UWE MAKINI KATIKA KUMPATA MCHUMBA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Uwe Makini sana katika kutafuta Mchumba.
Vigezo vyako vya kwanza vya mchumba anayekufaa naomba iwe Maisha safi matakatifu ya wokovu wa KRISTO.
Kuna watu  vigezo vyao vya wachumba wanaowafaa ni pesa au uzuri wa umbo na sura lakini katika wenye ndoa zenye migogoro ni pamoja na wenye sifa hizo za uzuri na pesa.
Kijana au binti katika harakati zako za kutafuta mchumba nakuomba sana sana ujifunze kumsikiliza MUNGU kwanza.
Zaburi116:1-2 '' Haleluya. Nampenda BWANA kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake, Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote.''
 
Sasa mtihani kwako kijana ni kwamba kama humchi MUNGU utamsikilizaje?
Kama unaishi maisha ya michanganyo utaielewaje sauti ya MUNGU?
Kama unawadharau watumishi hai wa MUNGU utapataje msaada wa kujua sauti ya MUNGU?
Kama hata kanisani huwa huendi na hata ukienda unaenda kimazoea tu, je utapate ufahamu sahihi hata uielewe sauti ya MUNGU?
Kama wewe kichwani mwako umejaza tu mambo ya kidunia na sio Neno la MUNGU je utaisikiaje sauti ya MUNGU inayosema na wewe?
Kama unamdharau mchungaji wako na viongozi wako wa kanisa, je utaielewaje sauti ya MUNGU inayozungumza na wewe?
Kama huheshimu wazazi wako wa kiroho na kimwili je utaielewaje sauti ya MUNGU?


MUNGU leo anasema kwako kwamba;
 ''Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu; Tazama, nitawamwagia roho yangu, Na kuwajulisheni maneno yangu.-Mithali 1:27''
Kuna watu kwa sababu ya kutokumsikiliza BWANA YESU wamejikuta wanaolewa na wachawi au waganga.
Kuna watu kwa sababu ya kutokumsikiliza ROHO MTAKATIFU wamejikuta wanaolewa  na mawakala wa shetani.
Kuna watu kwa sababu ya kutokumsikiliza MUNGU wamejikuta wanapishana na kusudi la MUNGU juu ya maisha yao.
Ndugu, najua nimekupa changamoto lakini nakuomba sana tendea kazi ujumbe huu kwa kuamua kumcha MUNGU na kumwabudu katika njia sahihi ya wokovu wa KRISTO YESU.


Zakaria 1:3 '' Basi, uwaambie, BWANA wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema BWANA wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. ''

 Kama uko mbali na wokovu hakikisha unaokoka na kuachana na dhambi.
Kumbuka ukikosea kuchagua itakuwa kukusumbua baade.
Na MUNGU anasema;
'' Maana mimi nakuchukia kuachana, asema BWANA, MUNGU wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema BWANA wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana-Malaki 2:16''

MUNGU anachukia wanandoa kuachana.
MUNGU hataki wanandoa muachane, tena kuachana ni dhambi.
Hakuna talaka katika ndoa za Wateule wa MUNGU hivyo jitahidi sana wewe ambaye hujaoa au kuolewa anza na BWANA YESU kwa kuokoka ili yeye ayanyooshe mapito yako na kwa maombi yako atakupeleka kwenye kuchagua mtu sahihi kwako, anayemcha MUNGU na atakayekusaidia ili wote wewe na yeye muishi maisha matakatifu ya kumpendeza MUNGU.

Lakini katika ulimwengu wa leo ni vigumu sana kumjua mcha MUNGU sahihi maana wasanii ni wengi sana.
Kuna baadhi ya mabinti uvaaji wao tu umesananisha wasiolewe.
Kama unatembea uchi unadhani ni nani atataka akuoe?
Ni nani anayependa mali zake ziwafaidishe wengine wasiohusika?
Mavazi ya ajabu ajabu yanaweza kukufanya binti usipate mchumba kwamwe.
Kama mtu anavyoweza kuficha pesa yake mbali ili isionekane na watu ndivyo hivyo hivyo mwanaume anataka sehemu nyeti za mwili wa mke wake mtarajiwa zisionekane na watu wengine.
Sasa wewe binti unayetamani kupata mchumba utampata mume mwema kweli? 

Maana mume mwema hutaka sehemu zako za mwili zilizo nyeti zisionekane na watu. Anaweza akaahilisha kukuoa kwa sababu tu ya mavazi yako ya kikahaba kahaba.
Kama binti utataka kupata mume mwema ni muhimu sana ukawa makini pia katika suala la mavazi.
Siku moja natoka gongolamboto naenda Kawe, nilipofika Mawasiliano stendi nikiwa natembea kuelekea kwenye magari ya kawe kuna binti mmoja alikuwa amevaa kisketi kifupi sana na amekaa akisubiri gari. Inaonekana yule binti alikuwa amesubiri gari muda mrefu hadi akajikuta hawezi kubana miguu muda wote hivyo akajikuta amepanua miguu yake na kubaki uchi kabisa. Kuna vijana fulani upande wa pili walikuwa ndani ya gani wakimvuta tu kwa camera zao za simu. Mapaja yote yalikuwa nje, nikiwa namkaribia yule binti akanitazama machoni na kunikuta nawaangalia wale vijana kwenye gari wanaomvuta kwa kamera, huku natikisa kichwa akawa amegundua kosa lake na kujitengeneza vizuri, mimi nikaendelea na safari yangu. Sasa kwa maswali ya kawaida kabisa binti kama yule mfano amekuja mchumba sahihi na akamkuta katika hali hiyo, je anamuoa?
jibu ni hapana maana apandocho mtu ndicho atakachovuna.

Wagalatia 6:7 ''Msidanganyike, MUNGU hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.''
 
Je binti kama huyo akivaa hivyo kanisani na vijana wakamuona si watatangaziana wote kanisani na nje ya kanisani na kumfanya binti yule asipate mchumba? Ndio watafanya hivyo.
Hivyo mavazi yako binti yanaweza kukuacha katika maisha yako unasema tu una laana ya kutokuolewa kumbe tabia yako na mavazi yako ndio laana yako ya kukufanya usiolewe.
Wacha MUNGU huwa hawako hivyo ndugu.
Badilika na okoka na anza kumcha MUNGU katika kweli.

'' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.-1 Yohana 2:15-17 ''
 
Kuna wengine mnadanganyana kwamba MUNGU haangalii mavazi bali roho lakini mnasahau kwamba wachumba wataangalia mwili na kama wakiukuta mwili uko kikahaba watakuita tu wakala wa shetani na kukuacha.
MUNGU anaangalia vyote, kama ulikuwa hujui basi jua leo na acha kuvaa kikahaba.
Unakuta binti amevaa kikahaba harafu anachelewa kanisani, na akifika kanisani anatembea kwa madoido kwenda kukaa kwenye viti vya mbele. Ndugu, wanaweza wakakuchekea baadhi ya watu lakini hiyo ni hasara kwako na hata unaweza ukabeba laana kwa sababu ya utoto wako huo.

Yakobo 4:7-10 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza. ''


Uwe makini sana katika kumpata mchumba sahihi.
Badilika kwanza wewe ndipo utaweeza kumpata aliye wa kufafa na wewe, yaani mtakatifu kama wewe.
Kama hujabadilika itakuwa rahisi kwako kumpata pia ambaye hajabadilika na wala hana hofu ya MUNGU.
Kama uasherati umekuwa nyoka kwako aliyekumeza mwili mzima basi badilika leo ndugu.
Uasherati una madhara mengi sana.
Unaweza ukaambukizwa magonjwa kwa sababu ya uasherati wako. Unaweza ukapata maagano ya kipepo kwa sababu ya uasherati wako.
unaweza ukasababisha ulinzi wa MUNGU juu ya uchumba wako ukaondoka na uchumba huo kuvunjika kwa sababu tu ya uasherati wako.
Uasherati unaweza ukasababisha mimba za mapema na kuharibu future ya maisha yako ya baadae.
Uasherati unaweza kusababisha ukafukuzwa shule au kazi.
Kuna madhara mengi sana katika uasherati.

Katika uchumba usikubali hata siku moja kufanya uasherati.
Kama huyo mchumba wako anakupenda basi akutolee mahali na mfunge ndoa takatifu kanisani na sio uasherati.
Kama huyo binti anakupenda basi akubali umtolee mahali na mfunge ndoa  na sio uasherati.
Ogopa uiasherati na usikubali hata siku moja kuingia katika uasherati.
1 Kor 10:8 ''Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu.''
Kuna watu zamani waliwahi kufa siku moja watu 23 Elfu hivyo uasherati hautakiwi kutajwa kwako ndugu yangu.
Waefeso 5:3 '' Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;'' 
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

Comments