MAVAZI YA MTU ALIYEOKOKA

Na Askofu Mkuu  Zakaria Kakobe.

Yesu ametuagiza watu tuliookoka katika MATHAYO 5:16,akisema, “Vivyo hivyo nuru yenu iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”. Ni muhimu kufahamu kwamba watu ambao hawajaokoka ingawa hawafahamu kwa undani mafundisho ya Biblia, lakini wanajua sana kipi ambacho hakifai mbele za Mungu; kwasababu kazi ya Torati au Biblia, imeandikwa mioyoni mwao na dhamiri yao kuwashuhudia (WARUMI 2:14-15). Ndiyo maana mataifa wanajua  kwamba wizi, rushwa, magendo, kutoa mamba, kulewa au kuvuta sigara, uasherati au uzinzi, masengenyo, uongo, n.k. vyote hivi ni dhambi, ingawa ukiwauliza maandiko hawajui. Hatuwezi kamwe kuangaza  mbele yao ikiwa tunavaa mavazi ambayo wanajua kwamba ni mavazi yasiyompasa mtu anayesema ameokoka. Ni kwasababu hii, leo tunajifunza kuhusu mavazi ya mtu aliyeokoka;  na tutaligawa somo letu katika vipengele vine:-
( 1 ). UTAKATIFU MWILI NA ROHO
( 2 ). JINSI MAVAZI YANAVYOMTAMBULISHA MTU
( 3 ). AGIZO LA MUNGU LA KUTOKUFUATISHA NAMNA YA DUNIA HII
( 4 ). MISINGI SITA YA KUFAHAMU MAVAZI YANAYOTUPASA KUVAA                                          WATU TULIOOKOKA

( 1 ).  UTAKATIFU MWILI NA ROHO
Watu wengine kwa kutokufahamu, wanafikiri kwamba utakatifu ni katika roho tu na kwamba eti Mungu anaangalia ndani tu, haangalii nje. Hii siyo sahihi kulingana na maandiko. Yesu anasema  “safisha kwanza ndani…………ili nje yake nayo ipate kuwa safi ( MATHAYO 23:26 ). Unaona, ni suala la ndani na nje.Utakatifu ni yote yanayohusiana na mwili unaoonekana nje, na roho inayoonekana ndani                               ( 1 WAKORINTHO 7:34; 2 WAKORINTHO 7:1 ). Yale ambayo mataifa watayaona kwetu ni yale ya mwili yaani ya nje na siyo ya roho wasiyoweza kuyaona kwa macho. Mtu aliyeokoka anatambulika kwa matunda yake na matunda ya mti huonekana nje ya mti siyo ndani ( MATHAYO 12:33 ).

( 2 ). JINSI MAVAZI YANAVYOMTAMBULISHA MTU.
Mavazi yana sehemu kubwa sana katika jamii, katika kumtambulisha kwamba yeye ni nani, ana tabia gain n.k.Kuna usemi wa kiingereza unaosema, “what you wear, tells what yourare”. yaani, “mavazi yako yanaeleza waziwazi  kwamba wewe ni nani”. Kutokana na mavazi ya mtu, tunaweza kumtambua mtu huyo kwamba ni askari polisi au wa usalama barabarani, askari wa magereza, J.K.T, au Jeshi la wananchi, Daktari au Nesi, mwanafunzi au makenika, motto mdogo au mtu mzima., mwendawazimu au mwenye akili timamu n.k. Tukimwona mtu mzima barabarani amevaa nepi, tutajua huyo ni mwendawazimu. Tukimwona mkulima analia huku amevaa suti, tutajua pia kuwa huyo ni mwenda wazimu n.k. Mavazi yanamfanya mtu  adhaniwe kwamba ni kahaba ( MWANZO 38:15 ) Mavazi ya Musa ambaye ni Mwebrania au Mwisraeli, yalimfanya aitwe Mmisri (KUTOKA 2:17-19). Watu tuliookoka, tunaweza kuitwa Wamisri au watu ambao hawajaokoka kutokana na mavazi yetu.

