Jinsi Roho Mtakatifu anavyowaongoza watu, ili waweze kuishi na kutembea katika mapenzi ya Mungu.-5

Na Mwl Christopher Mwakasege
Bwana Yesu asifiwe sana!
Wiki iliyopita tuliangalia mfano wa 1 ili kujifunza jinsi Roho Mtakatifu anavyotumia “Uhuru wa Kristo”, ili kumsaidia mtu aweze kutembea katika mapenzi ya Mungu.
Mfano huo wa 1, ulihusu namna ya kuyajua mapenzi ya Mungu, kuhusu “mahali pa kuhubiri neno la Mungu”.
Leo – nataka tuangalie mfano wa 2, unaohusu Roho Mtakatifu kutumia “Uhuru wa Kristo”, kumjulisha mtu juu ya “hatari liyopo mbele yake, ili aweze kukuepusha nayo!”
Nakumbuka miaka kadhaa iliyopita, mama mmoja alinisimulia jinsi Mungu alivyomuepusha na ajali, alipokuwa anatoka mji mmoja, na kwenda mji mwingine alipokuwa anafanya kazi.
Mama huyo alisema, alipokuwa kwenye kituo cha basi akisubiri usafiri, lilikuja basi la kwanza lililokuwa linaelekea alikokuwa anataka kwenda, lakini alisikia moyoni “kufungika” na “kukosa uhuru” wa kulipanda
Kwa hiyo, akaamua kutopanda lile basi, na kuamua kusubiri basi lingine. Lile basi baada ya kupakia abiria – likaondoka! Yeye akasubiri hadi basi lingine lilipokuja, na baada ya kusikia “uhuru moyoni” wa kulipanda – akapanda na kuondoka nalo.
Baada ya kusafiri kama mwendo wa lisaa limoja hivi ….wakakuta lile basi alilosikia moyoni – mwake “uzito” wa kulipanda, limepata ajali – na limeanguka, na kuua karibu robo tatu ya abiria waliokuwa wamepanda humo!
Yule mama akamshukuru Mungu kwamba, alitii ile hali aliyoisikia moyoni mwake – na kuamua kutolipanda lile basi! Mimi nikamwambia ya kuwa ni Roho Mtakatifu wa Mungu aliyemwekea ishara ile moyoni mwake, ili apate kumwepusha na hatari iliyokuwa mbele yake!



Yule mama asingetii vile viashiria vya Roho Mtakatifu moyoni mwake – vya “kusikia kufungika moyoni na kukosa uhuru wa kupanda” lile basi la kwanza, ina maana angekuwemo na yeye katika ile ajali mbaya iliyotokea!
Tunaona msaada huu wa Roho Mtakatifu, akipewa pia mtume Paulo katika safari zake. Kuna wakati mtume Paulo alipewa tahadhari ya hatari, katika safari ya kwenda Yerusalemu, iliyokuwa mbele yake.
Mtume Paulo aliwambia wenzake hivi: “Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja” (Matendo ya Mitume 20:22,23).
Mtume Paulo aliposema “Roho Mtakatifu….hunishuhudia akisema….”; alitaka wenzake wajue ya kuwa aliwekewa kiashiria cha “kufungika rohoni” mwake, kwa ajili ya kumjulisha hatari zilizokuwa mbele ya safari yake – ikiwa ataendelea na mpango wa kusafiri kama alivyopanga.
Lakini ukisoma Matendo ya Mitume 20:24, utaona ya kuwa, mtume Paulo aliamua kupuuzia lile onyo la Roho Mtakatifu, na kuamua kuendelea na safari kama alivyopanga!
Roho Mtakatifu hakumkatia tamaa – bali alisema naye tena, na kumwonya juu ya hatari zilizokuwa mbele yake, ikiwa angeendelea na safari yake ya kuelekea Yerusalemu!
Onyo la pili alipewa akiwa amefika Tiro (Matendo ya Mitume 21:3, 4), akiwa njiani akielekea Yerusalemu. Onyo la tatu alipewa akiwa amefika Kaisaria akitokea Tiro kwa kupitia Tolemai (Matendo ya Mitume 21:7 – 14).
Onyo la nne alipewa akiwa amefika Yerusalemu, na wakati ghasia zikiwa zimeanza mjini pale kwa ajili yake (Matendo 22:17 – 21).
Kutokutii huko kwa mtume Paulo, kulivuruga sana maisha na huduma yake – kiasi cha kuondolewa hapo “akiwa mfungwa” ili apelekwe Rumi kwa ajili ya kusikilizwa kesi yake!
Ndani ya shuhuda hizi mbili nilizokushirikisha – juu ya yule mama aliyepona ajali na juu ya mtume Paulo – tunajifunza yafuatayo:
(i) Unaposikia moyoni mwako “uhuru wa kusafiri” umeondoka, na badala yake unasikia “kufungika”, au “kukinai” au “uzito” kusafiri – wakati ulikuwa unajiandaa kusafiri – ina maana Roho Mtakatifu anakupa ishara ya kuwa, ukisafiri kama ulivyopanga, kuna jambo litakalotokea ambalo si zuri kwako. Tafadhali usipuuzie!
(ii) Ikiwa utapewa ujumbe kama huo wa (i) hapo juu, na ukauelewa, lakini mazingira hayakuruhusu kuahirisha – basi – ingia katika maombi ili Mungu akusaidie kubadilisha mazingira hayo ili usisafiri! Au hata kama ukisafiri, basi Mungu apate kukulinda na hatari zilizoko mbele yako! Hivi ndivyo ilivyotokea katika safari ya mtume Paulo, ya kutoka Yerusalemu akipelekwa Rumi kwenye kesi yake (Soma Matendo ya Mitume 27:9 – 44).
(iii) Si kila wakati ukisikia “kufungika” moyoni na kupoteza “uhuru” wa kusafiri – ina maana usisafiri kabisa! Kuna wakati mwingine ina maana – badili usafiri unaotaka kuutumia; au badili siku unayotaka kusafiri; au badili njia uliyokusudia kupita!
Ukijizoeza kuomba ushauri na ufafanuzi kwa Mungu, unaposikia viashiria vya Roho Mtakatifu kama hivyo moyoni mwako, uwe na uhakika Mungu atakupa maelekezo sahihi wakati huo, juu ya kile utakachotakiwa kukifanya!
La msingi ninalokushauri – usipuuzie viashiria kama hivi unapotaka kusafiri – hata kama sababu inayokufanya usafiri ni ya muhimu sana! Gharama ya kupuuzia inaweza ikawa kubwa sana kwako!


 Tujifunze pia jinsi Roho Mtakatifu anavyoongoza mtu ili aweze kuishi kwa kutumia tunda la “Kiasi” (Wagalatia 5:22,23), ili kile anachokifanya kisikinai watu, na asije akajikuta anachukiwa – bila kuelewa ni kwa nini iwe hivyo.
Mithali 25:17 inasema hivi: “Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi; asije akakukinai na kukuchukia”Neno hili “kiasi” lilivyotumika kwenye mstari huo wa biblia, lina maana ya: “Kipimo cha kukusaidia kupima, na kujua, kama unachokifanya hakijavuka, au hakijapita, au hakijapungua – kiwango kinachotakiwa, au kilichoruhusiwa”.
Tunda la “kiasi” aliloweka Roho Mtakatifu ndani ya moyo wako, lina kazi mojawapo ya kukusaidia, kuhakikisha ya kuwa kile unachofanya hakivuki “mpaka” wa kukubalika kwake, hakivuki “kiwango” cha kukubalika kwake!
Kufuatana na Mithali 25:17 unachokifanya kikivuka “kiasi”, au kikivuka “kipimo” kinachoitwa “kiasi”; matokeo yake ni unachokifanya kukinai na kuchukiza wale unaowafanyia na kuwafanya wakikatae – hata kama nia yako ya kukifanya ilikuwa njema!
Ni sawa na mpishi “kuzidisha” chumvi au mafuta kwenye chakula, zaidi ya “kiwango” au “kiasi” kinachotakiwa na walaji wa chakula chake. Walaji watakinai chakula kile, na kukichukia na kukikataa! Na ikiwa wataamua kukila kilivyo – watakula huku wakinung’unika!
Nia ya mpishi inaweza ikawa njema katika kuwapikia chakula na kuwapa; lakini kwa kuwa amezidisha “kiasi” cha chumvi, na cha mafuta kinachotakiwa na “walaji” wa chakula hicho, anajikuta kazi yake hiyo – walaji wakiikinai, na kuichukia na kuikataa!Na ndiyo maana Roho Mtakatifu huwa anaweka “tunda la kiasi” ndani ya mtu, ili aweze kumsaidia kujua “kiasi” cha anaohusiana nao, ili asije akapita “kiasi” kinachotakiwa!
Ndiyo maana mtume Paulo aliandika hivi: “Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunai; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani” (Warumi 12:3).
“Nia ya kiasi” ina maana ya kiwango cha kusudi ulilonalo na juhudi ulizonazo – katika kufanya unachokifanya, usivuke kiwango cha “kiasi” cha uwezo wa kupokea, wa wale unaowafanyia!
Mtume Paulo anaendelea katika Warumi 12:6 – 8 kueleza mifano ya maeneo ambayo yanatakiwa yasivuke “nia ya kiasi” yanapofanywa. Maeneo hayo ni kama vile: Katika kutoa “unabii”, na katika kutoa “huduma” yo yote, na pia “katika kufundisha”, na “katika kuonya”, na “katika kukirimu”.
Ukizidisha “kiasi” kinachotakiwa – utajikuta uliowafanyia hicho kitu – wakikukinai na kukuchukia na kukukataa – pamoja na kukikataa hata hicho ulichokuwa unakifanya – hata ikiwa nia yako ilikuwa njema!
Kumbuka: Hata kama nia yako ni njema, ni lazima iwe na kiasi, la sivyo unachokifanya kinapoteza kukubalika kwake, kwa huyo unayemfanyia! Hata kama ni kumtembelea mtu au jirani yako – usizidishe kiasi kinachotakiwa!
Changamoto ya jambo hili ni kwamba “kiasi” kinachotakiwa mtu mwingine huwezi kukijua bila ya kuambiwa kiwango cha kiasi kinachotakiwa ni kipi – au labda ubahatishe tu!
Kwa mfano, si rahisi mpishi akajua “kiasi” cha chumvi kinachotakiwa na mlaji wa chakula chake bila ya kuambiwa kabla ya kukipika!Na ikiwa walaji wa chakula hicho ni zaidi ya mmoja – changamoto inakuwa kubwa kwa mpishi, ya kujua kiasi cha chumvi kinachotakiwa na kila mlaji wa chakula chake! Ni lazima mmoja ataona chumvi ni kidogo ….maana yake haijafikia kiasi alichotaka kiwekwe; au mwingine ataona chumvi imezidi, ikiwa na maana chumvi imezidi kiasi kilichotakiwa kuwekwa! Na mwingine utakuta hapendi chumvi kabisa kwenye chakula chake!
Tunaweza kutafakari hili hata kwa kuangalia kiwango cha pilipili ndani ya chakula! Kiasi cha pilipili kinachotakiwa ndani ya chakula – kinatofautiana sana kati ya walaji wa chakula!
Ndiyo maana unapookoka, Roho Mtakatifu anaingia ndani ya moyo wako akiwa na “tunda la kiasi”, ili aweze kukujulisha “kiasi” cho cote unachohitaji kukijua – ili usijikute wale walio karibu na wewe wanakukinai, na kukuchukia, na kukukataa!
Tunda la “kiasi” linafanyaje kazi ndani ya mtu? Biblia inatuambia katika Warumi 12:3 – 8 ya kuwa “nia ya kiasi” inatakiwa ifanye kazi sawasawa na “kiasi cha imani” alicho nacho huyo mtu, na “kwa kadri ya neema” aliyopewa na Mungu.
Na kufuatana na Warumi 5:1,2 “imani” na “neema” ndani ya mtu vinafanya kazi na viashiria vya Roho Mtakatifu kama vile “amani ya Mungu”.
Na kiashiria cha “amani ya Mungu” huwa kinafanya kazi kwa karibu sana na viashiria vingine vya Roho Mtakatifu kama vile “uhuru wa Kristo”, na “huzuni ya Mungu”.
Kwa hiyo jifunze na kumbuka yafuatayo:
(i)Unapomfanyia mtu kitu mara kwa mara, na ukasikia moyoni mwako unapoteza “uhuru” wa kuendelea kukifanya – ujue ni kiashiria toka kwa Roho Mtakatifu kukujulisha ya kuwa umefikia kikomo cha “kiasi” ambacho mtu huyo anakihitaji toka kwako. Kwa hiyo usiendelee kufanya ulichokuwa unakifanya.
(ii) Unapomfanyia mtu kitu mara kwa mara, na ukasikia moyoni mwako kukosa “amani”, ujue ni Roho Mtakatifu anakujulisha kuwa; umevuka “kiasi” cha ulichokuwa unatakiwa kukifanya. Tena – ujue na huyo unayemfanyia “amekosa amani” na hicho unachomfanyia! ….hata ikiwa bado hajakuambia. Kwa hiyo acha na usitishe kukifanya mara moja …na utaona amani imerudi moyoni mwako.
(iii) Unapomfanyia mtu kitu mara kwa mara, na ukasikia “huzuni” moyoni mwako; basi ujue ni Roho Mtakatifu anakujulisha ya kuwa, umevuka “kiasi” kilichotakiwa na umesababisha jambo kuharibika. Na ili huzuni hiyo iondoke moyoni mwako, haitoshi tu kuacha kufanya ulichokuwa unakifanya. Lakini uombe toba ili Mungu arekebishe kilichoharibika.
(iv)Vivyo hivyo – ukiwa na mtu anakufanyia jambo mara kwa mara – hata kama ni zuri; lakini moyoni mwako ukaanza kukosa “uhuru” wa kulipokea, na ukakosa “amani” na wakati mwingine kupata “huzuni”; basi ujue ni Roho Mtakatifu anakujulisha ujumbe kama huo nilio utaja hapo juu katika (i) na (ii) na (iii).
Ni matumaini yangu hutaacha kumshirikisha mwingine baraka za mafundisho haya; na tena wiki ijayo utakuwa pamoja nasi katika kujifunza zaidi juu ya jambo hili!

Comments