KWANINI UKOSEFU WA UPENDO NDANI YA NDOA?.


 
Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.

Mithali 5:18 '' Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako.'' 

Biblia inaagiza kuwe na furaha katika ndoa lakini leo Ndoa nyingi hazina Upendo wala furaha.
Ndoa nyingi zimejaa manung'uniko Kwa sababu Upendo umepoa.
Wanandoa wengi hujiuliza kwanini wakati Wa uchumba walipendana sana lakini baada kufunga ndoa Upendo badala ya kuongezeka kwao umepungua?

Viko vyanzo vingi vya kuwepo Kwa Upendo wakati Wa uchumba na viko vyanzo vingi vya kuondoka Kwa Upendo katika ndoa Kwa baadhi ya ndoa.
Wakati Wa uchumba wachumba huonana Mara chache chache sana na kila wakionana vicheko vingi, vizawadi vingi na wakati Mwingine na uongo mwingi Kwa baadhi ya watu.
Lakini wakati Wa ndoa ule uongo Wa wakati Wa uchumba huonekana hadharani kwamba ulikuwa uongo.
Wakati Wa ndoa kila kitu ni mambo hadharani.

Wakati Wa uchumba kijana anaweza kumuaminisha binti kwamba yeye ni tajiri lakini ndani ya ndoa ni mambo hadharani, kama kufulia mnafulia wote.
Uongo Wa wakati Wa uchumba ni jambo baya sana ambalo linaweza kuondoa upendo wakati Wa ndoa.

Kumbuka uongo hautadumu siku zote bali ni wa kitambo tu kisha utajulikana hadharani kwamba ulikuwa ni uongo.

Mithali 12:19 ''Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.''

Kutokuishi maisha ya uhalisia wakati Wa uchumba kunaweza kuondoa Upendo utakapoanza kuishi maisha yako halisi ukiwa kwenye ndoa.
Uongo ni dhambi mbaya sana na ukiwekeza katika uongo utavuna uongo na maumivu makali.


Ndoa nyingi leo zina migogoro mingi kwa sababu ya uongo.
Wengine baada ya kuibuka migogoro katika ndoa zao ndipo wao huanza kutangaza kwa watu wa nje na hali hiyo kuongeza tatizo na sio kupunguza.  Ni vyema kama ndoa yenu ina migogoro basi mjitahidi kuimailiza migogoro hiyo ninyi wahusika wenyewe.
Mambo ya ndoa ni vyema yangeamuliwa na wanandoa wenyewe, ikishindikana wahusishwe wasimamizi wa ndoa hiyo, ikishindikana wahusishwe wazazi na ikishindikana basi wachungaji wahusishwe.
Lakini sio kusolve mgogoro tu Bali muhimu zaidi ni kushughulikia chanzo cha mgogoro.
Kama ndoa yenu haina msingi kwenye Neno la MUNGU hakika adui atapanda magugu na kusababisha migogoro.

Zaburi 128:1-4 ''Heri kila mtu amchaye BWANA, Aendaye katika njia yake. Taabu ya mikono yako hakika utaila; Utakuwa heri, na kwako kwema.  Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka meza yako. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye BWANA.''

Chanzo kingine kikubwa cha migogoro katika ndoa ni kukosekana kwa maombi.
Kumbuka ulimuomba MUNGU akupe Mke/Mume na baraka hiyo ukapewa lakini umesahau kwamba baraka uliyopewa na MUNGU huwa inalindwa na MUNGU kupitia maombi yako.
Maombi ni muhimu sana kwa wanandoa.
Kila mtu kukaa kwenye nafasi yake ni muhimu sana.
Maisha matakatifu ni silaha ya kumshinda shetani na yote anayotaka kuyaleta.
Ndoa Iliyo Safi Ni Kila Mmoja Kusimama Kwenye Sehemu Yake. Ni Vizuri Pia Wanandoa Wote Wakawa Waelekevu Yaani Wakawa Tayari Kujifunza. 
Uelekevu Ni Kuwa Tayari Kujifunza Na Kuelekezwa. 
Uelekevu Ni Kukubali Kuelekezwa Pale Usipopajua.
 Sio Kwamba Mume Katika Ndoa Anajua Yote Na Sio Kwamba Mke Katika Ndoa Anajua Yote. Kila Mmoja Anajua Baadhi Ya Mambo Na Anamhitaji Mwenzi Wake Amfundishe Katika Yale Mengine. Mfano Mdogo Baba Anaweza Akaachiwa Mtoto Wa Miaka 3 Na Mtoto Akamtoa Jasho Baba Kumlea Lakini Mama Akiwa Na Mtoto Huyu Ugumu Wote Unaondoka. Huo Ni Mfano Mmoja Katika Mingi Kwamba Mume Ni Muhimu Katika Ndoa Sawa Na Mke Alivyo Muhimu Katika Ndoa. 
Ni Muhimu Sana Wanandoa Kusaidiana Na Sio Kulaumiana Tu.

