USIKUBALI KUGEUKA MKE WA LUTU

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mwanzo 19:26 '' Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.''

Katika miji ya Sodoma na Gomora kulikuwa na uovu mwingi sana  na MUNGU akaandaa adhabu kwa miji hiyo iliyoasi kwa MUNGU, kwa kufanya uovu mkubwa sana hasa uzinzi na uasherati.
Familia moja tu katika miji hiyo ikapata neema mbele za MUNGU kwa sababu ya matendo ya haki ya Baba wa Familia hiyo aitwaye Lutu. Malaika wa MUNGU walipofika katika mji huo ili kuangamiza walimpa Lutu Neno la MUNGU la kumponya kwamba yeye na mke wake na mabinti zao wawili waondoke haraka Sodoma maana MUNGU anaenda kushusha moto ili kuangamiza wote wenye mwili katika mji huo pamoja na mji wa Gomora. Familia ile ikaondoka kwa msaada wa Malaika wa MUNGU lakini mbele kidogo ya safari mmoja aliasi Neno la MUNGU lililowakataza kugeuka nyuma.  Mama wa familia ile akageuka nyuma!!!
Yule mama alipogeuka nyuma  muda huo huo akawa nguzo ya chumvi. Habari yake ikaishia pale kwa sababu hakuitii sauti ya MUNGU.

Ungepewa nafasi ya kumshauri mke wa Lutu dakika moja kabla hajageuka na kuwa nguzo ya chumvi ungemwambia nini?
Leo wakristo wengi wamegeuka nguzo za chumvi kwa kuuacha Wokovu.

 BWANA YESU anasema juu ya jambo hilo kwamba;
 '' Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya.-Luka 17:32-33''
Mtu yeyote atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili ya YESU atakuwa anaiponya nafsi yake maana ufalme wa MUNGU ni wake.
Kuangamia huku sio kufa bali ni kuacha yale mazuri kwako ambayo ni ya muhimu sana kwako lakini kwa sababu hayo mazuri ni dhambi mbele za MUNGU unayaacha tu hata kama unayapenda, na baada ya kuyaacha unaamua kumpokea BWANA YESU kama BWANA na Mwokozi wako kisha unaanza kuishi maisha matakatifu.
 Inawezekana kabisa huwa unajisikia vizuri ukinywa pombe lakini kwa sababu ni dhambi unaiacha pombe na kuanza kumcha MUNGU katika Roho na kweli yake ya wokovu wa injili.
Kuendelea kunywa pombe ni kuendelea kuwa nguzo ya chumvi, Kuendelea na usaliti na uzinzi ni kuendelea kuwa nguzo ya chumvi. Kuendelea na uchawi na uganga wa kienyeji ni kuendelea kuwa nguzo ya chumvi
Kuna watu pia leo baada ya kuishi maisha ya wokovu baadae waliamua kuacha wokovu, huko ni kugeuka nguzo ya chumvi.
Tukio la mke wa Lutu ni tukio halisi ambalo lilitendeka katika ulimwengu wa mwili ili litufundishe sisi. Leo tukio la kugeuka nyuma na kuacha kufuata maagizo ya MUNGU linawakumba wengi, Tukio la kumwacha YESU kisa unataka kuolewa/kuoa na mtu wa dini nyingine linawakumba wengi. 
hawa hugeuka nguzo za chumvi.
Leo kuna wababa wameacha huduma ya kumtumikia KRISTO kwa sababu tu walioa wake ambao ni nguzo za chumvi tayari.
Kama unamcheka mke wa Lutu huku na wewe umemwacha YESU basi hakika hujui ufanyalo maana hata wewe ni nguzo ya chumvi.


1 Wafalme 11:2-4 '' Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, na wa mataifa BWANA aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda.  Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo. Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, MUNGU wake, kama moyo wa Daudi baba yake.''

Mfalme Sulemani alikatazwa kuoa kwa wasio mcha MUNGU lakini alishupaza shingo na wanawake hao hao wakaja kumgeuza moyo wake ili amwache MUNGU aliye hai, ni hatari sana. Japokuwa Mfalme suleiman alitubu katika kitabu cha Mhubiri lakini kosa lake hilo lilipelekea Israeli kugawanyika kutoka kuwa taifa moja na kuwa mataifa mawili, yaani Israeli na Yuda. Wanawake walimfanya kuwa nguzo ya chumvi kwa muda.

Kuna watu baada ya wao kugeuka nguzo ya chumvi na wao sasa wanajitahidi kutaka kuwageuza maelfu ya watu ili wawe nguzo za chumvi. Wamemuacha YESU na Wokovu wake sasa wameigeukia miungu na kuanza kuhubiri watu kwamba hakuna kuokoka duniani.
Kuna ambao tayari ni nguzo za chumvi na wanajitahidi kuwahamisha watu ili watoke kwa YESU na kuifuata miungu ambazo ni roho za kuzimu.

 2 Kor 11:14-15 ''Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.''

Wote wanaoukataa wokovu wa YESU KRISTO ni nguzo za chumvi tayari katika ulimwengu wa roho. Anayemkataa YESU na wokovu wake maana yake huyo mtu amembeba shetani, hivyo huyo ni nguzo ya chumvi. Wapo leo wengi tu wanaomkataa YESU, Wanafundisha uongo na hao ni watumishi wa shetani maana nje ya  YESU KRISTO kuna shetani.
kuabudu sanamu ni kujifanya nguzo ya chumvi kabisa. 
Kumwacha YESU moja kwa moja ni kuwa nguzo ya chumvi kama mke wa Lutu.

Walawi 19:4 '' Msigeuke kuandama sanamu, wala msijifanyizie miungu ya kusubu mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. ''

 
Nguzo ya chumvi haina uhai tena  mtu aliye nguzo ya chumvi ni yule ambaye hana  Neno la MUNGU ambalo ndilo huleta uhai wa kiroho. 
Kumbuka pia kwamba kuwa na Neno la MUNGU sio kukariri tu maandiko bali Kuyatii maandiko kwa jinsi ya KRISTO na kuyaishi.
Kmutumikia shetani ni kuwa nguzo ya chumvi moja kwa moja.
Kama Mchungaji au Askofu umegeuka nguzo ya chumvi kwa kumwacha KRISTO, Ni heri ukajiondoa katika nafasi hiyo maana hasira ya MUNGU ni kali juu yako.
Kuna wanadamu wengi waliogeuka nguzo ya chumvi baada ya kutokutii sauti ya MUNGU iliyowakataza jambo fulani.
Ndugu usikubali kuwa nguzo ya chumvi.
Itii sauti ya MUNGU ambayo ni Biblia takatifu.
Mtii YESU KRISTO maana ndiye pekee aliye na uzima wako wa milele.
Mtii ROHO MTAKATIFU maana bila kuwa na yeye huwezi kumpendeza MUNGU.
Kutenda dhambi ni kujifanya nguzo ya chumvi.
Mche MUNGU na jifunze Neno la MUNGU kila siku.
Kataa dhambi, iogope dhambi, ikimbie dhambi na usifanye dhambi tena.
Usiwafuate wanaomkataa YESU KRISTO na wokovu wake.
Hata kama unaishi nyumba ya wapinga Kristo lakini wewe endelea mbele na YESU KRISTO maana nje na yeye hakuna uzima.
Tulia kwa YESU na kwenye fundisho lake ili ukue kiroho na ili wapambe wa shetani wasikunase.

''Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti;  nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo. Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.-2 Timotheo 4:3-5 ''

Ndugu usikubali kumwacha YESU hata iweje. Kumbuka kumpenda YESU ni kutii Neno lake na ni kuishi maisha matakatifu katika yeye. 
Usifuate  hadithi za uongo ambazo ni maandiko yaliyo kinyume na Biblia. 

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili


Comments