NAFASI NA UZITO KATI YA AGANO LA KALE NA AGANO JIPYA KATIKA BIBLIA

Na Askofu mkuu Silyvester Gamanywa.

Wiki iliyopita niliwasilisha ujumbe wenye kutahadhalisha kuhusu injili za namna nyingine ambazo zimejikita kwenye sheria na nabii za Agano la Kale! Aidha nilisisitiza ya kwamba injili ya kweli imejengwa katika misingi ya maandiko ya Agano Jipya!
Baada ya mawasilisho hayo nimepata maswali kadhaa yenye kuhoji ni kwanini ninahubiri jumbe zinazochochea tabaka za ubaguzi wa maandiko matakatifu katika Biblia
Pamoja na uchambuzi wa kina nilioufanya katika mada zilizopita bado kuna maswali ambayo kimsingi yanatetea "nadharia ya usawa wa maandiko" kuwa yanatakiwa kutumika kwa ajili ya huduma za injili bila kujali ni kutoka agano la kale au katika Agano jipya
Kwanza ninapenda kuweka Mwongozo kwamba huu "usawa wa maandiko matakatifu" haimaanishi ya kwamba kila kila andiko linatumika kila mahali kwa kila wakati na kwa kila mtu! Yaani mtu hawezi kukurupuka na kuchukua andiko kutoka mahali popote na kulifanyia kazi pasipo kwanza kujua maana yake, na mipaka ya matumizi yake!
Mfano huwezi kusoma andiko kwamba "Yuda akaenda kujinyonga" halafu ukaamua na wewe kwenda kujinyonga kama Yuda au kumshauri mtu kujinyonga ati kwa kuwa imeandikwa katika Biblia!
Kuna maandiko ya kijifunza kwa maarifa ya mafunzo mbali mbali kama historia ya uumbaji wa Mungu, historia ya binadamu toka mwanzo mpaka hivi leo! Lakini kuna maandiko ya kinabii ambayo nabii zake zilikwisha kutimia na kuna nabii nyingine bado zinasubiriwa kutimia
Halafu kuna maandiko ambayo matumizi yake ni kwa ajili ya kuongoza kujenga mahusiano kati yetu na Mungu, au sisi kwa sisi; na maandiko mengine ni ya kutusaidia katika kufanya maamuzi ya kiroho, kijamii, kifamilia, mpaka hata kimaendeleo hapa duniani.
Pamoja na mengineyo mengi katika Biblia kuna maandiko ambayo yako katika MFUMO WA MAAGIZO NA MAELEKEZO ya Mungu KWETU yanayotuongoza katika KUMWABUDU NA KUMTUMIKIA MUNGU kwa kuizingatia maadili ya kiimani aliyotuwekea yeye ili sisi tuyafuate
Sasa haya maandiko ya aina hii ambayo ni maagizo ya Mungu kwetu ndiyo napenda kuyapa uzito katika ujumbe wa wiki hii! Nitasoma baadhi ya maandiko hayo ili tuuachambue kwa kuzingatia uzito wake ndani ya maagano yote mawili katika Biblia!
"Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa". (MK. 16:15-16)
"Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari." (MT. 28:19-20)
Haya basi, maandiko haya niliyonukuu yako katika mfumo wa maagizo makuu kwa wakati huu na sasa nitapenda tuichambue baadhi ya misamiati yake kwa kwa kuzingatia uzito wake wa matumizi yake katika Biblia kuanzia Agano la kale mpaka Agano jipya! Baadhi ya misamiati hii ni kama ifuatavyo: 1.Jina la Yesu; 2.Roho Mtakatifu; 3.Injili; 4.Ubatizo; 5. ondoleo la dhambi ; 6. Wanafunzi; 7.Kanisa/ekklesia ; 8. Kiroho/rohoni
Utaratibu utakaotumika katika uchambuzi wa misamiati ya maneno haya ni kujua maana zake, na matumizi yake katika maagano yote mawili na mwisho tufanye tathmini maagizo haya yanabeba uzito wa maandiko ya Agano lipi? La kale au Jipya? 

TAFSIRI NA MATUMIZI YA JINA LA YESU
• Tafsiri na idadi ya nukuu zake
Utafiti kuhusu jina la Yesu unaonesha ya kuwa limetajwa katika Biblia mara 983. Na nukuu zote hizi zinapatikana katika Agano Jipya peke yake. Agano la Kale halina kumbukumbu hata moja ya Jina la YESU
• Chimbuko la matumizi ya jina la Yesu
Jina hili YESU limetajwa kwa mara ya kwanza katika Injili na Malaika Gabrieli alipomletea Mariamu unabii wa kushika mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na kuzaa mtoto wa kiume ambaye atamwita jina lake YESU. Malaika Gabrieli alitabiri matumizi ya jina la Yesu akisema: “…maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”(MT.1:21)
Hata hivyo, naomba izingatiwe ya kwamba, kutungwa kwa mimba na kuzaliwa duniani kupitia Mariamu Hakumaanishi kwamba huo ndio mwanzo wa kuwepo kwake! Alikuwepo kabla kwa jina jingine la Neno (Logos):
“Hapo mwanzo kuliwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.” (Yh. 1:1-3) Kilichofanyika katika tumbo la Mariamu ni huyu Neno kufanyika mwili wa binadamu duniani kama ilivyoandikwa: “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee kwa Baba; amejaa neema na kweli” (Yh.1:14)
Kwa hiyo, matumizi ya jina la YESU yanawakilisha asili ya UUNGU na UBINADAMU wake. Kabla ya kuvaa mwili, alikuwako kabla akiwa sawa na Mungu mbinguni. Hii inathibitishwa na maandiko ya Wafilipi yasemayo:
"...ambaye yeye alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa mfano wa wanadamu; tena alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.” (Flp.2:6-8)
MAMLAKA YA JINA LA YESU
Mamlaka ya jina la YESU inatokana na Yesu kufanikiwa kukamilisha mchakato wa kazi ya ukombozi iliyomleta duniani. Hii ni pamoja na tamko lake kwa wanafunzi wake mara baada ya kufufuka kwake:
“Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.” (MT.28:18)
Mamlaka ya jina la YESU inatokana na Mungu kumwadhimisha mno kwa kumweka juu ya vitu vyote kama ilivyoandikwa: “Kwa hiyo Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vyote vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; ili kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” (Flp.2:9-11)
Pengine unaweza kuhoji kwamba kama Yesu alikuwapo tangu mwanzo akiwa sasa na Mungu inakuwaje tena anapewa mamlaka ya uungu ambayo aliwahi kuwa nayo? Jibu kamili ni kwamba kabla ya kufanyika binadamu alikuwa sawa na Mungu. Na kwa hadhi hiyo alikuwa na mamlaka ya uungu mbinguni.
Jambo jipya hapa ni "aliyekuwa sawa na Mungu kufanyika mwanadamu; na kubakia katika hali hiyo hiyo ya "uungu kamili na ubinadamu kamili" ambayo ndiyo inabeba jina jipya la YESU!
Hali hii ndiyo ilimfanya aadhimishwe mno baada kumshinda shetani akiwa binadamu kamili na akakamilisha kazi ya ukombozi kwa kuteswa, kufa na kufufuka akiwa binadamu kamili kama ilivyoandikwa: "Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu" (1.Tim.2:5)
Hivi sasa ukifika mbinguni kwenye kiti cha enzi utamkuta Mwana wa Adamu akiwa mkono wa kuume wa Mungu! Wakati Stefano anauawa kwa kupigwa mawe kwa ajili ya Yesu, alipotazama juu akanukuliwa akisema: "...Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu" (Mdo.7:56)
MATUMIZI YA JINA LA YESU DUNIANI
Ningependa kusema kwa kifupi ya kwamba matumizi ya jina la Yesu ndiyo msingi wa Imani yetu duniani! Yesu alitoa kibali kwa wanafunzi wake kuwafanya mambo muhimu yafuatayo:
•Kuwasiliana na Mungu kupitia jina la Yesu
Yesu aliwaelekeza wanafunzi wake kumwomba Mungu kwa kupitia jina lake na sio vinginevyo:
“Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.” (YN. 14:14)
“Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.” (YN. 16:24)
• Kutoa pepo na kuombea wagonjwa kwa jina la Yesu
Kisheria kuna kitu kinaitwa power of attoney maana yake mtu anapewa kibali cha maandishi kilichotiwa saini kwa ajili ya mtu kufanya maamuzi kwa niaba ya mwingine kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo Yesu alitupa sisi kibali cha kisheria (power of attoney) cha kutumia jina lake kwa niaba yake. Ndiyo maana Yesu alisema:
“Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.” (MK.16:17-18)
Baada ya Yesu kupaa tunawakuta akina Petro na Yohana wakimsimamisha kiwete kwa mamlaka ya jina la Yesu: "Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende." (MDO 3:6)
Katika kujumuisha hii mada kuhusu jina la Yesu naomba kusisitiza ya kwamba chanzo cha taarifa zote hizi ni kutoka katika Agano Jipya! Mamlaka ya uwakilishi wa kiungu duniani imo katika jina la Yesu peke yake!
Mambo yote yanapaswa kuombwa na kutendwa sio kwa jina la Musa, wala Eliya, wala Isaya, wala Danieli, wala Yeremia. Ni kwa jina la Yesu Kristo mjumbe na mwanzilishi wa Agano jipya. Tutaendelea na uchambuzi wa msamiati wa ROHO MTAKATIFU katika makala inayofuata.

Comments