Wewe Kupitia ROHO MTAKATIFU. Binti Uwe Makini Sana. Kijana Usiseme Umeonyeshwa Kwa Binti Fulani Kwa Sababu Tu Umeona Kwao Ni Matajiri. shetani Anajua Sawa Kuwatangizia Kwa Mbele Vijana Na Mabinti. 
Kuna Sauti Inaweza Kukujia Ukadhani Ni MUNGU Anakuambia Kumbe Ni shetani. 
Kuna Sauti Unaweza Kudhani Ni MUNGU Kasema Kumbe Ni Tamaa Tu Za Wanadamu. 
Uwe Makini Mpendwa. 

Kwa Haraka Haraka Njia Mbili Za Kukusaidia Kuijua Sauti Ya MUNGU Ni Hizi;
(1) Kujifunza Neno La MUNGU
 (2) kumjua ROHO MTAKATIFU Na Kwa Naye Ndani Yako

Kukaa mbali na kanisa la MUNGU ni kukosa ufahamu.
Kujiunga na marafiki wabaya ni kujipeleka kwa wasio na ufahamu.
Hata kama una Elimu kiasi gani lakini kama unatenda dhambi wewe huna ufahamu hata mmoja.
Wenye ufahamu wameokoka na wanaishi maisha matakatifu katika KRISTO.
Wenye ufahamu wanajifunza na kulitafakari Neno la MUNGU kila mara.
Wenye ufahamu wanalitii Neno la MUNGU siku zote.
 ''Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika BWANA na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.-Waefeso 6:10-11'' 
 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments