JE MOYO WAKO UMEJAZWA NINI?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.
Je moyo wako umejazwa nini?

Zaburi 139:23-24 '' Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu; Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele.'' 

Moyo Wa Mwanadamu Haiwezekani Kubaki Mtupu. 
Kama Mwanadamu asipojaza moyoni mwake mambo mema basi ni lazima atakuwa amejaza mambo mabaya.
Moyo Wa Mwanadamu Kila Siku Unahitaji Kujazwa Neno La MUNGU. 
Kama Mwanadamu Huyo Atalikwepa Neno La MUNGU Basi Moyo Wake Utajazwa Mambo Ya Kidunia Yasiyo Na Faida Hata Moja.
 Moyo Wa Mwanadamu Ukipungukiwa Neno La MUNGU Moja Kwa Moja Moyo Huo Utakuwa Umepungukiwa Na Nguvu Ya MUNGU. Na Matokeo Ya Moyo Uliopungukiwa Nguvu Ya MUNGU Ni Mtu Huyo Kupenda Anasa Za Kidunia Na Dhambi. Moyo Huo Hufifia Taratibu Taratibu Na Mwisho Hufa Kabisa Kiroho. 
 Kama Kuna Kitu Unatakiwa Kukishika Na Kukitii Siku Zote Basi Ni Neno La MUNGU La Wokovu.
 BWANA YESU Yuaja Hivyo Ndugu Huu Ndio Wakati Wa Matengenezo.
Ukiuruhusu Moyo wako kupenda mambo yaliyo machukizo kwa MUNGU basi hakika utakapotaka kutenda mema hutaweza maana moyoni mwako umejaza mabaya, hadi mabaya hayo yakutoke na yaingie mema ndipo utaweza kutenda mema.

Biblia inasema ;
''Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.-Luka 6:45'' 

Ndugu mmoja alisema kwamba anatamani sana kuokoka na anatamani sana kuacha uzinzi lakini hawezi kuacha maana haijawahi kupita wiki hata moja akiwa hajafanya, na hata akijaribu kuacha lazima tu atajikuta anarudia tena. Moyo wangu ulisononeka sana na nikajaribu kumuuliza je anapendelea vitu gani? Akasema anapendelea nyimbo za kidunia hasa nyimbo za mapenzi, anapenda sana kuangalia picha za uchi na video za uchi, anapenda sana kwenda club, anapenda sana kunywa pombe na kuvuta sigara na anapenda sana kwenda kwenye matamasha ya nyimbo za kidunia. Baada ya kunieleza hayo nikamwambia kwamba kuacha dhambi hiyo ya uzinzi itawezekana tu kama akiamua kujitenga na mambo hayo yote maana yote ni machukizo kwa MUNGU. Moyo wake huyo umejazwa machukizo ndio maana ni rahisi sana shetani kumuongezea dhambi ya tamaa na tamaa hiyo kuzaa uzinzi. Ndugu yule alipoacha tu machukizo hayo na akuanza kwenda kanisani alishangaa tamaa ya uzinzi ikaondoka. Yaliyokuwa yameujaza moyo wake yalipoondoka likaanza kujaa Neno la MUNGU na kumfanya awe mnyenyekevu kwa MUNGU ndipo akashinda.
Huwezi kuwa mlevi kisha eti ukawa mnyenyekevu kwenye Neno la MUNGU.
Ukienda disko huko kuna maroho ya shetani ambayo yataingia ndani yako na kukufanya uwe unaona kawaida kawaida tu mambo ya MUNGU na hivyo unaweza hata kukosa mbingu bure kama nuru ya KRISTO haitaingia ndani yako hata ujue umuhimu wa kuokoka.

Yeremia 17:9-10 ''Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, BWANA, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.''

Kila mtu atalipwa sawasawa na matendo yake siku ya mwisho ikifika.
Ukiruhusu moyo wako ujae mambo ya kidunia ni lazima tu utamsahau MUNGU Muumbaji wako na kujitenga naye.  Neno La KRISTO Ni Ujumbe Wa Mema.
Ujumbe huu ukiingia ndani yako na ukautii hakika shetani hatakuwa na nafasi tena katika moyo wako.
 Penda Kuukimbilia Ujumbe Wa Mema Na Kuutii Ili Uyaishi Mema Ya Sasa Kisha Mema Ya Milele Yaitwao Uzima Wa Milele.

  Mhubiri 2:1 ''Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili.''
Usitumainie Sana Mambo Ya Kidunia Ukamsahau Bwana  YESU. Watu Wengi Hujiona Wako Sawa Tu Na Huendelea Na Mambo Yao Ya Kidunia Lakini Hao Hao Humhitaji Sana Bwana  YESU Wakati Wakikata roho Lakini Huwa Wanakua Wamechelewa Hivyo Kukosa Uzima Wa Milele. 
Ndugu Yangu Nakuomba Wewe Endelea Kumtii BWANA Na Neno Lake, Jaza Neno la MUNGU ndani yako na litiii sana hilo.
Endelea Na Utakatifu Bila Kujali Nani Na Wa Wapi Anasema Nini Juu Yako.
 Shika Maungamo Yako Ya Kuamua Kumfuata KRISTO Siku Zote Za Maisha Yako.

Zaburi 119:11 '' Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.''

  Kuna tofauti kubwa sana kati ya waliojaza Neno la MUNGU ndani yao na wanalitiii na wale walijaza mambo ya kidunia tu ndani yao.
Unaweza Ukawa Mkubwa Kimwili Lakini Usiwe Mkubwa Kiakili. Unaweza Kuwa Mkubwa Kiumri Lakini Usiwe Mkubwa Kiakili. Akili Ninayozungumza Ni Akili Ya KiMUNGU Na Sio Kidunia. Akili Ya Kidunia Ni Hekima Iliyojaa Upumbavu Na Virus Za Shetani lakini akili ya Ki MUNGU ni Neno la MUNGU la uzima wako.
Kuwa Mkubwa Kiakili kwa mambo ya rohoni Inategemea Sana Uhusiano Wako Na MUNGU.
 Kumtii MUNGU Ni Chanzo Kikuu Cha Kuwa Na Akili Nzuri Ya Kutenda Mambo Mazuri Matakatifu. 
Akili Nzuri Ni Ile Tu Inayomtii MUNGU Na Neno Lake.
 Itake Akili Inayomtii MUNGU Na Neno Lake.
Jaza moyoni mwako Neno la KRISTO na litii Neno hilo na hakika utashinda. 
1 Yohana 2:15-17 '' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.''
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments