BWANA YESU ANAKUITA WEWE MCHAFU ILI AKUFANYE SAFI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Bwana YESU anakuita wewe uliye mchafu ili akufanye kuwa safi kama ukimtii yeye na Neno lake.
Dhambi zako ni uchafu kwa MUNGU lakini YESU anakuita leo ili akufanye kuwa safi.

Kwa kinywa chake Bwana YESU anasema leo kwamba 
 ''Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.-Mathayo 11:28'' 

Ni upendeleo wa ajabu anautoa Bwana YESU kwako mwanadamu uliye mchafu.
Uchafu ni mbaya na uchafu una madhara mengi.
Hakuna yeyote mwingine anayeweza kukufanya uwe safi kwa MUNGU ila ni Bwana YESU KRISTO pekee.
Usiridhike na uchafu wako bali amua kumfuata Bwana YESU ili akuondolee uchafu huo.
Dhambi zako ni uchafu kwa MUNGU lakini YESU anakuita leo ili akufanye kuwa safi.
Kwanini unatakiwa sana uondolewe uchafu wako na Bwana YESU?
Ni kwa sababu;
  ''Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa KRISTO na MUNGU. Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi.-Waefeso 5:5-6 ''

Dhambi zako ni uchafu kwa MUNGU lakini YESU anakuita leo ili akufanye kuwa safi.
Kusema kwako uongo ni uchafu.

Kila ukaidi  kwa MUNGU chanzo chake ni roho ya kutokutii.
Kutoa kwako mimba ni uchafu sana.
Kunywa kwako pombe na kuvuta sigara ni uchafu.
Kuua kwako ni uchafu, uganga wako wa kienyeji ni uchafu mkuu.
Kuroga kwako ni uchafu mkuu, ujambazi wako ni uchafu na wizi wako ni uchafu mkuu.
Uzinzi wako na uasherati wako ni uchafu mkuu sana na Biblia iko wazi ikisema ya kwamba hakuna uzima wa milele kwa mtu aliye mchafu, hakikisha unaokoka kwanza na kutubu ndipo uchafu wako utafutwa na utasamehewa na kuwa safi.

Dhambi zako ni uchafu kwa MUNGU lakini YESU anakuita leo ili akufanye kuwa safi.
Biblia inasema wachafu hawatauridhi ufalme wa MUNGU.


Wagalatia 5:19-21 '' Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa MUNGU.''

Dhambi zako ni uchafu kwa MUNGU  lakini kwa Neema ya MUNGU leo Bwana YESU ameshuka ili akufanye kuwa safi kama tu utamtii yeye na Neno lake.
MUNGU alikuchagua ili utoke katika uchafu wako na ukawe safi kupitia YESU KRISTO.
Ni kweli kabisa kwa sababu ya dhambi zako jina lako lilikuwa katika page ya waenda jehanamu lakini MUNGU Baba amekuhurumia ili badala ya kwenda jehanamu uende mbinguni kupitia YESU KRISTO kama tu utamtii huyo na kuliishi Neno lake.
YESU KRISTO anakuita leo ili akufanye safi.
Amua tu ndugu kumpokea YESU na kumtii na kuishi maisha matakatifu kuanzia leo ili akufanye kuwa safi.


Warumi 6:23 ''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.''

Kama hutahitaji kuokoka ili usamehewe na Bwana YESU hakika utakuwa unapishana kabisa na uzima wa milele aliouandaa MUNGU kwa ajili ya wateule wake.
Dhambi zako ambazo utagoma kuzitubia siku hiyo zitaongea.
Kuna wakati matendo yako yatakuwa yanaongea.
Jambo la kujiuliza ni kwamba matendo yako wakati huo yatakuwa yanaongea nini?

Ni muhimu sana kumpokea YESU na kuanza kuishi maisha matakatifu katika wokovu wake.
Usipompokea YESU na kuanza kulitii Neno la MUNGU tambua kwamba kuna hukumu na kuna siku matendo yako yatakufuata.

Obadia 1:15 '' Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.''

Ukimpokea YESU na kuokoka matendo yako mabaya yote yatafutwa na sasa utakuwa mtakatifu wa MUNGU. Lakini ukimkataa YESU na Wokovu wake hakika matendo yako hayatafutwa na siku ya mwisho matendo yako yatakuwa shahidi wa kukupeleka jehanamu, Ndugu amua tu kuondokana na uchafu kwa kuamua kuokoka.
Hii ni Neema ya ajabu sana aliyotuletea MUNGU Baba kupitia YESU KRISTO ili sasa tuliokuwa wachafu tuwe safi kupitia KRISTO.
Tuliokuwa hatuna haki kwa MUNGU sasa tunaipata haki ya MUNGU kupitia YESU KRISTO.
Tuliotengwa mbali na Muumbaji wetu sasa tunamkaribia MUNGU kama watoto wanaopendwa, na yeye anasema kwa waliookoka kwamba.
 ''Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,-2 Kor 6:17-18''

Ukijitenga na waganga na ukayatupa matunguri yao kisha ukamua kuokoka hakika MUNGU atakupokea.
Ukijitenmga na dhambi na ukajitenga na muchukizo yote ya dunia hakika utakubaliwa na MUNGU na yeye anasema atakukaribisha kwake uzima wa milele siku ile ikifika.
Usiwaige watu wa kidunia wasio na haja ya kumpokea YESU.
Usiige dhambi zao na uovu wao hata kama wao ni maarufu sana duniani au ni wasomi sana.
Unaweza ukawa msomo sana lakini huna akili hata moja ya kukusaidia kwenda uzima wa milele.
Mfano ni huu;
Inakuaje daktari mwenye degree ananunua pakti ya sigara na kuanza kuvuta sigara hizo zilizoandikwa "Ni hatari kwa afya yako"
Biblia inayo majibu:

Mathayo 11:25 "Wakati ule YESU akajibu, akasema, Nakushukuru, BABA, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga."

Wewe uliyeamua kuokoka ndio unaitwa heri kuliko msomi asiye na YESU.
Watoto wachanga ni watii kwa wazazi wao hivyo na wewe unayemtii MUNGU unafananishwa na watoto wachanga wanaomtii MUNGU Muumbaji wao.
Ni muhimu sana kumpokea Bwana YESU na kuanza kulitii Neno lake la uzima.
Dhambi zako ni uchafu kwa MUNGU lakini YESU anakuita leo ili akufanye kuwa safi.
Kuna faida kuu ukimpokea YESU kama Mwokozi wako.
Ukiwa ndani ya YESU hakikisha;
Unajitambua.
Unajikubali.
Unajifunza Neno la MUNGU.
Unalitii Neno na kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU.

Katika Bwana YESU uzima wa milele ni ndio na hakika.

Dhambi zako ni uchafu kwa MUNGU lakini YESU anakuita leo ili akufanye kuwa safi.
  Moja ya vitu ambavyo Bwana YESU anavifanya kwako ukiokoka na ukamruhusu akutawale ni;
-Anaondoa kiburi ndani yako
-Anaondoa uoga ndani yako.
-Anaondoa uasi ndani yako.
-Anaondoa balaa ndani yako.
-Anaondoa laana ndani yako.
-Anaondoa manung'uniko ndani yako.
Hayo yote atayaondoa kama tu ukimtii na kukitii Neno lake.

1 Yohana 1:9 '' Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.''

Baada ya kumpokea YESU kama Mwokozi wako na kuanza kuishi maisha mataktifu ya Wokovu wake hakika hata ukisema ''Bwana YESU asifiwe'' utakuwa unatenda haki kabisa maana  "Bwana YESU asifiwe" maana yake unatambua kazi aliyoifanya Bwana YESU ya ukombozi kwako.
Kuna wengine ni wepesi sana kusema ''Bwana YESU asifiwe'' lakini matendo yao yamejaa uovu na hawataki kuokoka, hiyo haiwasaidii kwa lolote.
Ndugu usiifanye "Bwana YESU asifiwe" kama salamu tu za kilugha Bali kwa kutambua kazi ya Bwana YESU basi mtukuze na tukuza jina lake maana katika jina hilo tu ndipo tunapata uzima wa milele.

 Dhambi zako ni uchafu kwa MUNGU lakini YESU anakuita leo ili akufanye kuwa safi.

 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments