KIPIMO CHAKO CHA KUMKUBALI MCHUMBA ISIWE NDOTO TU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.
Kusudi la MUNGU ni wewe uoe au uolewe na wa kufanana na wewe.
Sio kufanana sura au nywele au pua bali kufanana utakatifu sahihi.
Wewe ukiwa mtakatifu na MUNGU atakupa wa kufanana na wewe yaani atakupa mtakatifu kama wewe ulivyo mtakatifu.




Mwanzo 2:18 '' Bwana MUNGU akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.''


Mke au Mume wa kufanana na wewe anapatikana kwa MUNGU tu.

Kama wewe huishi maisha matakatifu basi MUNGU hatakupa ila utajichagulia wewe.
Mimi Peter nimeyapitia maisha ya ujana ndio maana nafundisha vijana kwa habari ya Mchumba.
Katika maisha yangu ya kabla sijaoa nimewahi kujulishwa na mabinti 4 kila mmoja kwa wakati wake kwamba amefunuliwa kuhusu mimi kwamba nitamuoa lakini mtu niliyekuja kumuoa ni yule aliyekuja kufunuliwa baadae sana baada ya mimi kufunuliwa.
Kwanini ninayasema haya?
Ndugu, MUNGU huwafunulia watu wake lakini pia shetani naye ana uwezo wa kuwafunulia watu watu wa MUNGU ili waende nje na kusudi la MUNGU.
Si kwamba hao waliofunuliwa kuhusu mimi hawakuwa watu waliookoka na wanaishi maisha matakatifu, ila sio kila mtakatifu ni wa kwako bali kutoka katika kundi la watakatifu MUNGU atakupa aliye wako.
Hivyo ndugu yangu ambaye hujaoa au kuolewa nakuomba tena nakuomba sana sana kwamba Mchumba wako usimthibitishe kupitia ndoto tu bali mthibitishe katika utakatifu na kumcha MUNGU, Tena mthibitishe katika nia ya KRISTO ndani yake.


 Kuna Ndoto za aina tatu(3).

1.  Kuna ndoto kutoka kwa MUNGU.

 Mwanzo 20:6 ''MUNGU akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse.''

 2.  Kuna ndoto huletwa na shetani 

Zakaria 10:2 '' Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji.''

3.   kuna ndoto kutoka kwako mwenyewe kupitia yale ambayo yameujaza moyo wako muda wote.

Mhubiri 5:3 ''Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno.''

 Leo sifundishi ndoto maana nimewahi kufundisha sana kuhusu ndoto ila nataka nikupe angalizo kidogo kama wewe huwa unataka mpaka uote ndoto ndipo ujue umepewa Na MUNGU huyo Mchumba wako.
Kwa sababu kuna aina tatu za ndoto, Je ndoto uliyoona wewe kuhusu mwenzi wako unadhani imetoka kwa MUNGU?
Sio ndoto zote hutoka kwa MUNGU ndio maana unatakiwa uwe makini sana.
Kuna Ndoto hutoka kwa MUNGU lakini zikionyesha jambo lisilotoka kwa MUNGU ili tu kukufundisha wewe ujue na ujue namna ya kuomba, Hivyo anahitajika sana ROHO MTAKATIFU ili kukusaidia kujua, na ROHO MTAKATIFU huwezi kumpata kama hujaokoka.
Kuna Ndoto hutokea kwa sababu ya kuwazia sana jambo hilo  utajikuta unaota ndoto na kwa sababu unampenda mtu huyo basi hapo hapo utaweka muhuri kwamba ni MUNGU amesema na wewe kumbe ni ufahamu wako unakudanganya.
Ni kweli kabisa MUNGU husema sana  na watu wake kwa njia ya ndoto lakini naomba ujue kwamba hata shetani naye huleta ndoto na hata mawazo yako yanaweza kuzaa ndoto hivyo uwe makini sana na sio ndoto tu ndio iwe kithibitisho chako cha kwamba huyo uliyemuota ndio anafaa kuwa mke mwema wako au mume mwema wako kutoka kwa MUNGU.
Ukiota ndoto naomba uwaze mambo yote matatu ili ujue jinsi ya kumuomba MUNGU na ili upate kitu sahihi.
Kuna watu walipendana tu na kuoana na wanaishi maisha mazuri sana kwa sababu ndoa hiyo ni mpango wa MUNGU, sasa wewe unayesubiri ndoto naomba ujue na hilo pia.
MUNGU anaweza akasema na wewe kupitia upendo tu wa utakatifu.
MUNGU anaweza akasema na wewe kwa ishara na pia MUNGU anaweza akasema na wewe kwa kupitia watu wengine, tena MUNGU anaweza akasema na wewe kwa mazingira tu, hivyo usitarajie MUNGU aseme na wewe kwa ndoto tu.
MUNGU ana njia nane za kibiblia za kusema na watu wake na tena MUNGU anaweza akasema na wewe kupitia njia hata zaidi ya hizo njia nane za kibiblia.

1 Kor 7:2 '' Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.'' 

Kipimo kikuu cha mtu sahihi kwako ni kama mtu huyo anamcha MUNGU katika KRISTO YESU na anamwabudu katika Roho na kweli.
Lakini pia naomba ujue kwamba kama  wewe huishi maisha matakatifu basi wewe mwenyewe pia hufai kuwa mke mwema au mume mwema hivyo hata suala lako la kutaka mke mwema au mume mwema kutoka kwa MUNGU lifute kwanza maana halikuhusu , hadi utakapompokea Bwana YESU kwa upya na kuanza kuishi maisha matakatifu.

Kuna watu husubiri mpaka wafunuliwe ndipo waoe au waolewe.
Ndugu shetani anaweza akakuwahi mapema sana na kukufunulia ukidhani ni MUNGU anakufunulia, lengo tu upishane na kusudi la MUNGU.

Kama Binti ni mcha MUNGU ukimpenda bila hata kufunuliwa na ukawa na amani kwake huyo anakufaa kuwa mke mwema wako.
Kama kijana ni mcha MUNGU na akakujulisha kwamba anataka kukuchumbia kama jambo hilo litapata amani moyoni mwako huyo ni mume mwema wako, sio mpaka uoteshwe ndoto ndugu.

Pia katika kuwa na amani na mtu unatakiwa uangalie kwamba una amani kwa sababu ya nini? na huna amani kwa sababu ya nini?
Kama una amani na kijana huyo kwa sababu tu ana elimu na ana gari basi hiyo ni amani feki.
Kama huna amani na kijana kwa sababu tu hana hela na hana kazi nzuri basi huko sio kutokuwa na amani bali ni tamaa inakutesa.


Waebrania 13:4-5 '' Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.''

Kuna waigizaji pia hivyo inabidi uwe mtu wa maombi sana ndipo utajua ni nani ana mcha MUNGU na ana hofu ya MUNGU ili akufae maishani mwako kama mwenzi wako wa ndoa takatifu.
Mtu ambaye yuko moto kiroho utamjua tu kama ana mcha MUNGU kisawasawa.
Anayemcha MUNGU kisawasawa huyo ndiyo yuko moto kiroho, tena huyo ndiye aliyekua kiroho kuliko hata yule mtu mwenye cheo kanisani na ana miaka zaidi ya 20 Kanisani lakini hamchi MUNGU.
Inabidi uwe makini sana katika kuchagua mwenzi.

Mithali 16:6 ''Kwa rehema na kweli uovu husafishwa; Kwa kumcha BWANA watu hujiepusha na maovu.''

 Usimthibitishe mchumba wako kwa ndoto tu labda kama umethibitisha ni MUNGU amesema na wewe.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments