MAFUNDISHO MAKUU SABA(7) YA KANISA LA KRISTO NI HAYA:

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

MAFUNDISHO MAKUU SABA(7) YA KANISA LA KRISTO NI HAYA:

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.
Kanisa la KRISTO ni mjumuiko wa wanadamu wote aliowaokoa YESU KRISTO na sasa wanaishi maisha ya wokovu katika yeye.
Yohana 1:12-13 '' Bali wote waliompokea(YESU) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.'' 

Kanisa la KRISTO sio dhehebu bali ni watakatifu wote kokote walipo duniani waliompokea YESU kama Mwokozi wao na wanaishi maisha matakatifu katika yeye.
Ili uishi maisha matakatifu ni lazima uhudhurie fundisho la Biblia na kwa jinsi hiyo ni lazima uwe na eneo la kukutanika na wenzako waliookoka kama wewe ili mfundishwe Neno la MUNGU na jinsi ya kushinda dhambi na jinsi ya kushinda mambo ya dunia.
Kwa mantiki hiyo ndio maana tunapata kitu kinachoitwa dhehebu na kitu kinachoitwa kanisa la mahali.
Japokuwa mteule yeyote wa KRISTO ni kanisa lakini inampasa mteule huyo aliye kanisa awe anahudhuria mafundisho ya Biblia pamoja katika kanisa la mahali.
Katika kanisa la mahali hapo ndipo kunatakiwa kuwe na fundisho linawafanya wasikiao kuendelea katika kumtiii MUNGU na Neno lake.
Katika kanisa la leo kuna changamoto nyingi sana lakini mimi Peter Leo nakuletea mambo saba muhimu sana ambayo kanisa la KRISTO popote liliko duniani wanatakiwa kufundishwa hayo ili waweze kumpendeza MUNGU na kuurithi uzima wa milele.
 Jambo muhimu kulikumbuka kuliko yote ni hili ;
''Mkristo bila KRISTO huyo sio Mkristo.''

Leo kuna mahali kanisa mafundisho yao makuu ni jinsi ya kubarikiwa mali, wanasahau kufundisha jinsi ya kuwa mtakatifu.
Leo kuna makanisa mafundisho yao makuu ni jinsi ya kuacha kula nguruwe na bata, wanasahau kufundisha jinsi ya kumwabudu MUNGU Baba katika ROHO na kweli.
Kuna makanisa leo mafundisho yao makuu ni jinsi ya kuitunza sabato wanasahau kufundisha jinsi ya kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU na  jinsi ya kuipeleka mbele injili ya BWANA wa sabato.
Leo kuna makanisa mafundisho yao makuu ni jinsi ya kumtii askofu wao aliye mwanzilishi wa dhehebu, wanasahau kufundisha kwamba amelaaniwa amtegemeaye mwanadamu na kumfanya kuwa kinga yake.
Leo kuna makanisa mafundisho yao makuu ni ujasiliamali, wanasahau kufundisha injili ya KRISTO iletayo wokovu.
Leo kuna makanisa mafundisho yao makuu ni Tiba mbadala, wanasahau kufundisha watu jinsi ya kuikimbia dhambi na kujitenga nayo.
Leo kuna makanisa mafundisho yao makuu ni kuoa mke zaidi ya mmoja, wanasahau kufundisha jinsi ya kuacha kuabudu miungu.
Leo kuna makanisa mafundisho yao makuu ni Mariamu na Yusufu, wanasahau kumhubiri KRISTO ambaye ni yeye pekee wa kuwapa uzima wa milele.

Yako mengi katika kanisa la Leo lakini naomba ujumbe huu umsaidie mtumishi yeyote au Mkristo Yeyote ili awasaidie na wengi kurudi katika misingi ya Biblia na mambo gani muhimu zaidi yatakayotusaidia kama kanisa kuingia uzima wa milele.

HAYA NDIO YANATAKIWA KUWA MAFUNDISHO MAKUU YA KANISA KOKOTE DUNIANI.


1. Kumjua na kumwabudu MUNGU wa pekee JEHOVAH/YAHWEH.

Zaburi 83:18 '' Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote.''

Ukimjua MUNGU utamheshimu na kumtii.
Kanisa likimjua MUNGU litamwabudu yeye peke yake.
Huyo MUNGU huabudiwa katika roho  na kweli.
Yohana 4:24 '' MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.'' 

