KUNG'OA, KUBOMOA,KUHARIBU NA KUANGAMIZA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Shalom mteule wa KRISTO.
Yeremia 1:8-10 '' Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA. Ndipo BWANA akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.''

Mteule wa KRISTO uliye muombaji naomba utambue Neno hili.
Wewe umeaminiwa na MUNGU; Hilo ndilo jambo la kwanza unalotakiwa kulijua, ndio maana umewekwa juu ya mataifa ili kumiliki na kutawala.
MUNGU anaposema usiogope ni kwa sababu kwanza yuko pamoja na wewe na amekupa nguvu kuliko adui zako wote.

Ufahamu wa Neno la MUNGU ni wa muhimu sana maana ufahamu huo utakusaidia kujua ufanyeje katika maombi ili ushinde kwa urahisi maadui zako walikufunga usiolewe, usizae, usipate kazi, usifanikiwe au usifanikiwe katika lolote ulitakalo. Kwa kulipitia Neno la kumsikiliza ROHO wa MUNGU hakika utabaini tu nini cha kufanya na ukiomba kupitia hicho unafanikiwa.
Mfano mmoja ni huu;
Mawakala wa shetani huwawahi wamama wengi kutoa sadaka ili kuwazuia kuzaa. Mteule unatakiwa utoe sadaka ya ukombozi wa uzao wako ambao mawakala wa shetani walishatoa sadaka siku nyingi ili kukuzuia kuzaa.
Huo ni mfano mmoja katika ile mingi ambayo mtu wa MUNGU akilitafakari Neno anaweza akajikuta anashinda maadui zake kirahisi sana katika ulimwengu wa roho.

Ukijua kwamba MUNGU yuko upande wako wala hutakiwi kuwaogopa wachawi na wakuu wa giza.
Ukijua ya Kwamba Uko na jina la YESU na Damu ya YESU KRISTO hutakiwi kuwaogopa mizimu na mashetani wote.
Yeremia 18:7 ''Wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuung'oa, na kuuvunja, na kuuangamiza; ''

Wewe ni silaha kali sana kama utaomba kwa imani bila hofu wala wasiwasi wowote.
Silaha lazima iue, iangamize, ibomoe na iharibu.
MUNGU akikutumia huna haja ya kuogopa.
MUNGU akikutumia huna haja ya kusitasita.
Hakikisha tu unaomba kupitia jina la YESU kwa imani na utakatifu.
Hakikisha kwenye ulimwengu wa roho unakuwa silaha ya kupiga mbali na sio karibu tu.
Kuna silaha za kuua mbali, hiyo inategemea na ufahamu wako wa Neno la MUNGU pamoja na imani yenye utakatifu ndani yake.
Katika maombi huwa inategemea na mamlaka uliyonayo na mamlaka hiyo unaiamini vipi.
Ukijua ya kwamba uko upande wa Bwana YESU hakika huna haja ya kuogopa maana mamlaka ambayo uko upane wayo ni kuu na haijawahi kushindwa.
Usiombe kwa kujaribu bali omba kwa kujua kabisa kwamba unashinda kwa jina la YESU.
Usipige sehemu ambayo adui hayupo bali piga adui alipo.
Ndio maana ni muhimu sana ukawa umeokoka na una ROHO MTAKATIFU ndani yako ndipo utashinda maana ROHO wa MUNGU kazi yake ni kukujulisha, kukukumbusha na kukufundisha kwenye mambo yote yakupasayo kutenda.
Una Mamlaka sana kama ukiwa na ufahamu mkubwa wa Neno la MUNGU.
Maneno yanayotoka katika kinywa chako katika maombi ya imani ni moto mkubwa na adui zako ni kuni tu mbele ya maneno yako ambayo unaomba kwa imani yenye utakatifu ndani yake.

Yeremia 5:14 '' Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala. ''

Maombi yako ya vita dhidi ya adui zako ni lazima uyaamini na uombe kwa juhudi baada ya toba ya kweli.

Siku moja tukiwa katika maombi tuliomba kwa juhudi lakini baadae nikasikia sauti ikitoka nje ya kanisa ikisema ''Wewe Kiihelehele tutakupiga na kukushinda leo leo'' Nikajikuta ghafla muda ule ule mwili wangu unasisimka lakini ndio hasira za rohoni zikaongezeka kabisa hivyo nikaongeza kuchochea moto wa jina la YESU na hatimaye nikaona katika ulimwengu wa roho wakiungua maadui wale muda ule ule. Adui anaweza akakutisha lakini hiyo haina maana atakushinda, labda uamue kumgawia ushindi wako kwa kujitenga na kanisa na utakatifu na maombi.
Biblia inakufundisha kwamba maneno ya MUNGU utakayoyatamka katika kinywa chako yana nguvu kama moto na adui zako wachawi na waganga, mizimu na wanadamu wabaya watakuwa kama kuni tu mbele ya moto huo mkubwa na moto utawala. Lakini ufahamu wako juu ya maombi unaweza kukufanya kinywa chako kitoe moto mdogo tu ndio maana unashindwa kupokea ushindi juu ya hitaji lako.
Ndugu ongeza imani ili ushinde katika maombi.
Ongeza utakatifu ili upanue wigo wako wa kupokea kutoka kwa MUNGU.
Ongeza maombi ili ubaki na nguvu za MUNGU siku zote.
Kama wachawi hawajawahi kukuogopa basi ufahamu wako utakapouruhusu umfahamu vizuri Mwokozi wako YESU KRISTO utashinda hakika.
Mithali 18:10 ''Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama. ''

Inawezekana wewe unaomba huku hujaachilia ndio maana hupokei.
Inawezekana wewe unaomba ila sio mwenye haki kwa MUNGU ndio maana hupokei.
Inawezekana wewe umeokoka kabisa na ni mwenye haki kwa MUNGU maana unaishi maisha matakatifu lakini tatizo lako ni kwamba huombi kwa imani ndio maana hupokei.
Ndugu yangu, ruhusu Neno la MUNGU liyatawale maisha yako ndipo utajua jinsi ya kuomba na kupata ushindi.
Jina la YESU linakungoja tu uombe kwa imani huku ukitimiza kumcha MUNGU katika utakatifu wa kweli katika Wokovu wa KRISTO YESU Mfalme wa uzima.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments