JILILIENI NINYI NA WATOTO WENU!

Na  Dk Frank P. Seth
“27Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea. 28Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.29Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. 30Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. 31Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?” (Luka 23:27-31)
Leo nimeamka na moyo mzito nikitafakari maisha na mambo mengi ambayo yamenipata mimi na watumishi wengine wa Mungu, wakubwa kwa wadogo. Nikatazama kwamba watu wananitazama vipi, kisha nikatazama ninavyowaona watumishi wengine wa Mungu. Nikaona jambo hili, nikijitazama mimi najiona niko kawaida tu, kumbe! Wapo wananitazama kwa matumaini makubwa wakitarajia jambo jema kutoka kwangu, ambalo mara nyingine sina jema zaidi kuliko walilo nalo wao; lakini wananitazama kwa matumaini makubwa.
Wakati natafakari haya, nikasikia ndani yangu, “msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.” Fikiri BWANA anapita wakati mgumu, anapigwa, wanafunzi wake na watu waliomtumaini wakiona. BWANA anahukumiwa na kusulubishwa machoni pa watu wote. Anavuliwa nguo hadharani na kudhihakiwa kwa namna nyingi, watu wanaona. Ghafla! Kijakazi tu, kijana mdogo, mtumishi wa kuhani mkuu amnasa kibao, watu wanona! Haya mambo yaliwaumiza sana watu waliompenda BWANA. Wale waoliweka matumaini yao kwake kama KIONGOZI na MWALIMU. Wakalia huku wakipigapiga vifua vyao.
BWANA akiyatazama hayo akauliza, ”kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?” Utagundua kwamba haya mambo yaliyomkuta BWANA yatamkuta na yeyote anayemfuata, japo kwa namna tofauti. Kama umeamua kumfuata, utabatizwa ubatizo wake na kukinywea kikombe chake. Hakuna atakaye faidi FURAHA yake bila kuonja MATESO yake. Kama BWANA ni NJIA basi jua sio pana, ni NYEMBAMBA na IMESONGA, wachache wataiona, na wachache zaidi wataipita. Imekupasa KUJIKANA nafsi yako na kubeba MSALABA wako KILA SIKU ndipo UMFUATE.
Kabla hujamtazama MTUMISHI fulani na kumlilia, jua neno hili, imekupasa KUJILILIA WEWE NA WANAO kwa maana hapo hao watumishi wapopita ndipo na wewe utapita, tofauti yako wewe na wao ni kwamba kwa sasa wao “wameangikwa mtini” na wewe utafuata! Jililie wewe na watoto wako.
Bado najifunza, nikitazama USHINDI na USHINDANI. Kama BWANA aliweza kukesha milimani usiku kucha akiomba, kufunga ilikuwa utaratibu wake wa mara kwa mara, Je! Sisi tutawezaje kupona wakati wa USHINDANI kama hatuombi? Kama kufunga ni mpaka tupangiwe na mchungaji na tena tunafanya janja-janja ya kupiga chenga? Je! Wakati wetu wa kujaribiwa ukifika tutavuka? Ni vyepesi kutazama watumishi wengine wakianguka, wakikosea na kufanya yasiyostahili na KUWASENGENYA badala ya kuwaombea, Je! Unajua siku yako inakuja? Je! Unajililia nafsi yako na watoto wako ili mpate kupona na hayo yote?
“Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa” (Marko 10:39b).
Frank P. Seth

Comments