Kanisa lazima lifundishwe kumwabudu MUNGU na sio kingine chochote.

KUMWABUDU MUNGU HUAMBATANA NA;
1.  Kumtii.
2.  Kumcha yaani kuishi maisha matakatifu katika KRISTO.
3.  Neno lake.
4.   Huambatana na kuenenda kwa ROHO wake Mtakatifu.

Usipomwabudu aliyekuumba hakika utakuwa hujitambui kabisa, lakini wapo wasio mwabudu maana wamefundishwa mambo mabaya. Kuna wengine humwabudu kwa midomo tu huku mioyo yao iko kwenye vitu vya kidunia.
Mathayo 15:8-9 ''Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.''

Kanisa lazima lifundishwe kumwabudu muumba ambaye ndiye mwanzo wa uhai wa kanisa na mwanzo wa uumbaji wote.
Biblia inawataka watu kumwabudu MUNGU lakini kama kanisa halifundishwi kuhusu kumwabudu MUNGU basi hakika watajikuta wanaabudu sanamu au watu au mali.

Zaburi 29:2 '' Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.''

2. Wokovu wa YESU KRISTO wenye injili ya amani.

 Yohana 3:16-18 ''Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''

 Wokovu ni mpango wa MUNGU kumuokoa mwanadamu na kumpa mwanadamu huyo uzima wa milele.
Wokovu wa MUNGU una YESU KRISTO. 
Ukimkataa YESU umemkataa MUNGU na wokovu wake.
Kanisa lazima lifundishwe jinsi ya kukaa katika wokovu wa KRISTO maana nje na Wokovu huo hakuna uzima wa milele.

 Waebrania 9:28 '' kadhalika KRISTO naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa WOKOVU.''

WOKOVU WA KRISTO HUAMBATANA NA;
1. Kmumtii KRISTO na Neno lake.
2. Kumtumikia KRISTO.
3.  Maombi.
4.  Utakatifu wa kweli.

Kama kuna fundisho muhimu kanisa kufundishwa ni kuhusu Wokovu wa YESU KRISTO maana ukijitenga na wokovu wa KRISTO umejitenga na mbingu.
MUNGU anasema;
'' Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali WOKOVU WANGU UTAKUWA WA MILELE, na haki yangu haitatanguka. Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao.-Isaya 51:6-7''

Kanisa lazima liambatane na Wokovu wa KRISTO.
Wokovu wa KRISTO ndilo fundisho muhimu la kwanza kabisa katika Kanisa na ndilo fundisho ambalo kanisa lazima liambatane nalo siku zote.
Siku moja mimi Peter nilisikia sauti ikiniambia ''Fundisho  sahihi ni lile tu ambalo YESU KRISTO ni fundisho hilo  kwa lengo la kuwaokoa wanadamu''
Hakuna mwanadamu anaweza kuingia uzima wa milele bila YESU KRISTO.
Biblia inathibitisha ikisema
Yohana 14:6-7 ''YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba(MUNGU), ila kwa njia ya mimi.  Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba(MUNGU); tangu sasa mnamjua, tena mmemwona.''

3. ROHO MTAKATIFU na kazi zake kwa kanisa.

 Yohana 14:26 '' Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. ''


ROHO MTAKATIFU ndiye msimamizi wa kanisa la KRISTO duniani, Hivyo Kanisa sahihi ni lile tu linaloongozwa na ROHO MTAKATIFU.
ROHO MTAKATIFU ndiye mwandishi wa Biblia, Hivyo Watu wakitaka kuijua vizuri Biblia na mpango wake wa wakati huu ni lazima sana kumhusisha ROHO wa MUNGU.
 2 Petro 1:20-21 ''Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa MUNGU, wakiongozwa na ROHO MTAKATIFU.'' 

ROHO MTAKATIFU ndiye anayemshuhudia YESU KRISTO ndani yetu, hivyo kama tukijitenga na ROHO MTAKATIFU hatutamfahamu YESU KRISTO.
Kanisa ambalo halimtambui ROHO MTAKATIFU hilo ni kanisa la shetani na sio la MUNGU na ni kanisa la kijiepusha nalo maana halina Neno la uzima wa milele.
Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.''

KAZI ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA KANISA NI;
1. Kufundisha Kanisa.
2. Kukumbusha kanisa wajibu wao.
3. Kujulisha Kanisa.
4. Kutoa Karama na huduma kwa Kanisa.

Hakuna jinsi unaweza kulitenganisha Kanisa la kweli na ROHO MTAKATIFU.
Warumi 8:9 ''Lakini ikiwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO wa KRISTO, huyo si wake.''

ROHO MTAKATIFU ndiye shahidi wa kwanza wa Kanisa na atakuwa na sisi kanisa milele.
Maufundisho makuu kabisa ya kanisa ni pamoja na mafundisho kuhusu ROHO MTAKATIFU.
Warumi 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''

4. Utakatifu.


 1 Petro 1:14-16 '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.''

Maisha matakatifu na jinsi ya kuishi maisha matakatifu ni fundisho muhimu sana kwa kanisa la MUNGU maana pasipo utakatifu hakuna uzima wa milele.
Zaburi 34:14 ''Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.'' 

Utakatifu ni kukamilishwa na KRISTO.
Utakatifu ni kujitenga na dhambi zote.
Utakatifu ni kuishi maisha kwa kulitii Neno la MUNGU.
Utakatifu unaanza baada ya kumpokea YESU na kuokoka kabisa.

2 Kor 5:17 '' Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.'' 

Utakatifu kwa kanisa hautakiwi kuwa wa msimu bali ni wa kudumu maisha yote.
Kanisa la MUNGU huwezi ukalitenga na utakatifu maana utakatifu ndio tabia ya mbinguni na ndio tabia wanayotakiwa kuiishi wateule wa MUNGU popote walipo.

UTAKATIFU KATIKA KRISTO HUAMBATANA NA;
1.  Kutii Neno la MUNGU.
2.  Kuwasaidia watu watoke dhambi na waje kwa YESU.
3.  Utoaji.
4.  Kuishi maisha ya haki na kutenda haki kwa watu wote siku zote. 

2 Kor 7:1 ''Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha MUNGU.''

Kama kuna fundisho muhimu sana kwa kanisa basi ni kanisa kufundhwa kuacha dhambi na kuishi maisha mataktifu.
Kanisa ni barua inayosomwa hivyo ni lazima isomwe kwa mema ambayo ni utakatifu katika KRISTO.
Isaya  35:8 ''Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.''

5.Kujifunza Biblia nzima kwa jinsi ya KRISTO.

 Waebrani 4:12 ''Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.''




Biblia ndilo Neno la Kweli pekee kutoka kwa MUNGU Muumbaji.
Ukitaka kumpendeza MUNGU basi tii Neno lake.
Biblia imeandikwa kwa miaka 1500 na inahusisha nyakati zote hadi mbingu mpya.
Ukitaka kujua kile anachokisema MUNGU basi jifunze Biblia.
Kanisa la KRISTO lazima lifundishwe kusoma Biblia na kutafakari Neno la MUNGU.
Neno la MUNGU halitapita kamwe.
 Mathayo 24:35 ''Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.''

Kwa sababu sasa tuko katika wakati wa Kanisa, na kanisa hilo ni la KRISTO basi ni vyema sana tukajifunza Biblia kwa jinsi ya KRISTO ndipo tutauelewa mpango wa MUNGU wa wokovu kwetu.

Biblia nzima ni Neno la MUNGU hivyo kanisa halitakiwi kufundishwa tu agano jipya na Zaburri. 
Haitakiwi kanisa kufundishwa tu Agano la kale bali Biblia nzima inatakiwa kuwa fundisho la kanisa.
Kuna maandiko ya Agano la kale yaliandikwa ili kutusaidia sisi katika zama zetu hizi za kanisa.
Kwanini nimesema kwamba li lazima kanisa lifundishwe kuijifunza Biblia kwa Jinsi ya KRISTO?
Ni kwa sababu ndipo tutaielwa Biblia vile atakavyo MUNGU.
Mfano.

=Katika Agano la kale tunaona kwamba MUNGU ndiye atakuja kuhukumu wanadamu wote siku ya mwisho(Zaburi 9:7-8), Lakini Agano jipya linasema kwamba YESU KRISTO ndiye atakuja kuhukumu wanadamu wote(Ufunuo 22:11-13). 
Usipoisoma Biblia kwa jinsi ya KRISTO hutaielewa vyema.
=Katika Agano la kale unaona Waisraeli walikatazwa kula baadhi ya vyakula(Kumb 14:7-8) lakini katika Agano jipya Biblia inasema usikiite najibu kile alichokitakasa MUNGU(Matendo 10:11-15). Kama hujaisoma Biblia kwa jinsi ya KRISTO hutaielewa vyema.
Hiyo ni mifano michache ya kukusaidia kuielewa Biblia vyema. 



KUISOMA BIBLIA HUZALISHA.
1  Kuuelewa mpango wa MUNGU juu yako.
2. Kupata ujasiri wa Ki MUNGU ndani yako.
3. Kuwa na uhakika wa Maisha ya sasa na maisha ya uzima wa milele.
4  Kuwa na msimamo thabiti katika KRISTO.

1 Petro 2:2 ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa(Neno la MUNGU), ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ''

Kanisa lazima lifundishwa sana Biblia.
Kila Mwana kanisa ni muhimu awe na Biblia yake na anawe anatembea nayo ili kujifunza Neno la MUNGU na kulitafakari. 
Kanisa litii Neno la MUNGU dhambi haitakuwa kwao.

Zaburi 119:11 ''Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.''

6. Wajibu wa Mkristo Duniani.


 2 Petro 1:3-4 '' Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.''

Kanisa la MUNGU lazima lifundishwe wajibu wao duniani.
Wajibu wa kanisa duniani ni kuishi maisha matakatifu.
Wajibu wa kanisa ni kuufundisha ulimwengu jinsi ya kumwabudu MUNGU muumbaji.
Wajibu wa kanisa duniani ni kuleta tabia njema duniani.
Kanisa lazima lifundishwe kazi yake duniani.
Kila Mkristo ni kanisa na huyo anatakiwa sana afundishwe kazi yake duniani na wajibu wake duniani.
Mathayo 3:8 ''Basi zaeni matunda yapasayo toba;''


WAJIBU WA MKRISTO DUNIANI NI;

1  Kuishi maisha matakatifu.
2.  Kuwashuhudia wengine injili ya KRISTO.
3.  Kutimiza kusudi la MUNGU la Wokovu.
4.   Kutangaza matendo ya MUNGU duniani.

Kanisa lazima lifundishe sana wajibu wao duniani.
Bwana YESU anasema;
 ''Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.- Yohana 15:16 ''


7.Miiko ya Mkristo Maisha yake.


Mathayo 5:37  ''  Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.''

Kuna miiko mingi ambayo kanisa la MUNGU linatakiwa kutii kulingana na Neno la MUNGU.
Ni miiko kwa sababu haitakiwi kuwa katika kanisa la MUNGU.
Kanisa lazima lifundishwe jambo hilo maana ni muhimu sana.
Kumbuka siku zote shetani hutaka kuwaondoa watu katika kweli ya MUNGU lakini kama tukiijua miiko ya Mkristo basi hatutamtii shetani wala dunia bali tutamtii MUNGU Muumbaji wetu.
Iko miiko mingi na mojawapo katika miiko hiyo ni;
=Kanisa halitakiwi kuipenda dunia na mambo mabaya yaliyomo duniani ambayo yanaweza kuwaondoa watu katika Wokovu na utakatifu.
 1 Yohana 2:15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele. ''

 = Wana kanisa hawatakiwi kuambiana uongo au kusema uongo popote.
Wakolosai 3:9 ''Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake;''

=Uasherati na uzinzi na machukizo yote hautakiwi kuwako  katika watu wa MUNGU.
Waefeso 5:3-4 '' Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. '

Iko miiko mingi ambayo ni machukizo na hayo hayatakiwi kuwako katika watu wa MUNGU.
=Watu wa MUNGU hawatakiwi kwenda kwa waganga wa kienyeji.
=Watu wa MUNGU hawatakiwi kwenda Disko wala kwenye amatamasha ya ynimbo za kidunia.
=Watu wa MUNGU hawatakiwi kuwa wachawi wala wasoma nyota.
 =Watu wa MUNGU hawatakiwi kuwa na nyota zao za unajimu wa aina yeyote.
  =Watu wa MUNGU hawatakiwi  kujitenga na fundisho sahihi la Biblia.
 =Watu wa MUNGU hawatakiwi kuwa na utakatifu wa kanisani tu bali wanatakiwa wawe watakatifu hata kama wako nyumbani au kazini au shuleni au kwenye biashara zao au njiani au popote pale.

Yako machukizo mengi ambayo kanisa halitakiwi kujihusisha.
Kanisa lazima lifundishwe sana kuhusu miiko ya mteule wa MUNGU ili kanisa liweze kutunza utakatifu wa KRISTO.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili


Comments