IJUE HUDUMA YA USALITI

Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa.
"Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti". (MT. 26:14-16)
TAFSIRI YA MSAMIATI
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, neno “Usaliti” maana yake ni “ tendo la kutoa siri za mtu, kikundi au nchi kwa adui wa mtu, kikundi au nchi hiyo.”
Kwa kifupi, "kusaliti" ni "kutoa siri kwa adui kwa nia ya kumharibia maisha na uhai mtu aliyekuamini"! Kusaliti ni "kula njama na adui ili kuhatarisha maisha au maslahi ya upande unaokuamini kuwa ni mwenzao"
Hapa tunaweza kuona kuna aina mbali mbali za Usaliti! Kuna Usaliti wa mtu dhidi ya mtu. Pili, kuna Usaliti wa mtu dhidi ya kikundi ambacho yeye ni mshirika wake. Na tatu, kuna Usaliti wa mtu dhidi ya nchi yake na huu unajulikana kama "UHAINI"
KWANINI MAFARISAYO WALICHAGUA KUWA MAADUI WA YESU?
• Hawakumwamini
Tangu mwanzo mafarisayo na makuhani hawakumwamini Yesu kama Masihi aliyetumwa na Mungu kwao. “Basi Mafarisayo wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika? Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo?...” (YN. 7:47-49).
Kana kwamba hii haikutosha mafarisayo walimtuhumu Yesu kuwa anatumiwa na mkuu wa pepo: “….Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. (MT.12:24)
• Hofu ya kupoteza umaarufu na maslahi binafsi
Pamoja na kutokumwamini Yesu, mafarisayo na makuhani walimchukia Yesu kwa sababu ya mvuto na ushawishi kwa maelfu ya watu kila mahali alipokwenda na jina lake likazidi kuvuma.
Hii ikawa ni tishio kubwa kwao wakajawa na hofu ya “kupoteza umaarufu” na “maslahi binafsi” pamoja na "tishio la warumi" kuwanyanganya uhuru wa kujiamulia mambo yao:
“…..tunafanya nini? Maana mtu huyu anafanya ishara nyingi. Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na warumi watakuja watatuondolea mahali petu na taifa letu.” (YH 11:47-48)
KWANINI MAADUI WA YESU WALIKUBALI HUDUMA YA YUDA YA USALITI?
* Mashtaka yao yalikuwa ya uongo
Maadui wa Yesu waliihitaji huduma ya usaliti kwa sababu hawakuwa na tuhuma za kweli dhidi yake. Walilazimika kutunga uongo ili kutimiza nia ya kumwua Yesu:
"Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione. Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana." (MK.14:55-56)
* Waliogopa kumkamata hadharani
Kwa kuwa Yesu alikuwa kipenzi cha maelfu ya wayahudi wengi kutokana na mema mengi aliyokuwa akiwatendea, maadui zake waliogopa kumkamata hadharani mbele ya umati wa watu kwa sababu wangepigwa mawe na makutano. (Luk.22:2)
Kwa sababu hizi zisizo na mashiko, mafarisayo na makuhani walihitaji mtu miongoni mwa wafuasi wa karibu wa Yesu ambaye angewapa taarifa na mkakati wa kumkamata pasipo umma kujua.
Ndiyo maana Yuda alipowaendea maadui za Yesu walifurahi sana na wakamlipa fedha ili watimize misheni ya kumwua Yesu!
Kama tujuavyo, Yuda alikuwa mtume wa kuchaguliwa na Yesu mwenyewe. Pamoja na hayo, Yuda aliaminiwa hata kuwa mtunza mfuko wa fedha wa huduma ya Yesu!
Kwa hiyo, Yuda alipoamua kumsaliti Yesu, aliwafaa sana Mafarisayo na makuhani kwa kuwa alijua wakati wa kumkamata Yesu ni usiku na nje ya mji! Akawapa ishara maadui za Yesu akisema nitakapowafikisha kwake huyo nitakayembusu ndiye mkamateni. Na ndivyo Yuda alivyofanikisha HUDUMA YAKE YA USALITI DHIDI YA YESU (MT. 26:47-50)
SIFA ZA HUDUMA YA USALITI
Kutokana na kisa hiki tunajifunza kuhusu sifa kamili za "mtu msaliti"! Baadhi ya sifa hizo ni pamoja na kuwa "mtu wa ndani" au "mtu wa karibu" au "mwenye kufahamu mengi ya ndani" na "mwenye kuaminiwa" kuwa ni mtu wa ndani
Katika maandiko tuliyonukuu mwanzoni mwa kisa hiki tumemshuhudia Yuda aliyekuwa mtume na mwanafunzi aliyepewa fursa ya kuaminiwa jinsi alivyofanya: "akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti Yesu"!
TUNAJIFUNZA NINI KUPITIA HUDUMA YA USALITI WA YUDA?
kuna mambo kadhaa ya kujifunza hapa. La kwanza ni ukweli kwamba iwe ni katika imani ya dini, kwenye siasa, au katika makundi mbali mbali katika jamii, lazima kuna watu maalum ambao fikira na hulka zao ni wasaliti!
Jambo la pili tunajifunza kwamba watu wenye kujisikia duni au hofu ya kupoteza umaarufu (insecurities) katika nyanja za uongozi au uzalishaji; au watu wenye tamaa ya mafanikio ya njia za mkato (madhalimu) pamoja na hali ya kutokutosheka ndio hujikuta wanakuwa wasaliti
Jambo la tatu la kujifunza ni kwamba ni vigumu sana kujilinda na "mtu msaliti" mpaka uwe ni mtu uliye karibu sana na Mungu!
Ushahidi hapa ni kwamba, (ukimweka kando Yesu aliyemjua Yuda tangu mwanzo ya kuwa ni shetani) wanafunzi wengine wote wa Yesu hawakuwahi kugundua ya kuwa Yuda ndiye msaliti mpaka alipokwisha kutimiza usaliti wake!
Naomba nikwambie ukweli! Kusalitiwa kunauma kupita maelezo! Na hasa unapokuja kugundua msaliti wako ni yule uliyemwamini, uliyemsaidia na uliyejitoa mhanga ili afanikiwe na pengine hata hapo alipofikia ni matunda ya juhudi zako! Halafu anaamua kukusaliti ili uangamie kwa sababu ya kutokujiamini kwake au ubinafsi wake uliokithiri!
Mwisho kabisa,ukitaka kunusurika na mtu msaliti njia pekee ni kujikabidhi mikononi mwa Mungu peke yake kwa ajili ya ulinzi wake! Hata hivyo, bado kuna nyakati na majira katika maisha haya tutasalitiwa kwa sababu Yesu alikwisha kututahadharisha akisema:
"Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lo lote mtakalopewa saa ile lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu. Na ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, na baba atamsaliti mtoto, na watoto watashambulia wazazi wao, na kuwafisha." (Mk.13:11-12)

Comments