( 3 ).  AGIZO LA MUNGU LA KUTOKUFUATISHA NAMNA YA DUNIA HII
“ wala msifuatishe namna ya dunia hii………..( WARUMI 12:2 )”,ni agizo la Mungu kwetu tuliokoka. Kuwa rafiki wa dunia yaani kuwa kama watu wa dunia, ni kuwa adui wa Mungu (YAKOBO 4:4 ). Hatupaswi kabisa kuzifuata njia za mataifa katika kufanya jambo lolote ( KUMBUKUMBU LA TORATI 18:9; 2WAFALME 17:8-11; 21:2; ZABURI 106:35; YEREMIA 10:2; WAEFESO 4:17 ). Kuna namna ya dunia au mataifa katika mavazi, hatupaswi kuifuatisha. Shetani ni mungu wa dunia hii ( 2WAKORINTHO 4:4 ). Atafanya kila namna kutufanya sisi  tuliookoka tuwe kama watu wa dunia katika mavazi ili tuwe adui wa Mungu. Tukifanya hivi kanisa la Mungu litanyonywa nguvu yake na hatuwezi kuwatiisha Mataifa kwa neno au kwa tendo kutokana na ishara na maajabu ( WARUMI 15:18-19 ). Hatuwezi pia kuwa barua au waraka wa injili unaosomeka kwa mataifa, ( 2 WAKORINTHO  3:2-3 ), Tutawanyoshea kidole kimoja vitaturudia vidole vine.
( 4 ).  MISINGI SITA YA  KUYAFAHAMU MAVAZI YANAYOTUPASA KUVAA WATU TULIOKOKA.
1. Mavazi  ni ya kuficha uchi-Mapambo yoyote hayatakiwi.
Kusudi la Mungu kutupa mavazi ni kuficha uchi wetu (MWANZO 3:21 ). Mapambo yoyote au Vyombo vya uzuri ni machukizo mbele za Mungu ( KUTOKA 33:4-6; HOSEA 2:13; EZEKIELI 23:26-30,40,42; YEREMIA 4:30 ).. Hatupaswi kuyaridhia mafundisho ya Yezebeli mwanamke aliyejipamba kwa uwanja machoni na kupamba kichwa na hatimaye akafa kifo cha kuhuzunisha ( 2 WAFALME 9:30-37; UFUNUO 2:20 ). Heleni au  pete za masikio, dusumali yaani mapambo ya kichwa, vikuku na mafurungu yaani aina zozote za bangili, pete, azama ( pete za puani ), vioo ( miwani ya jua ), marashi, mishipi mikubwa ( fingerbelt ), rangi za macho, midomo au kucha, wanja za macho, mikufu au chain, shanga za aina yoyote, mapambo ya dhahabu yoyote iwe ni mikanda ya saa ya dhahabu au mishipi ya dhahabu, vyote siyo vya lazima na ni machukizo mbele za Mungu ( ISAYA 3:16-26; 1TIMOTHEO 2:9; 1PETRO 3:3-5). Mishipi ni vazi  ( YEREMIA 13:1-2 ), lakini inapokuwa mikubwa kiunoni tayari ni namna ya dunia. Kujipaka marashi au manukato ya kutufanya tunukie kila mahali ni namna ya dunia hii. Yesu alimiminiwa marhamu au manukato ikiwa ni utabiri wa kuzikwa kwake (MATHAYO 26:7-12). Desturi ya wayahudi katika kuzika ilikuwa kuuzongazonga mwili wa maiti pamoja na manukato na madawa ili usinuke maana walikuwa wanakuja kuuangalia. Pia makaburi yao yalikuwa yanachongwa mwambani (YOHANA 19:38-40; MARKO 16:1; 2NYAKATI 16;13-14; MWANZO 49:33-50; 50:26 ). Dhahabu ni nzuri lakini siyo kwa ajili ya mapambo bali ni kwa ajili ya kutengenezea vyombo kama vya hospitali, katika eropleni n.k, ambavyo vinahitaji madini laini ( soft metal ). Wakati Mariamu na Yusufu alipopewa dhahabu kama zawadi kwa mtoto Yesu  ( MATHAYO 2:11 ), haikuwa kwa ajili ya mapambo ya Mariamu, bali kwa ajili ya gharama ya kuondoka Bethlehemu mpaka Misri na kuweza kuishi huko ugenini mpaka Herode alipofariki. Dhahabu ilitumika kama fedha yenye dhamani na iliwasaidia maskini Mariamu na Yusufu. Hekalu la Sulemani lilijengwa kwa dhahabu likaja kuvunjwa ili Mungu atufundishe kwamba hatasita kumwadhibu yeyote.Musa hakuingia Kanaani, hata kama mtu ni tajiri mkubwa ataanguka hukumuni pasipo wokovu ( ZABURI  49:16-20 )
2.  Mavazi ya kukosesha ni machukizo kwa Bwana ( MATHAYO 18:6-7 )
Ni wajibu wa wanawake kuwalinda wanaume kutokana na mavazi yao (YEREMIA 31:22 ). Mavazi yoyote ya kuonyesha ndani , mavazi mafupi yasiyoweza kufunika magoti mwanamke anapokaa, mavazi yanayoacha makwapa wazi yaani yasiyo na mikono, au yanayoacha kifua, tumbo au mgongo wazi, mavazi ya kubana, mavazi yenye matundu au yanayochanwa mbele au nyuma ili kuonyesha underskirt, kujifunga kanga bila kuvaa gauni na kuacha kifua na mgongo wazi, yote haya ni mavazi yanayokosesha wanaume siyo ya Kikristo. Wanaume kuvaa shati bila kufunga vishikizo na kuonyesha kifua hadharani au kufunga taulo na kuacha kifua wazi na kuonekana hadharani, kuvaa bukta hadharani, yote haya ni machukizo.
( 2 ).  Mavazi ya kututambulisha sisi sawa na Mataifa ni machukizo ( WARUMI 12:2 ). Mavazi yoyote ambayo yatatufanya tuonekane kama wahuni au mataifa siyo sahihi katika Ukristo. Jeans, Kadeti, mitindo yoyote ya mashono ya kihuni, viatu virefu vinavyotufanya tushindwe kukimbia na kuwa na mwendowa madaha ( ISAYA 3:16-17 ), kuning’iniza funguo na mafilimbi kwenye mkanda kama mapambo, mashati mapana au kofia za macheki bob n.k, yote haya ni machukizo. Ndevu za kutufanya tuitwe “Mzee Ndevu” au “Mzee Masharubu” tunapaswa kuziondoa.

( 4 ).  Mwanamke hana budi kuvaa mavazi ya kike na mwanamume mavazi ya kiume ( KUBUKUMBU LA TORATI 22:5 ).
Mwanamke hapaswi kuvaa suruali, bukta au kaputura. Brauzi zinazokuwa kama mashati ya kiume au fulana za kiume, mwanaume kuvaa kanga, wanaume kuvaa mikufu n.k., yote haya siyo sehemu ya Ukristo.
( 5 ).  Vaa kwa utukufu wa Mungu ( 1 WAKORINTHO 10;31 )
Hatuvai kwa  kushindana. Kuazimana nguo kwa lengo la mtu  kuonekana  ana nguo, siyo Ukristo. Kupamba kichwa ( 2 WAFALME 9:30 ), kwa kukali nywele, ku-relax kuweka rasta, kuchoma nywele n.k., siyo sehemu ya Ukristo. Mwanamke awe na nywele ndefu kama fahari yake kwa kuzitunza  kikawaida, mwanaume asiwe na nywele ndefu kama za kike ( 1 WAKORINTHO 11:14-15 ). Kwa  ajili ya malaika, mwanamke anaposali au kuomba au kuhubiri afunike kichwa kwakitambaa kisiwe chenye shanga  kama vitamba Arabuni. Hii pia ni kuonyesha dalili ya kumilikiwa na mwanamume ( 1 WAKORINTHO 11:5,8-13 ). Mwanamume wakati wa kusali au kuhubiri hapaswi kuvaa kofia ( 1WAKORINTHO 11:4,7 ).

( 6 ).  Maandishi katika mavazi yanapaswa kuwa yale tu ya kumtukuza Mungu (KUMBUKUMBU LA TORATI 11:18-21).
Kanga au T-shirt au nguo zozote tunazovaa ni lazima tuangalie maandishi yake. Maandishi ya kihuni kama “mtaa wa pili mtanikoma” “Mimi shangingi” “Sijui kosa langu” n.k., hatuna budi kuyafuta au kuyakata na kuyatoa katika kanga zetu na pia kanga zza jinsi hiyo hatupaswi kuziuza katika maduka yetu pamoja na mapambo yote. Vilevile mifuko ya plastiki iliyoandikwa “ MICHAEL JACKSON n.k.,haifai, kwa muhtasari, tuwe macho kuzijua hila za Ibilisi katika mavazi yetu. Anakuja kijanja sana. Saa zinazotoa sauti za muziki usio wa Kikristo ni namna ya dunia hii.

Comments