1 Timotheo 2:3-4 ''Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za MUNGU Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.''

Kuna ndoa zingine misingi yao imeanzia vichakani.
Kuna ndoa zingine zilianza kwa sababu tu ya tamaa za kishetani za uzinzi na uasherati.
Kuna ndoa zingine zilianza kwa kutokutii Neno la MUNGU.
Kwa mujibu Wa sheria ya ndoa Tanzania inasema kwamba mwanamke na mwanamume wakikaa pamoja muda Kuanzia Miezi Sita sheria ya Tanzania inawatambua ni mke na mume na hata wakitoka hapo na kwenda wilayami watapewa cheti cha ndoa kilekile ambacho na wewe uliyefungia kanisani unacho. Hiyo ni ndoa halali lakini haiko kibiblia  ni ndoa ya vichakani maana imeanza na uashetati.
 kuna watu huanza na uasherati Wa vichakani, chini ya miti au gesti kisha wanaenda kanisani kuzuga. 

Hao wanatakiwa kitubu maana msingi wa ndoa yao ni dhambi.

Malaki 2:14-16 ''Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu BWANA amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako. Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha MUNGU? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. Maana mimi nakuchukia kuachana, asema BWANA, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema BWANA wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana. ''
Kama watu Wa MUNGU tunatakiwa tuishi Kwa ROHO na tuenende Kwa ROHO.
 Wagalatia 5:25 ''Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.''


Wachumba wakiwa na hofu ya MUNGU wakati wa uchumba wao kutawafanya wawe wakweli na wawazi na jambo hilo litawafanya kuwa na ndoa yeye furaha. Na kwa tendo hilo hata migogoro isiyo na sababu haitakuwa katika ndoa yao.
Usiridhike wakati wa uchumba bali hakikisha kwamba unampata mtu sahihi na anyemcha MUNGU wa mbinguni.
Mithali 27:1 "Usijisifu Kwa Ajili Ya Kesho; Kwa
Maana Hujui Yatakayozaliwa Siku Moja"
.


Kujisifu wakati Wa uchumba kwamba wewe una vitu wakati kiuhalisia huna vitu hivyo inaweza kukufanya usiaminike Kwenye ndoa.
Kuna mabinti ili akubali kuchumbiwa na kijana lazima CV ya kijana yule iwe inazidi CV za vijana waliowahi kuja zamani akawakataa. Na CV anayoitaka binti huyo sio CV ya utakatifu Bali pesa na elimu, ukienda kwa staili hiyo usishangae kukutana na migogoro mikubwa katika ndoa yako maana hamkupendana bali mlitamaniana tu kwa sababu ya elimu na pesa.


 
Ndoa lazima iheshimiwe na watu wote.
 Inawezekana Wewe Huiheshimu Ndoa Yako Ila Nakuomba Heshimu Ndoa Za Watu Wengine. Biblia Inaagiza Kwamba Ndoa Iheshimiwe Na Watu Wote(Waebrania 13:4), Hivyo Heshimu Ndoa Yako. Mweshimu Mmeo Na Wewe Baba Mweshimu Mkeo. Na Wewe Ambaye Hujaingia Katika Ndoa, Nakuomba Iandae Ndoa Yako Ijayo. Ndoa Inahitaji Maandalizi Mazuri Yakiongozwa Na Utakatifu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments